Wafanyakazi wachapwa viboko na Mwajiri

Bilionea Asigwa

JF-Expert Member
Sep 21, 2011
16,515
28,504
Wafanyakazi wa Kampuni ya Usangu Logistics ya jijini Dar es Slaam wameilalamikia serikali kutokana na kampuni hiyo kuwachapa bakora, kufukuzwa kazi kinyume cha sheria na kunyimwa stahiki.

Wanasema mwajiri wao mwenye asili ya Kiarabu, amekuwa akiwachapa bakora na kuwakata mishahara bila sababu za msingi, akiwarejesha kwenye historia ya utawala wa kikoloni, jambo ambalo halina nafasi kwenye Serikali ya kutetea wanyonge ya Rais Dk. John Magufuli.Wameieleza JAMHURI kwamba kesi walizozifungua awali kuhusu kunyanyaswa na kuporwa haki zao ikiwamo mishahara, wanakusudia kuzifungua upya kwa kuwa sasa wana imani kubwa na utawala wa Rais Dk. Magufuli.

“Tuna familia zetu hadi wajukuu, tumeingizwa tena katika utumwa huu wa kuchapwa bakora na Waarabu hawa waliokuwa wakilindwa na baadhi ya watendaji katika utawala uliopita, na sasa hatutakubali kudhalilishwa namna hii,” ameeleza mmoja wa wafanyakazi hao.

Waliochapwa viboko na wamiliki wa kampuni hiyo ni Langson Nyansulu na Ali Dauda na kufungua mashauri yao mahakamani mwaka 2013.

Wengine ni Sam Mwakarobo, Joseph, Augustine Msigwa ambao ni madereva waliofungua mashauri yao mahakamani mwaka 2015 ambayo hayajapatiwa ufumbuzi hadi sasa.

Wanasema watendaji wengi katika Serikali zilizopita walikuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa kuwanyima haki, kwa sababu za kuendekeza kile kinachodhaniwa kuwa kurubuniwa kwa rushwa na maslahi binafsi.

Wafanyakazi hao wameeleza kuwa wamekuwa wakipeleka malalamiko Kituo cha Polisi cha Buguruni, Dar es Salaam, Wizara ya Kazi, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa zaidi ya kusikia kuwa baadhi ya maafisa wamekuwa wakipewa fedha na kutochukua hatua zozote na kuwaacha wanaotoa taarifa za manyanyaso wakifukuzwa kazi bila utaratibu.

Baadhi ya wafanyakazi wameeleza kwamba uongozi wa kampuni hiyo umeanza kuwapa vitisho na kuwasaka waliotoa habari kuhusu manyanyasho na ukwepaji wa kodi kwa kutumia namba za magari za bandia.

Kampuni hiyo pia imedaiwa kujihusisha na ukwepaji wa kodi za Serikali kwa kutumia namba bandia za magari ambazo zimekuwa zikibadilishwa mara kwa mara na kuiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuchunguza na kudai kodi yote iliyokwepwa na kwamba wako tayari kutoa ushahidi.

Wanasema Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Ibrahim Ismail, amekuwa akiwakata Sh 25,000 kila mfanyakazi (Red payment voucher) na haijulikani anakopeleka makato hayo.

“Kwa upande wa mafundi akitoa maelekezo ya kutengeneza gari na tukichelewa kukamilisha kwa muda anaoutaka yeye, anatukata mshahara kila mmoja Sh 200,000 na kwa watu watano anachukua milioni moja au zaidi.

“Mishahara yetu ni midogo, wengine tunalipwa Sh 150,000 hadi Sh 250,000 kwa mwezi ambazo anatudhulumu kwa madai ya kutuadhibu kwa kutokamilisha matengenezo ya magari kwa muda aliotupangia na pia hutuchapa viboko kama wanyama. Tunateswa mno Watanzania na watu hawa,” ameeleza mfanyakazi mmoja.

Wanadai kampuni hiyo inasafirisha mafuta ya petroli na bidhaa mbalimbali nchi za Afrika Mashariki na Kusini, lakini katika hali ya kushangaza wakati wa kupakia mizigo magari hayo hubandikwa namba bandia.

“Ubadilishaji huo wa namba za magari hufanyika wakati wote wa safari ikiwa ni ukwepaji wa kodi za Serikali,” anasema mmoja wa wafanyakazi.

Vyanzo vya habari kutoka TRA vimeeleza kwamba uchunguzi dhidi ya kampuni hiyo kukwepa kodi na kumiliki namba bandia za magari unafanyika, na ikibainika hatua zitachukuliwa mara moja dhidi ya wahusika.

Chanzo: Jamhuri
 
Ningekuwa mm hao walionicharaza muda huu wameshawatolea heshima za mwisho
 
Ningekuwa mm hao walionicharaza muda huu wameshawatolea heshima za mwisho
Hizo bakora wanachapwa kwa hiyari au huyo mwarabu anakuwa na mabaunsa wanamkamata mfanyakazi kwa nguvu wanamlaza chini halafu mwarabu anacharaza bakora? Maana baada ya kucharazwa bakora wanaenda polisi. Ufafanuzi kwa mliocharazwa tafadhari.
 
Aiseee kumbe Tanzania bado haya mambo yapo... ila watz sisi no wavivu(baadhi yetu)
 
Back
Top Bottom