Wabunge jengeni hoja na si vijembe

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
KATIKA siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ambayo si sawa katika Bunge la 11 la Bajeti lililoanza takribani wiki tatu zilizopita. Tabia hiyo ni ya baadhi ya wabunge kuacha kufanya kazi waliyotumwa na wananchi ambao ndio wapiga kura wao na badala yake kutumia muda wa kuchangia hoja muhimu za nchi kutoa lugha ambazo hazifai kwa wengine au vijembe ambavyo kimsingi havina tija yoyote.

Kuna baadhi ya wabunge wanawaita wenzao bebi (baby), kuna aliyemuita mbunge mwenzake kigodoro na hata waliowaita mawaziri wajinga na hata kusema waziri anastahili kupigwa makofi, hali ambayo imekuwa ikichafua hali ya hewa ndani ya Bunge.

Kutokana na lugha hizo zisizofaa na vurugu za hapa na pale kumesababisha ucheleweshaji wa kuendelea kwa shughuli za Bunge huku wengine wakionekana kutupa hewani vitabu vya Bunge vilivyokuwa kwenye meza zao za shughuli za Bunge kwa siku hiyo jambo ambalo linaonesha utovu wa nidhamu uliokithiri.

Napongeza hatua ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ya kuagiza maneno ya udhalilishaji kwa CCM na upinzani yafutwe taarifa ya Bunge. Pamoja na Naibu Spika kufuta maneno yasiyofaa, ni wajibu wa wabunge sasa kuacha kutumia lugha zisizofaa na badala yake wajenge hoja zenye tija ya kuwaletea maendeleo wananchi wanaowawakilisha na taifa kwa ujumla.

Wabunge wanatakiwa kujua kuwa macho na masikio ya Watanzania kwa sasa yako mjini Dodoma ambako wawakilishi wao wanajadili bajeti ya mwaka 2016/17 ambayo ni ya kwanza tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, John Magufuli.

Wabunge wanatakiwa kujua kuwa kazi ya wao kuwa Dodoma ni kwa ajili ya kujadili bajeti ya Serikali na zile za kisekta huku wakiwa na picha ya mwelekeo wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha uliopangiwa makadirio ya matumizi ya Sh trilioni 29.5 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo.

Kupitia bajeti hiyo, Mpango wa Serikali ni kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi iliyolenga kuinua maisha ya Watanzania huku kipaumbele kikubwa ni kuifanya nchi iwe ya viwanda, lengo likiwa kuharakisha kasi ya ukuaji uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu na mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara.

Vipaumbele vingine katika bajeti hiyo ni utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2016/2017 na maeneo yaliyoainishwa katika mpango huo wa miaka mitano, ulipaji madeni, bajeti inayotilia mkazo zaidi katika ukamilishaji wa miradi inayoendelea, miradi mipya, ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa na utekelezaji wa maeneo yote ya vipaumbele.

Ni vyema wabunge wakaacha kupoteza muda kwa vijembe na badala yake wajikite katika hoja za msingi zenye lengo la kuboresha bajeti hiyo kwa manufaa ya Watanzania. Wananchi wanataka kuona Bunge na wabunge wakichambua vyema Bajeti husika kwa lengo la kukidhi kiu ya Watanzania na itakayokwenda kuondoa changamoto mbalimbali za kijamii.

Watanzania wana changamoto nyingi katika nyanja za afya, elimu, miundombinu, umeme na umasikini uliokithiri, hivyo wanataka kuona wabunge wanaowawakilisha wakitumia kila dakika ndani ya jengo hilo kujadili namna bora ya kupambana na changamoto na si kutumia muda wanaopewa katika kutoa lugha zisizofaa ambazo zimekuwa zikivuruga mwenendo wa Bunge.

Kwa kuzingatia hilo, ndio maana ninawasihi wabunge watumie kila dakika ya nafasi ya kuchangia kwa kuja na hoja zenye kujenga na manufaa kwa Watanzania na si kupoteza muda kwa vijembe na kutoleana lugha zisizofaa. Watanzania wanataka kuona uwepo wao Dodoma kwa takribani miezi miwili unakuwa wa tija kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
 
Kwakweli mleta mada umeongea jambo jema.Kuna zomeazomea yahali ya juu mpaka ninajiuliza hivi hawa wabunge wanajiheshimu au wanatakatu kuitwa waheshimiwa?Ila ukikuta darasani wanafunzi wanapiga kelele na mwalimu yupo basi ujue huyo mwalimu nitatizo,hata bungeni akiwepo Zungu hamna kelele,kejeli wala matusi yaliyofumbiwa macho hongera Zungu na sijui kwanini mtu asiyeweza uongozi apewe kiti cha uspika aongoze wengine.Kusoma sana sio kuongoza sana
 
Back
Top Bottom