WATANGAZA NIA WAIVUA NGUO CCM.
Chama ambacho kimekuwa ni kisima cha viongozi bora. Chama ambacho kimekuwa na mfumo wa kuigwa kama uwepo wa misingi, kanuni, miiko na taratibu bora za kiutendaji. Chama ambacho kimekuwa mfano wa kuigwa katika uendeshaji wa taratibu bora za kupata viongozi, chama ambacho kimekuwa kikisifika kwa kanuni bora za uendashaji wa viongozi wa ngazi zote. Lakini kwa hali ambayo inaendelea wao kwa wao, kupeana maneno ya kashfa baina yao, kuonyesha mapungufu ya viongozi wa Serikali inayoongozwa na chama chao tena hadharani. Kwa kila mwanachama au kada kuona anafaa kuwa Rais hata kama hizo sifa hana, kwa kila mwanachama kutoa vipaumbele vyake badala ya kusubiri ilani ya chama chake na hivyo kuonyesha yeye ana sera nzuri kuliko za chama chake. Mambo yote hayo yamekuwa yakikikivua nguo chama cha mapinduzi.
Nafasi ya Urais siyo nafasi ya kuombwa na kila mwanachama, ni nafasi ambayo anayeomba awe amejitathimini vya kutosha na kuona anakidhi vigezo hivyo. Lakini tumeshuhudia wanachama hata wenye umri chini ya miaka 40 wakitangaza nia kama sio kuleta utani na kukivua nguo chama cha mapinduzi ni kitu gani hicho? Kwa nini chama hakiwachukulii hatua za kinidhamu wanachama hao ambao wanaleta mzaha katika jambo zito kama hili? Kama haitoshi watu wenye taswira mbovu kwenye jamii nao wamejitokeza kwa wingi na kuchukua fomu za uteuzi baada ya kutangaza nia. Chama kimekuwa kama vile hakina uongozi wala kanuni na miongozo. Hii yote ni dalili na ishara ya kuvuliwa nguo.
Tumeshuhudia wanachama wenye nyadhifa Serikalini tena za ngazi za juu, ambao wameshindwa kuendesha Ofisi zao, ambao kwenye Ofisi zao wameshindwa kuwa wakweli kwa kusingizia hawapo Ofisini kumbe wapo ambao kwao ndio ni hapana na hapana ni ndiyo, eti nao wametangaza nia na kuchukua fomu za uteuzi na kujinadi eti ni waadilifu, wacha Mungu, wachapa kazi na wenye uzoefu mkubwa kimataifa wanashangaza sana, maana chama kimepoteza hadhi yake, chama kimepoteza nguvu za kuwakemea wanachama wa aina hii. Na hivyo tukisea kimevuliwa nguo tutakuwa tunakosea? Jibu ni hapana, hatukosei hata kidogo. Hizi ni ishara tosha za kuvuliwa nguo.
Kwa muktadha huu, hali hii italeta vurugu na kazi kubwa katika uteuzi maana pumba na mchele na mawe vimechanganyika pamoja. Kazi ipo maana badala ya kuchambua mchele na mawe itabidi kuchambua pumba na mchele halafu ndio kuchambua mchele na mawe na hatujui hao wachambuaji kama wataweza hiyo kazi? Je hawatategeana? Je hawatakwepa lawama za kuhusika kufyeka baadhi ya wagombea? Je haitakuwa hali ya kulaumiana? Yote haya yasingetokea kama chama kingeweka utaratibu mapema kabisa, pumba na mawe wasingeweza kutangaza nia kwa fujo kama ilivyotokea sasa. Utitiri wa wagombea zaidi ya watu arobaini kwa kiti kimoja tena kilicho nyeti ni fujo. Wenye akili tunajiuliza, hali hii haitaweza kukisambaratisha chama. Tuombe Mungu yote yapite kwa usalama maana pamoja na kuvuliwa nguo kinaweza kusambaratika vibaya na kikabakia historia katika nchi hii yenye amani na utulivu.
Shabiri Mpaka
0715039991