EMT
Platinum Member
- Jan 13, 2010
- 14,477
- 15,325

DAR ES SALAAM: Vita bado nzito! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia vitendo vya uuzaji na utumiaji wa mihadarati aina ya bangi, cocaine, heroine na mingine kukithiri mitaani, ingawa serikali iko katika jitihada za dhati kuhakikisha mihadarati hiyo inatoweka nchini.
Hivi karibuni, baada ya vita dhidi ya uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya kuibuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ilisemekana kuwa mihadarati hiyo iliadimika kiasi cha baadhi ya mateja kujikuta wanapata madhara na wengine kutimkia kwenye nyumba za kusaidia waathirika (sober house.)
Ili kupima mafanikio ya mapambano hayo, Kitengo cha Kufichua Maovu cha Global Publishers (OFM) kiliamua kuingia mtaani kuchunguza kama madawa hayo ya kulevya yameadimika au bado yapo.

Waandishi wetu walianza kufanya uchunguzi mitaa ya Sinza, Tandale kwa Mtogole, Mwananyamala, Kinondoni, Temeke na Tandika ambapo baadhi ya maeneo ilionekana bado unga unauzwa ila kwa kujuana na kwingine ulikuwa haupatikani kabisa.

Akizungumza na Risasi Jumamosi, kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Yakuzo wa Tandale aliyeonekana ni teja alisema: “Daah, mwanangu unga umeadimika ile mbaya, sisi ambao ilikuwa ndo’ starehe yetu tunateseka ila sema nini, kuna sehemu unaweza kuupata lakini siyo kirahisi.”

…wakikagua kama mzigo upo sawa
Baada ya kuzungumza na watu katika maeneo mbalimbali na kubaini bado unga upo mitaani, waandishi walifika mitaa ya Tandika maeneo ya Dabo Kibini, sehemu ya kuoshea magari ambapo walitonywa kuwa, unga unauzwa waziwazi.

Mmoja wa waandishi alimfuata kijana mmoja na kumuuliza wapi anaweza kupata kilevi hicho ambapo alioneshwa mhusika. Kijana huyo aliyeonekana kuwa makini na biashara yake alipoulizwa kama anaweza kumpatia mwandishi cocaine kete 4 alikubali na kudai bei ya kiasi hicho ni shilingi 10,000.

Baada ya mwandishi kupewa unga huo, alikwenda kusimama kwa mbali na kushuhudia vijana wengi wakifika eneo hilo na kununua bidhaa hiyo bila wasiwasi.
Ushauri watolewa
Salum Jeti, mkazi wa Magomeni aliyedai ana watoto wake wawili mateja alikuwa na hili la kuishauri serikali: “Hawa waliotangaza vita dhidi ya madawa ya kulevya wasidili na mateja, kama kweli wanataka kutatua tatizo wazuie unga kuingia nchini kisha watafute njia nzuri za kuwasaidia hawa watumiaji. Wakidili na hawa watu wadogowadogo, unga utakuwa unaingizwa, utauzwa kwa siri na vijana wetu wataendelea kuumia.”

Risasi Jumamosi lilijaribu kumtafuta Kamishna wa Operesheni wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya nchini, Mihayo Msekhela ili kuzungumzia vita hiyo lakini alipopatikana kwa njia ya simu alieleza kuwa, yupo kwenye kikao hivyo atafutwe Jumanne ijayo.
Chanzo: https://globalpublishers.co.tz/125198-2/