Wabunge wapania kumuweka Ndungai Kikaangoni

Bilionea Asigwa

JF-Expert Member
Sep 21, 2011
16,515
28,487
WABUNGE wamepania kumuweka kikaangoni Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kile kinachodaiwa kuwa “amekuwa upande wa serikali kuliko wabunge” katika kipindi chake kifupi cha kuwa Spika wa Bunge.

Mmoja wa wabunge waandamizi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema ingawa yeye hatashiriki katika mpango wowote wa kutaka kumuondoa Ndugai katika wadhifa wake huo, anafahamu kwamba kuna kitu “kinaendelea”.

“Mimi Ndugai ni rafiki yangu na kusema kweli siwezi kushiriki katika jambo lolote linaloweza kumuweka katika nafasi ngumu. Hata hivyo, ninazungumza na wabunge wengi wa CCM na upinzani lakini picha ninayoipata si nzuri.

“ Hawamzungumzi vizuri kusema kweli na mimi inaniuma kwa kweli. Kuna kina kitu nadhani kinaendelea lakini kwa sababu siko kwenye mipango ya kumshughulikia, siwezi kujua nini kimepangwa,”

Taarifa toka kwenye korido za Bunge zinadai kwamba mpango wa kumshughulikia Ndugai unaandaliwa kwa siri na kikundi cha wabunge wa CCM wakishirikiana na wengine kutoka katika vyama vilivyo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mtoa taarifa mmoja ambaye ni mmoja wa wabunge wapya katika Bunge la Tanzania, alisema wabunge wameudhiwa na mambo makubwa matatu katika utawala wa Ndugai ambaye amechukua nafasi ya Anne Makinda aliyekuwa Spika katika Bunge lililopita.

Ndugai, kwanza, anadaiwa kuwa amekubali kinachoitwa “mkakati wa serikali kulidhibiti Bunge” kwa kuruhusu Kamati za Uwajibikaji za Bunge kama ile ya Hesabu za Serikali (PAC) kuongozwa na wabunge wa upinzani wanaodaiwa kuwa na uwezo mdogo.

Vyama vilivyo ndani ya Ukawa, vikiongozwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (PAC), Freeman Mbowe, havijaridhika na ukweli kwamba wabunge ambao wao waliwataka kuwa wenyeviti wa kamati hizo za usimamizi, wamepelekwa katika kamati ambazo hazina ushawishi kwa jamii.

Kwa mujibu wa taratibu za kibunge kwa mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, kamati za usimamizi zinatakiwa kuongozwa na wabunge kutoka katika vyama vya upinzani.
Hata hivyo, Kambi ya Upinzani Bungeni imekataa kushiriki katika uchaguzi wa kuchagua wenyeviti wa kamati hizo safari hii kwa maelezo kuwa ilitakiwa yenyewe ndiyo ipendekeze majina ya wajumbe wa kwenye kamati hizo wanaofaa kuwa wenyeviti.

Katika utetezi wake, Ndugai ameeleza kuwa alichofanya yeye ni kuwaweka wabunge katika kamati walizoomba kupangiwa na hawezi kulaumiwa kwa kufanya hivyo.
Kwa sasa, PAC na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zinaongozwa na Makamu Wenyeviti ambao ni wabunge kutoka CCM.

Lawama ya pili kwa Ndugai inatokana na wabunge wanne kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa; ambapo wapo wabunge wanaodai kuwa Bunge halikuwalinda dhidi ya tuhuma hizo.
Wabunge ambao tayari wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa ni Richard Ndassa, Suleiman Sadiki, Kangi Lugola na Victor Mwambalaswa; huku baadhi ya wabunge wakihamishwa kutoka kamati moja kwenda nyingine kwa tuhuma za rushwa.

Mmoja wa wabunge ambao wamefikishwa mahakamani alizungumza na gazeti hili Jumamosi iliyopita na kudai kwamba kwa wao kufikishwa mahakamani, taasisi nzima ya Bunge inaonekana kuwa haifai.

“Spika atasababisha wananchi watuone sisi hatuna maana. Sisi tunadhani kwamba hilo ndilo lengo kuu la serikali kwamba tuache kuisimamia ipasavyo kwa kuonekana ni wala rushwa.
“ Kama wabunge wataonekana ni wala rushwa, watakuwa na nguvu gani ya kuinyooshea kidole serikali kwamba iwajibike? Ndugai anaona hili ni jambo la kisheria lakini natamani angejua zaidi ya kinachoonekana kwa nje,” alisema mbunge huyo mashuhuri.

Sababu nyingine ya tatu inayodaiwa kuwafanya wabunge hao wajipange dhidi ya Ndugai ni kitendo cha Bunge kubana matumizi yake na kupeleka Ikulu shilingi bilioni sita ambazo Magufuli tayari amesema zitatumika kwa ajili ya ununuzi wa madawati.

Kuna kundi la wabunge wanaoamini kwamba fedha hizo bado zingeweza kutumika kwa ajili ya shughuli za Bunge na wabunge; hata kama matumizi ya ununuzi wa madawati yatawanufaisha kwa vile yatapelekwa majimboni kwao.

Source: Raia Mwema
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom