MAMBO YA WENYE DINI HAYA
Mchungaji atiwa mbaroni kwa kukutwa na viungo vya albino
Habari Nyingine
• Mchungaji kortini kwa madai ya kukutwa na viungo vya binadamu 21.02.2009 [Habari Zaidi]
• Mwanahabari ‘anasa' muuza viungo vya albino 21.07.2008 [Habari Zaidi]
• Wawili mbaroni wakisaka albino 17.12.2008 [Habari Zaidi]
NA PETER KATULANDA, MWANZA
WATU wanane wakiwemo waganga wa kienyeji wawili na Mchungaji wa Kanisa la Baptisti la wilayani Magu, wametiwa mbaroni wakiwa na viungo vya albino, Aron Mongo, aliyeuawa Mkolani wilayani Nyamagana jijini Mwanza.
Watuhumiwa hao walikamatwa juzi kwa nyakati tofauti, baadhi yao akiwemo mchungaji wakiwa katika harakati za kutafuta soko la kuuza kiungo hicho.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jamal Rwambow, akitoa taarifa za kukamatwa kwa wauaji hao jana, alisema polisi limewakamata watuhumiwa wakiwa na mfupa wa mguu ambao walikiri ni wa mlemavu huyo aliyekuwa mkazi wa Ibanda Relini Mkolani.
Alisema mbali na mfupa huo, walikamatwa wakiwa na nyama za marehemu ambazo walizitupa sehemu tofauti, ambazo zimekutwa zimeharibika na polisi wamezihifadhi kwa ajili ya vielelezo na uchunguzi wa kitaalamu.
Rwambow alisema kukamatwa kwao kumetokana na taarifa za raia wema wawili ambao jeshi hilo limewazawadia sh. Nilioni moja kama lilivyotoa ahadi kwa wananchi kuwa atakayefanikisha kupatikana kwa watuhumiwa wa mauaji ya Mongo, watazawadiwa kiasi hicho.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mchungaji Alfred Komanya (35) wa Kanisa la Baptist Irungu wilayani Magu, Chacha Jeremiah (30) na Mathew Mlimi (21) wakazi wa Mahina wilayani Nyamagana jijini hapa.
Waganga waliokamatwa ni Gervas Lutufu (58) mkazi wa Nyanguge wilayani Magu na Kishosha Lutambi au Komanya (60) mkazi wa Mahina wilayani Nyamagana ambao pamoja na viungo hivyo, wamekutwa wakiwa na nyara za serikali na tunguli za uganga.
Nyara walizokutwa nazo ni ngozi mbili za wanyama ambao hawakufahamika mara moja, ndege mmoja aliyekaushwa (hakufahamika jina) na mkia unaodhaniwa kuwa wa nyumbu.
Wengine ni Paschal Lugoye au Mashiku (28) mkazi wa kijiji cha Semba Katani Buhongwa, Paul Lumalija (36), mkazi wa kijiji cha Kishili Kanindo Katani Igoma na Alex Joseph au Bugwema Silola (24) mkazi wa Mahina.
Rwambow alisema baada ya kuhojiwa watumiwa walikiri kuhusika na mauaji ya Aron Mongo yaliyotokea Juni 26, mwaka huu Ibanda Relini.
Alifafanua kuwa wamebaini mganga wa jadi Kishosha, aliwahi kumtibu marehemu na mahali anapoishi si mbali sana na yalipokuwa makazi ya albino huyo na kuwa mganga na mchungaji huyo ni ndugu.
Kamanda huyo alisema polisi bado inaendelea na uchunguzi wa kina dhidi ya watuhumiwa hao na mtandao mzima wa wauaji wa walemavu hao na kuwaomba wananchi wazidi kulipa ushirikiano ili litokomeze mauaji hayo ya kikatili.