The Boss
JF-Expert Member
- Aug 18, 2009
- 49,226
- 116,839
- “Hapa kazi tu” kuwa “hapa fukuza kazi tu”
- Lengo ni kumchonganisha na watu wa tabaka la chini
NI zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu Rais wa awamu ya tano, Dk. John Pombe Magufuli, aingie Ikulu. Kila uchao, Watanzania hutega sikio kwa umakini kumsikia rais wao atachukua uamuzi gani. Maamuzi yote yamekuwa ni ya kushtukiza. Lakini kwa kuwa mengi ya maamuzi hayo yamelenga kuondoa uozo unaofanywa na watu wa tabaka la juu – vigogo wa serikali na wafanyabiashara wakubwa – basi yanaungwa mkono na watu wa tabaka la chini. Maamuzi ya Magufuli yamemfanya kuwa gumzo kila kona ya nchi. Nyuma yake yapo mamilioni ya wanyonge wanaosubiria kwa shauku maamuzi ya kushtukiza ya Rais wao aliyeazimia “kutumbua majipu”.
Umaarufu wa Magufuli umevuka mipaka ya nchi. Ndani ya bara la Afrika, habari zake zimeenea katika mitandao ya kijamii huku Waafrika wenzetu wakituonea gere na kutuomba tuwaazimishe rais wetu japo kwa wiki moja ili “akatumbue majipu” katika nchi zao. Nje ya Afrika vivyo hivyo, jina la Magufuli limevuma mpaka Australia ambako wananchi wanamng’anganiza Waziri Mkuu wao kuiga mfano wa Magufuli katika kupambana na wakwepa kodi, na kufyeka marupurupu ya vigogo na safari za nje ya nchi.
Mapambano yenye nakisi ya itikadi
Binafsi nimekuwa nikitahadharisha kwamba wanyonge wa Tanzania wanapaswa kuwa waangalifu kwa Magufuli. Wasimkasimishe mamlaka yao ya kufikiri na kuamua juu ya hatma yao. Mamlaka hayo yanapaswa kuwa mikononi mwa wavujajasho wenyewe na wayatumie kupambana dhidi ya tabaka wavunajasho. Kumkabidhi mtu mmoja mamlaka hayo ni kutengeneza dikteta. Mfumo wowote unaomkabidhi mamlaka mtu mmoja, kisha wengine kubaki kuwa washangiliaji au watoa lawama kwa mtu huyo, ni mfumo wa kiimla. Mfumo wa kiimla ni mfumo mbaya bila kujali mtawala huyo wa kiimla anayatumiaje mamlaka aliyojipa.
Hilo mosi, pili ni kuwa Rais pendwa Magufuli licha ya kuwa mtu mwenye nia njema, ni mtu mwenye nakisi ya uelewa mpana wa masuala ya kijamii, kihistoria na kiuchumi. Hana dira inayoeleweka wala msingi thabiti wa maamuzi yake. Jambo hili limemfanya kutoa maamuzi yanayokinzana. Kwa upande mmoja, ameshaweka wazi kuwa injini ya uchumi ni sekta binafsi na ameshakutana na wafanyabiashara wakubwa kuwahakikishia kuwa serikali yake itayalinda maslahi yao. Kwa upande mwingine amewaahidi wanyonge (machinga, mamantilie, bodaboda, wapiga debe, wakulima wadogo na wavuvi wadogo) kuwa serikali yake ni serikali yao.
Ahadi hizo zinanamaanisha kuwa serikali ya Magufuli inafikiria kuleta uhusiano rafiki kati ya wavuja-jasho na wavuna-jasho. Hii ni sawa na kudhani kuwa simba na mbuzi wanaweza kuwekwa katika zizi moja bila ya simba kumla mbuzi au papa kummeza dagaa. Mtu mwenye udhani huo basi ana nakisi ya uelewa wa tabia za asili za wanyama wa mwituni na majini au ana nia ya kumrahisishia simba kazi ya kupata mlo. Kwa vyovyote vile, kuwafungia simba na mbuzi katika banda moja hakuwezi kuwa kumefanyika kwa maslahi ya mbuzi. Mfaidika wa mwisho atakuwa simba. Vivyo hivyo kwa matabaka yenye maslahi kinzani. Ni hulka ya mabepari (wafanyabiashara wakubwa) kuwanyonya, kuwapora na hata kuwaua wafanyakazi pamoja na wazalishaji wadogo. Kufikiria kuleta urafiki kati ya matabaka hayo kielelezo cha upunguani wahistoria ya mapambano ya kitabaka au ni kuwahadaa wanyonge kwa makusudi ili wawe “kitoweo” kwa mabepari.
Viongozi wenye uelewa thabiti huchukua upande. Serikali ya Mwalimu Nyerere ilichukua upande wa wanyonge; ndio maana Azimio la Arusha likatangaza kuwa Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi na kwamba wao ndio watakua gurudumu la maendeleo. Serikali za Mwinyi, Mkapa na Kikwete zilichukua upande wa mabepari. Ndio maana ziliua Azimio la Arusha, zikasalimisha viwanda vya serikali na rasilimali za umma mikononi mwa mabepari chini ya kauli mbiu ya ubinafsishaji na uwekezaji. Magufuli mwenyewe, akiwa waziri katika serikali ya Mkapa, na baadaye Kikwete, alishiriki kikamilifu katika uporaji huo kwa kubinafsisha nyumba za serikali kwa vigogo, huku ndugu zake na kimada wake wakiwa ni wafaidika wakuu.
Kwa hiyo, mapambano yoyote yasiyoongozwa na itikadi ya wanyonge, na yanayomtegemea mtu mmoja, ni mapambano ambayo hulipa nguvu tabaka nyonyaji. Warasimu serikalini (bureaucrats) hushirikiana na mapebari wa ndani na nje katika kuyahujumu mapambano ili kumchonganisha kiongozi wa mapambano na wanyonge na kuleta mageuzi yanayolifaidisha tabaka la wanyonyaji na waporaji.
Hali hii imeanza kujidhihirisha wazi katika kipindi kifupi cha serikali ya Magufuli. Desemba 30, 2015 ulipangwa mkutano kati ya Rais na wakuu wa taasisi na mashirika ya umma nchini, wenye lengo la kutoa dira na maelekezo ya Rais kwa wakuu hao. Hata hivyo, kwa sababu ambazo hazijaelezwa mpaka hivi sasa, Rais Magufuli hakuwepo katika mkutano huo na badala yake alimtuma msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, kuzungumza na wakuu hao.
Hoja kuu ya Mafuru, ambayo alidai ni maelekezo ya Rais, ni kubana matumizi na kuongeza ufanisi katika taasisi na mashirika ya umma. Ili kufanikisha haya, mageuzi kadhaa yalipaswa kufanyika katika matumizi ya fedha. Mosi, serikali ilikusudia kuondoa ruzuku kwa mashirika ya umma na kuyataka yajiendeshe kibiashara kama ilivyo katika sekta binafsi. Pili, serikali ilipiga marufuku posho za kukaa kitako (sitting allowances) katika bodi za mashirika ya umma.Tatu, katika kubana matumizi, mashirika ya umma yalitakiwa kupunguza wafanyakazi ili kuifanya sekta ya umma ifanane na ya binafsi.
Suala la posho za kukaa kitako
Vyombo vingi vya habari viliyaripoti maelekezo ya Mafuru ama kwa makosa ama kwa juu juu bila kuhoji msingi wa kiitikadi unaoyaongoza maelekezo hayo. Mathalani, iliripotiwa kuwa suala la posho za kukaa kitako liliwagusa pia Wabunge hali iliyosababisha shangwe miongoni mwa jamii. Ukweli ni kwamba posho zote za wabunge zipo palepale; kilichopigwa marufuku wabunge kupewa posho na mashirika ya umma ilhali wanakuwa wameshapokea posho toka bungeni. Mafuru mwenyewe alifafanua katika mtandao wa twitter kwamba ofisi yake haina mamlaka ya kupiga marufuku posho za wabunge.
Pili, mjadala wenyewe wa posho za wabunge ni finyu na umelenga kuhalalisha malipo mengine wayapatayo. Mathalani, hata kama mbunge atakataa posho za kukaa kitako (sitting allowances) ataendelea kupokea posho zingine pamoja na malipo mengine ambayo ni zaidi ya milioni 12 kwa mwezi. Kwa hiyo, kuzungumzia sitting allowances peke yake ni njia ya kuwafanya watu wasihoji malipo mengine wajilipayo vigogo wa serikali.
Taasisi za umma kujiendesha kibiashara
Mafuru pia alizitaka taasisi na mashirika ya umma kujiendesha kibiashara ili kuondoa utegemezi kwa ruzuku toka serikalini. Hatuna budi kufanya uchambuzi kuhusu taasisi na mashirika ya umma ili kufahamu ni yapi, ambayo kwa asili yake, yanapaswa kujiendesha kibiashara na yapi hayapaswi kujiendesha kibiashara.
Yapo mashirika ya umma yaliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kufanya biashara ili kutengeneza faida. Haya ni kama mabenki, migodi, bandari, na viwanda. Mengi ya mashirika haya yalishaporwa toka umiliki wa serikali na kuwekwa mikononi mwa watu binafsi. Sehemu kubwa ya uporaji huu ilifanyika wakati wa Mkapa na imeendelea hata katika kipindi cha Kikwete. Ubinafsishaji uliofanyika miaka ya karibuni ulihusisha shirika la UDA ambalo liliuzwa kwa bei ya kutupa kwa kada wa CCM, Robert Simon Kisena, na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 6.3.
Aina ya pili ya mashirika ya umma ni yale yaliyoanzishwa mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi. Haya ni kama Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), vyuo vikuu vya umma, mashirika ya huduma za maji safi na maji taka pamoja na mashirika yatoayo huduma za afya. Lilipokuja wimbi la soko holela, mashirika haya yalitakiwa kugeuza huduma kuwa bidhaa. Yaani huduma za elimu, makazi, maji na afya zikageuzwa bidhaa na kuuzwa sokoni. Wenye fedha ndio wanaoweza kuzimudu huku wanyonge wakitaabika na hata kupoteza maisha kutokana na kutokuwa na fedha za kununulia “bidhaa” hizo.
Yapo mashirika mengine ambayo yanapaswa kujiendesha kati ya biashara na huduma. Mashirika ya reli na umeme, kwa mfano, yanapaswa kutoa “huduma” zao kwa gharama nafuu kwa wananchi wa kawaida, na wakati huo huo kutengeneza faida kutokana na kuuza bidhaa zao kwa bei kwa wazalishaji wakubwa. Jitihada za kuyabinafsisha mashirika ya umeme na reli ziligonga mwamba kutokana na upinzani mkali ulioongozwa na wafanyakazi wa mashirika hayo. Pamoja na kubaki mikononi mwa dola, mashirika haya yameendelea kuhujumiwa ili yafe au yatoe faida kwa makampuni binafsi.
Hata vyuo vikuu?
Mafuru hakutenganisha aina hizi za taasisi na mashirika ya umma katika maagizo yake kwa wakuu wa mashirika hayo. Katika uelewa wake, ni kwamba taasisi na mashirika yote yanapaswa kujiendesha kibiashara na kutengeneza faida kama ilivyo katika sekta binafsi. Amevishambulia hata vyuo vikuu vya umma na kuvitaka vijiendeshe kibiashara kama ilivyo katika vyuo binafsi. “Kwa mfano Chuo Kikuu binafsi cha Tumaini, kinajiendesha kutokana na ada za wanafunzi pekee. Kwa nini IFM inashindwa kufanya hivyo?” Mafuru amenukuliwa akihoji.
Akijibu swali la Dk. Ng’wanza Kamata wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliyetaka kujua iwapo nchi inaweza kuwa na vyuo vikuu vya umma bila kuvigharimia, Mafuru alisema, katika mtandao wa twitter, kuwa vyuo vikuu vya umma “vinapaswa kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini. Tunavitaka kudahili wanafunzi wengi zaidi, kufanya tafiti na machapisho, pamoja na ushauri-elekezi ili vijiongezee mapato” (tafsiri yangu).
Kama nilivyodokeza hapo awali, vyuo vikuu vya umma tayari vinafanya biashara ya kuuza vyeti kama vilivyo vyuo binafsi. Yalipofanyika mageuzi ya uliberali mamboleo (neoliberal reforms), vyuo vikuu vya umma vilianza kutoza ada kwa wanafunzi, ada ambayo huendelea kupanda kila siku na hivyo kusababisha watoto wa maskini wasio na mikopo kuikosa elimu ya chuo kikuu. Pia viliongeza idadi ya wanafunzi toka mamia hadi makumi elfu bila kufanya utanuzi wa miundo mbinu wala kuongeza idadi ya walimu na vifaa vya kujifunzia. Aghalabu utawakuta wanafunzi elfu moja wakigombania kitabu kimoja katika maktaba, au wamebanana katika ukumbi wa mihadhara ulioandaliwa kwa ajili ya wanafunzi mia mbili.
Idara nyingi zimeanzisha programu za jioni kwa ajili ya vigogo wenye pesa ambao hulipa ada zaidi. Kauli-mbiu imekuwa “lipa pesa zaidi, tukupatie cheti cha digrii”. Mageuzi makubwa ya mtaala yalifanyika ili kuzalisha wanafunzi wauzikao sokoni. Soko halitaki watu wenye kujitambua, wanaohoji na kudai haki zao. Soko linahitaji “vimashine” vyenye kuzalisha bila kuhoji, na vyenye tamaa ya kujilimbikizia mali ambayo hata hivyo haiwezi kutimizika.
Hicho ambacho Mafuru anakiita consultancy, yaani ushauri-elekezi, kiuhalisia ni ukahaba wa kitaaluma (academic prostitution), ambao humfanya mwanataaluma kuuza usomi wao sokoni ili kujipatia pesa zaidi. Ukahaba wa kitaaluma sio tu kwamba umeua tafiti za kinadharia pamoja na kiu ya tafakuri, lakini pia umewafanya wanataaluma kutokuwa na muda kwa ajili ya wanafunzi wao.
Mageuzi yote hayo yamekwishafanyika katika vyuo vikuu vya umma na ndio sababu kubwa ya kuua kiwango cha taaluma vyuoni hapo. Hivi sasa vyuo vikuu havina tofauti na shule za ufundi mchundo, ambazo haziwafundishi wanafunzi kufikiri.
Tukutane juma lijalo kwa sehemu ya pili ya makala hii ambapo tutachambua kuhusu dhana na dhima ya kupunguza wafanyakazi katika sekta ya umma, pamoja na wasifu wa Lawrence Mafuru.
Mwandishi wa makala haya Mwl. Sabatho Nyamsenda ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com (link sends e-mail)