Waandishi wa kibongo.... | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Waandishi wa kibongo....

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Kintiku, Aug 1, 2012.

 1. K

  Kintiku JF-Expert Member

  #1
  Aug 1, 2012
  Joined: Feb 3, 2011
  Messages: 611
  Likes Received: 72
  Trophy Points: 45
  ROSE HAJI Dhahabu ya kale isiyofubaa katika tasnia ya habari Send to a friend
  Sunday, 29 July 2012 13:22

  Florence Majani
  WENYE hekima waliwahi kusema kuwa, “Dhahabu haiwezi kung’aa, hadi ipite katika moto.”
  Maneno haya yanathibitishwa na historia ya Mwanahabari mkongwe nchini, Rose Haji, ambaye chimbuko lake la ajira ni Redio Tanzania Dar es Salaam, sasa TBC FM.

  Changamoto alizopitia katika ajira na pengine katika maisha yake binafsi, zimemuwezesha kuwa miongoni mwa lulu zinazosakwa katika tasnia ya habari duniani kote, chombo cha elimu kwa wanahabari wachanga na mama mlezi jasiri.

  Haji, kwa sasa ni Mtoa Mafunzo kwa Vyombo vya Habari katika Shirika la Umoja wa Mataifa, la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO), lakini pia ni mhariri na mwandishi wa masuala ya habari za kiswahili katika shirika hilo.

  Hatua za mafanikio ya Haji zilianza pindi alipokuwa shule ya msingi, alirushwa madarasa kwa werevu na alizoa zawadi lukuki kwa kung’ara katika mitihani yake.

  “Nilikuwa mdogo kuliko wote darasani, mfupi na mtundu lakini mwenye akili. Nilikuwa nikiliweza zaidi masomo ya Kiingereza, Hisabati, Sayansi na Maarifa ya Nyumbani,” anasema.

  Anasema, alirushwa kutoka darasa la kwanza kwenda la tatu baada ya kuweza kusoma kitabu cha darasa la pili na tatu kwa ufasaha.

  Mwaka 1966 alijiunga na Shule ya Sekondari ya Korogwe na aliendelea kupata alamu za juu akiwabwaga wenzake wengi.

  “Waliniita ‘mwanasayansi mwehu’ kwa sababu nilikuwa na akili na namna nilivyovaa na kuchana nywele zangu. Niliyapenda sana masomo ya sayansi na ndoto zangu zilikuwa ni kuwa daktari au rubani,” anasema.

  Hata hivyo, upepo humpeleka mtu pale ambapo Mungu amempangia kuwa, Haji hakuwa daktari au rubani kama alivyotamani, taratibu alijikuta akianza kutamani kuwa Mchunguzi na Ofisa wa Jeshi.

  “Hapo ndipo tasnia ya habari ilivyoanza kuingia maishani mwangu, mwaka 1977 nilishinda mashindano ya uandishi, nikapata ufadhili wa masomo ya kada hiyo nchini Urusi(nilipata ufadhili huo kwa msaada mkubwa wa Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT) kwa kushirikiana na Urusi” anabainisha.

  Mwaka 1982 alihitimu masomo yake ya ngazi ya Shahada katika fani ya Uandishi wa Habari katika Chuo Kikuu cha Don State huko Rostov, Urusi.

  Changamoto baada ya kumaliza masomo
  Baada ya kurejea kutoka masomoni, hali haikuwa kama alivyotarajia, alikumbana na changamoto kubwa, ya kwanza ikiwa ni ajira.

  Changamoto nyingine ni kunyanyapaliwa na viongozi wa Kampuni ya Huduma za Taarifa (TIS)ambao walikataa kumuajiri kwa sababu tu ni mwanamke.

  “TIS ni sehemu ya kwanza kupangiwa kufanya kazi baada ya kutoka masomoni, baada ya kuripoti tu sikuwa nikipangiwa kazi kwa sababu mbalimbali ambazo hazikuwa na maana. Leo watasema hawana fedha, kesho wanawake wamezidi katika kitengo hicho,” anafafanua Haji

  Hata hivyo, ujasiri uliendelea kumlinda kwani mwaka 1983 Mkurugenzi wa kituo hicho, Marehemu Abdallah Ngororo, alimuhamishia katika kituo cha habari cha Redio Tanzania kama mtangazaji.

  Anasema hata baada ya kuanza kazi RTD, aliendelea kupata changamoto lakini Watanzania walimtambua mwaka 1995 baada ya kuleta tuzo ya kwanza ya Kimataifa kwa kuripoti habari bora za kijinsia, mazingira na Ukimwi.
  “Nilipewa tuzo hiyo na Kituo cha Takwimu cha Marekani, mwaka 1996 nilizoa tuzo nyingine ya habari bora za masuala ya elimu ya uraia wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini,” anasema.

  Haji anasema hatosahau mwaka 2001 siku ambayo alipewa barua ya uhamisho iliyoletwa na dereva ikimtaka kuhamia Moshi.

  “Baya zaidi wakati huo mama yangu mzazi alikuwa mgonjwa na watoto walikuwa wadogo bado wakisoma. Nilijiuliza maswali mengi, kwa nini barua iletwe nyumbani? Ilikuwa na haraka kiasi hicho?. Balaa liliendelea na mama yangu alifariki, siwezi kusahau tukio hilo” anasema.

  Baada ya miezi mitano, Haji alipata kazi katika Taasisi ya Habari kwa Nchi za Ukanda wa Kusini(MISA) kama Mkurugenzi kwa Tanzania.

  ‘Lakini cha ajabu, bosi alinikatalia kuhama na badala yake alinitaka niwalipe fedha za uhamisho walizonipa kiasi cha shilingi 750,000. Niljionea maajabu kwa sababu sikuwahi kuona kitu kama hicho duniani,” anasema.

  Asichoweza kusahau
  Haji anasema anayakumbuka mazuri yaliyowahi kumtokea katika maisha yake na anaitaja siku asiyoweza kusahau kuwa ni siku aliyopewa tuzo na Taifa la China kupitia Radio ya Kimataifa ya China(CIR) mara baada ya kumaliza mkataba wake na MISA Tanzania.

  Wahenga walisema huwezi kula muwa bila kukuta fundo, na hilo linathibitika pia kwa Haji kwani anasimulia kuwa aliwahi kukumbana na matukio ya kuhuzunisha, moja likiwa ni kuwapoteza wazazi wake, mume na mtoto wake aliyekuwa ndiyo kwanza amemaliza darasa la saba na siku aliyovunjika mguu akiwa RTD, na asiwepo mtu aliyemjali katika ajali hiyo.

  Kuhusu kada ya habari, Haji anasema uandishi wa habari si tasnia ya ndogo kama inavyodhaniwa, ni kada muhimu mno kwa taifa lolote hivyo aliwataka wanahabari Tanzania kujikita katika kuripoti ukweli.

  “Wanahabari wanatakiwa wajitume, waiepende kazi yao, waripoti ukweli na si kingine, lakini ukweli huo unatakiwa uepuke masuala ya udaku, udaku una mahali pake,” anasema Haji

  Lakini pia aliwaasa wamiliki wa vyombo vya habari, kuwalipa vyema wanahabari wao, mikataba bora na marupurupu ili kuhimiza uadilifu katika kada hiyo.

  Haji, kwa sasa anaandika kitabu kinachohusu maisha yake na anatarajia kufungua kituo cha redio ili arudishe ujuzi wake kwa kazi anayoipenda daima.
   
Loading...