Ya Francois Compaore na Paulo Makonda wetu!

Ya Francois Compaore na Paulo Makonda wetu!

charz91

Member
Joined
Aug 10, 2013
Posts
34
Reaction score
12
Ya Francois Compaore na Paulo
Makonda wetu!

NIANZE makala hii kwa kukumbusha makala
yangu niyowahi kuiandika mara tu Mheshimiwa
Jaji Warioba alipotangazwa kuwa Mwenyekiti wa
Tume ya Kuandaa Rasimu ya Katiba.
Niliandika kumshauri Mzee Warioba akatae
uteuzi huo kwa kuwa aliwahi kuwa Mwenyekiti
wa Tume ya Kero ya Rushwa na akafanya kazi
iliyotukuka lakini ambayo wakubwa waliipuuza.
Nilisema kuwa, wakubwa hao hao wakikuteua
tena usimamie tume yenye uzito mkubwa zaidi,
ni vyema mtu kabla ya kukubali ukawauliza
kwanza kwa nini hawajatekeleza matokeo ya
kazi yako ya awali? Na hakika, ni bora kukataa
uteuzi mpya ili kulinda heshima yako.
Tuchukulie mtu amekuchagua uwe polisi
ukamate wahalifu. Umekamata wahalifu
ukampelekea, halafu kesho yake unakutana na
wahalifu wale wale wanavuta bangi mtaani!
Halafu Mkuu, baada ya mwezi mmoja, anakuita
tena na kukuagiza ukakamate viongozi wanaoiba
mali ya umma! Ukikubali uteuzi wa pili na
ukakumbana na dhoruba unapaswa, kabla ya
kulaumu wengine, ujilaumu wewe mwenyewe
kwanza!
Namheshimu sana Jaji Warioba na naamini
alikubali uteuzi wa pili kwa nia njema kabisa ya
kulisaidia taifa lake, lakini wahenga walisema
nia njema peke yake haitoshi kumpeleka mtu
peponi! Lazima iambatane na matendo mema!
Na ili mtu atende mema, lazima maamuzi yawe
mema! Na hili ndilo mie naona ulikuwa udhaifu
wa Jaji Warioba. Alikuwa na ile kitu Wazungu
wanaita ‘error of judgement’.
Haiyumkiniki utawala uliokupa kazi mwanzo,
ukaifanya vyema lakini ukaidharau halafu
utawala huo huo ukakupa kazi nyingine na
ukatazamia kuwa safari hii hawataidharau kazi
yako!
Waliotegemea kuwa kazi ya Tume ya Katiba ya
Jaji Warioba ingeheshimiwa na watawala hawa
hawa, hawakuwa na ‘sense of good judgement’!
Licha ya kwamba aliyepewa kuongoza kazi
aliwahi kupewa kazi na matokeo ya kazi yake
yakadharauliwa, hiyo kazi yenyewe anayeitoa
(Kikwete) ameitoa kwa ‘kulazimishwa’! Ni kazi
ambayo si tu haikuwepo kwenye mpango wake
wa kazi, lakini pia ni kazi ambayo ‘ma-
supervisor’ au wanyapara wake walishatamka
hadharini kuwa hawaitaki!
Sasa, hii haihitaji shahada ya uzamili kutambua
kuwa matokeo ya kazi hiyo yangetupwa kama
yale ya kazi ile ya mwanzo! Matokeo yake ndiyo
haya tuyaonayo sasa - kazi kudharauliwa,
waliotumwa kazi kutupiwa virago hadharani,
kutukanwa hadharani, na sasa kuvamiwa kwa
mitulinga hadharani!
Na watawala wetu kimyaa; kana kwamba
aliyetukanwa na kufanyiwa vurugu ni mkimbizi
toka ahera! Wamesahau anayetukanwa na
anayefanyiwa vurugu aliwahi kuwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu mstaafu - tena
enzi ya Nyerere ambao wao wanadai kumuenzi
kivitendo!
Hivi ukakuta watu wanamtukana hata mtumishi
wako tu wa nyumbani - tena nyumbani kwako,
hao utadai wanakuenzi? Wahenga walisema
matusi ni tiara, humrudia atukanaye kama si
mtondo basi mtondogoo! Tusibiri tuone.
Ushauri wangu kwa Mzee Warioba na wenzake
ni kwamba, safari ijayo (kama itakuwepo)
wasikubali uteuzi wa aina hii hadi wapatiwe
utekelezaji wa kazi zilizopita, na waridhike
kwamba kazi zao zimethaminiwa. Vinginevyo
umma hautawaelewa!
Sasa, nirudi kwenye mjadala kuhusu ‘kina
Francois Campaore wetu’! Sasa hivi Afrika habari
zinazovuma kwa kasi ni za Waburkinabe. Vijana
wa Burkina Faso wameamua kuleta ‘Arab Spring’
Kusini mwa jangwa la Sahara!
Ilianza kama mchezo hivi; wabunge kwa kujiona
wao ndio wao na kwa kutaka kulinda maslahi
yao na ya kiongozi wao anayewahakikishia ulwa
wakaamua kuanzisha mjadala wa kumuongezea
Rais Blaise Campaore muda wa miaka 5
kinyume na Katiba.
Ingawaje kwa kweli halikuwa jambo jipya (si
alishakaa madarakani miaka 27?), usahihi ni
kuwa walitaka kurudia kuvunja Katiba kwa kuwa
hata alipoingia madarakani hakuingia kwa
mujibu wa Katiba!
Hakuheshimu Katiba toka alifu, bee tee! Aliingia
madarakani kwa kumuua swahiba wake Thomas
Sankara na kumzika kinyama kwa kijiko cha
tingatinga la manispaa! Nadhani wabunge
walijiamini kuwa hawatafanywa kitu maana
wameshika dola!
Hata hivyo, safari hii, vijana ambao wengi wao
walizaliwa baada ya kuuawa Thomas Sankara
wakasema liwalo na liwe, na wakaamua kwenda
bungeni wanapojadili uhalifu!
Mshikemshike uliotokea sasa ni historia. Itoshe
tu kusema kuwa, kila mbunge alihaha binafsi
kujiokoa! Jengo la bunge likapigwa kiberiti! Si
jambo jema hili, lakini tujiulize; kwani kuvunja
Katiba ni jambo jema? Binafsi, nachukia zaidi
kuvunjwa Katiba kuliko kuchoma jingo la Bunge
linalotumika kuvunjia Katiba!
Jeshi lile lile lililokuwa linamtukuza Compaore
likaamua kuvunja serikali yake! Wanajeshi
wengine wakajiunga na vijana mitaani. Nyumba
binafsi za wabunge waliokuwa viherehere
zikapigwa kiberiti!
Compaore akajibaraguza lakini tayari akiwa
ameanza ‘riadha’ kukimbia mji mkuu! Eti
amekubali kuvunjwa kwa serikali yake lakini
hataachia madaraka mpaka atakapochaguliwa
rais mpya kikatiba!
Ubazazi wa hali ya juu huo! Yeye mwenyewe
aliingia madarakani bila kufuata Katiba na
chaguzi zote zikilalamikiwa kwa kuwa tume
haikuwa huru na vyombo vya dola vikishiriki
kuchakachua kura!
Hii ni sawa na mwizi awaibie radio mumkamate,
na kisha aseme hatarudisha radio mpaka
amuone mmiliki halali wa radio hiyo! Afrika
kweli ni jiko la vituko! Haviishi! Vinapikwa kila
siku!
Ndipo hapo sasa nataka kuwakumbusha
mabwana wadogo wa CCM - chama ambacho
kabla yake niliwahi kuwa mwanachama wa TANU
YOUTH LEAGUE, TANU na baadaye mwanachama
mwanzilishi wa CCM 1977 (na nina kadi zangu
zote)! Nina kadi yangu ya TYL, TANU na CCM
(ilee ya Mwalimu Nyerere)!
La kwanza; niwakumbushe kuwa vijana ndiyo
nguzo ya taifa na ya chama chochote cha siasa.
Vijana wakiwa dhaifu na taifa litakuwa dhaifu na
chama kitadhoofika sana. Vijana wakiwa imara
taifa halitayumba.
Tumeona kwenye ‘Arab Revolution’ huko Tunisia,
Algeria, Misri na sasa Burkina Faso. Vijana
wakiwa ni watu wakutumwa au kutumiwa na
wazee wanapotosha mantiki ya kuwa vijana.
Vijana wakishaweka ‘siasa za tumbo’ na
wakasahau maslahi mapana ya taifa, hawana
tofauti na wazee waliochoka!
La pili ninalotaka kuwakumbusha vijana wa CCM
ni kuwa, wao sio vijana pekee nchini mwao!
Kuna vijana wengi tu zaidi yao. Wengine ni
wanachama wa vyama vya siasa na wengine
ambao ndio wengi hawana chama chochote.
Wasijidanganye kuwa wao vijana wa CCM ndio
wanawakilisha vijana wote Tanzania.
Ninachomaanisha ni kwamba, siku kundi la
vijana wenzao wasio wanachama wa CCM
litakaposema ‘liwalo na liwe’, kama walivyosema
vijana wa Burkinabe, hapatatosha!
La tatu, na ambalo ndio hasa msingi wa makala
yangu hii ni kuwakumbusha vijana kuwa kuna
leo na kesho. Na hapa ngoja nitumie mfano wa
karibuni wa Burkina Faso.
Kule Burkina Faso kulikuwa (maana sasa ni
historia) na mdogo wa Rais Blaise Campaore
akiitwa Francois Campaore. Wengi wenu
Tanzania hamumfahamu huyu. Huyu alikuwa ni
‘Rais namba mbili’ (Le president numero 2) kule
Burkina Faso.
Japo hakuwa na cheo chochote rasmi serikalini,
lakini akitoa amri ilikuwa ifuatwe bila kuhoji!
Ukiacha kuifuata utaona cha mtema kuni!
Pale jijini Ougoudougou mahali alipofukiwa
(kusema kweli hakuzikwa) mwanamapinduzi
Thomas Sankara, vijana walipageuza ‘shrine’ ya
kwenda kumuenzi!
Vijana walijenga desturi ya kupafanyia usafi na
kukusanyika hapo kumkumbuka shujaa wao;
japo wengi walizaliwa baada ya yeye kuuawa!
Sawa na mtu mwema kijijini hujulikana hata na
mlevi wa gongo!
Lakini watawala wa Burkina Faso hawakupenda
hili la kumuenzi Sankara kama ambavyo
watawala wa Tanzania nao wasivyopenda sana
hili la kumuenzi Nyerere!
Ilikuwa kama vile nafsi zinawasuta maana Rais
Blaise Campaore na Thomas Sankara walikuwa
maswahiba wa pete na chanda!
Huyo kijana Francois Compaore ndiye aliyekuwa
mstari wa mbele kuongoza timuatimua ya vijana
wenzake kila wakikusanyika kwenye hiyo ‘shrine’
kumwomboleza Sankara! Si hivyo tu, Francois
akajilimbikizia mali si haba!
Sasa, majuzi kaka yake – yaani Rais Compaore
alipolazimika kukimbia Ikulu na kuachia
madaraka, huyu mdogo mtu ni miongoni mwa
wale viherehere waliosakwa kwa udi na uvumba
waadabishwe na vijana wa Burkina Faso.
Iliposemekana ameonekana akikimbilia uwanja
wa ndege, vijana walienda huko haraka ili
wamkamate. Uvumi ukaenea Francois
kakamatwa, lakini kumbe machale yalimcheza
hakwenda airport!
Hivi sasa amekimbilia Benin na anaishi kama
mkimbizi; huku mali zote alizofisadi kaacha
Burkina Faso! Kaka mtu - Rais Blaise Campaore
yeye na familia na marafiki zake wamekimbilia
Abidjan, Cote d’ ivoire! Yaani familia iliyokuwa
pamoja, na iliyokuwa na jeuri ya kupindukia
sasa imetawanyika!
Hili ni somo murua kwa vijana wetu kina Paulo
Makonda, Ridhiwani Kikwete na wengineo.
Wanapaswa kutizama hali hii na kujifunza mengi
sana!
Na viongozi wetu wanaoruhusu watoto wao,
ndugu zao, wanafamilia, marafiki na vijana
kupiga, kutukana, kuhujumu taifa na
kujilimbikizia vyeo na mali, wanapaswa
kutambua siku vijana wataamua kuiga msemo
wa kiongozi mwenzao kuwa ‘liwalo na liwe’,
inawezekana kabisa wengine wakakimbilia
Msumbiji, wengine Angola na wengine Zambia!
Watoto wao na ndugu zao na jamaa zao
wakajikuta wamekimbilia Sudan, Ethiopia au
Kenya! Watakutana mbele ya safari wakiwa wote
dhofu kul-hali!
Lakini nisimalize makala hii bila kuzungumzia
upuuzi wa vijana wa CCM wakiongozwa na Paulo
Makonda kwenye mdahalo ule wa Blue Pearl
Hotel pale Ubungo, Dar es Salaam.
Kwanza, nianze na huyu Paulo Makonda; maana
naona huyu ni hatari kwa ustawi wa vijana si wa
CCM pekee bali taifa kwa ujumla. Hivi kweli ni
lini vijana wa CCM wameanza huu utaratibu wa
kuvamia mikutano na mabango?
Haidhuru wamevamia na mabango na kufikisha
ujumbe, lakini ni nini kilipelekea huyu kijana
kumshambulia Jaji Warioba kiasi tulivyoona
kwenye mapicha?
Hivi Paulo hatoki kile chama tulichoona
wakijitapa na kunengua kuwa kazi ya kupitisha
Katiba imekwisha? Sasa huko kwa watu ambao
wanaona kazi haijaisha walifuata nini?
Na je, hivi Paulo hata ile nidhamu kuwa huyu
anaweza kuwa baba au hata babu yako
haikuwepo? Hivi katumwa au ni kichwa chake
tu?
Kisa hiki kimenikumbusha hadithi tuliyokuwa
tukisoma utotoni na kuimba ‘Paulo usije
kucheza na sisi una mikono michaaafu,
tutachafuka hadi kunuka una mikono michaafu’.
Hakika nategemea wenzie ndani ya chama
wamuimbie wimbo huu!
Nilimfuatilia sana huyu Makonda kwenye
mahojiano aliyofanya na EATV baada ya Bunge
Maalumu la Katiba kumalizika, na nilibaini kuwa
uwezo wake wa kuelewa na hata wa kujieleza ni
mdogo mno!
Kwa mfano, alisema Baraza la Vijana ni kwa ajili
ya Bara pekee na mtangazaji akamuuliza sasa
mswada ukija bungeni wabunge toka Zanzibar
watahusika? Badala ya kujibu alianza porojo na
kujitapa watu ndio hawajui. Hadi sasa hata mie
najiuliza itakapofika muda wa kujadili mswada
huu wabunge toka Zanzibar watatoka nje au
watawekewa kufuli midomoni?
Kijana huyu alishindwa kutoa jibu na kutokuwa
muungwana. Si angesema kwa kweli hata mie
sijui nitafuatilia? Kungekuwa na ubaya gani
kuliko kusema watu ndio hawajui!?
Katika mahojiano hayo, pia alidai kuwa uwepo
wa Baraza la Vijana kutawakomboa vijana katika
umasikini! Eti mabilioni ambayo yeye aliyaita ‘ya
Kikwete’ yatapatikana kwa urahisi kukiwa na hilo
baraza! Masikini Paulo wetu alisahau Baraza
litaundwa; ilhali Kikwete akiwa hayuko tena
Ikulu! Sijui atayaita mabilioni ya nani?
Pia nikajiuliza huyu kijana si anaitukana Serikali
ya chama chake? Ina maana toka haya
mabilioni yatolewe hayakuwafikia vijana kwa
kuwa hakukuwa na Baraza? Yalikuwa yanaenda
wapi? Nani hao walijigeuza ndio Baraza la
Vijana? Na huyo mwenye mabilioni yake ina
maana alitulia tuli wakati walio chini yake
wamejigeuza Baraza la Vijana?
Nikajiuliza tena hivi huyu kijana anataka
kutuaminisha kuwa kwa kuwa Ujerumani,
Uingereza, Marekani na kwingineko duniani
hawana Baraza la Vijana katika Katiba, vijana
wao ni masikini?
Yaani tukishapata Baraza la Vijana, basi vijana
wetu watakuwa matajiri kuliko vijana wa
Marekani na Uingereza? Hivi kweli hii ni akili ya
ujana? Ndiye kijana anayeweza kujakuwa
Mwenyekiti wa hilo Baraza!?
Napenda kumuasa kijana huyu kwa kumwambia
yeye si kijana wa kwanza ndani ya CCM!
Tulikuwapo vijana, wapo vijana na watakuja
vijana ndani na nje ya CCM wenye kujitambua
kuliko yeye!
Haijawahi kutokea vijana (ukiacha aliyemzaba
Mzee Mwinyi kibao kwa masuala ya kondomu)
aliyewahi kumvamia kiongozi wa CCM mstaafu
au aliye madarakani hadharani jinsi alivyofanya
yeye!
Tutashangaa sana kama kitendo hiki cha kihuni
kitaachwa bila kukemewa au mhusika kufikishwa
kwenye vyombo vya nidhamu vya chama chake
au hata vyombo vya sheria ili sheria ichukue
mkondo wake!
Na kama nilivyosema hapo mwanzo, wahenga
walisema matusi ni tiara - humrudia aliyeirusha!
Viongozi mnaoshabikia nyuma ya pazia vitendo
hivi vya utovu mkubwa wa nidhamu
alivyofanyiwa Jaji Warioba mjue kesho na nyie
mtakapokuwa mmestaafu mtakuwa mmetoa
kibali kwa vijana wa kesho wawazabe kelbu na
kuwakata mtama!
Nimalizie kwa kumshauri Paulo wetu kuwa
badala ya kuitisha mikutano (ambayo kwa
hakika kuna kila dalili wapo wanaomfadhili)
kudai eti hakumpiga wala kumfanyia vurugu Jaji
Warioba, afanye uungwana wa mtoto
aliyepotoka na kujirudi kwa kwenda na wazee
(hata kimya kimya) kumtaka radhi Mzee
Warioba!
Hakuna atakachopungukiwa. Kinyume chake
vijana wasafi watamuimbia kale ka wimbo ketu
ka shule ya msingi! Tafakarini.

Makala hii iliandikwa na Yahya Msangi na kuchapwa katika gazeti la Raia mwema toleo la No 379 la tarehe 12 Nov 2014, kwakweli wakati nilipokuwa nikiisoma nilipata kutafakari mambo mengi na ya msingi ambayo Mwandishi aliyatoa kama ushauri kwa kaka yetu Paulo Makonda, lakini binafsi nilikwenda mbali na kutafakari kwa kirefu na mapana hakika nilijiridhisha kuwa ushauri alioutoa Mwandishi ni ushauri ambao unapaswa kumfikia kila kijana. Hata hivyo nikaona niwamwagie hapa wana JF ili mpate kuipitia kwa wale walioikosa.
 
Back
Top Bottom