Wabunge: Wasaliti wa watanzania. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wabunge: Wasaliti wa watanzania.

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by amn, Jul 9, 2011.

 1. a

  amn Member

  #1
  Jul 9, 2011
  Joined: Jul 6, 2011
  Messages: 11
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  WABUNGE: WASALITI WA WATANZANIA.

  Nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu sana mjadala wa bajeti ya serikali
  unaoendelea huko bungeni mjini Dodoma.
  Miongoni mwa hoja zinazochukua sehemu kubwa ya mjadala ni suala la
  posho, na kwa kweli hili limeshajadiliwa na wadau mbalimbali hapa
  nchini.
  Nami nimeamua nijitose kwenye mjadala huu ili nipate kujenga msingi
  wa hoja yangu.

  Nianze kwa kuangalia aina mbili za posho kati ya 10 wanazopata wabunge
  wetu ambazo kwa mtazamo wangu zinachangia kwa kiasi kikubwa usaliti wa
  wabunge kwa watanzania.

  1. Sitting allowance (Posho ya kuhudhulia vikao vya bunge)
  2. fuel allowance (Posho ya mafuta).

  Niweke wazi kwamba nilikuwa sijui kuna jumla ya posho zote hizo, mpaka
  nilipomsikia waziri mkuu akizitaja siku alipohitimisha mjadala wa
  bajeti ya ofisi yake.

  1. Posho ya kuhudhulia kikao (sitting allowance).
  Ni dhahili hakuna mantiki ya kuwepo posho hii kwa sababu wabunge
  wanakuwa wanatimiza wajibu wao kama ambavyo kila mtumishi wa serikali
  anavyotimiza wajibu wake. Hii ni aina fulani ya rushwa/ushawishi na ni
  matumizi mabaya ya fedha za umma.

  Tulimsikia waziri mkuu akitolea maelezo; eti posho yenyewe ya kikao
  inayolalamikiwa ni kidogo ni kama Tsh. 4.4bilion kama nilimnukuu
  vizuri; hii ni kejeli kwa watanzania na kama ingekuwa ni kwenye nchi
  za wenzetu zenye utawala bora waziri mkuu angekuwa ameshajiuzulu kwa
  kudharau wananchi wake; kwangu mimi udogo au ukubwa wa hiyo posho si
  hoja, hoja ni matumizi mazuri ya kodi na rasilimali za watanzania.
  Hata kama ingekuwa ni shilingi moja; haramu ni haramu tu na mbaya
  zaidi imetengenezewa sheria ili kuhalalisha wizi wa kodi ya mtanzania.
  Naomba kumkumbusha waziri mkuu kwamba tulishawahi kuwa na sheria ya
  TAKRIMA ambayo ilikuwa haramu na ilifutwa.

  Ukija kwenye posho ya mafuta ya gari zao hapo ndipo kwenye kichekesho
  kingine, bei ya mafuta ya petrol/dizel ndiyo kwanza iko tsh. 2,100/=
  kwa lita moja, lakini posho ya mbunge kwa lita moja ya mafuta ni tsh.
  2,500/=. Na hizi siyo kwamba ndio wameanza kupewa hivi karibuni,
  zimekuwepo tangu siku nyingi hata kabla bei halisi ya mafuta
  haijapanda kama ilivyo hivi sasa.


  Ukujiuliza hii tofauti ya bei halisi ya mafuta hapa nchini na posho
  wanazopata (unaweza ukaiita chenji ya mafuta) ni kitu gani kama siyo
  rushwa/ushawishi kwa wabunge wetu? Leo hii wabunge wetu wanakwenda
  uingereza kufuatilia chenji ya rada kana kwamba waingereza walikuja
  kuvunja hazina yetu; kama ningekuwa ndiyo serikali ya Uingereza sharti
  namba moja ambalo ningeipa serikali ya Tanzania ili kurudisha chenji
  ya rada ni kuhakikisha wale wote waliohusika na ufisadi huu wako ndani
  ya mikono ya sheria; halafu ndiyo mambo mengine yatafuatia. Wabunge
  wetu waanze kujivua magamba na kufikiria kurudisha posho zote haramu
  walizopokea kwa kutumia sheria walizojitungia isivyo halali; Wabunge
  wetu watapata wapi ujasiri wa kuhoji ongezeko la mara kwa mara la
  mafuta wakati wao mpaka leo hii wakienda na posho ya mafuta kwenye
  vituo vya mafuta wanarudishiwa chenji? Kama huu si usaliti kwa
  watanzania ni kitu gani?

  Kwa mtazamo wangu hizi zote ni rushwa/ushawishi kwa wabunge wetu
  ambazo zina athari mbili kwa watanzania:
  Kwanza ni ufujaji wa fedha za walipakodi maskini wa tanzania na
  ukiangalia kwa undani utagundua kwamba hii ni aina nyingine ya ufisadi
  kama ulivyo ufisadi mwingine wowote unaopigiwa kelele na watanzania,
  kwa hili watanzania lazima tuamke tushikamane tuanze kudai chenji
  zetu, ziko chenji nyingi tunazotakiwa turudishiwe siyo ya rada tu,
  tuanze na hizi za posho haramu.

  Na kama wabunge wetu ni wazalendo kwelikweli wanapaswa warudishe
  malipo yote waliyopokea isivyo halali hata kama kisheria yako sawa.
  Hata kama waziri mkuu anasema posho zipo kisheria lakini atambue
  kwamba siyo sheria zote ni halali.

  Lakini athari ya pili na hii ndiyo mbaya zaidi ni kupunguza ufanisi wa
  wabunge wetu katika kutimiza wajibu wao wa kuisimamia serikali. Na
  hakuna ufisadi mkubwa unaofanyika nchi hii kama huu wanaofanyiwa
  wabunge wetu (kutokuwa na ufanisi).

  Hivi unatekelezaje jukumu la kuisimamia serikali kwa ufanisi
  unaotegemewa wakati tayari ulishachukua posho haramu?

  Matokeo yake ndiyo haya tunayoyaona mpaka leo; ufisadi wa rada,
  ufisadi wa EPA, ufisadi wa meremeta, deepgreen, ufisadi wa IPTL,
  ufisadi wa richmond/dowans na mwingine mwingi tu; kwa mfano nchi iko
  kwenye mgawo mkubwa sana wa umeme; kwa sababu zaidi ya miaka kumi
  sasa serikali imekuwa inaleta bungeni mipango ya kuongeza nishati ya
  umeme wakati haiitekelezi na wabunge kwa sababu wanachukua posho
  haramu ndiyo maana wanakosa ujasiri wa kufuatilia utekelezaji wake.
  Hali ni hiyo hiyo kwenye kilimo ndiyo maana tunaona karibu kila mbunge
  anayesimama kuchangia bungeni lazima azungumzie njaa kwenye jimbo
  lake, mara utawasikia wakisema wakulima wetu hawapati mbolea na
  pembejeo, na hata wakizipata huwa zimechakachuliwa na hii maana yake
  ni kwamba utekelezaji wa mipango mingi ya kilimo haipo au si halisi
  ila kwa sababu tayari walishatia ndani posho haramu wabunge wetu
  wanaishia kupiga makofi pasipo kufikiri kwa ufanisi.
  Mifano iko mingi sana, nenda kwenye sekta ya afya kila mbunge
  anayechangia analilia zahanati, vituo vya afya, hakuna madawa kwenye
  vituo vya afya huku tunaambiwa yanaharibika huko MSD nakadharika.
  Ukienda kwenye sekta ya maji, miundombinu ya barabara mambo ni
  hayohayo. Haya yote yanatokea huku wabunge wetu hasa wa CCM kila
  wanaposimama kuchangia hoja za serikali wanaziunga mkono, sasa mtu
  unajiuliza unaunga mkono hoja za serikali huku unalalamika wananchi
  wako wana njaa, hawana maji, barabara mbovu, utawasikia wengine
  wakilalamikia miundombinu ya umeme na maji inapita majimboni mwao
  wakati wananchi wao hawana umeme.
  Na sasa hivi nimesikia wabunge wetu mmeridhia bei ya mafuta ya taa
  kupanda eti ili kuzuia uchakachuaji, kwa hili mimi naona mmetuongezea
  watanzania maskini ugumu wa maisha, hilo ongezeko la bei ya mafuta
  litaliwa na mafisadi; kesho na keshokutwa mtarudi tena bungeni kuanza
  kuipigia kelele serikali.

  Kwenye kikao cha bajeti kinachoendelea nilibahatika kufuatilia
  majadiliano kuhusu CHC (Consolidated Holding Corperation),
  ukimsikiliza mwenyekiti wa kamati ya bunge ya mashirika ya umma ndugu
  Zitto Kabwe na mbunge wa Mwibara huko Bunda ndugu Kange Lugola
  wanavyozungumzia kwa uchungu uozo, ubadhilifu/ wizi/ ufisadi mkubwa na
  wa kutisha uliopo kwenye hayo mashirika yetu ya umma kwa haraka haraka
  mtu unaweza kufikiria ni kama mashirika yetu yamekabidhiwa
  majambazi/mijizi na mibakauchumi wa watanzania;
  lakini hayo yote yanatokea wakati tuna wabunge wetu ambao tumewapa
  kazi ya kuisimamia serikali hawafanyi kazi yao ipasavyo; kwa nini
  tusiseme kwamba ni kwa sababu ya hizi posho haramu ndiyo maana
  wanafumbia macho wizi mkubwa unaofanywa kwa ushirikiano wa viongozi wa
  serikali yetu na hao waliopewa kuyaendesha.
  Halafu nimesikia kwamba hiyo kamati ya bunge anayoiyongoza Zitto
  inasimamia yale mashirika ya umma ambayo serikali ina hisa za asilimia
  50 na zaidi; yale yote yaliyo na chini ya asilimia 50 wabunge wetu
  hawana taarifa ya nini kinafanyika huku. Hapa kuna matatizo makubwa
  sana kwa wabunge wetu na huu ni usaliti kwa watanzania maskini ambao
  tumewapa dhamana ya kuzisimamia rasilimali zetu. Wabunge wetu hebu
  jiulizeni; kama huko mnakoweza kuchungulia (kwenye zaidi ya asilimia
  50) mambo yako hivyo, je huko ambako mmepigwa marufuku kuchungulia
  mambo yakoje? Kwa nini tusiseme haya yote hamyaoni kwa sababu ya posho
  haramu mnazopokea. Wabunge kumbukeni kwamba mna wajibu na ni haki yenu
  kwa niaba ya watanzania wote kusimamia kila senti tano ya mlipakodi na
  rasilimali za watanzania ili hatimae kila mtanzania anufaike;
  kwa hili la nyinyi wabunge kutoruhusiwa kujua nini kinafanyika kwenye
  mashirika yetu ya umma ambayo tuna hisa chini ya asilimia 50; amkeni
  sasa bila kujali itikadi ya vyama vyenu vya siasa, ilazimisheni
  serikali muwe na fursa ya kuangalia huko kuna nini, msipofanya hayo
  mtakuwa mnaendelea kutusaliti watanzania. Halafu kila siku mnasimama
  bungeni mnalia matatizo matatizo matatizo huo ni unafiki na usaliti
  kwa watanzania tuliowatuma huko bungeni kusimamia rasilimali zetu.
  Kwenye madini nako ni hivyo hivyo; hata huo mrabaha tunaopewa kidogo
  na hao wawekeazaji hautumiki kumletea maendeleo huyu mtanzania.
  Taarifa zinaonyesha kwamba kile kinacholipwa serikarini kama mrahaba
  kutoka kwa wawekezaji sicho kilichopo huko serikalini, kwa mfano
  mwekezaji akikaguliwa ataonyesha kwamba alitoa tsh. 20/= serikalini
  lakini ukifuatilia huko serikalini wao wanaonyesha wamepokea tsh. 5/=.
  vikiombwa vielelezo vya hayo malipo ya tsh. 5/= unaambiwa vimechomwa
  moto. Huu ni usaliti wa wabunge wetu kwa watanzania hawa maskini,
  wabunge wetu hawatimizi wajibu wao kwa watanzania wa kuisimamia
  serikali na kulinda rasilimali za watanzania. Sasa tukisema haya yote
  yanatokea kwa sababu ya posho haramu walizotengenezewa na watawala
  wetu tutakuwa tunakosea?

  Wabunge wetu wamegeuka kuwa ni watu wa kulialia tu kila wanapokuwa
  huko bungeni huku serikali kila kukicha ikija na visingizio vingi.
  Mathalani kwenye mjadala wa bajeti unaoendelea tumeisikia serikali
  yetu kupitia waziri wa nishati na madini ndugu William Ngeleja
  akisingizia hali ya hewa (mabadiliko ya tabia nchi) kuwa ndio chanzo
  cha matatizo yetu ya umeme tuliyonayo, eti kwamba tumekuwa tukitegemea
  mvua kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na kwa sasa hivi mvua siyo
  nyingi. Huu ni uwongo, upuuzi na dharau kwa watanzania kupitia kwa
  wabunge wetu, kama ni mabadiko ya tabia nchi hayajaanza leo yamekuwepo
  kwa muda mrefu sasa lakini pia tanzania tuna vyanzo vingi sana
  vinavyotuwezesha kupata nishati ya umeme ambavyo havijaathiriwa na
  mabadiko ya hali ya hewa, tuna makaa ya mawe huko Njombe na Kiwira,
  tuna gesi huko Mikoa ya Kusini, tuna upepo mwingi wa kuzashalisha
  umeme huko Singida na Mbeya, tuna uranium huko Songea. Vyanzo vyote
  hivi havijaathiriwa na hali ya hewa, hali ya hewa imeathiri tu ujazo
  wa mabwawa yetu ya kuzalisha umeme. Lakini pia Ngeleja ameenda mbali
  zaidi anataka kufananisha tatizo letu la umeme na lile la japani. Ni
  kweli wajapani wako kwenye mgao wao wa umeme pengine utakaudumu kwa
  miaka miwili uliosababishwa na matetemeko makubwa ya ardhi
  yaliyoathiri kwa kiasi kikubwa mitambo yao ya nyukila hivi karibuni;
  lakini kabla ya matetemeko yale wajapani hawakuwa na mgawo wa umeme,
  tanzania hatujawahi kuwa na matetemeko makubwa kama yao lakini tuna
  mgawo wa umeme karibu miaka 20 sasa. Hapo unatulinganishaje na
  wajapani; na kwa jinsi wenzetu walivyo makini na utekelezaji wa
  mipango yao, watamaliza tatizo la mgawo wao ndani ya miaka miwili na
  wabunge wetu mtaendelea kuunga mkono na kupigia makofi hoja za
  serikali huko bungeni huku mkiendelea kuililia serikali na mgawo wa
  umeme, njaa ya chakula, huduma mbovu za afya pamoja na miundombinu
  hovyo. Tetemeko lililotokea Japan kama lingetokea hapa tanzania (Mungu
  aepushie mbali) inawezakana watanzania tungekufa wote.
  Wabunge wetu kuweni makini na visingizio visivyoisha vya
  watawala/serikali yetu; mara utawasikia wakisema mabadiliko ya hali ya
  hewa, kudorora kwa uchumi wa dunia, mara wafadhali hawakutoa fedha
  walizotuahidi, mara utasikia thamani ya shilingi yetu imeshuka na
  mambo mengi ya namna hiyo; badala ya kukaa na kuangalia ni jinsi gani
  ya kuyashughulikia matatizo tuliyonayo kwa kutumia rasilimali zetu
  wenyewe, serikali imekuwa makini sana kufuatilia chochote kinachotokea
  nje ya nchi na kukifanya kama kisingizio au tatizo kwenye maendeleo ya
  watanzania; mbaya zaidi wabunge wetu mmekuwa mnakubaliana na karibu
  kila kitu mnachoambiwa na serikali. Huu ni usaliti kwa watanzania!
  Ukiangalia vizuri huu mchezo wa serikali na wabunge wetu hasa
  wanaotoka chama tawala; utaona ni kama vile familia yenye baba, mama,
  watoto, wajomba, shangazi, bibi, babu na kila aina ya ndugu (hawa wote
  mimi nawaita watanzania), familia hii ina kitega uchumi cha daladala
  (hizi ni rasilimali zote za watanzania) kwa ajili ya ustawi wa
  wanafamilia; familia imemwajili dereva (serikari na vyombo vyake) ili
  aendeshe daladala, pia familia imemwajili
  Kondakta (wabunge wetu) ambaye jukumu lake ni kuhakikisha kila
  kilichopatikana kwenye ile daladala kinarudi kwenye familia ili
  kustawisha ustawi wa familia hii, kumbuka dereva na kondakta ni
  wanafamilia pia; kinachotokea; badala ya dereva na kondakta kila mtu
  kufanya kazi yake, wawili hawa wanaungana wanakuwa kitu kimoja baada
  ya dereva kumkatia kondakta kitu kidogo (posho haramu, mafao manono
  baada ya kustaafu n.k); wakirudi usiku nyumbani kupeleka hesabu
  (maendeleo) kwa wanafamilia (watanzania), unakuta hesabu haikufika
  imechakachuliwa; mara utamsikia dereva akisema tulikamatwa na trafiki,
  tairi ya nyuma ilipata pancha, bei ya mafuta leo imepanda ghafla,
  tumelazimishwa na trafiki kubeba wanafunzi kutwa nzima na visingizio
  vingi; kondakta (wabunge wetu) akiulizwa anakimbilia kujibu hayo yite
  yaliyosemwa ni kweli. Miaka inazidi kwenda, daladala (rasilimali) yetu
  inazidi kuchakaa. Mwisho wa siku unakuta daladala iko juu ya mawe
  (vifusi vya milima kwenye migodi ya madini yetu, mariasili ya
  wanyamapori wetu wanatoroshewa nje ya nchi, samaki wanapelekwa nje ya
  nchi n.k).

  Nilimsikia mbunge wa kilindi Mama Beatrice Shelukindo akichangia
  mjadala; moja kati ya vitu alivyozungumzia ni kuhusu watanzania kwamba
  ni kama vile tuko kwenye chupa (hatujadili vitu vya msingi) vya
  kumletea maendeleo mtanzania maskini, inawezakana ni kweli kabisa;
  mimi naona kuna makundi ya aina mbili ambayo yapo kwenye chupa mbili
  tofauti, kundi la kwanza ni ambalo liko kwenye chupa ambayo
  haijafunguliwa kizibo/kifuniko chake na la pili ni ambalo liko kwenye
  chupa ambayo kizibo/kifuniko chake kimefunguliwa.
  Nianze na wabunge wetu;
  karibu asilimia 99 ya wabunge wote wa CCM na wachache wa vyama vya
  upinzani wako kwenye kundi la kwanza, asilimia kubwa ya wabunge wa
  upinzani na wachache sana wa CCM wako kwenye kundi hili la pili hii ni
  kwa sababu hilo kundi la kwanza kwa kiasi kikubwa limeshindwa
  kuisimamia serikali yetu kwa ufanisi ili ilete maendeleo kwa wananchi
  wake, kinyume chake wamekuwa mstari wa mbele kushabikia utekelezaji
  mbovu wa mipango ya serikali na mwisho wa siku hatuoni maendeleo ya
  maana kwa watanzania ukilinganisha na rasilimali tulizonazo. Kwa nini
  tusiseme basi hii yote inasababishwa na posho haramu/rushwa
  inayotolewa na serikali kwa wawakilishi wa watanzania ili washindwe
  kutimiza wajibu wao kwa kiwango kinachokubalika.
  Hilo kundi la pili limekuwa likijitahidi kutimiza wajibu wao wa
  kuisimamia serikali angalau kwa ufanisi.

  Kwa wabunge wa kundi la kwanza ni kama vile watawala wa tanzania
  wamewaondoa wabunge wetu akili zao nzuri tu za kufikiri ambazo
  wanakuwa nazo kabla hawajaingia bungeni na kuwekewa zingine za hovyo
  ambazo mtu unashindwa hata jinsi ya kuzielezea. Watawala
  wamewatengenezea wabunge wengi wa CCM mazingila ambayo wanapotakiwa
  kuisimamia serikali yetu wanakuwa waoga/wanafiki; sehemu kubwa ya
  wabunge wa CCM wanakuwa wanafikiria ipo siku na wao watakuwa sehemu ya
  watawala, yaani kwao wako tayari kuwasaliti wananchi waliowatuma
  kwenda bungeni ili kutekeleza matakwa haramu ya watawala kwa matumaini
  kwamba na wao iko siku watakuwa sehemu ya watawala. Haya yote
  yanawezekana kama umetengenezewa mazingira ya kuchukua posho
  haramu/rushwa bila kujali kama maendeleo yanamfikia mwananchi wako
  aliyekutuma kumuwakilisha.

  Ukirudi kwa watanzania wa kawaida, nako kuna makundi mawili ya chupa;
  sehemu kubwa ya watanzania wa kawaida wako kwenye kundi la kwanza;
  hawa wako kwenye hili kundi kwa kutokujua haki na stahili zao kutoka
  kwa serikari yao, na sababu ya kutokujua haki na stahili zao ni
  serikali kwa kushirikiana na kundi la kwanza la wabunge wetu kutokuwa
  tayari kuwaelemisha watanzania kuhusu haki na stahili zetu na hili
  linafanyika makusudi siku zote waendelee kututawala na kupora
  rasilimali zetu.

  Na sehemu ndogo ya watanzania waliobaki wako kwenye kundi la pili,
  wanatambua haki na stahili zao na wako tayari kuzipigania, miongoni
  mwa hawa wachache ni lile kundi la pili la wabunge wetu, vyama na
  mashirika mbalimbali ya kiraia, baadhi ya vyama siasa na watanzania
  wachache mbalimbali waliodhubutu kuona na kukubali ukweli.

  Wabunge wetu wengi (hasa wa chama tawala) wamekuwa wakiiambia serikali
  kwamba wana imani na serikali yetu;
  Nawaomba wabunge wetu wajiulize yafuatayo;
  1. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama tatizo la umeme limekuwa sugu.
  2. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama mpaka leo hii bado kuna njaa.
  3. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama mpaka leo hii bado
  miundombinu ya barabara na maji huko kwa wapigakura wenu ni shida.
  4. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama mpaka leo hii bado
  huduma za afya na dawa huko kwenye majimboni yenu ni shida.
  5. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama mpaka leo hii
  mafisadi wa EPA, RADA, MEREMETA, DEEPGREEN, KIWIRA, IPTL,
  RICHMOND/DOWANS, MAGARI YA JESHI, TANGOLD, NDEGE YA RAIS, NDEGE YA
  ATCL, RITES n.k. hawajakamatwa.
  6. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama vyombo vya dola kama
  polisi wanaweza wakaua raia wema pasipo kuchukuliwa hatua zozote za
  kisheria.
  7. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama mabomu yanaweza
  kulipuka na kuua raia hakuna anayewajibika serikalini kwa mauaji hayo.
  8. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama mpaka leo hii bado
  waathirika wa mabaki ya sumu kwenye mto tigite mgodi wa north mara
  hawajalipwa fidia wala hakuna tathmini yoyote iliyofanyika.
  9. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama mpaka leo hii bado
  hakuna uchunguzi wowote uliofanyika huko kwenye mgodi wa bulyanhulu
  kahama kuhusu watu wanaosemekana kufukiwa huko.
  10. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama wanyamapori wa
  tanzania wanapakiwa kwenye ndege kiharamia kwenda nje ya nchi.
  11. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu iliyouza nyumba
  zilizojengwa kwa kodi za watanzania kwa watumishi wake wa ngazi za
  juu.
  12. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu ambayo inawazuia nyinyi
  wabunge wetu msipate taarifa ya baadhi ya mashirika yetu ya umma.
  13. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama waziri mkuu anaweza
  kuwatangazia watanzania eti nchi itatikisika ukikamata mafisadi wa
  KAGODA AGRICULTURAL.
  14. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama Rais wa nchi
  anaweza akawapa muda wa kujirekebisha vigogo wa madawa ya kulevya ili
  vijana wetu ambao ni nguvukazi ya taifa waendelee kuathirika.
  15. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama Rais wa nchi
  anaweza akawapa muda mafisadi kurudisha mali ya umma waliyopora.
  16. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama kima cha chini cha
  mshahara wa mtumishi wa umma ni tsh. 135,000/=. Mtumishi huyu
  anawezaje kuishi mpaka mwisho wa mwezi na mfumuko wote wa bei ya
  bidhaa.
  17. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama kwa miaka zaidi ya
  30 sasa imeshindwa kuwalipa wastaafu waliotumia ujana wao kwa manufaa
  ya nchi hii.
  18. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama huko kwenye
  halmashauri zetu kuna ufujaji mkubwa wa fedha za umma, rejea ripoti ya
  mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali.
  19. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu kama kuna watumishi wa
  ngazi za chini ndani ya serikali hawalipwi malimbikizo ya stahili zao
  (mfano; walimu, askari n.k).
  20. Ni imani ipi mliyonayo kwa serikali yetu ambayo haijui ina idadi
  ya watumishi wangapi; rejea taarifa ya serikali kupitia utumishi wa
  umma kwamba kuna ufisadi mkubwa wa fedha za umma (mishahara hewa).
  Licha ya kwamba ni ufujaji wa fedha za umma, lakini pia linapunguza
  ufanisi wa serikali yetu; tafsiri yake ni kwamba, serikali inapodhani
  kwamba, mathalani; ina watumishi 5000 kumbe siyo kweli, ukweli ni
  pungufu ya hao. Hapa tija itatoka wapi?

  Ukiangalia yote haya; unajiuliza hii imani ya baadhi ya wabunge wetu
  kwa serikali ambayo inaweza kuwafanyia wananchi wake mambo yote haya
  mabaya inatoka wapi kama siyo usaliti kwa watanzania. Wabunge wetu;
  hamna namna ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na serikali yetu?

  Kama ni elimu; mbona asilimia kubwa ya wabunge wetu ni wasomi; wapo wa
  viwango vya uprofesa, uzamivu, uzamili na bachelor za fani mbalimbali.
  Na hata wengine ni waganga wa tiba za asili, kwa nini mnashindwa
  kutimiza wajibu wenu ipasavyo?

  Wabunge wetu mnashauriwa mfanye maamuzi magumu yafuatayo; kwanza,
  fanyeni uamuzi mgumu sana wa kuanza kufikiri, kutenda kuamua, kushauri
  na kuisimamia serikali kwa maslahi ya watanzania wote; hili
  linawezekana kwa kujiweka wenyewe kwenye nafasi za wapigakura wenu
  kule vijijini, ikizingatiwa kwamba ni hivi karibuni mmetoka kutuomba
  kura zetu; fumba macho mfikirie mpiga kura wako ambaye hana uhakika wa
  chakula, maji hayapati kwa wakati na hata akiyapata si salama,
  hajawahi kufikiwa na nishati ya umeme, mfikirie mpiga kura wako ambaye
  huduma ya afya kwake ni duni, barabara zake ni za shida, pia usisahau
  kama mpiga kura wako atamudu bei ya mafuta; kwa sababu kwenye mjadala
  wa bajeti unaoendelea hivi sasa bungeni mlishamuongezea bei ya mafuta
  ya taa na mambo mengine mengi tu yanayofanana na hayo, ukiwa unafanya
  hayo hakikisha haujavaa nguo zinazotokana na POSHO YA MAVAZI; zisije
  zikakukwaza wakati unamfikiria mpiga kura wako. Baada ya kuyatafakari
  yote hayo ingia bungeni, iulize serikali kwa nini tuna mgawo wa umeme
  kwa zaidi ya miaka 20 sasa; Ngeleja akijibu ni kwa sababu ya
  mabadiliko ya ya hewa mabwawa hayana maji, mwambieni HAPANA; hali ya
  hewa haijaathiri makaa ya mawe, hali ya hewa haijaathiri gesi, hali ya
  hewa haijaathiri upepo na pia hali ya hewa haiwezi kuathiri mipango
  yetu; JIUZURU HAUNA MIPANGO. Fanya hivyo hivyo kwa kila waziri
  mbabaishaji anayekuja na visingizio vya namna hiyo, wako wengi sana
  huko serikalini. Kwa kufanya hivyo mtakuwa mnatuwakilisha vyema
  wapigakura wenu.

  Uamuzi wa pili siyo mgumu kama wa kwanza; baada ya kutoka kumfiria
  mpiga kura wako; kataa posho zote haramu; anza na ile kukaa, nenda
  kwenye ile ya chenji ya mafuta, ifikirie pia posho ya mavazi na
  zingine zote ambazo nafsi yako inakusuta unapokuwa unazipokea.
  ikiwezekana ziondoeni kwenye sheria mliyopitisha wenyewe;

  Uamuzi wa tatu pia siyo mgumu kama wa kwanza; ili mapato yetu madogo
  yamletee maendeleo mtanzania huyu masikini; tengueni vifungu vya
  katiba kama vipo au futeni sheria mlizotunga wenyewe, ili kuhakikisha
  wabunge wote wanaotokana na viti maalumu wanafutwa, hawa
  wanamwakilisha nani wakati eneo lote la tanzania lina wabunge wa
  kuchaguliwa? Lakini pia; mbona tunao wabunge wa kuchaguliwa ambao ni
  wanawake; waende wakapambane majimboni. Kama hoja itakuwa ni kupata
  uwiano wa wanawake na wanaume wawe nusu kwa nusu; tungeni sheria
  itakayovielekeza vyama vyote vya siasa huko mbele ya safari, viteue
  nusu ya wagombea wote majimboni wawe wanawake kwa majimbo yote kwa
  kadri watakavyokubaliana; hili linawezekana ukizingatia kwamba hata
  kwenye uchaguzi wa mgombea u-spika kupitia ccm kulikuwa na kigezo cha
  lazima mgombea awe mwanamke ambaye ndiye spika wa sasa. Pesa zote
  zitakazotokana na kufutwa kwa hawa wabunge zielekezwe kwenye miradi ya
  maendeleo ya mtanzania.

  Uamuzi wa nne pia siyo mgumu; hakikisheni mnajadili muswada wa katiba
  mpya kwa kumfikiria kwanza mpiga kura wako wa kawaida, jadilini kwa
  kuweka mbele maslahi ya nchi na watanzania wote kwa ujumla.

  Haya yote mnatakiwa myafanye sasa, siyo suala la kusubiri kwa sababu
  ni dhahili tumeshachelewa kwamba hizo posho haramu kwenu ni rushwa
  inayotokana na kodi halali za watanzania ili msitimize wajibu wenu wa
  kuisimamia serikali; msipofanya sasa inakuwa ni kama unamkamata mwizi
  wa mali yako halafu unamwachia aondoke nayo.
  Mkishindwa kufanya hivyo itabidi lile kundi la pili kwenye mfano wa
  chupa liendelee kwa nguvu zaidi kutoa elimu ya uraia kwa kundi la
  kwanza ili hatimaye watanzania wote tuzinduke kutoka kwenye chupa
  iliyofungwa ili tunufaike na rasilimali zetu.

  Wabunge wetu; kumbukeni kwamba kutumia vyama vyenu vya siasa ilikuwa
  ni tiketi ya kuingilia bungeni. Mko bungeni sasa wajibu wenu ni
  kuisimamia serikali iliyo madarakani ili itimize wajibu wake kwa
  watanzania wote, wekeni pembeni itikadi ya vyama vyenu; fanyeni kazi
  mliyotumwa na wapigakura wenu. Kumbukeni pia, hamkuchaguliwa na
  wanachama wa vyama vyenu pekee; mmechaguliwa na wananchi wote kwenye
  majimbo yenu. Je; mkikumbatia maslahi ya vyama vyenu; maslahi ya wale
  wasiokuwa na vyama ambao ndiyo wengi katiba nchi hii yatalindwa na nani?
   
Loading...