Madai kuwa Watanzania hawajui lugha ya Kimataifa, "English", si sahihi kwa asilimia mia. Lakini nakubali kuwa kuna Watanzania ambao kwa nafasi zao, walipaswa kufahamu Kizungu kwa ufasaha lakini kwa "bahati mbaya", imekuwa kinyume chake.
Wapo Watanzania wenye Elimu ndogo sana lakini wanaongea Kizungu kizuri utadhani wamekulia Uzungni, na kuna Watanzania wenye Elimu kubwa lakini "Vingereza" vyao ni vichekesho.
Kwa bara la Afrika, Tanzania ndilo Taifa linaloongoza kwa watu wake wengi kuongea Kiswahili. Ni Watanzania wachache sana, kama wapo, wasiofahamu Kiswahili.
Inafahamika hata kwa majirani zetu kuwa sisi tunafahamu Kiswahili. Lakini sisi tumeshajitadhmini katika hilo?
Kuna baadhi ya watu wanaosumbuliwa sana na matumizi ya R na L, madhalani, watu wa Kanda ya Ziwa na Pwani.
Utamkuta mtu anatamka neno "Buseru", lakini ukimwambia aandike, linakuwwa "Buselu". Mwingine atakuambia ametoka Isingiro, lakini kwenye maandishi, utalikuta Isingilo. Au Rwamgasa lakini akiandika linasomeka Lwamgasa. Mahali fulani, nikiambiwa kuna Sekondari inayoitwa Lubiri, lakini nilipofika maeneo hayo, nilikuta kibao chake kimeandikwa Lubili.
Mwingine, atataja jina la mtu kama Lama, lakini kwenye maandishi linaandikwa Rama.
Kurwa linatamkwa Kurwa, lakini kwenye maandishi, utalikuta Kulwa.
Mwingine, atatamka neno Mchele, lakini kwenye maandishi, ataandika "mchere".
Mwanzoni, nilifikiri hilo tatizo lipo kwa watu ambao hawajasoma.
Lakini sivyo, lipo na kwa wasomi wakiwemo Walimu.
Ikiwa Mwalimu anaongea na kuandika Kiswahili chenye matamshi "broken", si inaweza kuwa chanzo cha "ubroken" wa matamshi kuendelea kutamalaki kwenye Kiswahili?
Wakati mwingine, "ubroken" wa matamshi ya Kiswahili huathiri hata matamshi ya Kingereza. L hutumika sehemu ya R na R badala ya L.
Najua hata kama tutakidhiri kuongea Kiswahili "broken", majirani zetu hawataweza kutuzodoa katika hilo kama wanavyotusimanga kwenye Kizungu. Wataanzia wapi, hasa ikizingatiwa kuwa wako chali katika utumiaji wa hii lugha adhimu?
Pamoja na kwamba hatuna mshindani kwenye hii lugha nzuri, Kiswahili, isingekuwa vizuri zaidi kama tungeendelea kujiboresha zaidi na zaidi? Kwa nini kusingewekwa kigezo kuwa Walimu kuanzia Chekechea mpaka Sekondari sharti wawe na k3 fasaha?
Kuongea Kiswahili fasaha!
Kuandika Kiswahili fasaha!
Kusoma Kiswahili fasaha!
Naamini sababu mojawapo ya mwanafunzi Tanzania kumaliza Kidato cha Nne akiwa "hajui" Kizungu, ni kwa sababu Walimu wake nao "hawakijui". Isingekuwa vyema kama mamlaka husika ingehakikisha kuwa Walimu wote kuanzia Chekechea hadi "High School" wanafahamu kwa ufasaha Kiswahili cha kusoma, kuandika na kuongea?
Majirani zetu wamepata kile wanachokiita sababu halali ya kutukosoa kuwa hatujui Kizungu, na sisi tusijipe sababu yoyote ya kutokujua Kiswahili fasaha.