Wanamashairi wenzangu, waandishi na wapenzi wa kusoma mashairi karibuni tuienzi fani yetu pendwa

YHK geneous

Senior Member
Jun 24, 2017
188
120
Uzi huu ni maalum kwa ajili wa waandishi na wapenzi wa kusoma mashari kuja hapa kujadiliana na kufundishana vitu mbalimbali kuhusu ushairi.

Karibuni jamani tushirikishane na tutunge mashairi mbalimbali bila kusahau swala la kupeana fursa mbalimbali za kiuandishi wa mashairi au nyimbo sehemu mbalimbali.

Karibuni tujifunze pamoja...

Natanguliza utunzi wangu hapa chini

NAREJEA KIAMBONI

Wakati umeshafika, Nirejee kiamboni.
Nimemaliza pirika, Nahitaji ahueni.
Majira yashakatika, ninafuraha moyoni.
Chengoni ni kiamboni, nami nimepakumbuka.

Gange zilinigubika, zikanitoa nyumbani.
Majukumu nikashika, Nikaondoka nchini.
Sasa leo imefika, Narudi mastakimuni.
Chengoni ni kiamboni, Nami nimepakumbuka.

Mtima umeridhika, bashasha tele moyoni.
Aila kuikumbuka, lakini hauioni.
Hilo nilishalichoka, ni huzuni fuadini.
Chengoni ni kiamboni, Nami nimepakumbuka.

Wengi niliwakumbuka, Wazazi ndugu jirani.
Na watoto kadhalika, marafiki kwa utani.
Ni vingi vya kukumbuka, usipokuwa nyumbani.
Chengoni ni kiamboni, Nami nimepakumbuka.

Naona nimeshafika, Acha niingie ndani.
Kwa safari nimechoka, naomba nikae chini.
Sasa nukta ninaweka, Nawaaga kwaherini.
Chengoni ni kiamboni, aghalabu kupachoka.
 
MIE SINA NDUGU DAR
Likizo yakaribia,tupo tunajiandaa,
Kila kona nasikia,wengi wataenda Dar,
Eti watatembelea,bahari kuishangaa,
Nami najifikirisha,kweli sina ndugu Dar.

Mawazo nayabadili, siendi tena nyumbani,
Ngoja nisake nauli, Dar nimepatamani,
Kichwani nina maswali,Dar naenda kwa nani,
Leo nimeshagundua,mie sina ndugu Dar.

Nikaone magholofa, barabara njia nane,
Nimuone Lodilofa, na Madenge nimuone,
Dully na Papa Misifa, kwa Mkapa nipaone,
Hivi ninaenda Dar, nitafikia kwa nani?

Mori niende ziwani,si lazima baharini,
Kulala vibarazani,bora si nipo jijini,
Foleni barabarani,kuliko kutwa shambani,
Mori sina ndugu Dar,najiendea nyumbani.

Utaenda kutalii,si leo badae sana,
Kiibiwa haulii,kikazana kusoma,
Ni tabu sikutanii,Dar watu wabanana,
Wote mna ndugu Dar,mie nataka kuanza.

Eti jiji la maraha,wengi wamo taabuni,
Wengi kwao ni karaha,hasa wale masikini,
Nitaomba msamaha,mlalao sebuleni,
Mie sina ndugu Dar,mwenzangu upo kwa nani?

Nijibu uniambie,waweza kunipokea,
Nikija usikimbie,si jiji umezoea,
Ukweli uniambie,au nawe wazamia,
Mie sina ndugu Dar,rafiki upo kwa nani?
 
SIKU NIMEENDA DAR

Kama nilovyowaambia, kuwa Dar sina ndugu,
Kuna mwana kasikia, kapata sana uchungu,
Njoo nitakupokea, usafishe macho ndugu,
Siku nimeenda Dar, nusura mie nidate.

Nikaipanga safari, mwakani mwezi wa tano,
Ni mbali kuwa jasiri, uje hata jumatano,
Nikamwambia subiri, naja fanya mapambano,
Siku nimeenda Dar, nusura mie nidate.

Nikakimbiza miezi, huku roho yanidunda,
Nikamwaga na mpenzi, hata nende takupenda,
Tena nikipata kazi, sote tunaweza kwenda,
Siku nimeenda Dar, nusura mie nidate.

Mola kajalia kazi, huku mwitako mkoani,
Kamwambia kiongozi, huko naja mwezi juni,
Akanijibu kwa pozi, utanikuta mjini,
Siku nimeenda Dar, nusura mie nidate.

Mei ikakaribia, nikamwambia rafiki,
Mwamba nikamwambia, naja akaniafiki,
Siku zikaja wadia, njoo mbona haufiki,
Siku nimeenda Dar, nusura mie nidate.

Nimeshakata tiketi, basi lafika sa kumi,
Ninunulie visheti, utapofika Mikumi,
Sisahau matikiti, wanauza kwa makumi,
Siku nimeenda Dar, nusura mie nidate.

Njiani naulizia, bado sana kuingia,
Kijana bado tulia, Mikese twakaribia,
Sikai kwa kutulia, begi nimekumbatia,
Siku nimeenda Dar, nusura mie nidate.

Nasoma kila kibao, huku natizama muda,
Naona kila kituo, yaani nakaa kwa shida,
Nawacheki washukao, na wale wauza soda,
Siku nimeenda Dar, nusura mie nidate.

Nilipofika Chalinze, nikapiga simu yake,
Kibaha muimalize, hapo karibu mfike,
Ukifika we nijuze, naja tuje tuondoke,
Nilipofika Dar, nusura mie nidate.
 
SIKU NIMEFIKA DAR

Sasa naiona Ubungo, taa na lile daraja,
Ninaizungusha shingo, najiona kama soja,
Mwizi akaona bingo, kumbe chini aningoja,
Siku nimefika Dar, niliona jiji chungu.

Huyu anavuta begi, yule kabeba tikiti,
Yule ananita bigi, twende Kawe kuna siti,
Nawaza Migi hapigi, yule begi kwenye buti,
Siku nimefika Dar, niliona jiji chungu.

Ngoja nichukue simu, nimpigie mwenyeji,
Simu ilikuwa humu, mwenyewe ninajihoji,
Na Migi namlaumu, muda wote mbona haji,
Siku nimefika Dar, niliona jiji chungu.

Nikavuta begi langu, tikiti nikaliacha,
Huku nikimwomba Mungu, isivunjike pakacha,
Lile chozi la uchungu, simu imeshaniacha,
Siku nimefika Dar, niliona jiji chungu.

Kuna mwana kaniona, nayumba kule na huku,
Twende nasema hapana, asije niona kuku,
Twende mwenyeji hauna, boda yangu iko huku,
Siku nimefika Dar, jiji nikaona chungu.

Nikamfwata bibie, yeye anauza soda,
Kipi nikusaidie, nikasema msaada,
Wataka uniibie, nitolee zako shida,
Siku nimefika Dar, jiji niliona chungu.

'Kajisogeza langoni, nikamsubiri Migi,
Naangaza simuoni, wapi yupo huyu bigi,
Nabaki kono shavuni, nikishangaa mawigi,
Siku nimefika Dar, jiji niliona chungu.

Kigiza kinaingia, wala Migi simuoni,
Woga waninyemelea, nimejingiza shimoni,
Begi nimeshikilia, nalificha kama mboni,
Siku nimefika Dar, jiji niliona chungu.
 
LEO UTALALA DAR

Jua lilinikimbia, kama linanikomoa,
Nikatamani kulia, pale waliponitoa,
Nani wamsubilia, ama watoka mkoa,
Leo utalala Dar, bwege mmoja abwabwaja.

Kweli Migi atakuja, kichwani najiuliza,
Leo ntakuwa kiroja, stendi nikijilaza,
Hata jamaa akija, atanionaje na giza,
Leo utalala Dar, sauti yajirudia.

Nikajikaza kiume, nina hela mfukoni,
Wahuni wasinizame, kuna nyumba za wageni,
Kuna vibao nisome, nisijeke mashakani,
Leo utalala Dar, nikawaza nikitoka.

Nikafika mapokezi, kulala ni bei gani,
Hatulazi majambazi, nikajibiwa kihuni,
Kumbe sina makubazi, niko peku miguuni,
Leo utalala Dar, ila siyo nyumba hii.

Nielekeze sehemu, nizilaze mbavu zangu,
Wewe ni mwendawazimu, ama mgeni mwenzangu,
Bwana akanituhumu, akinacha nende zangu,
Leo utalala Dar, ila kama una hela.

Nikalivuka daraja, mara kamwona mrembo,
Mbele yangu akaja, kaka mzuri vipi mambo,
Akanionesha paja, twende nikakupe mambo,
Leo utalala Dar, hili jiji la maraha.

Nikamuwaza Semeni, kwa nini alinikanya,
We kaka hauoni, vipi shepu umehanya?
Twende tulale ndani, upweke nitakuponya,
Leo utalala Dar, twende huku kipenzi.

Mara naona warembo, wanizonga kwa mapozi,
Isije ikawa chambo, nikajatekwa kipuzi,
Siyawezi haya mambo, nisiende kama mbuzi,
Leo utalala Dar, chunga usijeibiwa.
 
KILIMO CHENYE TIJA HUANZIA SOKONI

1. Tumekuwa tukilima, tangu mwanzo wa dunia,
Hatupati takirima, mavuno kujivunia,
Ni wapi tulipokwama, hadi tukakosa nia?
Kwa kilimo chenye tija, tunaanzia sokoni.

2. Unapolima shambani, unapaswa kukumbuka,
Na hata bustanini, kazi ya kuheshimika,
Kilimo bila plani, huwezi kusalimika,
Kwa kilimo chenye tija, tunaanzia sokoni.

3. Kulima bila kujua, utamuuzia nani,
Unakuwa umeamua, kujiumiza shambani,
Na mbegu za kukamua, bila tija asilani,
Kwa kilimo chenye tija, tunaanzia sokoni.

4. Hutapoteza chochote, kwa kutenga muda wako,
Tembea soko lolote, tafuta wateja wako,
Kimaliza hayo yote, rejea shambani kwako,
Kwa kilimo chenye tija, tunaanzia sokoni.

5. Iwe pilipili hoho, mahindi au karoti,
Usijiumize roho, ukayakosa manoti,
Siku utavaa joho, na kupigiwa saluti,
Kwa kilimo chenye tija, tunaanzia sokoni.

6. Yapo masoko lukuki, hapa Morogoro kati.
Kote yametamalaki, ujenzi wa mkakati,
Kabla hujahamaki, jiingize katikati,
Kwa kilimo chenye tija, tunaanzia sokoni.

7. Wakulima tupambane, tuzalishe kwa ubora,
Sio mpaka tukabane, au kupigwa bakora,
Lima mazao manene, yanayokidhi ubora,
Kwa kilimo chenye tija, tunaanzia sokoni.

8. Beti nane kaditama, hapa twatia kituo,
Yote tuliyoyasema, yafaa mchanganuo,
Tusianze kulalama, kilimo ni ufunguo,
Kwa kilimo chenye tija, tunaanzia sokoni.
 
NYEGE NI KUNYEGEZANA

Na Amiri A. S. Andanenga (Sauti ya Kiza)

Peni yangu Andanenga, uwino unapotona
Mantiki huzilenga, na balagha na bayana
Hufaidika malenga, huvurugika akina,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Msemo wa Kiswahili, nyege ni kunyegezana,
Maana yaki kamili, “wema ni kutendeana’,
Wasiojua fasili, hunamba nimetukana,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ni msemo maarufu, ambao shaka hauna,
Kwenye kamusi sanifu, funueni mtaona,
Niwezeje kukashifu, nami mwana muungwana!
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ninataja ukurasa, wazi hapa naunena,
Soma mbili moja tisa, soma bila ya fitina,
Msemo siyo wa sasa, si juzi licha wa jana,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ushairi kubwa fani, mithili yake haina,
Kujua zake bayani, yataka kikubwa kina
Muoneni mwafulani, hata kuku wamguna,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ulipotamkwa mlo, kaja akitunatuna,
Akakabwa koromelo, akabaki kugunaguna,
Kabakia lolololo, uzamani umechina,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Alhaji Jitukali, pokea pongezi tena,
Kikubwa chako kilili, hapandi yule mtwana,
Atuache tule wali, yeye ugali wa dona,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Kaditama wa Busara, na Mbwezi heko kijana,
Pongezi ndugu Kagera, Yobu has ante sana,
Ndimi Mshairi Bora, kipofu ninaeona,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Amir Sudi Andanenga
(Sauti ya kiza)
Dar Es Salaam.
 
HAKUNA KISO NA MWISHO.
*********************
Nyumba yetu ya jirani, walifiwa mwaka jana.
Zilitawala huzuni, nyuso zilikunjamana.
Leo wapo shereheni, wamuoza msichana.
Hakuna kiso na mwisho, kila jambo litapita.
*
Alofeli mtihani, kisha akachekwa sana.
Kifo akakitamani, kahisi thamani hana.
Kwenye siasa kawini, Mbunge mwenye dhamana.
Hakuna kiso na mwisho, kila jambo litapita.
*
Walogombana ndoani, mwishowe wakaachana.
Na hawasalimiani, hawataki kuonana.
Saa hizi wapo chumbani, huku wakichekeana.
Hakuna kiso na mwisho, kila jambo litapita.
*
Walomwita mlaini, mlegevu wamuona.
Kimaisha hatowini, adhihakiwa kijana.
Kwa sasa yupo jeshini, na mali zimejazana.
Hakuna kiso na mwisho kila jambo litapita.
*
Kama wewe muumini, mshukuru maulana.
Usiwalani wahuni, hubiri kiuungwana.
Utaja kuta peponi, wala saluwa wa manna.
Hakuna kiso na mwisho, kila kitu kitapita.
*************
Saidi M Sadiki (Sauti ya nyikani)
+255756429820
 
NYEGE NI KUNYEGEZANA

Na Amiri A. S. Andanenga (Sauti ya Kiza)

Peni yangu Andanenga, uwino unapotona
Mantiki huzilenga, na balagha na bayana
Hufaidika malenga, huvurugika akina,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Msemo wa Kiswahili, nyege ni kunyegezana,
Maana yaki kamili, “wema ni kutendeana’,
Wasiojua fasili, hunamba nimetukana,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ni msemo maarufu, ambao shaka hauna,
Kwenye kamusi sanifu, funueni mtaona,
Niwezeje kukashifu, nami mwana muungwana!
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ninataja ukurasa, wazi hapa naunena,
Soma mbili moja tisa, soma bila ya fitina,
Msemo siyo wa sasa, si juzi licha wa jana,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ushairi kubwa fani, mithili yake haina,
Kujua zake bayani, yataka kikubwa kina
Muoneni mwafulani, hata kuku wamguna,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ulipotamkwa mlo, kaja akitunatuna,
Akakabwa koromelo, akabaki kugunaguna,
Kabakia lolololo, uzamani umechina,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Alhaji Jitukali, pokea pongezi tena,
Kikubwa chako kilili, hapandi yule mtwana,
Atuache tule wali, yeye ugali wa dona,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Kaditama wa Busara, na Mbwezi heko kijana,
Pongezi ndugu Kagera, Yobu has ante sana,
Ndimi Mshairi Bora, kipofu ninaeona,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Amir Sudi Andanenga
(Sauti ya kiza)
Dar Es Salaam.

Hiiii shairi ni nzuri sana... nimependa uandishi huu ingawa kule mwishoni nkaona tayari umehama kwenye mada husika na kuongelea mambo mengine kabisa.... anyway tuendelee kufundishana ndugu yangu...
 
HAKUNA KISO NA MWISHO.
*********************
Nyumba yetu ya jirani, walifiwa mwaka jana.
Zilitawala huzuni, nyuso zilikunjamana.
Leo wapo shereheni, wamuoza msichana.
Hakuna kiso na mwisho, kila jambo litapita.
*
Alofeli mtihani, kisha akachekwa sana.
Kifo akakitamani, kahisi thamani hana.
Kwenye siasa kawini, Mbunge mwenye dhamana.
Hakuna kiso na mwisho, kila jambo litapita.
*
Walogombana ndoani, mwishowe wakaachana.
Na hawasalimiani, hawataki kuonana.
Saa hizi wapo chumbani, huku wakichekeana.
Hakuna kiso na mwisho, kila jambo litapita.
*
Walomwita mlaini, mlegevu wamuona.
Kimaisha hatowini, adhihakiwa kijana.
Kwa sasa yupo jeshini, na mali zimejazana.
Hakuna kiso na mwisho kila jambo litapita.
*
Kama wewe muumini, mshukuru maulana.
Usiwalani wahuni, hubiri kiuungwana.
Utaja kuta peponi, wala saluwa wa manna.
Hakuna kiso na mwisho, kila kitu kitapita.
*************
Saidi M Sadiki (Sauti ya nyikani)
+255756429820

Malenga nakupongeza, Umenena yalomana.
Vizuri umeeleza, Na mifano tumeona.
Si kama umeoweza, utunzio umefana.
Walau tumeshaona, kwayo uloyasogeza.

Kwayo uloyasogeza, Walautumeyaona.
Ulumbi umeuweza, Mizani imeshikana.
Kwa vina unateleza, Na ujumbe umefana.
Walau tumeshaona, Kwayo uloyasogeza.

Japo swali latatiza, Kichwani linagongana.
Radhi nitatanguliza, usije kunitukana.
Naogopa kuuliza, pengine tutakosana.
Walau tumeshaona, kwayo uloyasogeza.

Ngoja nije kuuliza, nami nipate maana.
Janabi sauti kiza, kwayo ndiwe wake mwana?
Na kama sivyo' eleza, Sote tupate maana.
Walau tumeshaona, Kwayo uloyasogeza.
 
BIASHARA

Biashara ni sanaa, sanaa ya kutafuta.
Kutafuta ni kujua, kukosa au kupata.
Kukosa si kukosea, ndugu usije kujuta.
Biashara ni sanaa, kukosa au kupata.

Biashara ni kujua, nini wanachotafuta.
Watakacho ukijua, peke anza kutafuta.
Jawabu uking'amua, faida utaipata.
Biashara ni sanaa, kukosa au kupata.

Biashara ikimea, ajira hutotafuta.
Ajira utakataa, Faidae ukipata.
Biashara ukijiua, ajira hutoifata.
Biashara ni sanaa, kukosa au kupata.

Biashara kuchagua, amini kwenye kupata.
Jema ukitegemea, hakika litakupata.
Faida ikijongea, hasara hutoipata.
Biashara ni sanaa, kukosa au kupata.

Na hasara hutokea, maranyingi huijuta.
Hasara huibomoa, faida kutoipata.
Hasara ni kutokea, kukosa kwenye kupata.
Biashara ni sanaa, kukosa au kupata.

Hasara ikitokea, ujuzi utaupata.
Hasara ni kukataa, biashara ukipata.
Hasara inatokea, hutokea na kupita.
Biashara ni sanaa, kukosa au kupata.

Hapa nanga ninatia, kwanza wakati ukuta.
Lengo limeshatimia, tungo natia nukuta.
Biashara ikimea, ajira pia hufata.
Biashara ni sanaa, kukosa au kupata.


2023
MwanaFikra Maridhawa
Y.H.K
Mbagala, Dar es Salaam, Tanzania.
+ 255 (0) 757 028103
halidiyusuph@yahoo.com
 
Mbona umenikataa?

Mitindo yangu kisasa, napendeza ninang'aa
Ninaishi kwa anasa, ninakula ninavaa
Nina nyumba na verosa, na madege ya kupaa
MBONA UMENIKATAA,KIPI KWANGU UTAKOSA?


kipi kwangu utakosa, mbona umenikataa,
Hali nimetoa posa, na vikao vimekaa
kwako nimeshajitosa, moyo wangu umejaa
TONGE NIMESHA LITWAA, VINATOKA WAPI VISA?

Vinatoka wapi visa,tonge nimeshalitwaa
kwako nimeweka hisa, moyo wanienda paa
Hayo yote yawe tisa, kumi kwako nishakaa
WANIACHA NA BUTWAA, KIPI KISA NA MKASA?

Kipi kisa na mkasa, waniacha na butwaa,
Ujapo kuwa ni tasa, usiyeweza kuzaa
kwako nimekwisha nasa, kuwa mke unafaa,
KIPI KIMEKUHADAA , UWE MBALI NAMI HASA?
 
Back
Top Bottom