Watendaji wamuacha solemba Rais Kikwete

kikweteutabiri.jpg


Rais Kikwete

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, watendaji watano wa serikali mkoani Kilimanjaro, jana hawakutokea kwenye ziara ya Rais Jakaya Kikwete na kusababisha maswali yanayohusu kero za wananchi kutopata majibu ambayo mkuu huyo wa nchi aliyatarajia.

Hali hiyo ilimfanya mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Monica Mbega aliyekuwa pamoja na rais kwenye meza kuu kuonekana kukosa amani kila wakati mtendaji ambaye rais alimtaka asimame ili atoe majibu kwa wananchi, kukosekana kwenye ziara hiyo.

Sakata hilo lilitokea jana eneo la Marangu Mtoni wilayani Moshi Vijijini baada ya Rais Kikwete kumaliza hotuba yake ya ufunguzi wa tawi jipya la benki ya CRDB Marangu na kuamua kuingia kwenye siasa kutafuta kero za wananchi.
Akiwa kwenye mkutano huo, Kikwete alianza kwa kumwita kwa kumshitukiza mwenyekiti wa Kijiji cha Samanga, Thomas Makiponya ili aeleze shida zote zinazolikabili eneo hilo ili yeye kama mkuu wa nchi aweze kusikia na kuzitafutia majibu.

Ndipo mwenyekiti huyo alipoainisha kero mbalimbali ikiwamo tatizo la mifereji ya asili na zahanati ya kijiji ambayo ni ya zamani sana na kwamba alishaiandikia halmashauri ili iikarabati, lakini hakuna kilichofanyika.
Kero nyingine ambayo mwenyekiti huyo alimweleza rais ni kuhusu barabara za vijijini zilizo pembezoni mwa barabara kuu ambazo alidai zinawapa shida sana; kukosekana kwa kituo cha polisi na pia taabu wanayopata watumishi wastaafu.
Baada ya maelezo hayo, Rais KIKWETE alisema suala la ukarabati wa mifereji ya asili limezungumziwa pia na Mbunge wa Jimbo hilo, Aloyce Kimaro hivyo akataka mkurugenzi wa umwagiliaji asimame kutoa majibu, lakini mtendaji huyo hakuwepo mkutanoni.

Kukosekana kwake kulimlazimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi, Anna Mwahalende kujitutumua kujibu maswali mengi, likiwamo la mifereji ya asili akisema japo wanajitahidi kuikarabati, lakini bajeti haitoshelezi.
Wakati akieleza, Rais Kikwete aliingilia kati na kuuliza: "mkurugenzi wa umwagiliaji yuko wapi? maana yeye ndio mhusika ingawa halmashauri nayo ina nafasi yake…au hakualikwa?"
Na wananchi wakamjibu kuwa "kaangia mitini".

Baadaye, Rais Kikwete alimtaka mganga mkuu wa wilaya hiyo au daktari wa wilaya atoe maelezo kuhusu hoja ya zanahati, lakini kwa mshangao wa wengi hakuna aliyekuwepo hali iliyomfanya mkuu huyo wa nchi kuhamaki na kuhoji sababu za kutokuwepo kwa watendaji hao wote.

Japokuwa mganga mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Mtumwa Mwako naye alijitutumua kujibu, maelezo yake hayakumridhisha Rais Kikwete ambaye alisema kila swali linaloulizwa lina mwenyewe na watendaji hao wangekuwepo majibu mazuri zaidi yangepatikana.

Rais Kikwete hakuishia hapo, akamtaka mhandisi wa barabara wa wilaya atoe maelezo kuhusu kero ya barabara za vijijini, lakini kwa mara nyingine mtaalamu huyo hakuwepo katika mkutano huo, hali ambayo iliwafanya wananchi kuguna huku Mbega akionekana kukosa amani zaidi.

Hata Rais Kikwete alipomuulizia ofisa kilimo wa wilaya na ofisa anayeshughulikia mfuko wa Tasaf ili watoe maelezo kuhusu masuala yanayohusu ofisi zao, nao hawakupatikana, hali iliyoonyesha dhahiri kuwa ilimkera Rais Kikwete.
Baadaye Rais Kikwete alisema tatizo la halmashauri nyingi nchini ni wizi, akifafanua kuwa huwa zinapata fedha nyingi ambazo zingeweza kutekelezwa kwa shughuli nyingi za maendeleo vijijini, lakini zinaishia mifukoni kwa baadhi ya watendaji.

Alisema matatizo mengi yaliyoibuliwa na wananchi ameyasikia naye ameyachukua na atayafanyia kazi.

SOURCE: MWANANCHI
 
Nduku yangu wewe mbado unaishi katika ensi walisokuwa wanatumia mawe kama sana sa kuwindia? Ulitaka mtu kama huyo bwana mganga aache kutibia watu aende kusikilisa rais?


una hakika alikuwa anatibu wagonjwa? huyu alilala mbele kuogopa kujibu maswali ambayo wananchi wanayauliza kuhusiana na wajibu wake kwa umma. hawa ni viongozi wasio tekeleza majukumu yao na wanapopata habari kuwa rais amekuja wanakimbia hawana lolote ni mijizi mitupu.....
 
Back
Top Bottom