Mimi ni Amos Ngosha, ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vyombo vya Habari vya Utangazaji Tanzania. Huu ni umoja wa vyombo vya habari vyenyewe, sio wamiliki wa vyombo vya habari.
Kwanza tunasema kuna ule uhuru wa vyombo vya habari. Kwa ujumla ni kwamba kuna mikingamo mingi. Kwamba usifanye hiki, usisogee hivi, usijikune kichwani, sijui usiiname, yaani yote haya yanatukwamisha.
Kwa sababu sasa hivi huwezi ukaweka kila kitu. Kuna yale ambayo wananchi wanayataka au wasikilizaji wanataka, lakini wewe huwezi kuyapeleka kwa wananchi. Kwa sababu unajiuliza mara mbimbili. Kwa sababu kidogo umeandikiwa barua, na wakati mwingine barua za onyo haziji tu hivi, wakati mwingine na faini unapigwa.
Lakini sio hivyo tu, mara nyingi tumeonekana kama tunafuatwa nyuma kama vile mtu ambaye unauza madawa ya kulevya. Yaani, chochote kinachokwenda hewani kimeshaletwa kwako ni kosa. Wakati mwingine wanakuvizia, wanakuja wanakuvizia na yale mamitambo, wanarekodi, ghafla unaambiwa umekosea hiki na hiki na hiki.
Lakini utashangaa sasa, kule ambako kuna bajeti kwenye elimu kwa umma, hawahawa watu wa Serikali wakija kwenye vyombo vyetu vya utangazaji, wanakuja kuomba kutangaza bure ama kutoa elimu bure, bila kujali kwamba mmiliki huyu kuna umeme unamgharimu, kuna maslahi ya watu ya wafanyakazi yanaendelea kupotea kwa sababu halipi chochote.
Lakini sio hilo tu, kingine ambacho pia kimesababisha yote haya ni tozo. Vyombo hivi vina tozo zaidi ya 18, na tozo zote hizi zipo kisheria. Ukiangalia TCRA wenyewe tu wana tozo zaidi ya mbili wanatutoza kwa mwaka. Na ukiangalia lile pato unalopata wewe ni pato dogo sana kulingana na tozo ambazo unatakiwa uzilipe kwa mwaka.
Lakini nje ya hilo, pia ni kuangalia namna ya kukubaliana kwamba hii nayo, hivi vyombo vya habari na utangazaji ni uwekezaji. Kuna ufinyu au muda mfupi wa leseni zinazotolewa. Muda wa leseni ni miaka mitano. Huwezi kwenda kuomba bilioni na kuendelea halafu unamwambia mwenye fedha yake kwamba leseni yangu imebakia miaka mitatu tu mbele.
Na bahati mbaya sana leseni hizi hua unaomba kuhuisha, siyo unahuisha—unaomba. Kuna kukubaliwa au kukataliwa. Sasa huyu anayekupa fedha anaaminije kama utakubaliwa?
Kwa hiyo, bila kuwa na vyombo hivi imara ambavyo vitasimamiwa vizuri na kupeleka maudhui yaliyoshiba yenye weledi kwa hawa wasikilizaji ambao ndiyo wananchi wetu wa Tanzania na mikoa jirani, nakuhakikishia kabisa kwamba tutakwama. Tutakwama katika sekta zote: kuanzia kwenye ufugaji, kilimo, sijui uvuvi, na mambo mengine ambayo yanaibeba jamii kwa ujumla.
Sasa hivi tuna Mkurugenzi Mkuu mpya wa TCRA, na yeye tumeshamuomba tukutane naye ili tumwambie na yale mengine pengine hatujamwambia aliyekuwepo awali na yale mengine ambayo hayajafanyiwa kazi.
Bila kuwa na mshikamano na kuwa na kauli moja, hatutafika. Kwa sababu tunaposhughulikiwa, tunashughulikiwa mmoja mmoja, hatushughulikiwi kama kundi la watoa huduma za utangazaji. Tunashughulikiwa mmoja mmoja kulingana na jinsi ambavyo wao wanaona kukushughulikia wewe kwa yale madhaifu uliyonayo."