SULEIMAN ABEID
JF-Expert Member
- Feb 26, 2013
- 390
- 385
Waziri mpya wa Sheria na Katiba nchini, Profesa Palamagamba Kabudi
SIKU chache baada ya kuteuliwa kushika wadhifa wa wizara ya sheria na katiba nchini, waziri mpya wa wizara hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi ameshauriwa aangalie uwezekano wa kumshauri Rais Dkt. John Magufuli kuruhusu kuendelea kwa mchakato wa uandikwaji wa katiba mpya nchini.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja.
Ushauri huo umetolewa na mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Kahama mkoani Shinyanga ikiwa ni siku chache baada ya Rais Dkt. Magufuli kufanya mabadiliko madogo kwenye baraza lake la mawaziri.
Mgeja ambaye taasisi yake inajishughulisha na masuala ya uelimishaji jamii kuhusu utawala bora na haki za kibinadamu hapa nchini alisema, moja ya mambo ambayo Profesa Kabudi anapaswa kuyapa kipaumbele ni suala la kuendeleza mchakato wa upatikanaji katiba mpya hapa nchini.
Akifafanua Mgeja alisema Katiba mpya ndiyo itakayokuwa ufumbuzi wa uimarishaji wa demokrasia hapa nchini na itakoyotoa haki za msingi kwa raia tofauti na katiba iliyopo hivi sasa ambayo ikitumika vibaya inaweza kusababisha viongozi walioko madarakani kuongoza kama wafalme.
“Suala la katiba mpya katika nchi ye yote ulimwenguni siyo la watu wachache au kikundi fulani, ni suala la wananchi wenyewe, hivyo serikali zote zilizopo madarakani zinapaswa kuheshimu matakwa na maoni ya wananchi wake si vinginevyo,”
“Kwa hali hii basi, mara baada ya ndugu yetu Profesa kukabidhiwa mikoba ya wizara ya sheria na katiba, agenda yake ya kwanza ya kufanyia kazi iwe ni kuanzisha mchakato utakaoendeleza uandikwaji na kuwezesha kupatikana kwa katiba mpya, maana tayari mamilioni ya fedha za walipa kodi yalitumika katika mchakato wa awali,” alieleza Mgeja.
Mgeja alisema anamtambua Profesha Kabudi ni msomi aliyebobea katika masuala ya sheria hivyo ni vizuri sasa akaonesha uzoefu wake katika masuala ya sheria na amshauri Rais Dkt. Magufuli kwa umakini kuhusu matakwa ya wananchi wa Tanzania wenye kiu kubwa ya kupatikana kwa Katiba mpya.
Alisema ni vizuri suala la katiba mpya likaanza kushughulikiwa hivi sasa kwa vile linavyocheleweshwa ndivyo siku zinavyokwenda mbele kuelekea uchaguzi mkuu mwingine mwaka 2020 utakaotanguliwa na ule wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2019.
“Ukiangalia muda wa kuwepo madarakani kwa serikali hii ya awamu ya tano unazidi kuyoyoma kila siku, ki uhalisia tumebakiza mwaka mmoja pekee wa shughuli nyingine za kawaida, yaani mwaka 2018, hivyo ni vyema mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya ukaanza hivi sasa ili kutoa nafasi ya chaguzi hizo za 2019 na 2020,”
“Bahati nzuri mtu aliyepokea kijiti kutoka kwa ndugu yetu Mwakyembe, alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusiana na katiba mpya iliyokuwa ikiongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, sasa atumie fursa hiyo kuendeleza mchakto pale ulipokuwa umeishia,” alieleza Mgeja.
Wajumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya Katiba mpya kutoka kwa wananchi wakati huo wakiwa katika moja ya vikao vya kukusanya maoni.
Aliendelea kueleza kuwa mashaka yake ni kuona iwapo mchakato huo utacheleweshwa kuanza hivi sasa, baada ya mwaka 2018 viongozi walioko madarakani watakuwa na visingizio vingi wakidai muda wa kufanya mabadiliko ya katiba haupo tena na badala yake nguvu zote kuelekezwa kwenye mchakato wa uchaguzi.
Alisema watanzania wengi wana hamu ya kusikia lini mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya hapa nchini utaanza na kwamba wanaona kuwepo kwa wingu zito huku baadhi ya viongozi wakiamini suala la katiba mpya siyo kipaumbele chao ama cha Taifa kwa hivi sasa.
“Iwapo suala hili litashindikana ni wazi itakuwa ni “Jipu” jingine nchini na linahitaji kutumbuliwa kutokana na kusababisha hasara kubwa kwa watanzania ikizingatiwa fedha nyingi zilizotumika kwenye ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wananchi na Bunge maalumu la Katiba lililoongozwa na hayati Samwel Sitta,” alieleza Mgeja.