Kurzweil
JF-Expert Member
- May 25, 2011
- 6,622
- 8,410
Katika hali ya kusikitisha watu watatu wakazi wa kijiji cha Kauzeni wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wamekufa baada ya kula mihogo inayosadikiwa kuwa na sumu huku wengine wawili wakilazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro na mmoja kupata nafuu na kuruhusiwa.
Akizungumza na ITV akiwa hospitalini hapo mara baada ya kunusurika kifo Joshua Msiani amesema anachokumbuka walikuwa katika shughuli zao za kufyatua tofali ndipo wenzake wakamkaribisha mihogo ya kuchemsha na baada ya kula ndipo ghafula hali ikawa mbaya na kujikuta yupo hospitalini.
Kwa upande wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo ambapo amesema mamlaka husika zimechukua sampuli ya mihogo na uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha vifo hivyo .
Waliofariki dunia kwa tukio hilo ni Daudi Hermani mkazi wa Kauzeni, Omary Mohamed pamoja na Hamisi Mohamed ambao ni mapacha.
Chanzo: ITV