Ilikuwa 2021 nakumbuka ilikuwa mwezi wa 4, humu jamii forum nilikutana na binti mrembo hivi,
Siku Moja nikiwa online usiku saa sita, yeye ndo alinitumia ujumbe PM, " wewe mtu hulali tu"? Na Mimi nikamwuliza "mbona wewe hujalala" akasema Hana usingizi, tulichat kidogo nikawa nimelala, kesho yake asubuhi akanitumia ujumbe PM "umeamkaje" nikamjibu salama, hapo hapo akanitumia namba yake ya simu bila kumuomba, akaniambia hiyo namba chukua tutakuwa tuna juliana hali, nikasema sawa.
Baada ya wiki tulijikuta tuna ingia kwenye mahusiano rasmi, alikuwa binti mrembo wa kisukuma, anavaa nguo za kujistiri sana, Yani Kwa kifupi alionekana ni binti ambaye kalelewa katika maadili ya kikristo hata katika uongeaji wake, Kila jumapili anakuambia anaenda kanisani, ijumaa kwenye maombi, hayo tu yalitosha kuamini nimepata mke na nikawa Niko tayari Kwa Kila kitu, akili yangu ikaanza kufikiria tu kuhusu ndoa kitu ambacho mwanzoni sikuwahi kufikiria.
Mwezi wa sita mwaka huo 2021 aliniomba aje kwangu Ili tuonane, nikasema haina shida, nikamtumia laki na nusu, afanyie maandalizi na nauli pia, Yani nilituma hiyo pesa nikiwa Sina shaka juu yake,
Nakumbuka pesa nilimtumia kama ijumaa huku safari ilitakiwa aanze jumatatu, siku hiyo ya jumatatu niliamka nikiwa na furaha kwamba usiku naenda nampokea kipenzi changu,
Lakini ilivyo fika saa mbili asubuhi nikawa napiga simu haipatikani, nikawa najipa matumaini kuwa labda Huenda ni mtandao njiani, nikawa napiga namba zake zote mbili hazipatikani, bado nikawa najipa matumaini ni mtandao.
Saa tano asubuhi, nilipiga tena simu ikaita lakini haikupokelewa, piga tena, simu haipokelewi, mpaka saa kumi jioni simu haipokelewi, na mwisho kabisa akaniblock Kila sehemu, namba unayo piga inatumika, JF pia nikawa nimesha blokiwa.
Pale pale nikasema tayari nime tapeliwa, na Wala sikujaribu kumtafuta Kwa namba nyingine, ilibidi tu nimwachie MUNGU, ila ukweli ni kwamba niliumia sana, sijawahi kupata maumivu kama Yale aliyo nifanyia yule binti, nililia usiku Kwa uchungu mno.
2023 mwezi wa Saba nikiwa kazini asubuhi nilipigiwa simu na namba ngeni, nilivyo pokea, nikasikia sauti ya kike ambayo haikuwa ngeni masikioni mwangu akiwa anaongea Kwa hofu, alianza na neno samahani, akajitambulisha jina lake, Kweli niliye mfikiria alikuwa ni yeye, akasema, yeye Yuko muhimbili ame muuguza mama yake alivunjika nyonga, Wana siku tatu wako pale, binti akasema yeye analala nje pale hospital, ndugu waliye mtegemea hajaja hata kuwaona, nilicho mjibu nilimwambia jioni nikitoka kazini nitapitia hospital kuwaona.
Jioni saa 11 nilifika pale muhimbili nikampigia simu anielekeze ni wodi Namba ngapi, akaniambia nikae Getini anakuja kunifuata, nikasema sawa.
Nilimsubiri pale Getini, mara simu ikapigwa akaniuliza uko wapi? Nikamwambia zilipo paki Bajaj, nilimuona binti mrembo Asiye na mambo mengi Akija anaongea na simu nikajua ndo yeye, nikamfuata, tukasalimia japo alikuwa na aibu sana iliyo changanyika na hofu lakini nikawa namuonyesha uso wa tabasamu ila moyoni roho imefunga vibaya Kwa hasira.
Tulienda mpaka wodini, nilimkuta kweli mama yake kalala kitandani kawekewa chuma, nilimsalimia yule mama, alionekana ni mtu wa Imani sana mana biblia ilikuwa Iko pembeni ya kichwa chake, nilipiga sana stori na mama huku binti kakaa pembeni anatusikiliza tu huku ananitazama Kwa kuibia.
Muda wa kuona wagonjwa uliisha nikawa nime wakabidhi vitu nilivyo wanunulia, nikawaambia Kila jioni nitakuwa naenda kuwaona, yule mama alifurahi sana na akawa ameshusha maombi kwangu, alivyo maliza nikawaaga Ili niondoke, yule mama akaniomba niende na binti yake mana Hana pakulala,analala nje na Kuna mbu hatari, nilijifikiria sana, nikawaza sana, Sasa nikajisemea kwangu naishi mwenyewe na nimepanga chumba na sebule itakuwaje?! Nikisema nimpeleke kwetu awe analala huko napo ni mbali na muhimbili ilipo, nikasema potelea mbali acha niende naye nitamwachia chumba nitakuwa nalala sebuleni.
I will back
SEHEMU YA PILI NA MWISHO.
ILIPO ISHIA.
,,,,nikawaza sana, Sasa nikajisemea kwangu naishi mwenyewe na nimepanga chumba na sebule itakuwaje?! Nikisema nimpeleke kwetu awe analala huko napo ni mbali na muhimbili ilipo, nikasema potelea mbali acha niende naye nitamwachia chumba nitakuwa nalala sebuleni.
TUENDELEE
Ilibidi niondoke naye japo alikuwa hajiamini, nikawa najaribu mara Kwa mara kumuongelesha sana Ili kumuondoa hofu, tulitoka mpaka nje pale Getini muhimbili, tulipanda gari tukawa tumekaa siti Moja, niliendelea kuwa namuongelesha sana Ili aondoe hofu kabisa juu yangu mana niliona kama hayuko na Mimi muda wote anawaza.
Tulivyo fika nyumbani, nilimkaribisha mpaka ndani akawa amekaa nikaingia chumbani kutoa vitu vyangu vya mhimu Ili yeye aingie abadili nguo akaoge, nilivyo toka tu chumbani narudi sebuleni akanipigia magoti mbele yangu akiwa analia sana na kutoa machozi, akaniomba msamaha Kwa alicho kifanya, nikawa najaribu kumnyanyua lakini anazidi kulia huku akisema, eti kipindi Niko naye alikuwa tayari ana mchumba mwingine ndo maana hakuja, ilibidi nicheke kimoyo moyo huku najisemea huyu kima anajua Mimi ni mtoto, nilimnyamazisha na mwisho akatulia nikamwambia aingie chumbani akaoge.
Alivyo maliza, alivaa nguo ikabidi nimwambie twende gengeni tukanunue mahitaji yote yanayo hitajika Kwa ajili ya chakula Cha mama na sisi, tulienda gengeni tukanunua vitu vyote tukarudi nyumbani, alipika chakula chetu sisi na chakula Cha kesho Kwa ajili ya kumpelekea mama hospital.
Muda wa kulala nilimwambia akalale chumbani, Mimi nikawa nataka nilale sebuleni kwenye sofa, Cha ajabu alikataa akasema kama ni hivyo ni Bora yeye alale sebuleni kuliko alale chumbani halafu Mimi sebuleni, nilimbembeleza sana akalale chumbani ila mwisho alikubali, mida ya saa sita usiku akanifuata sebuleni tena na kuniamsha eti anakosa usingizi ni Bora na yeye alale sebuleni, nikaamka nikamwambia awe huru akalale chumbani Wala asihofu kuhusu Mimi, akaanza tena kulia huku akiomba nimsamehe, nikamwambia Mimi nilisha kusamehe na ndiyo maana nimejitolea kukusaidia, ilibidi tu arudi kinyonge chumbani kulala.
Mimi nilijitolea Kwa moyo mmoja kuwasaidia yeye na mama yake na ndiyo mana mahitaji yote ya hospital nikawa nagharamikia Mimi, asubuhi anaenda na bodaboda halafu jioni tuna rudi wote, ndani ya mwezi mzima nilio kaa na binti ndani kwangu, alitumia Kila njia Ili niweze kulala naye lakini aligonga mwamba, aliangusha sana khanga mbele yangu na kubaki na chupi lakini nikawa namwambia MUNGU nilinde sitaki hapa nirudi nyuma, naomba nitimize Wema huu Ili nimalize salama, nilifanyiwa mitego mle ndani mpaka nikawa nabaki nacheka wakati mwingine.
Baada ya mwezi mmoja mama yake alifanyiwa oparesheni ya kuwekewa chuma kwenye nyonga, Mimi niliwachangia laki mbili na nusu kwenye laki 4 ya oparesheni na nyingine walichangiwa na ndugu zao huko mwanza pamoja na watu wa kanisani alipo kuwa anasali yule mama,
Na baada ya siku mbili mama kufanyiwa oparesheni aliruhusiwa kurudi nyumbani ila akaambiwa baada ya wiki anatakiwa kurudi kliniki, ilibidi na mama pia nimchukue twende tukaishi kwangu, niliwahudumia vizuri sana, na sikujua ule Wema niliutoa wapi kipindi kile mpaka nilikuwa najishangaa.
Nilikaa nao wiki mbili kwangu, wanakula vizuri na kunywa, pesa ya kwenda kliniki na mazoezi nikawa natoa Mimi, yule mama ilikuwa Kila siku lazima aniombee Kwa kuniwekea mikono, alikuwa anapenda sana kupiga stori na Mimi Kila nikirudi kazini, mara nyingi akawa ananiambia najua binti yangu alikuumiza sana na ndiyo maana sijataka kuzungumzia kuhusu Hilo jambo, ila Mimi napenda sana nikushukuru Kwa wema wako, ila natamani ujaribu kumpa nafasi nyingine binti yangu huwa anajutia sana, na usiku huwa halali, nahisi amesha jifunza, nikawa namjibu mama, sawa haina shida mama yangu nitafanya hivyo.
Kipindi hicho walicho kuwa wanakaa kwangu niligombana na ndugu zangu sana, waliona kama nimelogwa, natumia pesa nyingi Kwa watu ambao siyo ndugu zangu na hawajui nime watoa wapi hawa watu, nakumbuka Kuna siku mama yangu alikuja kwangu kunitukana mbele Yao akanitamkia maneno mazito lakini moyoni mwangu nilikuwa najua ninacho kifanya, hivyo nilimuacha mama aongee aondoke, mama yangu alivyo ondoka ikabidi mama yake na binti naye aanze kulia Kwa uchungu huku akiomba waondoke kwangu, ilibidi nimtulize yule mama Kwa kumwambia aachane na mama yangu anisikilize Mimi niliye waleta kwangu.
Baada ya kumaliza kliniki na mama akawa anatembelea magongo vizuri akataka kurudi nyumbani kwake mwanza, nikamwambia sawa, nakumbuka ilikuwa mwezi wa 9 mwaka huo 2023 nilienda kukata tiketi za watu watatu, Yani Mimi, mama na binti, nilipanga niwasindikeze mpaka kwao mwanza, na kesho yake tulisafiri wote mpaka mwanza, tukaenda mpaka kwao, nilikaa siku mbili nikaaga nataka kurudi dar.
Siku hiyo naaga naondoka ilikuwa alfajiri, mama alishusha hayo maombi ya nguvu ya shukrani, sijawahi kuona maombi yenye nguvu kama Yale, aliomba ndani ya nusu saa maombi yaliyo Shiba, alivyo maliza tukaagana na nikawa nimeondoka huku binti haamini,
Toka siku hiyo mpaka Leo Mimi na binti hatuwasiliani japo mwanzoni alikuwa akinitafuta nikawa namjibu huku najikaza tu ila badae nikawa simjibu kabisa mana roho yangu bado ilikuwa na chuki juu yake, nikawa nawasiliana na mama yake tu mpaka Leo.
Mpaka muda huu binti kazalishwa Yuko tu pale nyumbani anauza genge na mama yake, Hana mwelekeo Kila siku ni ugomvi na wadogo zake, mwaka Jana aliolewa akakaa Kwa mume wake miezi nane tu wakaachana ndo akarudi na mimba ya huyo mtoto.
Mimi ninacho shukuru ni kwamba katika Wema nilio ufanya MUNGU kanilipa zaidi ya nilicho toa, Kwa Sasa nayaona matunda ya yake maombi aliyo kuwa ana shusha yule mama, sikuwahi kufikiria Mimi Leo hii nitakuwa na kwangu na kumiliki ka-usafiri kangu kangu ka-maana.
Nimejifunza Kuna watu wabaya wanakuja kwenye maisha yetu ila badae wanaweza kuwa daraja la kutufikisha sehemu Fulani licha ya wao kutuachia maumivu makubwa moyoni.
Yule mama nishamuambia akiwa na shida yoyote asisite kuniambia Niko tayari muda wowote kutatua tatizo lake, na hapa najiandaa kuwatumia Kila kitu watakacho tumia krismas na mwaka Mpya, nimeichagua Ile familia kuwa sehemu ya sadaka zangu