Watanzania wa nje walalamikaji - nyalandu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
NAIBU Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Lazaro Nyalandu, amesema sehemu kubwa ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi, wamekua walalamikaji tu kuhusu taratibu za uwekezaji, lakini hawachukui hatua.

Nyalandu alitoa kauli hiyo wiki iliyopita, wakati akizungumza na Mwananchi baada ya kuzindua Kampuni ya Ndege ya Bold Air, inayomilikiwa na John Ndunguru, Mtanzania anayeishi Marekani. Uzinduzi wa kampuni hiyo, ulifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Watanzania waache kulalamika tu kwenye mablog. Wengi wamekuwa walalamikaji tu, lakini hawachukui hatua,” alisema Nyalandu.

Naibu waziri huyo aliwataka Watanzania hao, watumie muda wa kukaa kwenye mitandao, kuangalia taarifa zinazohusu fursa za uwekezaji zinazopatikana pia hata kwenye mtandao wa Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania na kusaidia shughuli za uwekezaji hapa nchini.

“Kitendo cha kulalamika bila ya kuchukua hatua ni ishara kwamba wengi wao sio wabunifu. Nampongeza ndugu yangu John Nduguru, kwa kutumia fursa hiyo na kuanzisha kampuni hii,” alisema.

Nyalandu alimpongeza Ndunguru kwa uamuzi wa kuja kuwekeza nyumbani, jambo ambalo alisema litasaidia katika kuinua uchumi wa Tanzania.

"Pamoja na kwamba Ndunguru amekuwa akifanya biashara zake nchini Marekani, lakini ameona umuhimu wa kuwekeza nyumbani jambo ambalo litasaidia kuinua uchumi na kutengeza ajira kwa Watanzania wenzake," alisema Naibu waziri.

Kwa upande wake, Ndunguru aliishauri serikali iangalie na kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali za uwekezaji ukiwemo mlolongo mrefu kuhusu mchakato wa uwekezaji.

Alisema mchakato wa uwekezaji nchini ni mrefu, jambo linalowafanya Watanzania wengi walioko nje, wakate tamaa, na kwamba hiyo inachangiwa na tatizo la kutakiwa kutumia muda mrefu katika kumilisha taratibu za uwekezaji.

“Tataratibu zetu bado ni ngumu, maana mtu anatumia muda mrefu na gharama na kubwa, jambo linalowakatisha tamaa Watanzania wengi kuja kuwekeza nyumbani," alisisitiza.

Alisema ameamua kuwekeza katika usafiri wa anga kwa kuwa kuna nafasi nyingi za kufanya biashara na kwamba wakati umefika kwa watanzania, kuachana dhana kwamba huduma ya usafiri wa ndege ni ya watu maalum tu na wenye fedha nyingi.

“Zamani biashara hii ilitawaliwa na Wahindi na Waarabu ambao walitujengea hisia na dhana kwamba huduma hiyo ni ya gharama kubwa sana na kwa hiyo ni ya watu maalumu tu. Hii si kweli, hata Mtanzania wa kawaida anaweza kumudu gharama za usafiri huu,” alisema.

Kwa upande wake, Nyalandu alisema ni azma ya Serikali ya Awamu ya Nne, kuwaandalia Watanzania mazingira bora ya uwekezaji kama ambavyo imekuwa ikifanya, ili kila Mtanzania aliyeko nje na mwenye uwezo wa kuwekeza, aje kufanya hivyo.

Alisema kwa sasa serikali iko katika mchakato wa kuangalia mfumo mzima wa kodi za uwekezaji, ikiwa ni hatua ya kuboreesha zaidi mazingira ya uwekezaji, ili kuwavutia wawekezaji wengi wakiwemo wazawa.

Kampuni hiyo ya Bold imeingiza ndege mbili kwenye soko, moja ikiwa ni ya aina ya Cessna 310 na nyingine aina ya Seneca 1, zote zikiwa na uwezo wa kuchukua abiria sita kila moja kwa wakati mmoja.
 
Back
Top Bottom