esther mashiker
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 616
- 555
ZAIDI ya wakulima 10,000 katika mikoa 11 nchini, chini ya uendeshaji wa vikundi vya kilimo kupitia Shirika la Misaada la Makanisa Duniani (NCA) watanufaika na kilimo bora kinachokabiliana na magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao.
Utaalamu wa kilimo hicho utatekelezwa kwa unyunyiziaji wa dawa mashambani kupitia teknolojia ya kurusha ndege zisizo na rubani ‘Drone’ ambapo mbolea na sumu ya wadudu itapigwa katika mashamba ili kuokoa mazao yasiharibike. Meneja mradi wa NCA, Gilbert Mworia alisema mpango hayo jana mjini hapa na kusema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano na timu ya wataalamu wa kilimo na wasomi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Cha Sokoine (SUA) kupitia ushirika wao wa Sokoine University Graduates Cooperative (SUGECO) ambao watatoa elimu kwa wakulima na kuuratibu.
Mworia alisema hayo katika kikao cha kupokea ripoti za vikundi vya benki za kijami visivyo katika mrengo wa kidini kanda ya Kaskazini chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, kilichofanyika Moshi. Alisema katika msimu uliopita zaidi ya wakulima 3,000 walikabiliana na changamoto ya mashamba yao hususani ya mahindi kuvamiwa na wadudu aina ya viwavijeshi na kwamba kuwapo kwa teknolojia ya ‘Drone’ ni suluhisho. “Mpango huu tutaufanya kwa majaribio wilaya za Mvomero na Kilombero mkoani Morogoro kuanzia Januari 23 na 24 mwaka 2019...itagharimu zaidi ya milioni 40, hii tumeitoa nchini Afrika Kusini,” alisema.
Alisema tayari mipango imefanyika kuomba kibali Mamlaka ya usari wa Anga Tanzania (TCAA) kwa ajili ya kurusha angani teknolojia hiyo huku pia wakiishirikisha wizara ya kilimo, chakula na ushirika kwa ajili ya vibali na taarifa zaidi. Awali mratibu wa mradi huo, Kanda ya Kaskazini, Mchungaji Andrew Munisi alisema kuna vikundi 473 ambavyo vimebadili hali za maisha za wanachama wao katika kujiimarisha kiuchumi. “Tumeanzisha vikundi vingi na vyote vinafanyakazi vizuri, tumelenga zaidi kuwawesha vijana maana waliachwa nyuma sana,” alisema. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Athur Shoo alitaka vikundi vya ujasiriamali kuwa wabunifu katika miradi na suala la kuwa na ushirikiano wa pamoja ili kupata soko la uhakika la bidhaa watakazozalisha