Wote waliosimamishwa masomo vyuoni warudishwe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wote waliosimamishwa masomo vyuoni warudishwe

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by BAK, Jan 8, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Jan 8, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,611
  Likes Received: 82,195
  Trophy Points: 280
  Watakaorejea vyuo vikuu watangazwa
  Stella Nyemenohi
  Daily News; Thursday,January 08, 2009 @21:15​

  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na cha Sokoine cha Kilimo (SUA) vimetoa orodha ya wanafunzi waliokubaliwa kurudi chuoni huku ikibainika kwamba wengi wameachwa kutokana na kutokidhi masharti waliyopewa.

  Taarifa ya uongozi wa vyuo hivyo iliyotolewa jana kwenye vyombo vya habari, ingawa haikutaja idadi ya wanafunzi walioachwa kutokana na uchambuzi uliofanyika, umewaelekeza wanafunzi ambao hawataona majina yao, watambue kwamba hawakukubaliwa kutokana na kutokidhi vigezo.

  Kwa upande wa UDSM, habari kutoka ndani ya chuo hicho, zilisema kati ya wanafunzi 9,000 waliorudisha fomu zilizochambuliwa ni wanafunzi 3,000 pekee ndio waliokidhi vigezo na kutangaziwa kurudi chuoni. Wanafunzi hao wa UDSM walisimamishwa masomo Novemba 12 mwaka jana kutokana na migomo iliyofanyika chuoni hapo ambayo wanafunzi walikuwa wakipinga sera ya uchangiaji wakitaka Bodi ya Mikopo iwalipie ada kwa asilimia 100.

  Taarifa iliyotolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, anayeshughulikia Taaluma, Makenya Maboko, ilisema chuo hicho kitafunguliwa Januari 19 mwaka huu na wanafunzi watakaotakiwa kuripoti, ni wale ambao majina yao yamo katika orodha iliyotolewa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanafunzi hao watapewa vitambulisho vipya baada ya vile walivyokuwa navyo kufutwa.

  Vilevile wanafunzi waliokubaliwa, wamepangiwa upya vyumba vya kuishi na wameelekezwa kuangalia vyumba walivyopangiwa katika tovuti ya chuo. Taarifa hiyo ya chuo, iliwaelekeza wanafunzi ambao majina yao hayakutajwa katika orodha wajihesabu kwamba hawakufanikiwa na hivyo hawaruhusiwi kuingia katika mazingira ya chuo.

  Wale waliowasilisha fomu za maombi lakini hawakulipa ada ya mwaka 2008/09 walitakiwa kulipa kiwango wanachodaiwa kupitia benki kabla ya Alhamisi ijayo. Habari zilisema kutokana na asilimia kubwa ya fomu kubainika kuwa na dosari, chuo kilitoa muda hadi Alhamisi ijayo, wanafunzi hao wapatao 6,000 wawe wametatua dosari hizo.


  Orodha ya watakaorekebisha, itatolewa katika tovuti ya chuo Ijumaa ijayo. Ingawa taarifa kamili za walioachwa SUA hazikutolewa, lakini pia kulingana na orodha iliyotolewa, inatoa hisia kwamba wako wengi ambao hawakuchaguliwa kutokana na kutokidhi masharti.

  Kwa upande wa SUA, taarifa iliyotolewa, inawaelekeza wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza na wa pili wa Shahada ya Sayansi ya Mazingira na Utawala – (BSc. Environmental Sciences and Management) waliosimamishwa masomo Novemba 14 mwaka jana, kuwa wanapaswa kurejea chuoni hapo kuanzia jana hadi kesho.

  "Wanafunzi ambao majina yao hayataonekana katika orodha, wajue kwamba hawakukidhi masharti ya udahili na hawatatakiwa kuripoti kwa ajili ya masomo," ilisema taarifa hiyo. Wanafunzi waliotolewa majina yao, ni wale ambao wamekidhi masharti ya kudahiliwa upya ikiwa ni pamoja na kulipa ada ya mwaka 2008/09 .

  Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Ardhi, uchambuzi wa majina ulikuwa ukiendelea jana. Hata hivyo, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idrissa Mshoro, aliliambia gazeti hili kwa simu, kwamba kazi hiyo inatarajiwa kukamilika leo tayari kwa kutoa orodha ya majina ya waliokubaliwa kurudi chuoni.

  Wanafunzi wa vyuo vikuu saba, walirudishwa nyumbani kwa muda usiojulikana, kutokana na vurugu za kudai sera ya uchangiaji wa gharama za elimu ya juu ifutwe au kufanyiwa marekebisho. Wanafunzi hao walikuwa wanataka wapewe mikopo asilimia 100 badala ya utaratibu wa sasa wa kukopeshwa asilimia 60, 80 na wengine 100 ya ada na gharama nyingine, kulingana na uwezo wao wa kujilipia gharama hizo. Baada ya hatua hiyo, wanafunzi hao waliamriwa kujaza fomu upya za udahili na kulipa asilimia 40 ya ada kabla ya kurejeshwa vyuoni.
   
Loading...