Waziri Mkuu aagiza viongozi ushirika wa tumbaku wakamatwe

N'yadikwa

JF-Expert Member
Aug 10, 2014
7,121
10,231
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora kuwakamata viongozi wanne wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) pamoja na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama hicho utakapokamilika.

Pia Waziri Mkuu amevunja Bodi ya WETCU pamoja na Bodi ya Tumbaku Tanzania - TTB kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo jioni (Alhamisi Machi 16, 2017) katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mkoani Tabora, ambapo amesema Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa TTB, Bw. Vita Kawawa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo Bw. Wilfred Mushi.

Viongozi wa WETCU ambao Waziri Mkuu ameagiza wakamatwe ni Mwenyekiti Bw. Mkandara Mkandara, Makamu Mwenyekiti Bw. Msafiri Kassim, Mkaguzi wa Ndani na Mhasibu Mkuu. Pia amewasimamisha kazi watumishi wa kitengo cha uhasibu wa chama hicho hadi uchunguzi utakapokamilika

“Kuanzia sasa watumishi wote wa kitengo cha uhasibu pamoja menejimenti nimewasimamisha kazi pamoja na Mrajisi wa mkoa wa Tabora Deogratius Rugangila. Kamanda hakikisha ofisi hazifunguliwi kuanzia sasa hadi hapo timu ya ukaguzi itakapokamilisha kazi yake,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema kwa muda mrefu wakulima wameteseka na zao hilo kukosa tija kwa sababu ya usimamizi mbovu wa viongozi wa ushirika na Bodi ya Tumbaku Tanzania jambo ambalo Serikali haiwezi kulivumilia.

Amesema “Hatuwezi kuwa na ushirika ambao hauwasaidii wanachama. WETCU walipokea sh. bilioni 15 ambazo walizikatia risiti na hazijaonekana. Pia waliwalipa wazabuni sh, bilioni 10 ambazo hawajazikatia risiti,”.

“Wakati wanachama ambao ni wakulima wakiendelea kutesema WETCU walinunua gari la sh. milioni 269 kinyume na na maelekezo ya Mkutano Mkuu wa wadau ambao ulipitisha zitumike Shilingi milioni 40 tu,” amesema.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa chama hicho kimesababisha kupungua kwa uzalishaji kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa na menejimemti mbovu jambo ambalo limechangia wakulima wa tumbaku kukosa tija.

Amesema WETCU kimekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha ambapo alitolea mfano suala la ukarabati wa ofisi tatu ikiwemo ya makao makuu ambayo ilipangwa ikarabatiwe kwa sh. milioni 33 wakatumia sh. milioni 170 na ofisi za Tabora na Urambo zilipangiwa sh. milioni tano kila moja na hazikukarabatiwa.

Pia Waziri Mkuu amepiga marufuku ununuzi wa mbolea kutoka nje ya nchi wkatiikiwa inazalishwa hap nchini. Aidha, alimepiga marufuku matumizi ya kwa dola katika sekta ya tumbaku na badala yake zitumike fedha ya Kitanzania kwa sababu kitendo hicho kimekuwa kiwanyonya wakulima.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Aggrey Mwanri, wakuu wa wilaya zote za mkoa huo pamoja na Maofisa Kilimo na Ushirika kuhakikisha wanasimamia vizuri zao hili ili liweze kuwa na tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.

Pia amewaagiza Maofisa Kilimo waende vijijini na kuwatambua wakulima wa tumbaku katika kila kijiji na kuwasajili. “ Kuanzia leo Maofisa Ushirika wabadilishe mienendo ya kazi nataka wasimamie zao la tumbaku kwa umakini zaidi.”

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, MACHI 16, 2017.
 
Hatua hii mbona imechukua kipindi kirefu sana kuchukuliwa?
Wakulima wa tumbaku walimfuata hadi rais akiwa ziarani Mkoani Kagera kumtolea kilio chao jinsi walivyodhulumiwa na viongozi wa vyama vya msingi vya tumbaku mkoani Tabora.
Lakini ikawa kimya hadi leo linapotolewa tangazo hili.
Watu wasioelewa matendo ya kifisadi wanayofanyiwa wakulima wa tumbaku wa mkoa wa Tabora ni ya kinyama na ya kusikitisha sana. Hali hiyo imepelekea hadi kilimo cha tumbaku kufa.
Viongozi wamejitajirisha kwa kuchukua mikopo kwa tiketi ya vyama vya msingi vya wakulima.
Wakulima wanapopeleka kuuza mazao yao kwenye soko la tumbaku hawalipwi wakielezwa kuwa wanadaiwa, yaani mazao yao yanapokelewa, lakini pesa haitoki hadi madeni waliyokopa viongozi wao yaishe.
Sasa hayo niliyoeleza ni machache, mengi ya kusikitisha wanayo wakulima wenyewe. Kuna simulizi za kutia jazba sana, ukipata kusikiliza kilio cha dhulma wanaxofanyiwa wakulima wa tumbaku wa mkoa wa Tabora.
Nadhani sasa Mungu atakuwa anesikia kilio chao, ijapo kwa kuchelewa.
 
Back
Top Bottom