Ziara ya Zitto Mikoa ya Kusini Yaibua Mambo Sita

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
607
1,540
Masuala sita (6) yaliyoibuliwa na wananchi: Mrejesho wa Ziara ya Kiongozi wa Chama Mikoa 3 ya Kusini (Selous, Mtwara na Lindi)

Utangulizi
Kati ya tarehe 15 hadi 21 Novemba 2022 nilihitimisha Ziara ya Chama katika Mikoa mitatu (3) ya Kusini (Selous, Mtwara na Lindi). Katika ziara hii niliambatana na Wasemaji wa kisekta Ndg. Mtutura Abdallah (Msemaji wa Kilimo, Mifugo na uvuvi), Ndg. Halima Nabalanganya (Msemaji wa viwanda na biashara) na Ndg, Isihaka Mchinjita (Msemaji wa Sekta ya Nishati).

Tumetumia siku saba (7) kuyafikia jumla ya majimbo sita (6) kutoka kwenye mikoa hiyo mitatu, majimbo tuliyoyafikia ni Tunduru Kaskazini, Tunduru Kusini, Tandahimba, Ruangwa, Lindi Mjini na Kilwa Kusini. Lengo Kuu ya Ziara ilikuwa kuamsha ari ya ujenzi wa chama na kusikiliza changamoto za wananchi, wanachama na viongozi katika ngazi ya majimbo na mikoa na kutoa msimamo na mwelekeo wa Chama katika siasa za Nchi.

Kwanza, ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Wananchi, wanachama, wapenzi na viongozi wa ACT Wazalendo kwa ushirikiano waliotupatia katika siku zote kuanzia Songea Mjini hadi Kilwa Kusini. Ushirikiano wao umekuwa na mchango mkubwa sana katika kutoa maoni, kuuliza maswali na kero mbalimbali zilizowakabili.

Aidha, kupitia mazungumzo, maoni, maswali na mapendekezo yametupatia uhalisia wa kero, changamoto na madhila yanayowakumba wananchi hao.

Katika Ziara hii yapo mambo ambayo yameibuliwa na wananchi kwa hisia kubwa, sisi kama Chama tumeona ni vyema kuyaeleza kwa umma wa watanzania kwa muhtasari pamoja na hatua tulizozichukua, tunazopendekeza kuchukuliwa na Mamlaka mbalimbali na namna ambavyo tutayasimamia ili kuona jamii hizi zinapata ustawi au kuondokana na kadhia hizo.

Pia, jana tumemwandikia barua Waziri Mkuu ili kufanyia kazi masuala yaliyoibuliwa katika ziara hiyo.

A: Masuala sita(6) yaliyoibuliwa na wananchi katika ziara.

i. Migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji

Majimbo yote tuliyopita tumekutana na vilio vya wakulima kuhusu mahusiano yao na wafugaji. Wakulima wanalalamika kuvamiwa na wafugaji kwenye mashamba yao na mifugo hiyo kula mazao ya wakulima. Viongozi wa Serikali wakipatiwa taarifa juu ya kadhia hizo hawachukui hatua stahiki kushughulikia matatizo yao. Wafugaji wananywesha mifugo yao kwenye vyanzo vya maji vinavyotegemewa na wanakijiji.

Athari za migogoro hiyo imepelekea kuwa na mapigano baina ya wakulima na wafugaji, mapigano yanayohatarisha amani na usalama nchini. Tatizo hili limekuwa kubwa zaidi katika Wilaya za Tunduru, Ruangwa, Nachingwea, Liwale, Lindi Vijijini na Kilwa.

Mfano kwa Mkoa wa Lindi (Kilwa na Nachingwea) pekee migogoro hiyo ndani ya mwaka mmoja imepelekea vifo vya watu 12, taarifa za watu waliojeruhiwa wanakadiriwa kufikia 36. Nachingwea inakabiliwa na baa la njaa miongoni mwa sababu ni mashamba ya wakulima kuvamiwa na wanyama waharibifu pamoja na mifugo.

Hisia nzito walizonazo wananchi wenyeji (wakulima) kwenye maeneo hayo dhidi ya wafugaji na viongozi wa Serikali ni dhairi kuwa kuna chuki kubwa na uhasama baina ya makundi haya. Hali hii kwa maoni yetu tunaona inaweza kuhatarisha Amani katika nchi na ilipaswa kushughulikiwa mapema sana.

Tunafahamu kuwa wakulima na wafugaji ni makundi ya uzalishaji yanayotegemeana na kila mmoja anamuhitaji mwenzie. Lakini, uamuzi wa Serikali kuwaruhusu wafugaji kwenye ardhi ya Kilimo bila kuwashirikisha wanavijiji wenyewe ni kupandikiza mapigano yasiyo ya lazima. Tukiwa katika Ziara tulitoa wito kwa Serikali kuchukua hatua kadhaa kumaliza migogoro hiyo, tunaendelea kusisitiza kuwa.

Kwanza, Serikali itumie majukwaa rasmi kama Kamati za Mashauriano za Wilaya na Mikoa (RCC na DCC) kujadili masuala haya kwa upana na kuhusisha wawakilishi wa wakulima na wafugaji ili kujenga maelewano miongoni mwao.

Pili tunapendekeza kuwasikiliza wanavijiji na kuwashirikisha kwenye mipango bora ya matumizi ya ardhi ya vijiji. Na pia, kusimamia utekelezaji wa mpango ulioamuliwa na vijiji vyenyewe bila uonevu wa kundi lolote.

Serikali iwawekee wafugaji mazingira mazuri ya kufugia kwa kujenga malambo ya kunyeshea mifugo na kutengea maeneo ya malisho. Utaratibu wa sasa unasabaisha vurugu, wanalisha kwenye mashamba ya wakulima, wananywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji ambavyo vinahudumia wanavijiji.

Pia, Serikali ichunguze kwa kutumia vyombo vyake tuhuma za rushwa ambazo wafugaji wanatoa kwa viongozi wa Serikali kwenye ngazi za Wilaya ili kukandamiza Wakulima.

Tunalichukulia suala la migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji katika mikoa ya Kusini kama bomu litakalo lipuka siku za usoni. Serikali ilipe uzito unaostahiki suala hili ikiwemo kuwa na Wakuu wa Wilaya wenye uwezo mkubwa wa kutatua migogoro kwa njia ya Amani badala ya watumiaji wa nguvu za dola.

ii. Uvamizi wa Tembo kwenye mashamba ya wakulima na makazi ya wananchi.
Maeneo mengine tuliyopita hususani vijiji vinavyozungukwa na hifadhi ya Wanyama pori ya Selous tumepokea malalamiko ya wananchi kutokana na kuibuka kwa kasi kubwa wimbi la uvamizi wa Tembo.

Tatizo hili limeikumba zaidi jimbo la Tunduru Kusini na Kaskazini, wilaya ya Nachingwea, Ruangwa, Lindi Vijijini, Liwale na Kilwa. Uvamizi wa tembo kwenye makazi na mashamba unasababisha hasara kubwa sana kwa kuharibu mazao ya wakulima, wanajeruhi watu, kuharibu makazi na hata kusababisha vifo vya watu.

Taarifa za hivi karibu mathalani wilaya ya Liwale Mkoani Lindi inakabiriwa na janga la njaa kutokana na Tembo kuharibu mazao yao (korosho na mazao ya nafaka).

Sisi ACT Wazalendo mara kadhaa kupitia kwa Katibu Mkuu wa Chama Ndg. Ado Shaibu tulipaza sauti na kuishauri Serikali hatua za kuchukua hususani kuitaka iwajibike kwa kufanya utafiti wa kina ili kujua kwanini kuna Ongezeko kubwa la matukio ya tembo kutoka Mbugani na kuvamia vijiji. Pia, tuliitaka Serikali kuongeza uwezo wa kudhibiti matukio hayo kupitia idara ya wanyapori.

Lakini tunashangaa kuona hadi tumeenda tena maeneo hayo Serikali haijali kabisa vilio vya wananchi wala kuchukua mapendekezo hayo kuzima vilio na kufuta machozi yao.

Tunaendelea kusisitiza kwa kuitaka Serikali iwajibike kwa kuongeza idadi ya askari wanyamapori hususani wakati wa kilimo na mavuno angalau kila Kijiji chenye uvamizi wa mara kwa mara kuna kuwa na askari. Pia, tunaitaka Serikali itoe fidia (vifuta jasho na machozi) za uharibifu unaofanywa na wanayama hao. Fidia zizingatie hali halisi za gharama za maisha na uharibifu.

iii. Kushuka kwa bei ya korosho na mfumo wa stakabadhi ghalani
Wananchi wengi ambao wanategemea korosho kama uti wa mgongo wa uchumi wao wamelalamikia kuporomoka kwa bei ya Korosho. Minada yote iliyotangazwa haizidi Shilingi 2100 kwa kila Kilo moja. Wananchi wengi wanalalamika kuwa bei katika minada zinapangwa na hivyo kuufanya mfumo wa stakabadhi ghalani kutokuwa na msaada kwao.

Aidha, kuna kilio cha wananchi juu ya kutoridhishwa na mfumo wa stakabadhi ghalani. Wakulima wanalalamikia kucheleweshewa malipo yao wakiuza mazao wanasubiri malipo wiki mbili kwa kuwahi lakini hadi miezi mitatu kwa baadhi ya maeneo.

Jambo jingine uendeshwaji stakabadhi ghalani haumshirikishi Mkulima Serikali na viongozi wa vyama vya ushiriki wanaanzisha Makato, tozo na ushuru usiokuwa halali kwa wakulima. Tatu, Mfumo wa Stakabadhi ghalani unavyoendeshwa umekuwa udalali wa mazao bila ridhaa ya Mkulima Mwenyewe.

Vilevile, Wilayani Tunduru malalamiko makubwa yalikuwa kwenye zao la mbaazi ambapo wananchi wanalalamika kuwa bei ya Mbaazi wilaya ya Masasi ilikuwa shs 1200 kwa kilo bila mfumo wa stakabadhi ghalani wakati Tunduru ilikuwa shs 700 kwa kilo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

Zaidi ya hapo wananchi walilalamika sana kuhusu dawa ya kupuliza mikorosho kuwa feki na hivyo kupelekea mikorosho kutozaa na kuathiri mavuno yam waka huu. Wakulima walitaja makampuni yaliyopewa kazi hiyo na kugundulika kusambaza sulpher isiyofaa nab ado wameendelea kupewa zabuni hiyo msimu uliofuata.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kutafakari pendekezo letu la kuanzisha mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wakulima ili kuanzisha Fao la Bei kuweza kudhibiti kuporomoka kwa bei. Mfumo huu pia utasaidia kuwezesha wakulima kulipwa papo kwa papo wanapouza mazao yao kwa kutumia simu zao za mkononi na vile vile kuwapa wakulima Bima ya Afya.

Tunaitaka Serikali ifanye uchunguzi kuhusu madai ya wakulima wa mbaazi huko Tunduru na hatua zichukuliwe kama ikithibitika tuhuma hizo zina ukweli.

Kuhusu Stakabadhi ghalani iende kidigitali kwenye mfumo wa malipo ya Mazao ya Korosho ili iwe inawalipa wakulima papo kwa papo, yaani unauza Ufuta au Korosho zako unapata fedha yako hapo hapo. Mifumo ya kukopana ni ya kizamani na yAa kinyonyaji.

Mwisho, wakati umefika sasa tutumie teknolojia rahisi kuwezesha wananchi kubangua korosho vijijini. Nchini Vietnam kuna teknolojia hii ambayo wananchi wakiwezeshwa itasaidia sana kuongeza thamani ya Korosho na kuondoa umasikini wa watu wa Kusini.

iv. Utawala bora na vitisho dhidi ya wananchi wanapotekeleza haki zao za kisiasa.

Kuhusu masuala ya vitisho dhidi ya wananchi hili tumekutana nalo katika Wilaya ya Tunduru na Wilaya ya Ruangwa. Wananchi bado wanalalamikia matendo ya wagombea wa vyama vya upinzani kutekwa bila hatua zozote kuchukuliwa dhidi ya watekaji.

Mfano ambao umerejewa sana ni mgombea wa Jimbo la Ruangwa kutoka ACT Wazalendo aliyetekwa na kutupwa msituni Mkuranga. Hakuna uchunguzi wowote umefanyika mpaka sasa. ACT Wazalendo tunaendelea kutoa wito kwa Serikali kujenga mahusiano mema na wanasiasa wa upinzani kwani nchi hii ni ya kidemokrasia, sio nchi ya Chama kimoja na kuwa upinzani sio uadui.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iweke wazi ratiba ya utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi cha Mheshimiwa Rais kuhusu masuala ya demokrasia nchini. Mapendekezo haya yakitekelezwa yatarejesha Imani ya wananchi katika mfumo wa demokrasia nchini na kupunguza malalamiko na nyongo za wananchi kwa kiasi kikubwa.

Tunashauri pia kuwa viongozi wa kitaifa wawe mfano bora wa kuheshimu demokrasia katika maeneo wanayotoka ili kuwa mfano kwa maeneo mengine. Jimbo la Ruangwa ni eneo ambalo wananchi ambao ni wanachama wa vyama vya upinzani wanaishi kwa hofu kubwa sana.

Mheshimiwa Waziri inabidi uwe mstari wa mbele kuondoa hofu hii kwa kukaa na viongozi wa vyama vya upinzani katika jimbo hili, kuzungumza yaliyopita na ikibidi kuombana radhi na kujadili kwa pamoja namna ya kusukuma ajenda ya maendeleo ya Ruangwa kwa pamoja.

v. Malalamiko ya wananchi fidia kupisha Mradi wa Gesi Asilia.

Kuhusu suala la mradi wa LNG Lindi malalamiko makubwa ni kutoka kwa wananchi ambao walikuwa walipwe fidia na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi katika eneo la Mita 300 kutoka barabara kuu ya kwenda Lindi. Manispaa imekalia fidia hii kwa miaka 8 sasa wakati fidia ya TPDC imeshalipwa. Tunapendekeza kuwa Manispaa ya Lindi itafute mbia kutoka sekta binafsi ili wamiliki eneo hili kwa ubia na kulipa fidia wananchi.

Hata hivyo ACT Wazalendo inaishauri Serikali kuwa na Sera mpya ya fidia kwa wananchi kupisha maeneo ya uwekezaji kama haya. Tunapendekeza kwa nguvu zote kuwa mfumo wa Land for Equity uanze kutumika katika miradi kama hii ambapo ardhi ya wananchi itumike kama mtaji katika mradi na hivyo kuzipa Serikali za mitaa za maeneo husika umiliki katika miradi.

Wananchi wajengewe makazi mbadala maeneo yaliyopimwa na yenye huduma zote za kijamii na vile vile wapewe shughuli mbadala za kiuchumi kama vile ufugaji wa samaki, ufugaji wa kuku, kilimo cha mbogamboga nk.

Pili, kwenye uwekezaji huu wa Mradi kuna changamoto ya kutowawezesha kikamilifu wazawa kushiriki na kufaidika na uwekezaji huu mkubwa. Ili kuhakikisha Mradi unawanufaisha watanzania tunapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe;

Katika mazungumzo yanayoendelea kati ya TPDC, Serikali na Wawekezaji wa Mradi wa LNG Lindi ni muhimu suala la Manispaa ya Lindi kumiliki angalau 2.5% ya Mradi mzima lizingatiwe na mchango wa manispaa uwe ni Ardhi yake kama Mtaji.

Umma wa Lindi na mikoa jirani uanze kuandaliwa ikiwemo VETA ya Lindi, Mpango kabambe wa Mji wa Lindi (City master plan) na Chuo Kikuu Mtwara.

Tatu, tunazishauri Serikali ya Tanzania na Serikali ya Msumbiji kuingia makubaliano ya kuifanya Mtwara kuwa Kituo cha Huduma (services hub) kwa sekta ya Mafuta na Gesi katika Eneo RUVUMA RIVER DEVELOPMENT ZONE (Cabo Delgado, Mtwara, Niassa, Lindi na Ruvuma).

vi. Rasilimali madini kuvunwa bila kuwafaidisha wenyeji.

Tumekutana na malalamiko makubwa ya wananchi wa Kata za Mandawa (Mandawa na Hoteli Tatu) na Kiranjeranje ni kutoona faida ya shughuli za uchimbaji wa Jasi katika eneo lao.

ACT Wazalendo imebaini kuwa jumla ya tani 600,000 za Jasi zinachimbwa kila mwaka kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kilwa. Iwapo wananchi wangepata 3% tu ya thamani ya madini haya Serikali za vijiji ambamo Jasi inachimbwa vingepata Zaidi ya shilingi milioni 800 kila mwaka kama ushuru. Fedha hizi zingesaidia sana juhudi za maendeleo katika vijiji na Halmashauri ya Kilwa.

Ili kuwapa nguvu wananchi katika kujadiliana na wachimbaji tunashauri kuwa mfumo wa kutoa leseni za uchimbaji wa madini uwe na sharti la kupata kibali kutoka kwa Serikali ya Kijiji husika kupitia mkutano wa kijiji (yaani Free Prior Informed Consent).

Kabla ya Tume ya Madini kutoa leseni kwanza iwe imethibitisha na kusajili consents za wananchi katika eneo husika ikiwemo mikataba ya namna wenyeji watafaidika. Hii itapunguza malalamiko ya wananchi na vile vile itapunguza sana migogoro kati ya wawekezaji na wananchi.

B: Masuala Mengine
Moja, Suala wazalishaji wa Chumvi kukosa soko la uhakika na lenye tija kwa sababu ya kiwanda kilichopo Mkuranga kinachomilikiwa na ‘Neel Salt’ kuruhusiwa kuagiza chumvi kutoka India na hivyo kusababisha chumvi ya Tanzania kukosa soko. Tulitoa wito kwa mamlaka za Serikali kulishughulikia hili ili kuwasaidia wazalishaji wa ndani.

Pili, Kusuasua kwa Mradi wa Maji wa RUWASA wa Namwinyu amabao unahudumia vijiji vya Namwinyu na Namakungwa ambao wenye wakazi zaidi ya elfu na nane, Wilayani Tunduru. Tulimshauri Waziri wa Maji kufuatilia ili kudhibiti uzembe kwa kuwa fedha zimeshatolewa, watendaji wake hawatekelezi majukumu yao.

Tatu, Miradi ya zahanati ambayo imeachwa bila kukamilika kwa muda mrefu sana. Mfano Zahanati moja katika Kata ya Kivinje Singino jengo limekamilika kwa zaidi ya miaka 11 lakini halijasafishwa ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Nne, Kupaa kwa gharama za maisha. Kote tulikopita kilio chao ni gharama za bidhaa kama vile unga, mchele na maharage. Mifano wanayoitoa wanalinganisha na bei za mazao yao mathalani wanasema wanahitaji wastani kilogramu tatu za korosho kupata kilo moja ya mchele. Hali za wananchi ni mbaya sana. Ni muhimu kwa Serikali kulitazama suala kupanda kwa gharama za maisha kila uchao.

Hitimisho
Pamoja na mapendekezo haya kwa vyombo na mamlaka mbalimbali za nchi ninatoa wito kwa viongozi wa Chama kufuatilia kwa karibu masuala yanayohusu watu na kupaza sauti ili hatua zichukuliwe. Mwanzo mwa mwaka huu tumeunda chombo za kusimamia Serikali kinachoitwa idara ya wasemaji wa kisekta. Imekuwa ikitekeleza majukumu yake kila siku, nitumie fursa hii pia kuwaomba wananchi na wanachama wangu kuitumia fursa hiyo kuibua kero na kukisaidia chombo hiki kutekeleza wajibu wake.

Ndg. Zitto Zuber Ruyagwa Kabwe
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Dar es Salaam
24 Novemba, 2022
20221116_195518.jpg
IMG-20221116-WA0012.jpg
 
Back
Top Bottom