“Wasouth” wanaua lakini sisi nasi ni wale wale

Dr. Wansegamila

JF-Expert Member
Feb 3, 2012
2,858
7,847
*Anaandika Pd. Titus Amigu*

Nina sababu nyingi sana ninazompendea Mungu. Moja wapo ni hii, mara kwa mara anaruhusu mambo ya kushadidishia hoja na maoni yangu yatokee. Kwa hili linaloendelea Afrika ya Kusini (South), ananisaidia kushadidia nilichopata kusema mara nyingi kwamba sisi Waafrika ni mabingwa wa kukosea kutoa sababu ya matatizo yetu na kwamba waliodhani sisi si watu kamili pengine hawakuwa mbali sana na ukweli. Kwa mfano, huwa nasema yafuatayo: Tunadanganyika kirahisi (the gullible and manipulable). Sisi ni wakatili. Sisi asipokuwapo mtu wa kututukana, hujitukana wenyewe. Sisi asipokuwapo mtu wa kuiba vyetu, huviiba wenyewe. Mada za laana, uchawi, mizimu, majini na mapepo zinatudumaza. Tunaweza kupiganishwa kama kuku na kadhalika.
Ajabu, hata mahali wanapoamini sana uwapo wa uchawi, utakuta watu weusi watatuhumiana wao kwa wao. Wataua vikongwe vyao, Wazungu ama Wahindi wazee na vikongwe wanaokaa kati yao hawatawagusa hata kidogo. Yaani sisi ni maadui wenyewe kwa wenyewe.
“Wenzetu” wa Afrika ya Kusini, wamepoteza vichwa. Hawana ardhi. Hawana ajira. “Vyuma vimewakazia.” Ukitembea huko Kusini mwa Afrika, hali ndivyo ilivyo Afrika ya Kusini, Namibia, Zimbabwe na hata Zambia.
Mzee Mugabe alijaribu kurekebisha hali hiyo, Waafrika tukadanganywa na kusadikishwa na Wazungu (kupitia BBC, DW na VOA tunakokopi habari) kwamba alikuwa dikteta. Leo amekufa, baadhi ya Waafrika eti wanafurahi. Wachache wanamkumbuka kama ng’ombe aliyepoteza mkia. Maskini sisi!
Nakwambieni sisi tumekamatwa hata katika habari. Hatujui ukweli, radio, televisheni na magazeti yetu kazi kukopi mambo ya BBC, DW na VOA, vyombo ambavyo maslahi ya wamiliki wake si ya bara hili. Vyombo hivi vikisema fulani mzuri, tutamsifu na vikisema fulani mbaya, tutataka sote tuchukue mapanga tumchinje hata kama hatumfahamu. Jiulize kama ulifikiri kwa kujitegemea kuhusiana na Said Barre wa Somalia, Saddam Hussein wa Iraki au Muhamar Gaddafi wa Libya. Huko walikojidai watu kujenga demokrasia, kwa kumtoa aliyeitwa “dikteta” mmoja kunaendelea vita na mauji ya wengi kwa miongo mingi. Faida yake nini, kumtoa dikteta mmoja na kishapo mauji ya maelfu yaendelee?

Kupigika kwa Watu Weusi
Popote tulipo watu weusi hali yetu ni ngumu. Wamerika weusi wana hali ngumu ili kuuana wanauana wenyewe kwa wenyewe na hata wewe Mwafrika ukienda kule wanakuchukia. Ukienda Brazili na Haiti mambo ni hivyo hivyo.
Jamani, hali ya Afrika ya Kusini ni ngumu, hata mzee Nelson Mandela mwenyewe alishindwa kuitatua. Kwa kuogopa kuchafua CV yake, akajiuzulu mapema. Alilishindwa fupa la ardhi na umaskini wa weusi. Thabo Mbeki akalishindwa pia. “Wasouth” wakatumaini Yakobo Zuma atawafanyia kitu, yeye akaishia kuoa wanawake watano na kujijengea kasiri kubwa. Sasa Cyril Rhamaphosa ni ndumilakuwili. Ushahidi upo kwamba aliahidi kuwafurusha wageni hivyo hivyo! Hata kijana Julius Malema ana nguvu ya kinywani tu, akipewa nchi atashindwa kuchukua ardhi ya Wazungu na kuwagawia watu weusi. Anajidai kumjua paka anayekula ndugu zake, lakini atashindwa kumfunga kengele paka huyo.
Kwa muhtasari huu wa mambo, hata kama hujawahi kufika huko “Bondeni”, ujue hali ya watu weusi ni tete. “Wamepigika.” Katembee huku Kusini mwa Afrika uone watu weusi wanavyoishi katika mabanda ya “fullsuit” za mabati katika maeneo ya pambizoni mwa miji. Haya mabati ya “msauzi” yanawapita juu kwa juu kuja huku kwetu. Inatia huruma kweli!

Ubingwa wa Kukosea Kutoa Sababu
Sasa ubingwa wa kukosea kutoa sababu ndiyo nini? Ni hivi, kwa umaskini uliowabana “Wasouth” kwenye vitongoji na miji yao sababu wanayotoa ni uwapo wa “wageni” kutoka Nigeria, Zimbabwe, Zambia, Malawi, Msumbiji, Tanzania, Kongo, Somalia, Kenya na kadhalika. Hawa ndiyo mbuzi wa kafara. Wanawachoma moto, wanawakata kwa mashoka, wanachukua mali zao na kuchoma makazi na vibanda vyao vya biashara. Wapi na wapi! Mmeziona wenyewe picha za kikatili, kutisha na kusikitisha mno. Wazungu wanaomiliki ardhi hawawaoni. Wachina wanaochukua mali za kweli hawawaoni. Wahindi wanaovuna mali za gharama hawawaoni. Anayewaonea kweli hawamwoni, wanamwonea anayeonewa kama wao. Anayewaiba kweli, hawamwoni, wanamwonea anayeibiwa kama wao. Wanawaonea wageni wenye ajira dhalili tu mashambani mwa Wazungu, au viwandani mwa wazungu au kwenye machimbo ya Wazungu. Wanawaonea watu wenye viduka na vioski vidogo vidogo, wanawaacha wenye “masupamaketi”. Badala ya kumfunga kengele paka anayewala, wanawaua panya wenzao wenye madoadoa ambao waliwa na paka kama wao wenyewe.

Nyani Atazame Kundule
Lakini hili ninalolisema, tunadhani ni la “wenzetu Wasouth” tu. Hapana. Sisi ni wale wale. Humu mwetu mna kuoneana kwa sampuli hiyo hiyo. Mtu anakosa ajira, lawama anamtupia babu yake eti alimlaani au alimpa jina baya. Mtu anakosa chakula nyumbani mwake, anasema Mungu hajamwona, wakati hela anamalizia kumpa mchungaji au nabii kila siku. Lawama anamtwisha Mungu asiyehusika. Mtu anashindwa kufaulu shuleni, anasema kuna mwenzake alimwibia ubongo darasani na kadhalika, wakati kusoma alikuwa ananyanyapaa mwenyewe. Je, katika mifano hiyo hatujakosea sababu?
Nawapanueni mawazo. Tuseme mtu anaumwa maradhi fulani, ukimwi, ukoma au kifua kikuu na kadhalika; virusi, bakteria, au vimelea vinginevyo vimesababisha ugonjwa wake, yeye anamchukulia upanga bibi mwenye macho mekundu, anamuua. Je, si “Msouth” huyo?
Mtu anakosa ajira, anasema ni kwa sababu ya laana kutoka kwa babu yake ambaye zamani aliiba mahindi au kuku kwa mwenzie au babu aliyempa jina baya, anamlaumu babu yake na watu wanamsadikisha kwamba dawa yake ni kukata mti wa ukoo au kufanyiwa ibada ya kufunguliwa, je, hapo hatujakosea sababu ya adha yetu? Hii maana yake huyo babu angerudi duniani, tungemchoma moto au kukatakata mapanga vile vile. Je, hapo hatujafanana na “Wasouth?”
Mtu hajapata kuolewa kwa sababu ya tabia yake mbaya, siku zote alikuwa haambiliki, sasa anasema amekaliwa na jinni au kuna mkono wa mtu, je, hapo sababu haijakosewa? Huyo jinni angeonekana au huyo mtu mwenye mkono wake katika shauri hilo angeonekana tusingemchoma moto vile vile? Kwa kuanza na fikra za namna hiyo tofauti yetu na “Wasouth” iko wapi?
Waafrika tunashindwa kuwa na mikakati ya kununua mazao yetu na kuyasindika, mathalani, kahawa, pamba, korosho, mbaazi, kunde, mahindi, ndizi, nazi na kadhalika; umaskini ukitukunja, watu tunakatana mapanga eti tunachawiana, je hatujafanana na “Wasouth?”

Utamaduni wa Kukosea Sababu
Kwa kukata maneno, Waafrika tunashindwa sana kutoa sababu kwa matatizo yetu, ndiyo kisa wanaotucheka wanasema tuna Hisa ya Akili (IQ) ndogo kuliko watu wa mabara yote. Ni kwamba hatuwezi kutoa sababu za kweli za maradhi yetu, wala umaskini wetu, wala kukosa kwetu ajira, wala matatizo yetu ya kijamii kama ndoa na kadhalika. Tunakosea sababu za matatizo binafsi, matatizo ya familia, matatizo ya nchi na hata matatizo ya bara letu. Mtu anasongana na watu wengine kwa matatizo yake binafsi. Wananchi wanasongana wao kwa wao wakichukua sababu dhalili za wao kwa wao na kadhalika. Lakini, tujue, mtu au daktari akitoa sababu batili ya ugonjwa, dawa atakayotoa itakuwa batili vile vile. Nikikopea maneno ya kidaktari, daktari akishindwa “DIAGNOSIS” atashindwa pia “PRESCRIPTION.” Hii haina ubishi, ndiyo mantiki yake. Wenzetu “Wasouth” wameshindwa hapo na sisi wengine hushindwa vivyo hivyo. Tusiwacheke wala tusiwatumbulie macho kwa kuwashangaa bali tujihurumie watu weusi wote.
Hata hivyo ipo hatari mpya. Ni kwamba kiroja cha kukosea sababu ya matatizo yetu kimepiga hodi hadi makanisani mwetu. Eti hatuna magari au majumba, au afya njema na baraka zingine, kwa sababu hatujampa Mungu “sadaka iliyo njema”, matokeo yake tunasali sala za kumkemea Mungu huku tukikesha pasi kupumzika. Tunaweheka na matatizo yetu. Ajira tunakwenda kuomba kwa Mungu, kwani yeye Bwana Kazi? Magari tunaenda kuyaomba kwa Mungu, kwani yeye Kampuni ya Toyota? Utajiri wa Ulaya, Marekani, Japani, China, Korea ya Kusini waliomba makanisani na misikitini? Sivyo. Tusimrudishie Mungu kazi aliyotuachia tuifanye wenyewe. Hivi, huyu Mungu, tunayedhani hatusikii, angelijitokeza mbele yetu tusingemchoma moto au kumkatakata kwa mapanga? Je, huo si moyo wa “Wasouth?”
Wanaotubia ni watu, tunayemlaumu ni Mungu. Mchungaji au nabii anatuambia tumlishe vyema, la sivyo, Mungu hatatujalia maombi yetu, tunamwamini, tunampa pesa, wenyewe tunalala njaa, wapi na wapi! Mchungaji au nabii anayetuibia hatumwoni, lawama tunamtupia Mungu, je hatujakosea sababu hapo? Hakika, na sisi ni wale wale! Mhubiri anatueleza eti nchi, mikoa, wilaya au vijiji vimelaaniwa kwa sababu ya maagano ya mababu zetu, sisi tunamtegea sikio tu na kumpigia makofi, je hajatukosesha sababu kwa hayo maneno yake? Ingetokea hao mababu wangerudi duniani, tusingewachoma moto bure?

Sisi ni Wale Wale
Acha niongezee mambo. Kichekesho kimetokea Bariadi mwaka huu, eti waganga 900, kisha kujichafua miili yao kwa masizi na uchafu mwingineo, wakafanya mkutano na kutangaza “watampoteza” yeyote atakayejitokeza kugombea urais mwaka 2020 kinyume na matakwa yao, maana yake Mwafrika fulani, huku wakishindwa kufanya chochote dhidi ya wanaochimba na kujineemesha kwa dhahabu na almasi katika machimbo mbalimbali katika mikoa yote ya jirani yao! Je, huku si kufanana na “Wasouth?” Akili yenyewe si hiyo hiyo ya kuacha madini ichukuliwe na wajanja na sisi tukate vidole albino wetu? Tatizo lingine, dawa nyingine! Je, hapo hatufanani na “Wasouth?”
Jamani, sisi ni wale wale! Tunachoshangaa ni nini? Hatuchomi moto wanaoiba kuku, simu au mikufu ya watu, na kuwaacha Wazungu, Wachina na kadhalika wanaoiba urani, chuma, dhahabu, almasi na kadhalika katika viunga vyetu? Nakwambieni sisi ni wale wale!
Sipendekezi tucharuke na kutafuta dawa za kibabe, isipokuwa siku zote busara itawale katika kubainisha shida zetu, kubaini sababu zake na hatimaye kutoa “masuluhisho” mema.

Ni mzee wenu Pd. Titus Amigu
 
Huyo ameandika andiko nzuri sana la wakati huu japo kuna mahali amejikaanga. Napo ni pale aliposema BBC DW VOA na ndugu zao wanatupatia taarifa kengemfu/potofu kuhusu Afrika.

Yaani kwa hilo nimempunguzia maksi. Ni nani hasiyejua madudu ya viongozi wa kiafrika , tukuchukulie mfano Yule mzee wa Uganda, njoo Burundi njoo Tanganyika njoo Congo shuka hadi South Africa. Kote huko wamejaa viongozi wa ovyo na wapenda rushwa waliotukuka.
Sasa BBC ikiripoti hayo madudu ndio mnasema inatulisha taarifa potofu.

Kwenye hilo naamini mkono wa Padri uliteleza. Cha muhimu wa waafrika tuache kulaumu mabeberu kwa mambo yetu ya kingese ngese. Tujifunze kukubali mapungufu na kuwa tayari kufanya mabadiliko.

Mfano Uganda inajulikana wazi kwamba Museven na Chama chake wamechoka kufanya kazi lakini bado wanapewa nafasi ya kuongoza nchi
 
Back
Top Bottom