Wanamtumikia Mungu, CCM, Serikali au wananchi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wanamtumikia Mungu, CCM, Serikali au wananchi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by dosama, Jul 1, 2012.

 1. dosama

  dosama JF-Expert Member

  #1
  Jul 1, 2012
  Joined: Dec 25, 2010
  Messages: 786
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 35
  KWA tabia yake na kwa mazoea tangu alipoingia madarakani mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete “anapenda wagonjwa”.

  Kwa miaka takriban saba sasa, Watanzania wamemfahamu kama Rais aliye mwepesi wa kutembelea watu maarufu wanaoumizwa au wanaougua na kulazwa hospitalini. Wala hakosi kwenye misiba yao inapotokea.

  Lakini wiki hii, Rais ameshindwa kufika hospitalini kumjulia hali Dk. Steven Ulimboka, kiongozi wa mgomo wa madaktari, ambaye siku chache zilizopita alinusurika jaribio la kuuawa na watu ambao hawajulikana hadi sasa.

  Hata hivyo kwa kuwa Dk. Ulimboka amekuwa katika mgogoro na serikali tangu mwaka 2005, akiongoza harakati za kutetea maslahi ya madaktari na wagonjwa na katika mazingira ambamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisikika akisema “liwalo na liwe”, tayari hisia za watu wengi zinaelekeza kwamba waliomuumiza Dk. Ulimboka wana uhusiano na serikali; hili haliwezi kuiacha serikali salama.

  Ndiyo maana familia yake, jumuiya za wanaharakati na wanasiasa wasio wa CCM, wametamka wazi kwamba hawana imani na tume iliyoundwa na serikali kuchunguza mazingira na sababu za mkasa huu wa jaribio la kumuua Dk. Ulimboka. Na hawataki serikali ijihusishe na ugonjwa wake. Hawaiamini tena.

  Na Rais anajua kuwa yeye na serikali yake ni watuhumiwa; hawaaminiki, wala hawahitajiki katika kitanda cha mgonjwa huyu!

  Sababu kubwa ni kwamba kwa miaka isiyopungua sita sasa, Dk. Ulimboka amekuwa mmoja wa maadui wakubwa wa serikali.

  Matamko ya serikali, na vitisho vya serikali dhidi ya madaktari ni ishara mojawapo ya uadui huu kati yake na serikali.

  Na katika mazingira ambamo Dk. Ulimboka mwenyewe alidai juzi hospitalini kwamba amemtambua mmoja wa watesi wake akiwa katika ujumbe wa tume hiyo ilipomtembelea hospitalini, na kwa kuwa mtu huyo ni kiongozi mwandamizi wa jeshi la polisi, hatupati shida kuelewa kwa nini kiongozi mkuu wa serikali na watu wake hawajamtembelea hospitalini kama ilivyo mazoea.

  Ninazo taarifa za uhakika kwamba wakubwa hawa wameshindwa kwenda hospitali kwa sababu hawana uhakika na kinachoweza kuwatokea wakiwa kule.

  Hadi jana wakati mgonjwa anahamishwa kuepelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi, watawala hawakuwa na uhakika wa hisia na matendo ya wananchi dhidi yao iwapo wangeonekana katika mazingira ya hospitali alikokuwa amelazwa Dk. Ulimboka.

  Na katika mazingira ambao Rais juzi alirushiwa mawe katika zogo lisilomhusu, ni wazi kwamba hofu yake itakuwa imeongezeka mara dufu anapowaza masahibu yaliyompata Dk. Ulimboka.

  Hofu hii ya watawala inatuma ujumbe mzito katika mioyo na akili za Watanzania. Inaleta tafsiri tata katika jamii. Na haitatoka kirahisi, hata kwa propaganda zinazoanza kusambazwa kulilainisha suala hili.

  Ni hofu ile ile ambayo imeonekana pia Bungeni katika macho na kauli za Pinda na Spika Anne Makinda. Hawataki Bunge lijadili suala hilo, kwa kisingizo kwamba liko mahakamani.

  Pinda na Makinda wanagoma kulijadili huku wakijua kwamba mjadala wa matukio haya ya hivi karibuni hauna uhusiano na kesi iliyo mahakamani; na ndiyo maana vyombo vya habari vimeendelea kuandika habari hizo kila siku.

  Wanajua pia kwamba hata katika suala lililo mahakamani Bunge lina haki na mipaka ya kulijadili, bila kuingilia au kuathiri mwenendo wa kesi.

  Kwa makusudi au kwa kutojua, Makinda amejikuta akilizuia Bunge kufanya kazi ya kuisimamia serikali kama linavyotakiwa na Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

  Huku akitambua kuwa si kazi ya Bunge kuendekeza uzembe wa serikali; na huku akijua kuwa serikali ina mgogoro na madaktari, hivyo haiwezi kuamua mgogoro wake yenyewe, Makinda analizuia Bunge kuingilia kati na kuleta suluhu kati ya serikali na madaktari.

  Amefika mahali, akaanza kuwaita baadhi ya wabunge – hasa wa upinzani waliokuwa wanaomba mwongozo wake kuhusu suala hilo – kuwa ni “wabunge wa miongozo”. Kejeli!

  Hakuishia hapo, bali amekwenda mbali na kutoa maneno makali dhidi ya waandishi wa habari walio Bungeni, wanaoandika habari, makala na uchambuzi kuhusu mwenendo wa Bunge katika kikao kinachoendelea, akisema wanaandika “upuuzi.”

  Ni kauli ya kuudhi, ambayo haipaswi kutolewa na mtu wa haiba ya Spika; tena akiwa Bungeni, ambapo wabunge wanaoitoa wanakemewa na kuamriwa kuifuta! Spika ametumia kiti chake vibaya.

  Spika amefika mahali angependa waandishi waache kazi yao, wawe makarani wa kuandika kinachompendeza yeye. Wala haoni kama wanatekeleza majukumu yao kwa misingi ya kitaaluma, bali anaona hata kuwa kwao Bungeni ni upendeleo maalumu kwa ofisi yake.

  Na kauli ya Pinda kwamba wameshazungumza na mihimili mingine – mahakama na Bunge – maana yake ni kwamba mhimili mmoja (serikali) unaingilia mihimili mingine na kuamuru ifanye vile iache vile.

  Ni wazi kuwa hatua ya serikali kutumia mahakama mara kwa mara kuzima madai ya watumishi wanaodai haki zao kwa njia za kidemokrasia, na hatua ya kulinyamazisha Bunge kuhusu masuala nyeti kama haya, ni ishara ya kushindwa kwa serikali; ni udhaifu wa uongozi na udikteta usiotarajiwa katika zama hizi za demokrasia ya ushindani.

  Hatua ya Spika kunywea mbele ya serikali, na kutumia kanuni kulinyima Bunge fursa ya kuiwajibisha serikali, ni uthibitisho kwamba amekuwa mateka wa serikali. Maana yake ni kwamba mhimili wa Bunge haujitegemei tena, na umepoteza uwezo wa kuisimamia serikali.

  Haya nayo ni matumizi mabaya ya madaraka. Ni kigezo cha nyongeza katika madai yetu ya muda mrefu kwamba Spika asitokane na chama chochote cha siasa.

  Maana sasa imedhihirika kwamba Makinda anatumia fursa yake ya uspika kuitetea CCM; maana anajua kuwa kushindwa kwa serikali ni kushindwa kwa CCM.

  Katika wiki hii Spika ameonyesha ukali uliopitiliza dhidi ya wakosoaji wa CCM na serikali, kiasi cha kuwafanya wananchi wengi kuendelea kuona ukweli ulio katika kauli ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, kwamba “tumefika hapa kwa sababu ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na upuuzi wa CCM.”

  Naona kama amedhamiria kubariki uzembe wa Bunge, na kulifanya liwe nyonge mbele ya CCM na serikali.

  Yawezekana tabia hii ya Spika imekolezwa na “mazungumzo” ya serikali na mihimili mingine. Yawezekana anafanya kazi kwa maagizo ya serikali au chama chake.

  Anaweza kulizuia Bunge kujadili suala hili Bungeni. Anaweza kutumia kanuni, kwa tafsiri atakayo, kuzuia wabunge kuibana serikali. Anaweza kuruhusu hata majibu ya hovyo hovyo ya mawaziri kwa wabunge, kama walivyofanya juzi (Ijumaa) jioni.

  Lakini je, ataweza kuwazuia wananchi kuhoji suala hili? Anaweza kuwakejeli waandishi; lakini atafanikiwa kunyamazisha vyombo vyote vya habari?

  Je, anajua hasira na chuki anayopandikiza kwa wenye Bunge lao (wananchi)? Makinda na Pinda wataweza kuhimili kishindo kitokanacho na chuki hizi wanazopandikiza?

  Na wabunge wanaweza kunywea, wakatii amri, kanuni na vitisho vya serikali na Spika. Lakini Rais Kikwete, Pinda na Makinda kwa mwenendo huu na matokeo yake, wanamtumikia nani? Mungu? Serikali? CCM? Wananchi?

  Chanzo Tanzania Daima
   
 2. Return Of Undertaker

  Return Of Undertaker JF-Expert Member

  #2
  Jul 1, 2012
  Joined: Jun 12, 2012
  Messages: 2,376
  Likes Received: 8,524
  Trophy Points: 280
  Shetani
   
Loading...