Huo utakuwa ni ushahidi wa jinsi TFF na Kamati yake ya Ligi zinavyofanya kazi kwa mazowea (ya kuviburuza vilabu) na kwa zinavyojisikia (au wanaowatuma wanavyojisikia). Haiwezekani kubadilisha kanuni ndani ya kipindi cha usajili, hasa ambao umeongezwa muda bila ya kutolewa maelezo. Haiwezekani kwa sababu:
1. Katiba, sera, sheria, kanuni, na taratibu hutungwa na wanadamu kwa ajili ya wanadamu. Ili iwe hivyo, ni lazima watumiaji na wasimamiaji wa miongozo hiyo washiriki na kushirikishwa. Ndio maana sheria za nchi yoyote hutungwa na wananchi kupitia wawakilishi wao bungeni, hata kama mchakato utaanzishwa na wasimamizi watarajiwa wa sheria hizo. TFF na Kamati ya Ligi ni wasimamizi tu wa kanuni inayosemekana kutaka kupitishwa. Ni lazima kwanza watumiaji (vilabu) wa kanuni hiyo waijadili na kuiridhia.
2. Mpaka msimu wa 2014/15 unaingia, wazo lilikuwa ni kupunguza wachezaji wa kigeni kutoka 5 hadi 3. Inakisiwa Yanga walichelewa kumpa mkataba mpya Kavumbagu kwa kuchelea mabadiliko hayo. Inasemekana Yanga walifikia hatua ya kuomba ufafanuzi juu ya hilo, kwa bahati mbaya hawakujibiwa kwa wakati. Baadaye TFF ikaridhia kubaki na haohao 5. Ndio kusema tayari TFF ilikwishapitisha kanuni hiyo kwa ajili ya msimu huo. Itashangaza kusikia kanuni hiyohiyo moja kubadilishwa mara mbili ndani ya msimu huohuo mmoja.
3. Usajili ni kujipanga, ni mawindo. Na mawindo ni kunyatia, huwezi kukamata windo kwa kukukurupuka wala kukurupushwa. Vilabu vyote vilikwishajipanga, vilikwishaingia mawindoni, vilikwishanyatia usajili kwa kanuni ya wageni 5. Kuongeza 2 zaidi ni kuvichanganya vilabu, na hakutavisaidia. Haitamsaidia duma aliyekwishalenga kumfukuza swala iwapo ngiri atakatisha ghafla katikati yao.
4. Kauli ya Kiingereza kuhusu kubadili vigezo ghafla katikati ya utekelezaji imetolewa kutoka kwenye medani ya soka: changing the goal post. Itasikitisha iwapo mchezo wa soka wenyewe ndio utaitumia kauli hiyo kupitia marekebisho ya kanuni katikati ya mchakato wa usajili. A football federation changing the goal-post?
5. Mimi ni muumini wa dhana ya soko huria kwenye ligi, kwa maana ya kuruhusu idadi yoyote ya wachezaji wa kigeni. Kama kulivyo na mkono usioonekana (the invisible hand) kwenye soko huria, unaosawazisha uwiano wa uzalishaji na bei, ndivyo kuwepo kwa ushindani wa wachezaji kutavyosawazisha uwiano wa viwango vya wachezaji wetu wa ndani na soko lao kitaifa na kimataifa.Lakini mimi si muumini wa kufanya mambo kiwogawoga, kisirisiri, kiujanjaujanja. TFF ivishirikishe vilabu kuamua hilo kwa misimu ijayo, siyo katikati ya msimu huu ambao kanuni ihusuyo hilo ilikwishabarikiwa na TFF hiihi.
Nilikwishaeleza kutovutiwa kwangu na uongozi wa Malinzi tangu siku anachaguliwa. Nikamwomba kupitia Jukwaa hilihili kuusuta wasiwasi wangu huo kupitia utendaji wake. Iwapo hili la kubadili kanuni katikati ya msimu litasibu, wasiwasi wangu kuhusu utendaji wake utakuwa umepata muhimili wa kuegemea.