Waziri wa JK aanza fitina za urais 2015

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
270
Mkakati wake wa kwanza ni kuivuruga UVCCM
Akifanikiwa ataanza kupanga safu uongozi Wazazi, UWT
Awaita Dar kimya kimya wenyeviti wa mikoa wa UVCCM
WAZIRI katika Baraza la Mawaziri la sasa ambaye katika Awamu ya Kwanza ya Rais Jakaya Kikwete alikuwa naibu waziri, ameanza kujipanga kuwania urais mwaka 2015, akianza kujenga mtandao ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na tayari ameanza mpango wa kuwakusanya baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa umoja huo ili washinikize mabadiliko ya uongozi yatakayomnufaisha, Raia Mwema limebaini.

Gazeti hili limethibitishiwa kuwa waziri huyo ameitisha mkutano wa siri wa baadhi ya wenyeviti wa UVCCM wa mikoa watakaokutana Dar es Salaam Desemba 20, wiki ijayo, ili pamoja na mikakati mingine washinikize kupatikana kwa mwenyekiti wa UVCCM waliyemwandaa kutoka Zanzibar.

Kwa sasa nafasi ya mwenyekiti wa UVCCM inashikiliwa kwa kukaimu na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Benno Malisa, baada ya aliyekuwa Mwenyekiti, Hamad Yusuf Masauni kuachia ngazi kutokana na kudanganya kuhusu umri wake.

Kwa mujibu wa habari zilizotufikia waziri huyo ameamua kutumia mbinu za pembeni zilizo kinyume na taratibu za UVCCM na CCM kwa ujumla ili kufanikisha mkakati wake ikielezwa katika kundi lake la harakti za kusaka urais, yeye ni kati ya watarajiwa kama mtarajiwa mkuu atashindwa kusafishika kutokana na jamii kuamini kuwa si mtu wa maadili safi na tayari amehusishwa katika kashfa kubwa za kitaifa ndani ya miaka mitano iliyopita.

Habari hizo zinabainisha kuwa ili afanikishe mkakati huo ameanza kwa kuvuruga UVCCM. Ameanza katika umoja huo kwa imani kuwa viongozi wa sasa wakuu ambao ni Makamu Mwenyekiti, Beno Malisa, akisaidiwa na Katibu Mkuu, Martin Shigela hawamuungi mkono na hawana dalili za kufanya hivyo.

Malisa aliingia madarakani Novemba 14, 2008 na baadaye kukaimu uenyekiti uliokuwa chini ya Masauni ambaye alijikuta katika kashfa ya umri iliyounguruma mwaka jana mjini Iringa, akidaiwa kughushi tarehe ya kuzaliwa wakati akiomba nafasi hiyo kwa kutaja alizaliwa Oktoba 3, 1979 wakati ukweli ni kwamba alizaliwa Oktoba 3, 1973.

Kwa upande wake, Shigela aliteuliwa na Kamati Kuu ya CCM kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM Februari 28, mwaka jana. Taarifa zaidi zinabainisha kuwa tayari waziri huyo ili kufanikisha mkakati wake, amewaita kwa siri wenyeviti wa UVCCM wa mikoa yote nchini jijini Dar es Salaam na kupanga kufanya nao kikao Desemba 20.

Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umeshindwa kuthibitisha moja kwa moja juu ya nani atakayekigharamia kikao hicho na kiasi cha fedha kitakacholipwa kwa waalikwa huku uchunguzi zaidi ukibaini kuwa viongozi rasmi wakuu wa UVCCM, Malisa na Shigela wamekataa kuhusishwa na kikao hicho.

Gazeti hili lilizungumza na baadhi ya wenyeviti wa UVCCM wa mikoa ambao pamoja na kuthibitisha kuwapo kwa kikao hicho Dar es Salaam, wameweka bayana kuwa ni kwa ajili ya kutathmini mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 31, mwaka huu. Aidha, baadhi ya wenyeviti hao wamekiri kutaarifiwa kuwapo kwa uchaguzi wa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa.

Hata hivyo, wakati juhudi za kufanikisha mkutano huo zikiendelea kwa siri imebainika kuwa mkutano husika utakuwa kinyume cha kanuni za UVCCM ambazo zinaweka wazi kuwa, wenyeviti wa ngazi zote huchaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa ngazi husika na si wenyeviti na kwamba, mikutano yote hiyo huandaliwa na Baraza Kuu la UVCCM kwa kila ngazi husika.

Hadi tunakwenda mitambani, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shigela na Naibu Katibu Mkuu wake Athman Kizigo, hawakupatikana kuzungumzia suala hilo.

Kwa upande mwingine, mpango huo wa siri umezusha upinzani mkali na tayari baadhi ya maofisa waandamizi wa UVCCM wanasema haiwezekani wenyeviti wa mikoa wafanye kikao cha kitaifa cha kutathmini Uchaguzi Mkuu wakati kazi hiyo ilipaswa kufanywa na Baraza Kuu la Taifa la UVCCM kwa kuzingatia Ibara ya 89(m) ya kanuni ya umoja huo inayotumika sasa.

“Lakini pia hawawezi kufanya tathmini ya kitaifa, iwe kwa vyeo vyao na hata vinginevyo, wakati bado katika mikoa yao wenyewe hawajakutana kwanza kwa ajili hiyo,” kinasema chanzo kimoja cha habari hizi na kuongeza:

“Kama wanalijua hilo, lazima baraza kuu la kila mkoa lifanye tathmini kwanza, ndipo tathimini hizo zitumwe Makao Makuu ya UVCCM na hatimaye kazi hiyo ifanywe na wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa wanaotajwa katika Ibara ya 88(a) hadi (p) ya kanuni zetu, na vikao vyote vinakwenda kwa utaratibu maalumu.”

Watu walioko karibu na waziri huyo kijana wanaeleza kuwa uamuzi wake unalenga si tu kujiwekea mazingira bora ya urais yeye na kundi lake lakini pia unalenga kuwadhibiti Malisa na Shigela.

“Malisa, kwa waziri huyo anaonekana kuwa kikwazo kinachoweza kumfanya asiwe Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano mwaka 2015, ndiyo maana hajashirikishwa,” kinasema chanzo kingine.

Vyanzo vyetu vya habari kutoka kundi la mkakati la waziri huyo vinamtaja mtu aliyeandaliwa kuwa mwenyekiti wa UVCCM ili kulinda maslahi ya waziri huyo kuwa ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la UVCCM kutoka Zanzibar ambaye ametajwa kwa jina moja la Jamal.

Hata hivyo, uchunguzi zaidi umebaini kwamba Ofisi ya Katibu Mkuu wa UVCCM haifahamu chochote kuhusu uchaguzi huo wa mwenyekiti Taifa, hali inayopambanua kuwa mpango huo mzima ni kinyume cha Ibara ya 89(b) ya Kanuni ya UVCCM.

Wakati Ofisi ya Katibu Mkuu ikiwa haina taarifa rasmi, baadhi ya Wakuu wa Idara za Makao Makuu ya UVCCM, wakiwamo wabunge wa Viti Maalumu kupitia umoja huo wanatajwa kuwa sehemu ya mpango huo wa siri wakifanya hivyo ili kulipa fadhila. Wabunge hao wa vitimaalumu wanatajwa kusaidiwa na waziri huyo ambaye aliwahi kuwa kiongozi mwandamizi wa UVCCM kupata nafasi walizonazo sasa.

“Baadhi ya wabunge hao walibebwa sana kisiasa na (anatajwa waziri huyo) hadi wakafika hapo walipo sasa, hivyo wanachofanya ni kumrudishia fadhila bila ya kujali kuwa jambo hilo kwa kweli lipo nje ya kanuni zetu,” anasema mmoja kati ya wenyeviti wa mikoa bila kutaka jina lake litajwe.

Hata hivyo, utekelezaji wa mkakati huo wa siri wa kumpachika Jamal kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM kuchukua nafasi ya Masauni ni wa muda kabla ya kupisha awamu nyingine ya mkakati husika. Inaelezwa kuwa Jamal atadumu kwenye uenyekiti hadi 2013 ili kumpisha mdogo wa waziri huyo ambaye jina la ukoo wake lilianza kusikika kwenye siasa za Tanzania kuanzia kwa baba yake aliyekuwa kada maarufu katika CCM.

Mdogo wa waziri huyo atapachikwa nafasi hiyo katika wakati ambao atakuwa amehitimu masomo katika moja ya vyuo vikuu mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Tayari inatajwa kuwa Mwenyekiti huyo mtarajiwa wa UVCCM kuanzia mwaka 2013, alikuwa Zanzibar hivi karibuni kwa lengo la kuwahamasisha wenyeviti wa mikoa ya Tanzania Zanzibar kuhudhuria mkutano huo uliopangwa kufanyika siku yoyote kuanzia Jumatatu wiki ijayo.

Utekelezaji wa mpango huo pia unahusisha uteuzi wa Makatibu wa Mikoa wa UVCCM watakaomtii kwa kila jambo atakaloagiza mwenyekiti huyo mpya kwa maslahi ya waziri husika na kwamba makatibu hao mwaka 2015 watakuwa pia ni Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM tayari kupiga kura kuteua mgombea urais wa Tanzania.

Mbali na kuweka Makatibu wa Mikoa vibaraka, kazi nyingine iliyopangwa na waziri huyo katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa UVCCM wa mwaka 2013 ni kuhakikisha mdogo wake anasimikwa uenyekiti wa UVCCM Taifa.

Wengine watakaochaguliwa kwa ajili hiyo ni mjumbe mmoja wa mkutano mkuu wa Taifa wa CCM kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ili kukidhi Ibara ya 104(z) ya Katiba ya CCM Toleo la Mwaka 2010.

Hayo yanatajwa kuwa ni mazingira yanayomhakikishia waziri husika uwingi wa kura katika mkutano mkuu wa CCM wa 2015 utakaoteua mgombea urais kwa tiketi ya CCM.

Sehemu nyingine ya mkakati au mpango wa waziri huyo baada ya kuvuruga UVCCM ni kujipenyeza na kupanga safu zake katika jumuiya nyingine za CCM ambazo ni Umoja wa Wazazi na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), sambamba na kupanga safu ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM kupitia jumuiya hizo tatu zinazotajwa na Ibara ya 128(1)(a) – (c) ya katiba ya chama hicho tawala.

Malisa na Shigela ambao ndio viongozi wa juu zaidi katika UVCCM kwa sasa, wanaelezwa kuwa na msimamo tofauti na waziri huyo, wakidaiwa kutokuwa tayari kugeuzwa vibaraka na baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa urais, ambao tayari wanajipanga ili kusaka ushindi kwa njia zozote zile ziwe halali au haramu.

Wachambuzi wa masuala ya siasa za ndani ya CCM, wakiwamo baadhi ya wastaafu wanasema endapo siasa chafu zilizopangwa kufanywa na waziri huyo zitafanikiwa, CCM itaingia Uchaguzi Mkuu ujao ikiwa hoi.

Wanasema wazi kwamba endapo chama hicho kitapitisha jina la waziri huyo, ambaye kwa mujibu wao hafai hata kwa nafasi hiyo aliyonayo, CCM ijiandae kuwa chama cha upinzani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

source raia mwema
 
Sasa kama anajiandaa kugombea tatizo lako nini?We nae kagombee huko kwenye chama chenu cha kutimuana!
 
Sasa kama anajiandaa kugombea tatizo lako nini?We nae kagombee huko kwenye chama chenu cha kutimuana![/QUOTE

Sasa wagombea wameisha, lakini sidhani kuisha kwao pia kunaweza kumaliza uwezo wa wanachama wao kutathmini upepo unavyokwenda., Jamani kusoma hamjui hata picha hamuoni!
 
Back
Top Bottom