Vitendawili vya uchaguzi(1): Kupinga sera ya kutenga dini na siasa ni kunadi sera ya kuunganisha kofia hizo

Deus J. Kahangwa

Senior Member
Jan 7, 2013
189
122
1601784216899.png

USULI

Uchaguzi Mkuu huzalisha vitendawili vingi vinavyopaswa kujibiwa na wapiga kura katika harakati zao za kusimamia ujenzi wa jamii inayowajibika kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kitendawili kimojawapo ni swali lifuatalo: Kati ya Taifa linalotekeleza sera ya kutenganisha kofia ya kisiasa na kofia ya kidini na Taifa linalotekeleza sera ya kuunganisha kofia hizi, Taifa lipi linazalisha jamii iliyostaarabika zaidi kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimaadili? Makala hii inatoa jawabu kwa swali kwa kuonyesha kwamba sera ya kutenganisha kofia hizi ni bora kuliko sera ya kuziunganisha kofia hizi. Imegawanyika katika sehemu sita zifuatavyo: A. Utangulizi; B. Utetezi wa hoja ya kutenganisha kofia; C. Mapingamizi dhidi ya hoja ya kutenganisha kofia; D. Majibu ya kubutua mapingamizi; E. Muhtasari wa makala; na F. Hitimisho la makala.

  • Makala hii imetafitiwa na kuandikwa na: Deusdedith Kahangwa; Simu: 0758341483 na 0682702333; Barua pepe: deus.jovin@gmail.com
  • Kwa mara ya kwanza, makala hii ilichapishwa katika gazeti la Raia Mwema, ikiwa na kichwa cha maneno, “Kutenga dini, siasa: Tuchague sera ya ACT, CCM au ya Chadema?,” na ilitoka kwenye matoleo yafuatayo: Toleo Na. 728, uk. 9&21; Toleo Na. 729, uk.9&23; Toleo Na. 730, uk.23; na Toleo Na. 731, uk. 9&20.
  • Makala hii inayo maneno 11,629
  • Makala hii imeninginizwa hapa kama nakala pepe kwenye fomati ya Microsoft Word (MS Word Format).
A. UTANGULIZI

Kampeni za uchaguzi Mkuu wa 2020 zimekutana uso kwa uso na mjadala unaohusu uteguzi wa kitendawili kinachouliza iwapo kuwa na serikali iliyotenganisha kofia ya madaraka ya kidini na kofia ya madaraka ya kisiasa ni sera bora kuliko sera ya kuwa na serikali iliyovaa kofia ya madaraka ya kidini na kofia ya madaraka ya kisiasa kwa mpigo.

Kwa maneno mengine, hiki kitendawili kinachouliza iwapo kuwa na makanisa yanayotenganisha kofia ya madaraka ya kidini na kofia ya madaraka ya kisiasa ni sera bora kuliko sera ya kuwa na makanisa yanayovaa kofia ya madaraka ya kidini na kofia ya madaraka ya kisiasa kwa mpigo.

Mjadala huu umefufuliwa tena kupitia sakata la Padre Ildefonce Katundu wa Jimbo la Bukoba aliyemwandikia barua Askofu wake kumtaarifu kwamba kwa kuwa majukumu ya kipadre kwa mujibu wa sheria za Kanisa Katoliki yanagongana na haki za raia wa Tanzania ambaye ni padre anayetaka kufanya siasa za dola kwa mujibu wa Katiba ya nchi, ameamua kuachana na majukumu ya kipadre ili apate fursa ya kufanya siasa kama raia.

Tarehe 24 Julai 2020 Askofu Desiderius Rwoma, wa Jimbo Katoliki la Bukoba, aliandika barua kwenda kwa viongozi wote wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania akiwataarifu juu ya uamuzi wake wa kumsimamisha Padre Katundu kutoa huduma za kipadre.

Askofu Rwoma alitumia kifungu cha 285(3) cha Sheria za Kanisa Katoliki (1983), chenye kuwazuia mapadre kuvaa kofia ya madaraka ya kisiasa, ambacho kimantiki, kinafanana na ibara ya 19(2) katika Katiba ya Tanzania (1977), yenye kuizuia serikali kuvaa kofia ya madaraka ya kidini.

Tayari wengi wametoa maoni yao juu ya tukio hili. Kwa mfano, tarehe 12 August 2020, kupitia gazeti la Raia Mwema, ukurasa wa 10, Joseph Magata alisema kwamba, “Kanisa na siasa ni vitu wawili tofauti,” kwamba, “kazi ya kanisa ni kuhubiri ukweli na haki ili watu wauchukie … uovu,” kwamba “wanasiasa wanaweza kuukataa ukweli kama ukweli wako siyo utashi wao.”

Magata anaona kwamba, kwa sababu hiyo, kitendo cha padre kuvaa kofia ya “uongozi wa kisiasa” ni “kukaribisha matatizo” kanisani, kwani, “kama kuna mapadre bungeni, serikalini, [na] mahakamani, wote hawa watakuwa wameuleta [uovu unaoungwa mkono na dola] kwa kutumia mamlaka yao” ya “uongozi wa kisiasa unaokatazwa na kanuni ya 285(3) ya Sheria za Kanisa.”

Aidha, tarehe 01 Agosti 2020, Askofu Benson Bagonza, wa Kanisa la KKKT Jimbo la Karagwe, alitoa maoni juu ya uamuzi wa Askofu Rwoma kupitia jukwa la mtandao wa “whatsapp” liitwalo “Friends of Anatropia,” kwa kuandika kwamba, japo “kila nyumba ina mambo yake” yanyoatutaka “tuheshimu maamuzi” kama haya, lakini bado “tuna kesi kubwa mbinguni” kwa sababu ya kujenga ukuta unaowazuia watu “kuchanganya dini na siasa.”

Kwa hiyo, ni hitimisho langu kwamba, sasa tuna kambi kuu mbili za wanazuoni kuhusu tamko kwamba, “sera ya kujenga ukuta kati ya nyumba za ibada na dola ni bora kuliko sera ya kujenga daraja kati ya nyumba za ibada na dola.

Ndio kusema kuwa, tuna kambi kuu mbili za wanazuoni kuhusu tamko kwamba, “sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni bora kuliko sera ya kuunganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa.”

Kila kambi inao waumini ambao ni wafuasi kwenye vyama vya siasa vilivyosimika wagombea urais, ubunge na udiwani kwenye uchaguzi Mkuu wa 2020. Waumini hawa watapiga kura baada ya kutathmini sera, weledi wa mgombea na itikadi ya chama cha siasa.

Hivyo, kuna haja ya kuupa mjadala huu umbo la kimantiki linalokidhi vigezo vya kimdahalo na hatimaye kuwaalika wagombea wa ubunge na urais kutusaidia kutegua kitendawili kilicho mbele yetu.

B. Utetezi wa hoja ya kutenganisha kofia

Kwa upande mmoja, upekuzi wa maktaba yangu unaonyesha kuwa, kambi ya watu wanaosema kuwa “sera ya kujenga ukuta kati ya nyumba za ibada na dola ni bora kuliko sera ya kujenga daraja kati ya nyumba za ibada na dola” wanazo sababu nyingi, lakini kubwa ni kumi zifuatazo:

MOSI, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda uhuru na uimara wa dola dhidi ya vita vya kidini vitokanavyo na ubabe kati ya dini na dini na mabavu kati ya dhehebu na dhehebu, kila upande ukijaribu kutafuta fursa ya kuwa dini rasmi ya kitaifa.

Historia ya ulimwengu inatufundidha kwamba watawala wenye ukatili wa kupindukia waliowahi kutokea hapa duniani ni wale viongozi wa dini waliokuwa wanavaa kofia mbili, yaani, kofia ya madaraka ya kisiasa na kofia ya madaraka ya kidini.

Na sababu kubwa iliyozalisha wazo la kuundwa kwa dola iliyotenganisha kofia ya madaraka ya kisiasa na kofia ya madaraka ya kidini ilikuwa ni upinzani dhidi ya vurugu na ukatili wa kidini uliotokea katika karne ya 16 na 17 huko Ulaya. Chini ya utaratibu huu maamuzi ya mtawala wan chi hayakuhitaji tena kibali cha kiongozi wa dini, kama vile Papa.

Katika Ulaya ya Kati kulitokea vita ya miaka thelathini (1618-1648), vilivyoua watu wapatao milioni nane. Vilikuwa ni vita kati ya Mataifa ya Kiprotestanti (Sweden na Denmark) dhidi ya Mataifa ya Kikatoliki (Austria na Hipania) yaliyokuwa chini ya himaya ya Papa. Vita hivi vilikomeshwa kwa njia ya Mkataba wa Westaphalia (1648), uliosainiwa nchini Ujerumani. Mkataba huu ndio chimbuko la dhana ya madola huru yaliyo sawa, kama inavyofahamika leo.

Kutokana na historia kama hii, wanazuoni wakahimitisha kuwa, dini zote zinaweza kuwa chimbuko la ukatili, machafuko na vita kwa sababu katika kila dini kuna mbegu tano za kuzalisha machafuko ya kidini. Kila dini inadai kwamba inayo hatimiliki ya ukweli turufu juu ya ukweli wa kimungu; kwamba waumini wanapaswa kuonyesha utii bila kuhoji; kwamba, viongozi wa dini wanayo hatimili ya weledi wa kuutambua “wakati wa Mungu” wa kutenda muujiza; kwamba “lengo jema huhalalisha mbinu yoyote,” mfano ukiwa ni Kanuni ya Kayafa katika Biblia, isemayo kuwa ni afadhali mtu mmoja afe kwa faida ya watu wengi (Yohana 11:50); na kwamba dini inayo mamlaka ya kutangaza vita vitakatifu kwa jina la mungu wake. Charles Kimball (2008), wa Wake Forest University, huko Amerika, ni mwandishi wa kitabu kiitwacho “When Religion Becomes Evil: Five Warning Signs,” chenye kufafanua sababu hizi kwa kina.

Ni kwa sababu hizi, dini zimekuwa kigezo kikuu cha kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe katika karne ya 20. Kwa mujibuwa tasnifu ya uzamivu iitwayo “A Dissertation on the Canon and Feudal Law (1765)” iliyoandikwa na Dr. John Adams (1735-1826) wa Marekani, baadhi ya viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiprotestanti ni miongoni mwa wakatili hawa.

Mifano ya karibuni kuhusu vita vya kidini imetajwa na Monica Duffy Toft (2006), wa Chuo Kikuu cha Harvard, katika andiko lake la kitafiti liitwalo, “Religion, Civil War, and International Order.” Toft (2006) anatufahamisha kuwa, kati ya mwaka 1940 na 2000, duniani kote kulikuwepo na vita vya kidini 42, ambapo, dini ilikuwa sababu ya kwanza katika vita 25, sawa na 60% ya vita vyote, wakati dini ilikuwa sababu ya pili katika vita 17, sawa na 40% ya vita vyote.

Kusema kwamba dini ilikuwa sababu ya kwanza ya vita, maana yake ni kwamba, wapiganaji walitamka kuwa walinzisha vita ili kuhakikisha kuwa nchi yao inatawaliwa kwa mujibu wa mafundisho ya imani yao. Vita vya aina hiyo vilitokea huko Afghanistan, Chad, na Sudan. Na kusema kuwa dini ilikuwa sababu ya pili ya vita, maana yake ni kwamba, wapiganaji hawakutaka dini yao ipate utambuliko wa kitaifa, lakini walijitambua na kujitambulisha kwa kutumia jina la dini yao. Vita vya aina hiyo vilitokea huko Yugoslavia ambako waasi walikuwa ni Waislamu wa Bosnian (Uislam), Kroatia ambako waasi walikuwa ni Wakatoliki, na Sebia ambako waasi walikuwa ni Wakristo jamii ya Otodoski.

PILI, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda uhuru na uimara wa nyumba za ibada dhidi ya ubabe wa kiserikali. Tangu karne za kwanza, huu ndio ulikuwa msimamo wa Wakristo wengi, kama tunavyosoma mahali Fulani kwenye “Tamko la Milan” (313BK) kwamba “makundi ya kidini yanapaswa kuwa na uhuru wa kuabudu na kujiendesha yatakavyo.”

Tamko hili maana yake ni kwamba, kila nyumba ya ibada ni taasisi yenye haki ya kufanya maamuzi yafuatayo: kuchagua msahafu rasmi, kuchagua mungu rasmi; wakati, mahali na jinsi ya kuabudu mungu husika; kutengeneza kanuni za kimaadili; kuchagua na kutengua viongozi wao; kutengeneza kanuni ya imani; kutengeneza mafundisho ya kijamii; kumiliki mali; kutoa elimu ya dini kwa waumini; na kueneza mafundisho ya kidini kwa wasio waumini ili kuwasajili kama waumini wapya; kupatiwa ulinzi wa haki hizi kutoka kwenye vyombo vya dola; na kufanya mambo yote haya bila kuelekezwa na vyombo vya dola.

TATU, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda uhuru wa dhamiri ya kila raia dhidi ya ama mabavu ya kidola, au ubabe wa kidini, au shurutisho inayotokana na uswahiba kati ya viongozi wa dini na viongozi wa dola.

Kihistoria tunaambiwa kuwa, dhana ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa , ilifafanuliwa kifalsafa kwa mara ya kwanza kupitia maandiko ya Mwingereza aitwaye John Locke (1632–1704), yaitwayo “Letter on Toleration (1689)” na “The Second Treatise on Government (1690).

Katika maandiko haya, John Locke alijenga hoja kwamba, dola na dini ni taasisi zenye mbinu na malengo tofauti. Kwamba, lengo la dola ni kukuza na kuhami malimwengu kama vile uhai, uhuru na mali, wakati lengo la dini ni kumwokoa kila muumini dhidi ya makucha ya uovu wa shetani na kumpeleka mbinguni kwa Mungu.

Na kwamba, dola na dini hutumia mbinu tofauto kufukuzia malengo haya, ambapo dini hutumia ushawishi wa hoja mara zote, wakati dola hutumia mseto wa mabavu na hoja. Kwa kuwa hakuna mabavu au vitisho vinaweza kumfanya mtu abadilishe mtazamo wake wa ndani ya moyo kuhusu ukweli anaoukubali na kuusimamia, dola inapaswa kujizuia kutumia mabavu na vitisho kwa raia. Ni vivyo hivyo kwa taasisi za kidini.

Anachosema John Locke hapa ni kwamba kuna mkataba wa kijamii kati ya raia na dola; kwamba, kwa mujibu wa mkataba huu, dola huwa haipewi haki ya kuingia kwenye chumba cha uhuru wa dhamiri ya mtu binafsi; kwamba, ni kwa sababu hii raia hutumia haki yao ya uhuru wa dhamiri ya mtu binafsi kuiondoa serikali madarakani pale inapothibitika kuwa serikali hiyo imevunja mkataba wa kijamii; na kwamba, ni kwa sababu hii raia hutumia haki yao ya uhuru wa dhamiri ya mtu binafsi kujiondoa kanisani au mskitini pale inapothibitika kuwa viongozi wa dini hiyo wamevunja mkataba wa kijamii unaowaunganisha na waumini.

Kwa hiyo, uhuru wa dhamiri ya mtu binafsi ni haki asilia inayopaswa kuheshimiwa na mamlaka ya kidola na kustahiwa na mamlaka ya kidini. Katiba ya Tanzania (1977) inaitambua haki ya kuwa na uhuru wa dhamiri ya mtu binafsi kupitia ibara ya 19(1), ambako neno “conscience” linatafsiriwa kama “maoni.” Kamusi Kuu ya Kiswahili (BAKITA 2015) inasema kuwa “dhamiri” ni “moyo uelekezao kufanya jambo fulani.” Hivyo, nionavyo mimi, tafsiri sahihi ya neno “conscience” inapaswa kuwa “dhamiri.”

Mivutano juu na masuala haya tata inaweza kusababisha uvunjifu wa amani. Serikali inalo jukumu la kulinda amani na kuzuia vurugu. Kwa hiyo, kunahitajika refa asiyefungamana na dini yoyote. Yaani, kunahitajika serikali isiyo na dini yenye kuwaongoza watu wenye dini.

Lakini, kadiri masuala haya tata yanavyohusika, kwa sababu ya zile mbegu tano za kuzalisha machafuko ya kidini tulizoziona hapo awali, ni wazi kwamba, kuvaa kofia ya mamlaka ya kidini na kofia ya mamlaka ya kidola kwa mpigo ni kama kutengeneza mkorogo wa petrol na sukari ili kuzalisha bomu la mkono ambalo linasubiri kulipuka wakati wowote, pale litakapopata joto la kutosha.

Ndio kusema kuwa, mseto wa mamlaka ya kidini na mamlaka ya kidola ni bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote.

Kwa hiyo, mataifa yameweka mikakati ya kulinda uhuru wa dhamiri ya mtu binafsi dhidi ya makucha ya dola na mapembe ya makanisa. Mkakati mmojawapo ni kutofautisha kati ya kosa la jinai na dhambi. Kosa la jinai linatamkwa na sheria ya Bunge wakati dhambi inatamkwa na sheria za dini.

Baadhi ya sheria za kidini zinapingwa na sheria za Bunge. Kwa mfano, wakati baadhi ya sheria za dini zinakataza talaka, uasherati kati ya watu wazima walioridhiana na kuzuia uzazi kwa kutumia kingamimba, sheria za nchi kadhaa zinaruhusu mambo haya, na hivyo kumruhusu raia kuamua afanye nini kulinaga na dhamiri yake inavyomtuma.

Vivyo hivyo, baadhi ya sheria za nchi hazitambuliwi katika sheria za kidini. Kwa mfano, sheria za usalama wa barabarani pamoja na adhabu zake hazimo kwenye sheria za kidini.

Kwa sababu hii, hapa Tanzania, raia wanao uhuru wa dhamiri katika kufanya maamuzi juu ya masuala kama vile: kulipa zaka kwenye nyumba za ibada, kuapa kwa kutumia msahafu wa kidini, kuhudhuria ibada Jumapili, kushiriki mchezo wa ngumi, kucheza kamari, kunywa pombe, kufanya kazi Jumapili, watu wa dini tofauti kufunga ndoa, wanandoa kuivunja kwa kuomba talaka mahakamni, kupanga uzazi kwa kutumia kingamimba, kufanyika kwa mapenzi kabla ya ndoa kati ya watu wazima walioridhiana, kumiliki mali, kupiga kura, na wazazi kuchagua elimu ya dini ya mtoto.

NNE, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda misingi ya kidemokrasia katika uchaguzi na kudhibiti madhara hasi ya theokrasia. Katika uchaguzi wa kidemokrasia viongozi huchaguliwa kwa mujibu wa kura zinazotokana na matakwa ya watu wengi walioridhika na weledi wa wagombea. Lakini, katika theokrasia, viongozi huchaguliwa kwa sababu ya madai kwamba wanayo baraka ya kimungu (divine right) hata kama hawana weledi. Katika theokrasia wapiga kura husikiliza viongozi wa dini wanasema ni yapi “mapenzi ya Mungu,” nao huyathibitisha kwa kupiga kura ya ndiyo kwa sasa viongozi wa dini wamesema. Kazi ya kudadisi weledi wa wagombea wanamwachia Mungu na viongozi wao wa dini.

Mwandishi John Witte Jr (2006), kuptia makala yake, “The History of Separation of Church and State: Facts, Fictions, and Future Challenges,” iliyochapishwa kupitia jarida liitwalo, “Journal of Church and State” (volume 48, page 15-46),” ametupa mfano mzuri kuonyesha jinsi ambavyo kuendekeza theokrasia kunaweza kuwafanya wapiga kura wakose fursa ya kudadisi ubora wa sera na weledi wa wagombea.

Witte Jr (2006) anasema kuwa, mwaka 1800 kulifanyika uchaguzi mkuu wa Marekani. Wagombea muhimu hapa walikuwa wawili. Kuna mgombea wa chama cha “Republican,” Thomas Jefferson, ambaye alikulia katika dini ya Anglikana na baadaye kuukana Umungu wa Yesu na kujiunga na dini ya “deism.” Pia alikuwepo mgombea wa chama cha “Federalist,” John Adams, ambaye alikuwa ni muumini wa dini ya “Unitarianism” isiyokubali fundisho la Utatu Mtakatifu.

Chama cha Adams kilimtuhumu wazi wazi Jefferson kuwa ni “mpinga Kristo” anayepigania utenganisho wa kofia ya kidini na kofia ya kisiasa kwa dhamira ya kubomoa miongozo ya kidini ambayo ni msingi wa sheria nzuri za nchi.

Nacho chama cha Jefferson kilimtuhumu Adams kuwa ni “dikteta wa kidini” (“religious tyrant”) anayekusudia kuliweka Taifa zima cini ya ukandamizaji wa kidini. Mjadala wa sera na weledi wa wagombea viliwekwa pembeni na akili za watu kuhamia katika kujadili nani anakubali “Umungu wa Yesu” na fundisho la “Utatu Mtakatifu.” (uk. 19).

TANO, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda uhuru wa dola dhidi ya usumbufu unaoweza kuifanya kununua ugomvi wa kidini usiosuluhishika na hivyo kupoteza muda mwingi katika masuala yasiyo ya msingi kwa Taifa zima.

Kuhusu tuweze kuelewa uzito wa sababu hii, hebu tiuone mifano inayotajwa na mwandishi John Witte Jr (2006:19-24), niliyemtaja hapo juu.

Witte Jr (2006) anasema kuwa, katika miaka ya 1830 na miaka ya 1840 kulitokea mzozo mkubwa wa kidini kati ya Wakatoliki na Waprotestanti, ambapo Waprotestanti walikuwa wanawapinga Wakatoliki kwa sababu zinazoanzia kwenye tofauti za kiteolojia. Makanisa ya Wakatoliki yalichomwa moto, vipeperushi wa kashfa dhidi yao vikasambazwa, mahubiri ya kejeli yakaelekezwa kwao.

Mzozo huu ulianzia baada ya Makao Makuu ya Kanisa Katoliki yaliyoko Vatican kuchapisha maandiko kadhaa yaliyowaudhi Waprotestanti.

Kwa mfano, katika waraka wa Papa Gregory XVI (1765–1846) uitwao “On liberalism and religious indifferentism (1832),” Papa alipinga uhalali wa Makanisa ya Waprotestanti, demokrasia, uhuru wa dhamiri, na sera ya kutenganisha kofia ya madaraka ya kidini na kofia ya madaraka ya kisiasa.

Katika waraka huu Papa Gregory XVI aliandika kuwa, ni “upuuzi na mtazamo potofu kufundisha kwamba uhuru wa dhamiri ni haki ya kila mtu” (par. 14); kwamba, kiongozi wa Waprotestanti Martin Luther ni chukizo kuu mbele za Mungu kwa sababu yeye na wafuasi wake ni “makuwadi wa malaika aliyeanguka” na hivyo watu wasio na “heshima wala uaminifu” wowote (para. 19); kwamba, “mipango ya watu wanaotaka kutenganisha Kanisa na dola” na “kutenganisha kofia ya siasa na kofia ya upadre” ni haramu (para. 20); na kwamba, viongozi wa serikali “hupokea mamlaka, sio kwa ajili ya kutawala dola pekee, bali hasa, kwa ajili ya kulinda Kanisa” (para. 23).

Naye Papa Pius IX (1792–1878), kupitia waraka wake uitwao, “the syllabus of errors (1864),” alirudia kauli hizi katika ibara za 18, 19, 24, na 55, kabla ya kulaani “uliberali mamboleo” katika aya za 77 hadi 80. Papa Pius IX alisisitiza kwamba, Kanisa Katoliki ndio Kanisa la kweli pekee, lenye haki ya kuvaa kofia ya mamlaka ya kidini na kofia ya mamlaka ya kisiasa kwa mpigo.

Mwaka 1970, Vatican ilitoa tamko kufundisha juu ya “utakatifu wa kila Papa,” yaani “Papal infallibility,” na kuwataja Waprotestant kuwa ni waasi wa kiimani ("heretics") wanaokweza "akili ya binadamu mmoja " dhidi ya ukuu wa "majisteria takatifu ta Kanisa." Tamko hili linapatikana katika waraka uitwao “the Dogmatic Decrees of the Vatican Council Concerning the Catholic Faith and the Church of Christ (1870).”

Waprotestant wa sehemu mbalimbali duniani, na hasa Marekani, walijibu kwa maneno na vitendo nyaraka za Vatican. Wakitumia maandiko ya kina Martin Luther, John Calvin, na wengine, Waprotestant walikosoa kwa hoja matamko ya Vatican, wakisisitiza demokrasia, uhuru wa dhamiri na sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa.

Hitimisho na mnyukano huu wa miaka mingi kati ya Waprotestanti na Wakatoliki ulihitimishwa mwaka 1983 na Papa Yonanne Paul II alipotunga sheria mpya za Kanisa. Sasa, kupitia ibara ya 285(3), Kanisa Katoliki linakubali sera ya kutenganisha kofia ya madaraka ya kidini na kofia ya madaraka ya kisiasa. Huu ni mgogoro uliotatuliwa kwa miaka 150, yaani tangu miaka ya 1830 hadi miaka ya 1980. Hakuna serikali hudumu madarakani kwa kipindi kirefu hivyo!

SITA, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda misingi ya kidemokrasia katika kutunga sheria za bunge na kudhibiti madhara hasi ya ya theokrasia katika mchakato huo.

Katika mchakato wa kutunga sheria kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia sheria za bunge hutungwa baada ya maoni ya umma kukusanywa na kuchambuliwa kwa kutumia vigezo huru, kwa maana ya vigezo vya kirazini vinavyoweza kuunganisha dini zote. Lakini, katika theokrasia, sheria hutungwa kwa kuzingatia ufunuo katika misahafu na jinsi viongozi wa dini wanavyotafsiri misahafu hiyo. Wananchi hawana nafasi ya kutoa maoni yao.

Kulingana na mawazo ya Robert Audi (2000), wa Chuo Kikuu cha Nebraska huko Marekani, katika kitabu chake kiitwacho “Religious Commitment and Secular Reason,” mchakato wa aina hii unapaswa kuongozwa na sababu zisizo za kidini zenye uwezekano wa kubalika kwa watu wote (“secular reasons”) hata kama kuna sababu nzuri za kidini (“religious reasons”) pia, kwani sababu za kidini hazikubaliki kwa watu wa dini zote wala kwa watu wasioamini katika dini yoyote.

Kwa mfano Audi (2000) anasema kuwa, kama ambavyo serikali ya kidemokrasia inahitaji sababu zisizo za kidini ili kuwashawishi wanajeshi kwenda vitani, vivyo hivyo inahitaji sababu za aina hiyo ili kutetea uhalali wa kutunga sheria itakayowaelekeza walimu wa sayansi kufundisha somo la uumbaji kama linavyopatikana katika misahafu wa Kikristo na Kiislamu na Kiyahudi (uk.211-12). Pasipo sababu za aina hiyo, sababu za kimisahafu pekee hazitoshi, kwani kuna raia wasio amini katika misahafu hiyo, na raia wasioamini katika dini yoyote pia.

Katika jamii ya kidemokrasia, utungaji wa sheria za Bunge kuhusu masuala yote unapaswa kutumia utaratibu huu unapoendekezwa na Audi (2000). Masuala hayo ni pamoja na afya, elimu, ikolojia, ofisi za utawala bora, na uchumi.

Pia kuna matumizi ya kingamimba; utoaji wa talaka; utoaji mimba; picha na mikanda ya ngono; kufanya umalaya; kufunga ndoa kati ya watu wa dini tofauti; kusali jumapili; kutoa sadaka na zaka; ubaguzi wa kwa midingi ya rangi, dini, jinsi, kabila; uzinzi; uasherati; mchezo wa ngumi za kulipwa; mchezo wa kamari; adhabu kwa watu wanafanya kufuru; ulawiti.

Kutenganisha kofia ya mamlaka ya kidini na kofia ya mamlaka ya kisiasa maana yake ni kwamba, Bunge linaweza kutunga sheria juu ya mambo haya, hata kama sheria hizo zinapingana na mafundisho ya baadhi ya dini au madhehebu ya dini hizo. Bila kutenganisha kofia hizo, serikali inaweza kujikuta njia panda kwa sababu ya tofauti za kidini kuhusu masuala haya.

SABA, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda uhuru wa kuabudu kwa kuwaruhusu raia kuchagua madhehebu ya dini watakayoona inafaa, na baadaye kujiondoa kama wataona sababu ya kufanya hivyo. Bila kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa, kuna uwezekano kwamba, serikali itawapangia raia wasajiliwe dini gani, hata kama hawakubaliani na mafundisho ya dini husika. Lakini, kwa kutenganisha kofia hizi watu wanapata uhuru wa kuchagua dini wanayoitaka na pia uhuru wa kuchagua kutojiunga na dini yoyote.

NANE, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda uhuru wa shule za umma dhidi ya mabavu ya serikali kuzitaka zifundishe maadili ya dini rasmi ya kitaifa. Kwa kutenganisha kofia ya siasa na kofia ya dini, shule za umma hazifundishi elimu ya dini kwa lazima. Hivyo, wazazi wanapata fursa ya kuwalea watoto wao kupitia maadili ya dini wayatakayo.

TISA, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda haki ya uswa katika ajira. Pasipo kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa, ajira katika utumishi wa umma zitapatikana kwa kuangalia watu wanaoamini katika dini rasmi ya Taifa. Watu wanaoamini katika dini baki watabaguliwa na hivyo kupoteza haki zao za kiuchumi.

NA KUMI, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni muhimu kwa sababu inalinda uhuru wa mijadala ya kisayansi, kiteknolojia na kiutafiti dhidi ya vikwazo vya kidini. Mfano mzuri kuhusu hoja hii ni mafanikio ya kisayansi katika jamii kwa miaka 300 iliyopita.

Bertrand Russel, katika kitabu chake, “The Impact of Science on Society (1949)” anatoa mwangaza wa kutosha juu ya ukweli huu. Sayansi imezalisha maarifa ambayo yamefanya kazi kama kimiminika cha kuyeyusha mapokeo ya kishirikina yaliyo katika misahafu ya kiteolojia na misahafu ya kifalsafa.

Utafiti wa kisayansi, umetusaidia kufuta imani na matendo potofu. Matendo hayo ni pamoja na kutoa kafara ya mtu, kama tunavyoona Abraham anajaribu kumfanya mwanaye Isaka katika Agano la kale, kunaifanya ardhi kuwa na rutuba; kutabiri kifo cha mfalme kwa kuangalia kupatwa kwa jua, kupatwa kwa mwezi, na kuonekana kwa vimwondo; kudai kwamba jua linaizunguka dunia, kama Biblia inavyosema; kutupilia mbali imani kwamba magonjwa huletwa na mizimu; na matendo mengine kama hayo.

Kwa ujumla, ulimwengu wa sayani, unaongozwa na kanuni ya kuona, kuhoji, hubuni jawabu la mpito, kukusanya ushahidi, kutengeneza nadharia na kutumia nadharia kutatua matatizo katika maiosha ya watu.

Yaani, “observation, problematisation, hypothesization, evidentiation, theorization and aapplication,” yaani “OPHETA.” Mijadala yote ya sayansi na teknolojia inaanzia na kukomea kwenye OPHETA. Angalau watu wawili wakitumia OPHETA na kufikia hitimisho moja, basi maarifa ya kisayansi yamezaliwa. Tekinolojia inafuata mara baada ya makubaliano hayo.

Kwa mfano, Alfred Kinsey (1894 –1956), wa Marekani, alitumia kanuni ya OPHETA katika sekta ya ujinsia wa binadamu na kugundua mduara wa mabadiliko ya kimwili wakati wa kutiaa, yaani “sexual response cycle.”

Makanisa kadhaa yalimlaani sana kwa sababu ya kuendesha utafiti huo. Lakini leo, washauri wa ndoa ndani ya Makanisa haya wanawafundisha wanandoa juu ya “sexual response cycle,” kwa kutumia matokeo ya utafiti huo.

Kama serikali ya marekani ingesikiliza kelele za makanisa maarifa haya yasingepatikana. Kwa hiyo, utafiri, sayansi na teknolojia ni michakato inayoshamiri katika mazingira ambako kofia ya kidini na kofia ya kisayansi zimetenganishwa.

Hizo ndizo hoja kumi za kutetea sera ya kutenganisha kofia ya madaraka ya kidini dhidi ya kofia ya madaraka ya kisiasa. Lakini, wanaopinga sera hii nao wanazo hoja zao. Nitazijadili katika sehemu inayofuata ya makala hii.

Pamoja na uzuri wa hoja zinazotolewa ili kutetea uhalali wa sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa, bado hoja hizi zinakosolewa na watu wanaotetea muungano wa kofia ya kidini na kofia ya kisiasa. Nimefanikiwa kukusanya mapingamizi saba yanayotumiwa kupinga hoja inayohusu sera ya kutenganisha kofia ya kisiasa na kofia ya kidini. Sasa tuone mapingamizi hayo.

C. Mapingamizi dhidi ya hoja ya kutenganisha kofia

MOSI
, wapinzani wa sera ya kutenganisha kofia ya dini na kofia ya siasa wanadai kwamba, sera ya serikali kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni mbaya kwa sababu inaongozwa na kanuni ya dola kutofungamana na upande wowote wa maadili ya kidini (state neutrality) wakati kanuni hii ni sumu kwa uhai wa Taifa.

Wanasema kwamba, kanuni hii ni sumu kwa uhai wa Taifa kwa sababu ya kupingana na jukumu asilia la dola kusimamia amani na utulivu nchini.

Miongoni mwa watetezi wakuu wa hoja hii ni Dakta John Attarian, kupitia makala yake yenye jina, “In Dispraise of Tolerance, Sensitivity and Compassion.” Makala hii ilichapishwa mwaka 1998 kwenye jarida la “The Social Critic,” katika ukurasa wa 14-23.

Mwingine ni Profesa J. Budziszewski, kupitia kitabu chake kiitwacho “True Tolerance: Liberalism and the Necessity of Judgment.” Kilicchapishwa mwaka 2010 mjini “London” kupitia kampuni ya “Routledge.” Hoja yake kuu inapatikana kwenye kurasa za 5-35 na 103-116.

Dakta Attarian (1998) na Profesa J. Budziszewski (2010) wanajenga hoja ifuatayo, ili kuonyesha mtanziko wa sera ya ubakiakati wa dola.

Kwanza, wanasema kuwa, kanuni ya ubakiakati ni tunu inayotutaka kusimama katikati ya tunu chanya kwa jamii, kwa upande mmoja, na tunu hasi kwa jamii, kwa upande mwingine. Yaani, ni tunu inayoitaka serikali kujizuia kutoa hukumu inayoonyesha wema au ubaya wa masuala ya kimaadili yanayobishaniwa na makundi tofauti ya maadili ya kidini.

Wanaeleza kuwa, ukweli halisi wa maisha ya kila siku unaonyesha kwamba, jamii haiwezi kufanya kazi vizuri, ikaishi kwa amani, ikawalinda wasio na hatia dhidi ya uonevu, na ikadumu, bila kuwa na serikali inayokataa kuvumilia maovu kadhaa, yaani, kuwa na serikali inayolalia upande fulani wa kimaadili.

Ndio kusema kwamba, dola inapaswa isivumilie wizi, ujambazi, ukatili, utukutu darasani, kukaidi mamlaka ya wazazi, unyang’anyi wa kutumia silaha, kutumia madawa ya kulevya, uzinzi, kuzaa watoto nje ya ndoa, kusambaza picha za ngono, biashara ya kukodisha jenitalia (umalaya), na biashara ya kukodisha tumbo la uzazi (usarogasi).

Pia, wanasema kuwa dola inapaswa isivumilie biashara ya utumwa, biashara ya kuuza viungo vya binadamu, ubakaji, ukatili kwa watoto, ukatili wa kijinsia, ukatili wa kiuchumi, ukatili wa kisiasa, ukatili wa kielimu, ukatili wa kibiashara, udanganyifu, uzembe, kukwepa majukumu, kula nyama za watu, ulawiti unaohusisha watu wawili wenye jinsi tofauti, ulawiti unaohusisha watu wawili wenye jinsi moja, ndoa za jinsi moja ya kike, ndoa za jinsi moja ya kiume.

Kwa maoni yao, jamii inayovumilia maovu haya, hatimaye itafutika pamoja na uvumilivu wake. Hivyo, wanahitimisha kwamba, kanuni ya ubakiakati inapingana na majukumu asilia ya dola kuhusiana na kutunza amani na utulivu, ambayo ni maslahi ya pamoja katika Taifa. Kwa sababu hizi zote, wanasisitiza kwamba, katika utendaji wa serikali hakuna kitu kinachoitwa ubakiakati wa kimaadili.

Hatimaye, wanapendekeza kwamba, kwa vyovyote vile, katika utekelezaji wa majukumu yake, serikali inalazimika kukweza maadili ya kambi mojawapo ya kidini yenye ushawishi mkubwa dhidi ya maadili ya kambi baki ya kidini.

Hata hivyo, tayari hoja hii kutoka kwa kina Dakta Attarian (1998) na Profesa Budziszewski (2010) imejibiwa kwa sehemu kubwa na upande wa pili.

Kwa mfano, Peter Balint (2017) ametoa jibu kupitia kitabu chake kiitwaco, “Respecting Toleration: Traditional Liberalism and Contemporary Diversity.” Kilichapishwa katika mji wa “Oxford” kupitia kampuni ya “Oxford University Press.”

Balint (2017:32-34) anadai kwamba, tunu za uvumilivu na ubakiakati ni tunu zenye mipaka. Yaani, hakuna uvumilivu ambao hauna mipaka kama ambavyo hakuna ubakiakati usio na ukomo.

Anasema kwamba, kwa sababu hii, hakuna dola inayopaswa kuvumilia kila tabia kama ambavyo hakuna dola inayopaswa kusimama katikati ya kila tabia. Badala yake, anasema kuwa, japo mjadala haujafungwa, uzoefu unaonyesha kuwa, kuna mipaka ya aina tatu kuhusu ukomo wa uvumilivu na ukomo wa ubakiakati.

Mpaka wa kwanza ni mstari unaotenga tabia za watu zinazoongozwa na maadili ambayo yanaafikiwa na dini zote, kwa upande mmoja, na tabia za watu zinazoongozwa na maadili ambayo yanabishaniwa na dini kadhaa. Palipo na mwafaka, sera na sheria ruksa kutungwa na ni jukumu la serikali kusimamia utekelezwaji wa sheria hizi bila kuyumba.

Lakini, palipo na mabishano, serikali inapaswa kukaa pembeni ili kuruhusu mnyukano wa hoja uendelee mpaka mwafaka utakapopatikana. Kwa mfano kama dini moja inapinga matumizi ya kingamimba na dini ya pili inaruhusu matumizi hayo, basi, serikali haipaswi kutunga na kutekeleza sera zinazofungamana na upande wowote.

Mpaka wa pili ni mstari unaotenga tabia zinazoongozwa na maadili binafsi dhidi ya tabia zinazoongozwa na maadili ya umma. Serikali inaruhusiwa kuingilia kati kwenye mazingira ya aina mbili.

Kwa upande mmoja, serikali inapaswa kuingilia kati katika kipengele cha maadili ya umma yanayoongozwa na sera pamoja na sheria za nchi. Na kwa upande wa pili, serikali inapaswa kuingilia kati katika kipengele cha maadili binafsi yanayoumiza upande wa pili pasipo ridhaa, yaani “non-consensual harm.” Hapa, mtu aliyeumizwa bila kuridhia akilalamika serikali lazima kuingilia kati kumlinda.

Lakini, katika kipengele cha maadili binafsi yanayoumiza upande wa pili uliotoa ridhaa kwa upande wa kwanza, yaani “consensual harm,” serikali haina uhalali wa kuingilia kati. Mfano ni mchezo wa masumwi ya kulipwa.

Na mpaka wa tatu ni mstari unaotenga tabia binafsi zinazotishia kudhoofisha maslahi ya pamoja katika jamii, maslahi ambayo yanatambuliwa kwa kutumia miwani ya maadili ya kiasili pekee, yaani “natural moral law.”

Kwa mfano, matumizi ya madawa ya kulevya ni tabia binafsi inayotokea katika faragha, lakini inaweza kuwa na madhara kwa jamii pana, kwa sababu ya uwezekano wa hatimaye kumomonyoa nguvukazi ya jamii, ambayo ni maslahi ya pamoja. Kwa hiyo, sheria za kimabavu lazima zitungwe ili kuruhusu serikali kuingilia kati kwenye maadili binafsi ya aina hii.

Kwa ujumla, hebu tuchukue mfano wa maadili ya ngono yanayofundishwa na viongozi wa Kanisa Wakatoliki. Tuchukue mfano wa fundisho la kupinga matumizi ya kingamimba. Hawa wanalo jukumu la kuwavumilia watu baki wenye maadili ya ngono yaliyo hasimu na maadili yao.

Lakini, pia wanalo jumumu la kupinga jaribio la kuyafanya maadili wanayoyakataa kuwa sehemu ya sera na sheria ya elimu kwa ajili ya shule za umma zinazosimamiwa na serikali na kupokea watoto kutoka dini tofauti. Yaani, japo tabia za kufanya ngono kwa kutumia kingamimba ni suala la maadili binafsi yanayojadiliwa chumbani, mtaala wa elimu ya ngono shuleni ni suala linalogusa maadili ya umma yanayojadiliwa hadharani kwenye darasa.

Hata hivyo, upinzani wa Wakatoliki lazima ufanyike kwa kutumia hoja mtambuka. Yaani, upinzani dhidi ya maudhui ya mtaala kama huu lazima ufanyike kupitia mchezo wa masumbwi ya hoja unaofanyika kwenye jukwaa lenye umbo la mraba—yaani, “public reason square.

Hili ni jukwa ambalo linapokea kujadili, na kuhitimisha ushahidi wa aina nne. Kuna ushahidi wa kifalsafa, kisayansi, kiteolojia na kihistoria—yaani “philosophical reason, scientific experience, scriptural theology, and traditional history.”

Mjadala huu hufanyika katika mazingira yanayoongozwa na kanuni mbili za ujasiriadola. Kuna kanuni ya uvumilivu na kanuni ya ubakiakati—yaani “tolerance and neutrality.” Hatimaye, hitimisho hilo huchukuliwa kama mwafaka wa kijamii unaoweza kuingizwa katika sera na sheria za nchi moja iliyo na utitiri wa makundi ya dini tofauti.

PILI, wapinzani wa sera ya kutenganisha kofia ya dini na kofia ya siasa wanadai kwamba, sera ya serikali kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni mbaya kwa sababu ya kukumbatia kanuni ya ubakiakati wa dola ambayo ni mkakati wa muda mrefu wa kumfukuza Mungu kutoka katika taasisi za umma, sekta binafsi, na kwenye Taifa zima kwa ujumla.

Wanasema kuwa, kutenganisha dola na maadili ya kidini, ni hatua ya kwanza katika msululu wa matatizo yafuatayo: kuwanyima watoto wa shule nafasi ya kufundishwa tunu njema za kimaadili zinazopatikana katika dini, na hivyo kuwa na watoto wasiojua tofauti kati ya mema na mabaya.

Wanaona kuwa hii ni hatua ya kwanza katika kuzalisha kundi la vijana wasiojua maadili ya kimungu katika ngazi ya familia, makampuni, asasi za kiraia, na hatimaye Taifa zima.

TATU, wapinzani wa sera ya kutenganisha kofia ya dini na kofia ya siasa wanadai kwamba, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni mbaya kwa sababu ni jaribio la kufanya kitu kisichowezekana, kwani, kwa mujibu wa sheria za nchi, maadili ya kidini na maadili ya siasa ni vitu viwili visivyoweza kutenganishwa, kwani vyote vinaanzia kwa Mungu.

Wanadai kwamba, viongozi wa dini nyingi ni raia wenye haki ya kutoa maoni yao kuhusu siasa za dola na kugombea nafasi za kisasa; kwamba, waumini wa dini mbali mbali ni raia wenye haki ya kutoa maoni yao kuhusu siasa za dola na kugombea nafasi za kisasa; kwamba, hata viongozi wa dini wanaozuiwa na sheria zao za kitaasisi kugombea nafasi za kisasa, bado wanayo nafasi ya kuwaambukiza mawazo waumini walei na mawazo hayo kupenyezwa katika sera na sheria za nchi; na kwamba, maadili ya kiasili ni seti mtambuka (intersection set) yenye kuunganisha seti ya maadili ya kisiasa na seti ya maadili ya kidini.

Kwa sababu hizi, wanahitimisha kwamba, maadili ya kidini na maadili ya siasa ni vitu viwili visivyoweza kutenganishwa kabisa.

Lakini pia, wanasema kuwa, wavaaji wa kofia ya madaraka yaliyo katika taasisi za kidini hupata madaraka hayo kutokana na misahafu ambayo ni kazi ya mikono ya Mungu, wakati wavaaji wa kofia ya madaraka yaliyo katika taasisi za kisiasa hupata madaraka hayo kutokana na ridhaa ya umma mpana, ambao ni kazi ya mikono ya Mungu.

Kutokana na ukweli huu, inahitimishwa tena kwamba, kofia ya madaraka yaliyo katika taasisi za kidini na kofia ya madaraka yaliyo katika taasisi za siasa ni vitu viwili visivyoweza kutenganishwa kwa sababu, hatimaye, madaraka ya kidini na madaraka ya kisiasa ni kazi za mikono ya Mungu yule yule.

NNE, wapinzani wa sera ya kutenganisha kofia ya dini na kofia ya siasa wanadai kwamba, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni mbaya kwa sababu kanuni ya uhuru wa dhamiri ni mkakati wa muda mrefu wa kutetea uhuru usiojali mipaka ya kanuni za maadili ya kidini.

Kwa maoni yao, uhuru usiojali mipaka ya kanuni za maadili ya kidini ni chanzo cha mmomonyoko wa maadili ya kijamii.

Kimsingi, wanaona hofu juu ya fasili ya “uhuru” iliyobuniwa na waliberali kama vile Profesa Gerald MacCallum (1967), katika andiko lake liitwalo “Negative and Positive Freedom,” kupitia jarida la “Philosophical Review,” toleo namba 76, kwenye ukurasa wa 312–314.

Profesa MacCallum (1967) aliandika, na wanazuoni baki wakakubali, kwamba “uhuru ni hali ya kuwepo kwa uwezekano wa mtendaji kufukuzia malengo yoyote aliyojichagulia kwa sababu tayari ni mtu aliyekomboleka dhidi ya utumwa wa vikwazo vyote vya ndani na nje ya mwili wake.” (uk.314)

Wanalalamika kwamba, fasili hii inawafundidha watu kuamini kimakosa kwamba inawezekana kuwepo na uhuru usio na mipaka. Wanakumbusha kwamba, hakuna uhuru usio na mipaka, kwani hakujawahi kuwepo na “mtu iliyekomboleka dhidi ya utumwa wa vikwazo vyote vya ndani na nje ya mwili wake,” kama fasili hii inavyopendekeza.

Kwa ajili ya kutetea mtazamo wao huu wanataja aina nne za vikwazo dhidi ya uhuru wa binadamu.

Kwanza, wanataja vikwazo vinavyoendana na kanuni za kimaumbile zinazofanya kazi nje ya mwili, kama vile minyororo, kamba, uzio, kuta za magereza. Mtu anayekwazika anakwama kufanya jambo kwa sababu ya kitu kilicho nje ya mwili wake.

Pili, wanataja vikwazo vinavyoendana na kanuni za kimaumbile zinazofanya kazi ndani ya mwili wa mtendaji kwa sababu ya maumbile yake, kama vile hasira, chuki, huruma, huzuni na hisia nyingine. Pia, hapa kuna vijidudu vya magonjwa, woga, ujinga, michakato ya kifiziolojia inayoendelea mwilini, kusinzia na uzito wa mwili. Kwa mfano, wanasema kuwa, kama watu tungekuwa huru dhidi ya uzito wetu tungekuwa tunapaa angani kama wanyama jamii ya ndege.

Tatu, wanataja vikwazo vinavyoendana na kanuni za kisheria zinazoanzia nje na kufanya kazi ndani ya mwili wa mtendaji, kutokana na amri ya mtawala mwenye mamlaka ya kudhibiti utashi wa watu walio chini ya mamlaka yake kwa kuwapangia majukumu chanya na majukumu hasi wanayopaswa kuyatii.

Na nne, wanataja vikwazo vinavyoendana na kanuni za kimaadili zinazofanya kazi ndani ya mwili wa mtendaji, kutokana na maumbile yake kumlazimisha kukubali na kubeba majukumu kadhaa anayopaswa kuyatii kila mahali na kila wakati bila kulazimishwa na mtu baki. Mfano ni jukumu la kukwepa kifo kwa njia ya kula chakula cha kujenga na kulinda mwili na jukumu la kukwepa kifo kwa njia ya kuwakimbia wanyama wakali.

Hivyo, wanahitimisha kuwa, kwa sababu ya uwepo wa vikwazo tofauti dhidi ya uhuru wa binadamu, mtu anaweza kuwa na uhuru dhidi ya kikwazo kimojawapo lakini bado akabaki ni mtumwa wa vikwazo vingine.

Kwa mfano, wanasema, mtu anaweza kuwa na uhuru wa kimwili, kwa maana ya mitulinga ya kufanya jambo fulani, lakini bado akakosa uhuru wa kisheria wa kufanya jambo hilo, kwa sababu kuna sheria inayozuia jambo hilo kufanywa.

Pia wanasema kuwa, kila mtu aliye katika nchi yake yuko huru dhidi ya sheria za Bunge la nchi baki, lakini ni mtumwa wa sheria za Bunge la nchi yake. Na, wanaongeza mfano kwamba, mtu anaweza kuwa huru dhidi ya sheria za Bunge la nchi jirani, lakini hawezi kuwa huru dhidi ya sheria za maadili ya kiasili, maana ndiyo njia pekee ya kumfikisha katika kilele cha maisha yake kama binadamu.

Kwa sababu hizi zote, wanasema kwamba, uhuru wa dhamiri unao mipaka inayowekwa na sheria za nchi, sheria za maadili ya kiasili, sheria za kibayolojia; kwamba, sheria hizi ni kama alama za vibao vya barabarani kwa ajili ya kumsaidia mtu aliyepotelea msituni kusudi aweze kutambua njia ya kupitia, kuondoka kwenye msitu huo na kufika nyumbani kwake.

Wanaeleza kuwa, japo mtu huyo, anayo hiari ya kufuata alama za vibao hivyo au kuzipuuzia, lakini, ukweli ni kwamba, akizipuuzia adhabu yake ni kubaki katika msitu huo, jambo linaloweza kumfanya aliwe na wanyama wakali, na kukosa kufika nyumbani kwake kabisa.

Wanachosema ni kwamba, kazi ya sheria zote ni kumsaidia binadamu kufikia lengo lake asilia la kukua na kustawi mpaka uzeeni. Yaani, uhuru wa kweli sio leseni ya kufanya kitu chochote, popopte na vyovyote; bali ni haki ya kufanya tunayopaswa kuyafanya, na sheria ni mshale wa kutuonyesha tunakopaswa kupita bila kupoteza uhuru wa dhamiri zetu.

Kwa kuwa dhamiri ni uwezo wa kiakili wa kupitia katika mchakato wa kimantiki wa kutofautisha mema na mabaya katika tukio maalum; na kwa kuwa, mchakato huo unaweza kuzalisha hitimisho lenye dosari; basi, wanahitimisha kwamba, dhamiri sio mwongozo thabiti wa kimaadili kwa kila mtu, kila mahali na kwa kila wakati.

Wanachosema hapa ni kwamba, dhamiri inafanya kazi kwa kutumia utaratibu wa kawaida wa kimantiki. Kwa kutumia kitendo cha wizi, mfano ni huu: “Sheria inakataza wizi; kitendo hiki hapa na sasa hivi kilichofanywa na mtu huyu ni kitendo cha wizi; kwa hiyo, kitendo hiki kinapaswa kuepukwa.”

Ni katika hatua ya pili ya hoja hii, mtu anatumia akili yake na ushahidi alio nao kufikia hukumu maalum, na kisha kufanya hitimisho. Kwa hiyo, dhamiri ni uwezo wa mtu kutumia sheria ya kimaadili anayoifahamu katika mazingira yake maalum. Yaani, dhamiri haiwezi kufanya kazi bila kuwepo kwa sheria ya kimaadili inayofahamika.

Kwa hiyo, dhamiri inaweza kukosea kwa njia mbili. Kwanza, dhamiri inaweza kukosea kwa kutumia madokezo yasiyo sahihi, kwani ujinga ni kwazo kimojawapo cha uhuru wa binadamu. Na pili, dhamiri inaweza kukosea kwa kutumia madokezo sahihi lakini ikafikia hitimisho lisilo sahihi. Yaani, kunaweza kuwa na dhamiri safi na dhamiri potofu.

Dhamiri safi inao uwezo wa kutofautisha kati ya mema na mabaya, wakati dhamiri potofu haiwezi. Pia kunaweza kuwepo na dhamiri yenye shaka na dhamiri yenye uhakika. Dhamairi yenye shaka inafikia hitimisho ambalo hailiamini kwa asilimia zote mia.

Hivyo, wapinzani wa sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa wanaona hofu juu ya fasili hii ya “uhuru” kwa sababu, wanafikiri kuwa, uhuru wa dhamiri unaopendekezwa unamaanisha kwamba, sasa watu wote wanayo haki ya kufanya kitu chochote, vyovyote, wakati wowote, na mahali popote, bila kujali mipaka ya uhuru inayowekwa na majukumu ya kimaadili na kisheria tuliyo nayo kwa watu baki, familia, mapokeo, kanisa, dola na mungu.

Wanapinga fikra kwamba mipaka inayowekwa na maadili na sheria hizi ni minyororo inayopaswa kuvunjwa ili kutoa mwanya kwa ustawi wa uhuru wa dhamiri ya mtu binafsi. Wanasisitiza kwamba, uhuru wa kweli ni uhuru unaojali mipaka ya vigezo vya maadili ya kidini visivyobadilika kwa kuzingatia mhusika, mahali na majira.

Wanaona kuwa, kuna vigezo vya maadili ya kimungu vinavyopaswa kuheshimiwa na kila raia, kila serikali, kila asasi za kiraia na kila taasisi za kidini. Kwa hiyo, wanasisitiza kwamba, serikali inalo jukumu la kusimamia maadili yanayotokana na vigezo vya maadili visivyoyumba; na kwamba, chimbuko la vigezo hivyo ni dini, na sio vinginevyo.

Wanachukizwa na pendekezo kwamba serikali isiyofungamana na upande wowote wa kimaadili ni serikali inayoamini kwamba mitazamo na tunu zote vinayo hadhi sawa ya kimaadili. Kwa hiyo, wanasema kwamba, sera ya kuitaka serikali kutofungamana na upande wowote wa maadili ya kidini ni sera ya kuiruhusu serikali kukwepa majukumu yake ya kushiriki katika kazi ya kujenga dhamiri za watu.

Ndio kusema, serikali inalo jukumu la kulinda sheria za nchi zinazotokana na maadili asilia yaliyoasisiwa na Mungu. Yaani, serikali ni mwalimu wa dhamiri za raia anayetumia sheria za nchi kama kitendea kazi muhimu kukamilisha jukumu lake.

Hayati Padre Austin Fagothey alikuwa mtetezi muhimu wa hoja hii, kupitia kitabu chake kiitwacho, “Right and Reason: Ethics in Theory and Practice Based on the Teachings of Aristotle ans St. Thomas Aquinas.” Nimepitia toleo la pili, lililochapishwa mwaka 1959 mjini St. Louis, kupitia kampuni ya “The C. V. Mosby,” ukurasa wa 110-112 na 138-145.

TANO, wapinzani wa sera ya kutenganisha kofia ya dini na kofia ya siasa wanadai kwamba, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni mbaya kwa sababu utekelezaji wake unategemea uwepo wa kanuni ya uvumilivu wa kijamii ambayo imesheheni mkanganyiko wa kimantiki unaowalazimisha wananchi kutumia mwongozo wa maadili ya kidini unaowachanganya akili (logical incohrence).

Mkanganyiko wa kimantiki unaoongelewa uko hivi: Fikiria kwamba, kuna mtu A anayemaini kuwa kitendo X ni haramu kimaadili, na hivyo kuamini kuwa kitendo hiki kinapaswa kupingwa.

Lakini, kwa mujibu wa sera ya uvumilivu, mtu A anatakiwa kuamini kwamba ni sahihi kujizuia kupinga kitendo X, endapo kitafanywa na mtu baki B, kwa sababu kitendi hicho ni miongoni mwa matendo yanayopaswa kuvumiliwa na wanajamii.

Kwa hiyo, uamuzi wa mtu A kuvumilia kitendo cha B unamaanisha kwamba, anakubali imani kwamba “X ni kitendo kinachopaswa kupingwa” na imani kwamba “X ni kitendo kisichopaswa kupingwa,” imani mbili zinazopingana kimantiki.

Hata hivyo, kina McKinnon (2003), wanasema kwamba, kama sera ya uvumilivu ikitafsiriwa vizuri haitaonekana kuwa na mkanganyiko wa kimantiki. Wanashauri kwamba, kwa mujibu wa tafsiri sahihi ya sera ya uvumilivu, kukubalika na kukataliwa kwa kitendo X hunategemea mazingira ya kitendo hicho.

Yaani, wanasema kuwa, uvumilivu wa mtu A kuhusu imani X, katika mazingira M, haumaanishi kwamba mtu A anapaswa kuonyesha uvumilivu kuhusu imani X, katika kila mazingira mbali na mazingira M. Ndio kusema kwamba, kitendo X sio haramu kila wakati, kila mahali na kwa kila mtendaji. Yaani, wema wa kitendo X, au ubaya wake, unategemea mazingira ambako kitendo hicho kitafanyika.

Kwa hiyo, kwa mujibu wa kina McKinnon (2003), tafsiri sahihi ya sera ya uvumilivu iko hivi: fikiria kwamba kuna mtu A anayemaini kuwa kitendo X ni haramu kimaadili, na hivyo kuamini kuwa kitendo hiki kinapaswa kupingwa katika mazingira M.

Lakini, kwa mujibu wa sera ya uvumilivu, mtu A anatakiwa kuamini kwamba ni sahihi kujizuia kupinga kitendo X, endapo kitafanywa na mtu baki B, kwa sababu kitendi hicho ni miongoni mwa matendo yanayopaswa kuvumiliwa katika mazingira N.

Kwa hiyo, uamuzi wa mtu A kuvumilia kitendo cha B unamaanisha kwamba, anakubali imani kwamba “X ni kitendo kinachopaswa kupingwa” katika mazingira M na imani kwamba “X ni kitendo kisichopaswa kupingwa,” katika mazingira N. Mgongano wa kimantiki umeondoka.

SITA, wapinzani wa sera ya kutenganisha kofia ya dini na kofia ya siasa wanadai kwamba, sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni mbaya kwa sababu utekelezaji wake unategemea uwepo wa kanuni ya uvumilivu miongoni mwa wanajamii wakati kanuni hiyo inafundisha watu kuamini katika mfumo wa maadili yanayobadilika kama kinyonga (moral relativism).

Wanaona kwamba, mfumo wa maadili yanayobadilika kama kinyonga ni jambo ambalo linawanyima watu mwongozo thabiti wa maamuzi.

Maadili kinyonga yanayoongelewa yako hivi: fikiria kwamba kuna mtu A anayemaini kuwa kitendo X ni haramu kimaadili, na hivyo kuamini kuwa kitendo hiki kinapaswa kupingwa katika mazingira M.

Lakini, kwa mujibu wa sera ya uvumilivu, mtu A anatakiwa kuamini kwamba ni sahihi kujizuia kupinga kitendo X, endapo kitafanywa na mtu baki B, kwa sababu kitendi hicho ni miongoni mwa matendo yanayopaswa kuvumiliwa katika mazingira N.

Kwa hiyo, uamuzi wa mtu A kuvumilia kitendo cha B unamaanisha kwamba, anakubali imani kwamba “X ni kitendo kinachopaswa kupingwa” katika mazingira M na imani kwamba “X ni kitendo kisichopaswa kupingwa,” katika mazingira N.

Kwa njia ya mfano, basi, wanacholalamikia ni kitu cha aina hii: Mwislamu akisimama sokoni mbele ya Wakristo na kusema kuwa “Mungu anayo nafsi moja” anaweza kuvumiliwa. Lakini Mwislamu huyo huyo akiingia kanisani waliko Wakristo wanaoamini kwamba “Mungu anazo nafsi tatu” na kutamka maneno yake tena, hatavumiliwa. Hivyo, kauli moja inaonekana ni uwongo sokoni, na kuonekana ni ukweli kanisani.

Hata hivyo, tayari hoja hii, imekosolewa na upande wa pili. Miongoni mwa wakosoaji wakuu ni Isidora Stojanovic, kupitia makala yake, “Metaethical Relativism,” iliyochapishwa kwenye kitabu kilichohariri wa na Tristram McPherson kwa kushirikiana na David Plunkett, kiitwacho “The Routledge Handbook of Metaethics,” ukurasa wa 119-132. Kilichapishwa mwaka 2017 kupitia kampuni ya Routledge.

Wanachosema ni kwamba, katika maisha ya kila siku, hakuna kitendo cha binadamu kinachoweza kuhesabiwa kuwa ni adilifu kila mahali, kila wakati na kwa kila mtendaji. Kwa maoni yao, ukweli wa kimaadili, yaani ukweli kuhusu wema na ubaya wa tabia, ni ukweli tegemezi.

Kwanza, unaweza kutegemea mfumo wa kanuni za maadili unaotumiwa na jamii fulani. Na pili, unaweza kutegemea mfumo wa parameta kadhaa za kiimani zinazounda ulimwengu fulani wa kimaadili.

Kwa ajili ya kuimarisha hoja yao, wanatoa mfano wa kanuni za mwendo. Wanasema kuwa, kabla ya ugunduzi wa Galileo Galilei (1564–1642), dunia nzima ilikuwa inafikiri kwamba inawezekana kukawepo na “mwendo ambao ni absoluta.” Mwendo ambao ni absoluta ni mwendo ambao unaongozwa na kanuni isemayo kwamba, “ama kitu X kinaweza kuwa katika hali ya kutembea au katika hali ya kusimama na sio vinginevyo.” Yaani “absolute motion.”

Lakini, Galileo aligundua na kutufundisha kwamba, hakuna kanuni ya aina hiyo, kwani kitu kinaonekana kwamba kinatembea au kimesimama kwa kutegemea kinatazamwa kwa kuanzia kwenye fremu ya marejeo gani.

Kwa mfano, mchezaji aliyesimama katikati ya uwanza wa mpira anaweza kuonekana ama amesimama au anatembea kwa kutegemea anatazamwa na mtu aliyesimama wapi. Mtu aliyesimama kwenye goli la uwanja wa mpira, anaweza kuona kwamba kuna mchezaji amesimama kwa sababu anaona kwamba umbali kati ya mchezaji huyo na mlingoti wa goli haubadiliki. Lakini, kama mchezaji huyo akitazamwa na mtu aliyesimama kwenye jua, mchezaji ataonekana “anatembea” kwa sababu sayari ya dunia aliyoikanyaga “inatembea” kwa kulizunguka jua muda wote ikiwa inasafiri naye.

Kwa hiyo, tukisema “kuna mchezaji anatembea” tunakuwa hatujajieleza vizuri. Inabidi kukamilisha kauli hii kwa kusema kwamba, “kuna mchezaji anatembea kama akitazamwa kwa kuanzia kwenye fremu ya marejeo fulani.”

Katika mfano wa kwanza, fremu ya marejeo ni mlingoti wa goli. Na katika mfano wa pili, fremu ya marejeo ni mwezi. Na hizi fremu za marejeo zote zinayo hadhi sawa kadiri suala la kubaini mwendo au mtuamo wa vitu unavyohusika.

On the metaphysical construal, relativism about motion is the (uncontroversial) thesis that there is no absolute motion, there is only motion relative to a frame of reference.

Kwa kuzingatia mantiki hii, kina Stojanovic(2017) wanasema kwamba, hakuna maadili ambayo ni “absoluta,” kwa maana kwamba, ukweli wa kimaadili unategemea ulimwengu unaotumika kama fremu ya marejeo ya kimaadili.

Kwa mfano, kuna maadili yanayotegemea fremu ya marejeo inayopatikana katika kitabu fulani. Yaani, kauli kwamba “kitendo X ni halali kimaadili” inapaswa kukamilishwa kwa kusema kwamba “kitendo X ni halali kimaadili kwa mujibu wa kitabu K cha maadili.” Kwa mfano, kwa mujibu wa kitabi cha Biblia, kula nyama ya nguruwe sio dhambi, lakini ni dhambi kwa mujibu wa kitabu cha Kurani.

Na kwa ujumla, maadili yanategemea fremu ya marejeo inayopatikana katika ulimwengu U wenye kuundwa na seti ya parameta S, ambapo, seti S inajumuisha memba kama vile kitabu cha maadili, tunu za kimaadili, mapokeo ya jamii husika, na kadhalika.

Kwa mujibu wa hitimisho hili, kauli kwamba “kitendo X ni halali kimaadili” inapaswa kukamilishwa kwa kusema kwamba “kitendo X ni halali kimaadili kwa mujibu wa seti S ya parameta zilizounda ulimwengu U1.”

Kwa maneno mengine, wakosoaji hawa wanasema kwamba, kila kauli inayotaja ukweli wa kimaadili inataja maadili yanayobadilika kutokana na mazingira kwa sababu majukumu ya binadamu yanafungwa na mipaka ya mazingira hayo.

Ndio kusema kwamba, kila kanuni ya maadili inayotaja jukumu, kama vile jukumu X, inakuwa inatwambia kwamba, jukumu X ni kanuni inayopaswa kuheshimwa na kila mtu, kila mahala, na kila wakati, lakini ndani ya mipaka ya ulimwengu U1.

Wanakubali kwamba, amri za kimaadili kama vile usiibe, uziue, usizini, usiseme uwongo, ni amri nzuri na halali. Lakini wanaongeza kusema kwamba, kuna mazingira ambako wizi ni haramu, na mazingira ambako ni halali.

Mfano ni kitendo cha msafiri aliye katika hatari ya kufa kwa njaa, kuamua kuingia katika shamba la jirani na kuchuma nanasi, bila ridhaa ya mwenye shamba, kuila hapo hapo na kisha kuendelea na safari yake. Katika ulimwengu huu, tuseme U2, tunu ya uhai inapewa kipaumbele dhidi ya tunu ya umiliki wa mali.

Wanasema kwamba, kuna mazingira ambako uwongo ni haramu, na mazingira ambako uwongo ni halali. Mfano ni kumwambia gaidi “sijui James aliko” wakati unajua James aliko na unafahamu kwamba kufichua aliko ni kufungua milango ya kifo chake. Katika ulimwengu huu, tuseme U3, tunu ya uhai inapewa kipaumbele dhidi ya tunu ya ukweli.

Wanasema kwamba, kuna mazingira ambako kuua mtu ni haramu, na mazingira ambako kuua mtu ni halali. Mfano ni kitendo cha askari asiye na hatia kuamua kumwua adui yake vitani kama njia ya kuokoa uhai wake unaohatarishwa na mashambulizi ya askari adui wake. Katika ulimwengu huu, tuseme U4, tunu ya uhai wa mtu asiye na hatia inapewa kipaumbele dhidi ya tunu ya uhai mwenye nia ovu.

Wanasema kwamba kuna mazingira ambako kuzini ni haramu, na mazingira ambako kuzini ni halali. Mfano ni, mwanamume asiye na mtoto wa kiume, anayeamua kuchepuka, kwa ridhaa ya mkewe, ili apate mtoto wa kiume, kutoka kwa mwananke jirani; na mwanamke asiyepata mimba kutoka kwa mume wake, anayeamua kuchepuka ili apate mimba, kwa ridhaa ya mumewe. Katika ulimwengu huu, tuseme U5, tunu ya uhai mpya inapewa kipaumbele dhidi ya tunu ya uaminifu katika ndoa.

Na wanasema tena kwamba kuna mazingira ambako kuzini ni haramu, na mazingira ambako kuzini ni halali. Mfano wao ni mke mwenye ridhaa ya mume wake kuiongezea kipato familia kwa kufanya kazi ya kukodisha tumbo lake la uzazi kwa wanaume walio na wanawake wasioweza kuzaa, kwa maana ya kutiana na waume hao, kubeba mimba, na kisha kukabidhi watoto kwa wake wa wanaume hao mara tu baada ya kujifungua (surrogacy business). Katika ulimwengu huu, tuseme U6, tunu ya kipato cha kiuchumi inapewa kipaumbele dhidi ya tunu ya uaminifu katika ndoa.

Wanachosema hapa ni kuwa, mipaka ya ulimwengu wa kimaadili U inapobadilika, ama kwa kuongezeka au kupunguka kwa parameta yoyote, basi, ulazima wa kuheshimika kwa jukumu X unabatilika kwa kiwango hicho.

SABA, wapinzani wa sera ya kutenganisha kofia ya dini na kofia ya siasa wanadai kwamba, sera ya serikali kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa ni mbaya kwa sababu inaongozwa na kanuni ya uvumilivu kati ya makundi tofauti yenye maadili ya kidini yanayopingana (individual tolerance) wakati kanuni hii inachakachua jukumu asilia la kila raia kusimamia amani na utulivu nchini kwa kumlazimisha raia kutumia kanuni ya uwiano wa mema na mabaya (moral proportionalism) ambayo ni kanuni ya maadili ya kubahatisha.

Miongoni mwa watetezi wakuu wa hoja hii ni Bartholomew M. Kiely, kupitia makala yake, “The Impracticality of Proportionalism,” iliyochapishwa katika jarida la “Gregorianum,” chapisho namba 66, toleo la 4, mwaka 1985, katika ukurasa wa 655 hadi 686.

Wanachosema watetezi hawa ni hivi: Kwanza, wanasema kuwa, tunu ya uvumilivu inamruhusu mtu au kikundi cha watu kufanya hukumu juu ya tabia gani ni nzuri kwa jamii yake na juu ya tabia gani ni mbaya kwa jamii yake. Baada ya kufanya hukumu hii anaelekezwa kwamba, anapaswa kukumbatia uovu pale ambapo anaona kwamba jaribio la kuzuia uovu uliobainiwa litasababisha uovu mkubwa zaidi ya ule uovu anaotaka kuuzuia.

Mchakato wa kupima uzito wa uovu unaopaswa kuzuiwa na uovu mpya utakaotokana na jaribio la kuzuia uovu wa kwanza unahitaji kipimo huru kitakachoonyesha kwamba uovu wa pili ni mkubwa kuliko uovu wa kwanza.

Lakini, wanasema kwamba, uhalisia wa mambo unaonyesha kuwa, hakuna kipimo chenye uwezo wa kupima uwiano wa maovu mawili na kutofautisha kati ya kiasi kikubwa cha uovu na kiasi kidogo cha uovu.

Aidha, wanasema kuwa, hakuna kipimo chenye uwezo wa kupima uwiano wa mema mawili na kutofautisha kati ya kiasi kikubwa cha mema na kiasi kidogo cha mema. Badala yake, wanasema kuwa, kinachotokea hapa ni mtu kutumia hisia binafsi kufikia hitimisho, jambo ambalo ni sawa na utaratibu wa maadili ya kubahatisha.

Wanatoa mfano wa fao la usingizi na fao la mlo wa usiku, ambayo ni mafao ya mpito (instrumental goods) yakiwa yanafanya kazi kama daraja linalomsaidia kila binadamu kuelekea kwenye kilele cha fao la afya bora, ambalo ni fao tamati (terminal good).

Wanasema kuwa, haiwezekani kulifanya fao la usingizi kuchukua nafasi ya fao la mlo wa jioni, kwani haya ni mafao yanayokamilishana bila kubatilishana. Ndio kusema kuwa haiwezekani kusema kwamba usingizi ni fao ambalo ni bora zaidi kuliko mlo wa jioni.

Ni kwamba, haya ni mafao mawili yasiyojumulishika, yasiyogawanyika, na hivyo yasiyoweza kuwianishwa kwa kutumia kipimo chochote kilicho huru.

Kwa maoni yao basi, kufanya maamuzi kwa kutumia kanuni ya uwiano wa mema na mabaya (proportionalism) inamfanya mtu kuchagua kutenda uovu na hivyo kupata jina baya kimaadili, kwani matendo yetu hutubatiza majina.

Kwa mfano, wanasema kuwa, ukiiba unaitwa mwizi, ukiua unaitwa mwuaji, wanasema. Kwa sababu hii, wanauliza na kujibu swali lifuatalo: “ni jambo jema au jambo baya kwa mtu X kuwa mtu-aliyefanya-kitendo-Y?”

Katika kujibu swali hili wanasema kuwa, jawabu linategemea jinsi ambavyo kitendo Y kitafanyiwa tathmini ya kimaadili. Kwamba, kama kitendo X ni kibaya kimaadili, basi mtu X atakuwa mtu mbaya kimaadili. Kwamba, kama kitendo Y ni kizuri kimaadili, basi mtu X atakuwa mtu mzuri kimaadili. Na kwamba, kama kitendo Y ni kitendo kisichofungamana na upande wowote wa kimaadili, basi mtu X atakuwa mtu mzuri kimaadili.

Kwa hiyo, wanasema kama tathmini ya kimaadili inayofanywa kuhusu kitendo Y itatumia kanuni ya uwiano wa mema na mabaya, basi, ni vigumu kutofautisha kati ya mtu mwema na mtui mbaya.

Lakini, wanaongeza, kama tathmini ya kimaadili inayofanywa kuhusu kitendo Y itatumia kanuni ya vigezo vitatu vya kimaadili, isemayo kwamba, uhalali wa kimaadili unatukataza kulikumbatia doa lolote katika mwenendo, dhamira, na mazingira ya kitendo, basi, ni rahisi kutofautisha kati ya mtu mwema na mtui mbaya.

Sasa, hebu tutumie mfano mwingine wa jaribio la mwanandoa kutoa mimba ili kubainisha mtazamo wao. Mwanandoa huyu atafikiria juu ya faida na hasara za kutoa mimba. Anaweza kusema kuwa, hasara ya kutoa mimba ni kuua mtoto wake mchanga.

Na pia, anaweza kusema kuwa, faida za kutoa mimba ni kupata utulivu wa kiakili na kurejesha uimara wa kiuchumi katika familia. Kwa sababu faida ni mbili na hasara ni moja, anaweza kujishauri au kushauriwa kutoa mimba. Yeye pamoja na washauri wake watakuwa wameamua kuvumilia kitendo cha utoaji mimba, japo wanajua kwamba ni kitndo haramu kimaadili.

Hapa, kanuni ya uvumilivu imetumika kuhalalisha utoaji mimba kwa kutumia mantiki ifuatayo: kwamba tunu moja ya amani ya moyo ikijumlishwa na tunu moja ya uimara wa kiuchumi tunapata kitu kimoja kikubwa ambacho kina uzito mkubwa wa kimaadili kuliko uhai wa mtoto aliye tumboni.

Lakini, wakosoaji wa kanuni ya uvumilivu, wanakosoa utaratibu huu wa kufikia hitimisho la kuvumilia utoaji mimba kwa sababu, tunu ya uhai, tunu ya utulivu wa kiakili, na tunu ya uimara wa kiuchumi katika familia, ni tunu tatu zinazoanguka katika makabila tofauti ya tunu. Kwa hiyo, wanasema, kitendo cha kuzijumulisha tunu hizi ni sawa na kujumlisha embe moja na kiazi kimoja, halafu tukasema kwamba unayo mihogo miwili.

Ndio kusema kuwa, hakuna mizania huru inayoweza kuonyesha kwamba tunu ya amani ya moyo ikijumulishwa na tunu ya uimara wa kiuchumi tunapata kitu kimoja ambacho kina thamani kubwa kuliko uhai wa mtoto aliye tumboni.

Yaani, kama ambavyo hesabu za kujumlisha embe na kiazi, na kisha kutafuta uwiano kati ya jumla hiyo na tunu ya uhai ilivyo hesabu ya kubahatisha, vivyo hivyo, wanadai kwamba, jaribio la kutafuta uwiano wa mema na mabaya kwa mujibu wa maelekezo ya kanuni ya uvumilivu ni maadili ya kubahatisha.

Lakini, tayari hoja hii imekosolewa na upande wa pili. Nitatumia mfano wa ukosoaji uliofanywa na Askofu Denis Hurley (1915–2004) wa Durban, Afrika ya Kusini. Hurley alifanya ukosoaji huu kupitia makala mbili.

Makala moja ina jina, "A New Moral Principle: When Right and Duty Clash," iliyoyochapishwa mwaka 1966 kwenye jarida liitwalo,”Furrow,” Chapisho la 17, ukurasa wa 619-22. Na makala ya pili ina jina, “In Defense of the Principle Of Overriding Right,” iliyoyochapishwa mwaka 1968 kwenye jarida liitwalo, “Theological Studies,” Chapisho la 29, kwenye ukurasa wa 301-309.

Kwa mfano, Hurley (1968:301-304) alibuni kanuni aliyoiita "The principle of overriding right,” yaani “kanuni ya haki uzito kuchukua nafasi ya jukumu jepesi,” au tuseme “kanunu ya maslahi makubwa kuchukua nafasi ya maslahi madogo,” inayotamkwa kama ifuatavyo:

Kwamba, “endapo katika mazingira fulani kuna haki nzito na jukumu jepesi, na kuna mgongano katika utimizaji wa haki nzito na utekelezaji wa jukumu jepesi, basi, utekelezaji wa jukumu jepesi unapaswa kupisha kazi ya kutimiza haki nzito.” Yaani, "When the infringement of an obligation is necessarily involved in the exercise of a proportionate right, the obligation ceases." (Hurley 1968:301).

Kwa maoni yake, “kanuni ya haki uzito kuchukua nafasi ya jukumu jepesi,” inao umantiki usioweza kupuuzwa. Anasema kwamba, kuna wakati haki hugongana na majukumu, kwa mfano, mtu akishambuliwa na adui haki yake ya kuishi inagongana na jukumu lake la kuheshimu uhai wa mtu baki; kwamba, kiungo cha mwili kinachoumwa kikitishia uhai wa mtu, haki yake ya kuishi inagongana na jukumu lake la kuheshimu ukamilifu wa kimwili; na kwamba, kitendo cha kusema ukweli kinapotishia uhai wa mtu baki katika mazingira fulani, haki ya kutunza siri inagongana na jukumu la kusema ukweli.

Katika kila mfano hapo juu, Hurley anasema kuwa, haki inaonekana kuwa na uzito mkubwa kuliko jukumu. Kwa hiyo, anahitimisha kwamba, mifano hii inatuongoza kwenda katika hatua ya kubuni kanuni ya jumla, ambayo ni hitimisho kutokana na mifano hii.

Kwa maoni yake, hitimisho la kimantiki ni kwamba: “endapo katika mazingira fulani kuna haki nzito na jukumu jepesi, na kuna mgongano katika utimizaji wa haki nzito na utekelezaji wa jukumu jepesi, basi, utekelezaji wa jukumu jepesi unapaswa kupisha kazi ya kutimiza haki nzito.”

Kwa mujibu wa tathmini yake, hii ni kanuni ya kimaadili, kama zilivyo kanuni baki za kimaadili. Anasema kuwa, kanuni ya kimaadili ni dokezo kuu katika mchakato wa kufanya tathmini ya kimaadili; na kwamba, mara zote kunahitajika dokezo dogo ili kutoa mwanya wa kufikia hitimisho linaloweza kuruhusu kanuni husika kutumika katika mazingira fulani. Anatoa mfano wa kufunga kizazi cha mwanamke kama ifuatavyo:

Dokezo kuu ni kwamba, endapo katika mazingira fulani kuna haki nzito na jukumu jepesi, na kuna mgongano katika utimizaji wa haki nzito na utekelezaji wa jukumu jepesi, basi, utekelezaji wa jukumu jepesi unapaswa kupisha kazi ya kutimiza haki nzito. Dokezo dogo ni kwamba, kufunga kizazi cha mwanamke aliyefunga ndoa kwa sababu za kiafya ni kitendo cha kukiuka jukumu la kuheshimu ukamilifu wa kimwili kwa lengo la kutimiza haki nzito zaidi ya kujamiiana na mumewe. Na hitimisho ni kwamba, kwa hiyo, katika mazingira haya, jukumu la kuheshimu ukamilifu wa kimwili linakoma.

Anasisitiza kwamba, katika mfano huu, dokezo dogo lazima lithibitishwe, kabla ya kutumia kanuni hii. Yaani, ni lazima kuthibitisha kwamba, mwanamke hawezi kutimiza haki yake ya kujamiiana na mumewe bila kufunga kizazi; na kwamba haki ya kujamiiana na mumewe ni nzito zaidi ya jukumu la kuheshimu ukamili wa viungo vya mwili vilivyo katika mfumo wa uzazi. Anachosema Askofu Hurley ni kwamba, katika maisha ya kila siku, binadamu wote wanatumia kanuni ya uwiano wa mema na mabaya (proportionalism), na sio vinginevyo.

D. Majibu ya kubutua mapingamizi

Watetezi wa hoja ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa wanayo majibu kadhaa kwa ajili ya kuyabutua, yaani kuyatia ubutu, mapingamizi yanayowekwa dhidi ya hoja zao. Majibu haya tuyaite vibutuzi. Baadhi ya vibutuzi nimevitaja hapo juu, kila nilipoona inafaa, chini ya pingamizi husika. Hapa, nataka kubainisha vibutuzi viwili vinavyogusa mapingamizi yote kwa pamoja.

Kibutuzi cha kwanza kinasema kwamba, maadili ya kisiasa sio lazima yawe maadili ya kidini. Hii maana yake ni kwamba, tunaweza kuwa na Taifa la watu waadilifu, hata kama tukiyapiga kisogo maadili ya kidini.

Kuna fursa ya kuandaa mtaala wa maadili ya kiasili na tukawafundisha watoto maadili haya katika shule na vyuo vyote kwa kuwa haya ni maadili mtambuka yenye chimbuko lake katika mema ya kila binadamu. Mema haya ni chimbuko la mfumo wa haki na majukumu kati ya mtu na mtu, mtu na jamii, jamii na jamii, jamii na serikali, Taifa na Taifa.

Kwa hiyo, mapingamizi yanayoanzia kwenye hofu isemayo kwamba “bila maadili ya kidini hakuna maadili nchini” hayana mashiko.

Na kibutuzi cha pili kinasema kwamba, mapingamizi yote yanayoanzia kwenye dhana ya “maadili ya kidini” hayakubaliki katika jamii ya kidemokrasia yenye dini nyingi, kwa kuwa kila dini inaye “mungu” wake. Natumia neno “mungu” kama nomino inayohesabika (count noun), na sio kama nomino-pekee (proper noun).

Na ukweli ni kwamba, sasa yapata miaka 2000 wanateolojia wakiwa wanajaribu, bila mafanikio, kutafuta jawabu la swali, “mungu ni kitu gani na sio kitu gani?

Waislamu wanasema “mungu” wao anayo nafsi moja. Baadhi ya Wakristo, kama vile Mashahidi wa Yehova, wanasema “mungu” wao anayo nafsi moja. Baadhi ya Wakristo, kama vile Wakatoliki na Wakristo wa Kanisa la Mashariki (Greek Orthodoxy Church), wanasema “mungu” wao anazo nafsi tatu.

Lakini bado, Wakatoliki wanasema kwamba, nafsi ya tatu ya “mungu” wao inatoka kwa Baba kupitia kwa Mwana, wakati Kanisa la Mashariki linasema kwamba, nafsi ya tatu ya “mungu” wao inatoka kwa Mwana bila kuanzia kwa Baba.

Lakini sio hivyo tu. Huyo “mungu” wa Wakatoliki hapendi wafuasi wake watumie kingamimba kama vile kondomu, wakati “mungu” wa Waanglikana anapenda watu watumie kingamimba kama vile kondomu.

Kwa hiyo, mpaka leo Wakristo wenyewe hawakubaliani kuhusu jawabu la swali juu ya “mungu ni kitu gani na sio kitu gani.” Tayari wanazuoni wamerekodi ukweli huu vema.

Kwa mfano, tarehe 6-9 Juni 2001, kulifanyika Kongamano la Dunia Kuhusu Fundisho la Kikristo Juu ya Utatu Mtakatifu, mjini Moscow, huko Urusi. Kongamano hilo liliandaliwa na Jumuiya ya Wanafalsafa Wakristo Duniani kwa kushirikiana na Tume ya Kiteolojia ya Kanisa la Orthodoksi la Urusi. Kongamano lilijumuisha Wakristo Wakatoliki, Waprotestanti na Waorthodoksi.

Profesa Melville Y. Stewart amehariri maandiko yote yaliyowasilishwa kwenye kongamano hilo na kuyafanya kitabu kimoja chenye jila, “The Trinity: East-West Dialogue.” Kilichapishwa mwaka 2003 na Kampuni ya “Springer Science Business Media,” huko mjini Dordrecht.

Wataalam wote waliochangia katika kitabu hiki walikubaliana kutokubaliana juu ya ukweli juu fundisho la “mungu” mmoja mwenye nafsi tatu. Na huo ndio msimamo wao wa pamoja mpaka leo. Hatupaswi kupuuzia utata huu wa kiteolojia tunapotengeneza sera na sheria za kitaifa.

Kwa hiyo, mapingamizi yote yanayoanzia kwenye dhana ya “maadili ya kidini” yanasambaratika hadi kuwa kifusi, kwa sababu hii.

E. Muhtasari wa makala

Mpaka sasa tumeona kwamba, watetezi wa sera ya kutenganisha kofia ya madaraka yanayopatikana katika taasisi za kidini dhidi ya kofia ya madaraka yanayopatikana katika taasisi za kisiasa wanayo hoja moja kubwa inayotaja mambo matatu.

Mosi, wanasema kwamba, kama hatutaki matokeo mabaya tunapaswa kuepuka sababu ambayo ni chanzo cha matokeo hayo.

Pili, wanasema kwamba, katika jamii yenye makundi mengi yaliyo katika mabishano yasiyo na suluhu juu ya maana ya maisha bora, sera ya serikali kuunganisha kofia ya madaraka ya kidini na kofia ya madaraka ya kisiasa ni chanzo cha msululu wa matatizo yanayoweza kubomoa jamii zenye ustaarabu wa kutoa haki sawa kwa watu wote walio sawa (just societies).

Na tatu, kutokana na sababu mbili zilizotajwa hapo juu, wanahitimisha hoja yao kwa kusema kwamba, tunapaswa kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya siasa kwa kuhakikisha kwamba makundi yanayobishana yanaishi pamoja kwa kuzingatia kanuni ya uvumilivu chini ya uongozi wa serikali inayoheshimu kanuni ya kujitenga na mabishano ya kidini kwa kuonyesha ubakiakati unaoiweka serikali hiyo katikati ya dini na dini, kwa upande mmoja, na kuiweka katikati ya wapenda dini na wakana dini, kwa upande mwingine.

Maneno ya msingi katika hoja hii ni msululu wa matatizo, uvumilivu, na ubakiakati. Msululu wa matatizo unaotajwa, kama tulivyoona awali, unajumuisha matatizo yapatayo kumi.

Kuna ubabe kati ya dini na dini unaoweza kuleta vita vya kidini nchini; ubabe wa kiserikali dhidi ya taasisi za kidini; mabavu ya kidola na ubabe wa kidini dhidi ya uhuru wa dhamiri ya kila raia; madhara hasi ya theokrasia dhidi ya misingi ya kidemokrasia katika uchaguzi; serikali kupoteza muda katika kutatua mabishano ya kidini yasiyo na suluhu; na madhara hasi ya ya theokrasia katika mchakato wa kutunga sheria za bunge.

Matatizo mengine ni serikali kuingilia uhuru wa kuabudu kwa kuwalazimisha raia kujiunga na dini ya kitaifa bila ridhaa yao; serikali kuingilia uhuru wa shule za umma kwa kuzitaka zifundishe maadili ya dini rasmi ya kitaifa bila kujali matakwa ya wazazi na wanafunzi; ajira katika utumishi wa umma kupatikana kwa kuangalia watu wanaoamini katika dini rasmi ya Taifa; na viongozi wa dini kuingilia uhuru wa mijadala ya kisayansi, kiutafiti na kiteknolojia.

Ubakiakati ni hali ya upande mmoja kutofungamana na mawazo au tabia ya upande wowote ulioko katika pande baki zenye mitazamo inayogongana, kwa maana ya kujizuia kueleza mtazamo binafsi juu ya jambo linalobishaniwa na kujizuia kuchukua hatua za kivitendo zinazonufaisha upande wowote.

Uvumilivu ni hali ya upande mmoja kutokubaliana na mawazo au tabia ya upande mwingine, lakini bado upande wa kwanza ukajizuia kuupinga upande wa pili, kwa sababu inaonekana kwamba uamuzi wa kujizuia kuupinga ni mbinu muhimu kwa ajili ya kufanikisha tunu kubwa zaidi ambayo ni maslahi ya pamoja kwa pande zote mbili.

Katika kuendesha nchi yenye utitiri wa makundi ya kijamii ambayo yanachukuliwa kama “raia walio sawa,” kanuni ya “uvumilivu” na kanuni ya “ubakiakati” ni kama pande mmbili za sarafu moja ya “usawa wa raia.” Kuna mambo saba ya kuzingatia hapa.

Kwanza, “ubakiakati” ni kanuni inayokataza mtendaji kuhukumu au kuchokonoa kwa namna yoyote ile tofauti za kimaadili zilizopo kati ya makundi tofauti.

Pili, Katika Taifa lenye utitiri wa makundi ya kijamii, ubakiakati ni tunu inayopaswa kutekelezwa na serikali. Tatu, kutokana na haya mawili, inafuata kimantiki kuwa, dola zisizofungamana na upande wowote wa kimaadili huwa hazihukumu wala kuchokonoa tofauti za kimaadili katika makundi anwai ya kijamii.

Nne, “uvumilivu” ni kanuni inayomruhusu mtendaji kuhukumu tofauti za kimaadili zilizopo kati ya makundi tofauti ya kijamii na kisha kumtaka kujizuia kuingilia kati kwa namna yoyote ile katika maisha ya makundi hayo baki.

Tano, kutokana na pointi ya tatu na nne hapo juu, inafuata kimantiki kwamba, kwa ajili ya kulinda usawa wa raia na usawa wa makundi, vyombo vya dola vinapaswa kutekeleza kanuni ya ubakiakati na kujitenga na kanuni ya uvumilivu.

Sita, tunajua kwamba, kila raia na kila kundi la kijamii linayo hiari ya kuhukumu mitazamo ya kimaadili ya pande baki.

Na saba, kutokana na namba tano na sita, inafuata kimantiki kwamba, raia na asasi za kiraia wanapaswa kutekeleza kanuni ya kuvumiliana na kujitenga na kanuni ya ubakiakati.

Huu ni mgawanyo wa majukumu kati ya kanu ya “uvumilivu” na kanuni ya “ubakiakati” ambao umefanikisha utitiri wa makundi ya kijamii yenye mitazamo tofauti ya kimaadili kuishi pamoja kwa amani ndani ya Taifa moja.

Kanuni hizi mbili zimefafanuliwa vema katika kitabu kilichohaririwa kupitia ushirikiano wa Dario Castiglione na Catriona McKinnon (2003), chenye jina “Toleration, Neutrality and Democracy.” Kilichochapishwa mjini “Dordrecht” kupitia kampuni ya “Kluwer Academic Publishers,” na kinajadili tunu hizi kwenye kuraza za 68-104.

Kina McKinnon (2003) wanasema kwamba, hali ya uvumilivu inaweza kuwepo mahali endapo mambo yafuatayo matano yatatimia:

Kuna makundi yenye mitazamo tofauti yanayoishi pamoja; kuna migongano ya kimitazamo kati ya makundi hayo; kuna uamuzi wa hiari wa kila mtu kujizuia kupinga mitazamo hasimu iliyo katika pande baki; kuna busara ya kutofautisha kati ya imani zinazogongana na watu wanaoshikilia imani imani zinazogongana, ambazo ni imani za mpito kwa sababu zinazoweza kubadilika; na kuna utamaduni wa kukweza watu wanaoshika imani zinazogongana dhidi ya imani zinazogongana.

F. Hitimisho la makala

Nilianza makala hii kwa ajili ya kujibu maswali matatu. Swali la kwanza ni, kwanini baadhi ya watanzania wanatetea sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa? Swali hili limejibiwa kikamilifu.

Swali la pili ni, kwanini baadhi ya watanzania wanapinga sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa? Aidha, swali hili limejibiwa ipasavyo kwa kujadili mapingamizi kadhaa na vibutuzi vyake.

Kutokana na maswali mawili hapo juu, kuna swali la tatu lililojitokeza kimya kimywa, yaani, Kati ya Taifa linalotekeleza sera ya kutenganisha kofia hizi na Taifa linalotekeleza sera ya kuunganisha kofia hizi, Taifa lipi ni jamii iliyostaarabika zaidi?

Kusudi tuweze kujibu swali la tatu kikamilifu, lazima kujua kitu kinachowafanya watu wasema jamii fulani imestaarabika. Yaani, “what makes a just society?” Kuna majawabu mengi tofauti kwa swali hili, kulingana na nadharia ya ustaarabu wa kisasa (“a theory of political justice”) itakayozingatiwa na mwenye kulijibu.

Kwa ajili hii nimepitia nadharia za ustaarabu wa kisasa kadhaa, kama zilivyojadiliwa na Karen Lebacqz, kwenye kitabu chake kiitwacho “Six Theories of Justice: Perspectives from Philosophical and Theological Ethics,” kilichochapishwa huko Minneapolis kupitia kampuni ya “Augsburg Publishing House” mwaka 1986. Nimependa uchambuzi wake.

Anataja nadharia za John Stuart Mill, John Rawls, Robert Nozick, Mafundisho ya Kanisa Katoliki Kuhusu Jamii, mafundisho ya Kanisa ya Kiprotestanti Kuhusu Jamii, na kwa njia ya mzunguko anamtaja Aristotle kama mwasisi wa nadharia ya maadili ya kiasili kama msingi wa ustaarabu wa kisiasa katika nchi.

Baada ya kuzipitia nadharia hizi zote, nimejiridhisha kwamba, nadharia ya ustaarabu wa kisiasa inayofaa kutuonyesha jamii yenye maisha bora zaidi ni nadharia ya maadili asilia. Na kwa kutumia nadharia hii nmeridhika kwamba, Taifa linalotekeleza sera ya kutenganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa linakuwa na ustaarabu mkubwa kuliko Taifa linalotekeleza sera ya kuunganisha kofia ya kidini na kofia ya kisiasa.

Hivyo, nawaalika wanazuoni walioko ACT Wazalendo, Chadema, CCM na kwingineko kuelekeza nguvu katika kufafanua nadharia ya ustaarabu wa kisiasa kwa mujibu wa maadili ya kiasili, lakini, kulingana na mahitaji ya Tanzania.
 

Attachments

  • Kutenganisha kofia ya kidini dhidi ya kofia ya kisiasa--Combined with References Appended.docx
    123.5 KB · Views: 10
JF wanapenda umbeya tuu hii ndefu sana na ya kufikiria ndio maana hakuna mtu huku😂, warushie za Haji Manara watafufuka wote.
 
Back
Top Bottom