Waziri Mkuu mpya Tanzania apendelea baraza dogo la mawaziri

Gembe

JF-Expert Member
Sep 25, 2007
2,483
159
WAZIRI Mkuu mpya, Mizengo Pinda amesema suala la ukubwa wa Baraza la Mawaziri litakuwa moja ya ajenda za mwanzo kabisa kwake, pale atakapokutana na Rais Jakaya Kikwete kujadili baraza jipya linalotarajiwa kutangazwa kesho.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana kwa njia ya simu kutoka mjini Dodoma, Pinda alikiri kusikia malalamiko hayo ya wananchi lakini akasema mwenye mamlaka ya kupunguza ukubwa huo ni rais mwenyewe na jambo hilo anaweza kulifanya kulingana na mahitaji ya wakati uliopo.

“Ni kweli kumekuwa na maneno mengi kwamba Baraza la Mawaziri lilikuwa kubwa sana, pia nadhani hapo kuna mantiki ila ngoja kwanza niape ndipo tutajadili suala hilo na Rais Kikwete,” alisema muda mfupi kabla ya kwenda kuapishwa.

Alisema bila shaka katika kipindi cha miaka miwili ya baraza lililovunjwa, Rais Kikwete atakuwa ameona kama mawaziri wake wamekidhi kiu yake ya kuwaletea Watanzania maendeleo kadri ya makusudio yake.

Kwa mujibu wa Pinda baraza hilo linaonekana ni kubwa kutokana na mazoea ya Watanzania kutoka uhuru, lakini Rais Kikwete aliliunda baraza hilo kutokana na mahitaji yake kwa Watanzania.

“Kama ni suala la kutimiza walau malengo ya Rais Kikwete ya kuunda baraza la namna ile, yeye ndiye anafahamu, hivyo kama kutakuwa na haja ya kulipunguza atafanya hivyo” alisema waziri mkuu na kusisitiza kuwa, yeye ni mshauri tu hivyo atatumia nafasi yake ya ushauri kama itakavyojitokeza.

Kumekuwa na minong’ono mingi kwamba, Baraza la Mawaziri lililovunjwa na Rais Kikwete lilikuwa kubwa mno ukilinganisha na mahitaji yake kwa wananchi.

Baraza lililovunjwa lilikuwa na jumla ya Mawaziri 29 pamoja na manaibu mawaziri 32, jambo ambalo linasemwa kuwa walikuwa wakitumia fedha nyingi za serikali kuendesha wizara hizo kuliko kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Karibu kila Mtanzania sasa anasubiri kuona kama Rais Kikwete ameliona tatizo hilo na kupunguza ukubwa wa baraza ili kuwa na baraza lenye watu wachache wanaowajibika kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Pinda amesema kipaumbele chake ni kuimarisha utawala bora na kusimamia fedha za umma ambazo zinapotea katika Halmashauri za Wilaya na katika miradi mingine ya maendeleo.

Pinda alisema atachukua hatua hiyo ikiwa ni mkakati wake wa kuhakikisha kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania yanafanikiwa tofauti na ilivyo sasa.

“Kipaumbele changu kwa kweli ni kusimamia utawala bora, hapo ndipo ninaona kumekuwa na tatizo kubwa sana, maana hata pesa nyingi za miradi ya maendeleo ya wananchi imekuwa inapotelea mikononi mwa wajanja, nadhani nitajitahidi kudhibiti hali hiyo,” alisema Pinda.

Waziri Mkuu huyo aliongeza kuwa, amekuwa akilifuatilia suala la utawala bora pamoja na uwajibikaji tangu akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kuona mapungufu ambayo sasa ndiyo changamoto katika uongozi.

Waziri Mkuu Pinda alisema anachukua nafasi hiyo akiwa anafahamu matatizo kadhaa yaliyopo katika serikali, likiwamo la matumizi mabaya ya fedha, kutokuwajibika na suala la utawala wa sheria.

“Nina imani nikilivalia njuga suala la matumizi mabaya ya fedha, utawala wa sheria na uwajibikaji, nchi hii itabadilika na hatimaye kuwaonjesha Watanzania maisha bora ambayo Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiwaahidi,” alisema.

Alifafanua kuwa utawala bora ni pamoja na kusimamia vizuri fedha zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, ambazo zimekuwa zinatumiwa vibaya na hakuna mtu anayewajibishwa kutokana na hilo.

Akizungumzia kashfa ya Richmond, Pinda alisema imetokana na kutokuwepo utawala bora, hivyo yeye ameahidi kusimamia dhana hiyo kwa kuamini kwamba, umma wa Watanzania una matarajio makubwa sana kutoka katika serikali hii mpya.

Pinda alisema katika sehemu kubwa wananchi wameanza kupoteza imani na serikali yao kutokana na watendaji wabovu, ambao wamekuwa hawaweki mambo yanayowahusu wananchi wazi, ili kila mmoja afahamu kinachoendelea katika serikali yake.

“Ninayo mifano mingi sana ya wananchi kutopewa taarifa sahihi za mapato na matumizi, au hata ile ya michango yao, hali inayowafanya kukosa imani na viongozi kama hao,” alisema.

Waziri Mkuu alisema kwa kushirikiana na Rais Kikwete atahakikisha wanalipatia majibu sahihi suala la kutenganisha biashara na utumishi wa umma.

Katika suala hilo, Pinda alisema kumekuwepo na tafsiri isiyo sahihi kuhusiana na Azimio la Zanzibar lililokuwa na nia nzuri ya kupanua wigo wa utekelezaji wa Azimio la Arusha, lakini limechukuliwa vibaya na baadhi ya wafanyabiashara ndani ya serikali.

“Lazima mtu akiwa ni mfanyabiashara na kiongozi wa umma kutakuwa na mgongano wa kimaslahi, ambao unasababisha matatizo makubwa hasa pale panapotokea zabuni, katika hilo nitashauriana na Rais tuone jinsi ya kufanya,” alisema Waziri Mkuu.

Wakati huo huo, Mwasu Sware anaripoti kuwa; Wanaharakati wa Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu Kusini mwa Afrika (SAHRINGON) na mitandao ya vikundi vya kijamii nchini, wamelaani vitendo vilivyobainishwa na kamati teule iliyochunguza mchakato wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura huku wakimtaka Rais kuunda baraza jipya kwa kufuata maadili ya uongozi.

Wakitoa tamko kwa rais, wanaharakati hao wamesema ni vema serikali mpya na wabunge kuhakikisha kwamba, Kamati ya Rais ya Madini na ile ya BoT zibadilishwe na kuundwa kamati za bunge za kuchunguza masuala ya madini na rasilimali za taifa.
Pia wamemtaka rais aunde Baraza la Mawaziri lenye watu wachache ambao ni waadilifu, wenye uwezo wa kufanya kazi kwa maslahi ya nchi, na si kwa lengo la kujinufaisha wao wenyewe.
Source:www.Mwananchi.co.tz
 
Back
Top Bottom