Walimu wahamishia familia kwa mwajiri

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
JUMLA ya walimu 12 na familia zao wa shule ya sekondari Mkandawile, Kata ya Chanika Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, wamehamishia makazi yao kwa
Mkurugenzi wa shule hiyo Bw. Alphonce Mkandawile.

Walimu hao wamefikia hatua hiyo baada ya kufanya kazi kwa miezi saba bila kulipwa mishahara yao huku wengine 19 wakilazimika kuacha kazi kutokana na maisha magumu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, nyumbani kwa Bw. Mkandawile kwa niaba ya walimu wenzake Makamu Mkuu wa shule hiyo Bw. Michael Sigore, alisema wanamdai Mkurugenzi huyo jumla ya sh. milioni 43 kama malimbikizi ya mishahara yao kuanzia mwezi Julai mwaka jana.

Alisema kitendo cha kuhamishia makazi yao kwa mmiliki huyo wa shule kunatokana na kushindwa kutekeleza makubaliano ya kikao cha pamoja kilichofanyika Oktoba 4, 2010.

Alisema katika kikao hicho walikubaliana kulipwa malimbikizo hayo ifikapo Oktoba 6 lakini tangu siku hiyo hakuweza kuonekana tena shuleni hapo hadi jana.

Alisema baada ya kuhamia kwake Januari 2, mwaka huu walimpata mke wake Bi. Stella Mkandawile, ambaye awali aliwakaribisha kabla ya kujua kiini cha shida yao.

Alisema baada ya wao kueleza wanachotaka Bi. Mkandawile aliwataka waondoke katika eneo la mji wake.

Alisema baada ya wao kuondoka ndani mwake Mama huyo alifunga mlango na kuhamia pasipojulikana huku akitoa lugha za vitisho kwao na familia zao.

Alisema baada ya kufukuzwa waliamua kuishi nje wakiwa wamefunga vyandarua juu ya miti na kutandika magodoro chini wakisubiri ujira wao.

Alisema wataendelea kuishi hapo hadi watakapolipwa fedha wanazodai na kuiomba serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru maisha yao pamoja na kufunga shule hiyo.

Alisema hawana pa kwenda kwa sasa kwa kuwa tayari wamefukuzwa katika nyumba walizokuwa wamepanga baada ya kushindwa kulipa kodi.

Majira ilishuhudia walimu hao na familia zao wakiwa wametandika godoro zao chini wakiendelea kuandaa chakula walichodai ni msaada kutoka kwa wasamaria wema.

Alisema shule hiyo iliwahi kusimamishiwa mitihani ya kidato cha pili kutokana na kukosa vigezo hivyo kulazimua wanafunzi 37 kuhamishiwa katika shule ya Sekondari ya Halisi iliyo jirani na shule ya Mkandawile.

Akijibu madai hayo kwa njia ya simu akiwa Mbeya Bw. Mkandawile alikiri kuwepo kwa madai ya walimu hao huku akisisitiza kwamba shule hiyo ipo chini ya Benki ya CRDB na Kampuni ya udalali wa Majembe ya Jijini Dar es Salaam.

Alisema shule hiyo ilipokonywa kutokana na deni lanye thamani ya zaidi ya milioni 970 alilokuwa akidaiwa.

"Mmmiliki wa shule kwa muda huu sio mimi bali ni Benki ya CRDB na Majembe, nilijiondoa tangu Disemba mwaka jana, walimu hao kuhamia kwangu nawashangaa, shule haipo kwangu na sio yangu.

"Nawaona kama wageni wangu na ndio maana nimeagiza mke wangu awakaribishe ingawa hivi sasa hayupo hapo baada ya kupata msiba wa shangazi yake Ubungo,"alisema Bw. Mkandawile

Alisema hivi sasa shule hiyo haina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne na kwamba waliopo ni kidato cha sita ambao tayari walisajiliwa kufanya mtihani wa mwisho mwezi Februari mwaka huu.
 
Back
Top Bottom