kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,676
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amesema serikali ya awamu ya nne, chini ya Jakaya Kikwete, ililegalega katika usimamizi wa mambo kutokana na kile alichokiita mtazamo wa ‘kichwa cha familia’.
Kitwanga, ambaye katika serikali ya Kikwete alikuwa Naibu Waziri wa mawasiliano, Sayansi na Teknolojia (2010-2012); Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira- 2012-2014) na Nishati na Madini (2014-2015), alisema hali hiyo ilisababisha kwa kiasi kikubwa mambo kutofanyika vizuri.
Kabla ya kuingia kwenye siasa mwaka 2010, Kitwanga tangu mwaka 1988 mpaka 2010 alifanya kazi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika nyadhifa mbalimbali akiwa mtaalamu wa mambo ya teknolojia ya habari (IT). Miongoni mwa nyadhifa alizoshika ni ofisa utawala na naibu mkurugenzi wa mifumo ya habari na mawasiliano.
Kichwa cha familia
Akizungumza wakati alipohojiwa na Nipashe hivi karibuni, Kitwanga alisema serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais Dk. John Magufuli, itapiga hatua haraka ikilinganishwa na ile iliyopita ambayo alisema iliweka dhana kwamba ili kitu kiende lazima kitegemee mtazamo wa kichwa cha nyumba (kiongozi ambaye ni Rais).
“Mimi nikuhakikishie kwamba tutapiga hatua tena kwa haraka, kwa sababu ninavyomfahamu Rais (Magufuli) si mtu wa maneno. Hata sisi wa chini yake lazima tujitafakari sana kuhakikisha tunaendana na kasi aliyo nayo ili kuhakikisha tunaisaidia nchi yetu. Tunafanya kazi na wanachi na nchi yetu iende kasi zaidi,” alisema.
Alipoulizwa ni kwa nini kwa sasa nchi iende kwa kasi zaidi kuliko wakati wa serikali ya awamu ye nne, alisema: “Ukiangalia sana, na haya ni mawazo yangu, ni kwamba inategemea na kichwa (kiongozi), na inategenmea pia na mtizamo tulio nao ambao sasa Watanzania wengi wanapenda walinganishwe na nchi ambazo zimeendelea.
“Kwa hiyo ukiangalia Watanzania wote sasa hivi wana msisimko wa kutaka kujiletea maendeleo. Kwa hali kama hiyo, kwa vyovyote vile, lazima twende kwa kasi zaidi,” alisema Kitwanga.
Alipoulizwa kwa nini miaka ya nyuma Watanzania hawakuwa msisimko wa maendeleo, alisema: “Sina uhakika kama walikuwa hawana mtizamo huo, lakini kama nilivyosema ni kwamba baba mwenye nyumba ndiye anayeongoza.
‘’Kwa hiyo inawezekana nyuma hatukuwa na kasi kama sasa lakini nina uhakika kabisa kwamba mheshimiwa Ali Hassan) Mwinyi (Rais wa awamu ya pili), (Benjamin) Mkapa (Rais wa awamu ya tatu), na Mheshimiwa Kikwete, wamefanya vitu vizuri. Pia hiyo inategemea vile vile na muda na wakati, inatokea tu kwamba sasa hivi tumefikia wakati kwamba ndiyo hali iliyopo (msisimko wa maendeleo),” alisema Kitwanga.
Tofauti uongozi wa Magufuli na Kikwete
Kitwanga alipolizwa tofauti ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne ambayo yeye aliihudumia kwa miaka mitano akiwa naibu waziri, na ya Rais Magufuli, alisema: “Ukichukua serikali ya awamu ya nne na ya awamu ya tano, tofauti iliyopo ni kasi, lakini mtazamo wa kuwaleta wananchi maendeleo ni ule ule.
“Ukiangalia awamu ya tano, inafanya kazi kwenye msingi uliojengwa na awamu ya nne, unajua kuchimba msingi na kutengeneza msingi wakati unapojenga nyumba, haionyeshi sana kwa sababu unajenga kwenda chini.
Lakini ukishamalizan msingi ukianza kujenga kwenda juu ni rahisi sasa kuliona boma. Kwa hiyo Watanzania wasilinganishe hizi awamu mbili kwa sababu kila awamu ina nafasi yake,” alisema Kitwanga.
Kashfa awamu ya nne
Alipotakiwa kutoa mtizamo wake juu ya kashfa za serikali ya awamu ya nne, kama vile Akaunti ya Tegeta Escrow, ukwepaji kodi na wanyama hai kusafirishwa nje ya nchi, ambazo zimefanya mara kadhaa Rais Magufuli kusema nchi ilifanywa shamba la bibi, Kitwanga alisema:
“Serikali iliyopita tofauti yake na sasa hivi kikubwa ni usimamizi tu. Mabadiliko makubwa ninayoyaona sasa hivi ni usimamizi.
Nilikuwemo kwenye serikali iliyopita na sasa hivi nimo. Inawezekana hatukusimamia vizuri kwenye sarikali iliyopita.”
Alipoulizwa ni wapi walilegalega kwenye usimamizi mpaka kukawa na kashfa kama hizo, alisema tatizo lilikuwa ulegevu na lilisababishwa kwa kiasi kikubwa na ‘kichwa cha nyumba’.
Alipolizwa kwama ‘Kichwa cha Nyumba’ kilikuwa hakina mtizamo, alisema: “Ahaaa, ukweli ni kwamba sisi hatukuwa tumeweka nguvu zaidi kwenye usimamizi, tuliweka nguvu zaidi kwenye kujenga mfumo wa msingi.”
Alipoulizwa ilikuwaje waweke mfumo wa msingi halafu nchi ikawa inaibiwa hivyo, alisema: ‘’Sina uhakika kwamba tulipigwa (kuibiwa) kiasi hicho. Tukizungumzia suala hilo, watu ambao si waaminifu wakipata kamwanya watafanya vitu kama hivyo, ndiyo maana awamu ya tano inatafuta Hao kwanza, watu ambao si waaminifu, kwa sababu kikubwa ni uzalendo na uhadilifu, ndicho kinachoongoza watu.
Kitengo cha bandari
Kitwanga alisema ili kuhakikisha hakuna ukwepaji wa kodi bandarini kwa makontena kutoroshwa bila kulipiwa kodi, alisema: “Hata sasa hatupaswi kusikia makontena yameondoka (yametoroshwa bandarini). Kikubwa sasa ni kujenga mfumo mzuri na kutoa motisha kuhakikisha kila aliyeajiriwam, anafanya kazi, wajue kuna wengine wapo pembeni hawana kazi.
Lazima kuwe na kitu kinaitwa kuajiri na kufukuza, watu wasijue kwamba wameajirwa maisha, kwamba chochote kikitokea atalalamika. Lazima turudishe nidhamu, hivyo kuajiri na kufukuza ifanye kazi mtu asionewe, haki itendeke, mwajiri awe na haki zake na mwajiriwa awe na haki zake.”
Kasi ya kutumbua majipu
Akizungumzia kasi ya Rais Magufuli na wasaidizi wake katika utumbuaji majipu, Kitwanga alisema: “Hatutumbui tu majibu, tunafanya uchunguzi, ni vyema kutenda haki. Hata mimi kila ninachofanya lazima kutenda haki. Sitaki mtu aje kufungua kesi ashinde aitie hasara serikali. Ninachotaka ni kujiridhisha kama amefanya kosa.”
Alisema mpaka sasa anaimani sheria zinafuatwa kwa wale wote waliosimamishwa au kufukuzwa kazi kutokana na sababu mbalimbali.
Juu ya sera ya Rais Magufuli ya kubana matumizi, Kitwanga alisema mpaka sasa yeye biinafsi hajasafiri kwa sababu tu hajapata mwaliko. Alisema angekuwa amepata mwaliko wa safari nje ambayo ina manufaa kwa taifa, angemuomba rais asafiri.
Hata hivyo alikiri kwamba kubana matumizi kumewasaidia kuweka misingi imara na kufanya mambo mbalimbali mpaka sasa.
“Tofauti ya sasa na wakati ule, wakati ule yawezekana safari watu walikuwa wanaenda sana, ile safari hii mtizamo ni tofauti,” alisema.
SOURCE: NIPASHE