Elections 2010 Vunjo Mwendo Mdundo

Kamende

JF-Expert Member
Mar 1, 2008
416
45
:mad2:Waheshimiwa nawaletea hapa chini hotuba ya Mhe. John Mrema aliyoisoma katika kikao cha Mkutano Mkuu wa CHADEMA jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro:mad2:

HOTUBA YA KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA CHADEMA JIMBO LA VUNJO TAREHE 29/05/2010 ULIOFANYIKA BBC HOTEL HIMO.

Waheshimiwa wajumbe,
Shukrani zangu za kwanza ni kwa Mwenyezi Mungu aliyetujalia uhai na afya akatuwezesha kukutana hapa kwenye mkutano mkuu wetu wa Jimbo ambao kwa muda mrefu haujafanyika kutokana na sababu mbalimbali zilizokuwa nje ya uwezo wetu.

Nawashukuru sana viongozi wote na wanachama kwa jinsi walivyoweza kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika October mwaka 2009 , kwani kila mmoja aliweza kujitolea na kufanya kazi kwa nia ya dhati na kwa kweli tuliweza kupiga hatua kubwa kwani sasa tunao wenyeviti wa Vijiji , Vitongoji na wajumbe wengi kwenye serikali zetu za vijiji zilizopo Vunjo.Hii ni historia kwa upande wa Jimbo letu kwani ni kwa mara ya kwanza kuweza kupata fursa za kuongoza vijiji na vitongoji kwa wingi kiasi hiki.

Kupitia mkutano huu napenda kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Vunjo kwa kukiunga mkono sana chama na pia kwa kuendelea kukiamini CHADEMA kuwa ndio chama pekee chenye nia ya kweli ya kuwatumikia wananchi na kujenga uchumi imara kwenye Jimbo letu.

Napenda kuwashukuru sana viongozi wa chama ngazi ya Taifa kwa kukubali kunipa ruhusa ya kuweza kuja na kukaa nanyi kwa muda wa zaidi ya siku 30 sasa ili tuweze kujenga chama chetu.Nawashukuru sana viongozi na wananchama kwa ushirikiana mkubwa ambao mmenipatia kila wakati nilipokuwa nauhitaji.

Kipekee napenda kumshukuru sana Katibu wa Jimbo Ndugu Clemence Assey kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa kipindi chote cha ziara yangu na kwa kweli ndio kiongozi pekee wa ngazi ya Jimbo ambaye aliweza kushirikiana na kufanya kazi pamoja nami bila manunguniko wala kuchoka ,namshukuru sana .



HALI YA CHAMA JIMBO LA VUNJO.

Waheshimiwa wajumbe,

Nimefanikiwa kufanya ziara jimbo zima la Vunjo na kuweza kufika kwenye kata zote 15 za Jimbo hili na changamoto kubwa ninazokutana nazo ni kukosekana kwa uongozi uliokamili kwenye kata ,kukosekana kwa matawi ya chama na yenye uongozi uliokamilika na pia kukosekana kwa vifaa ya uenezi kama vile kadi na bendera.

Hata hivyo mapungufu yote haya yamesababishwa na kukosekana kwa uongozi madhubuti ngazi ya Jimbo kwani kwa kipindi kirefu Jimbo letu ama limekuwa halina viongozi na au viongozi waliokuwepo wameshindwa kusimamia vizuri majukumu yao ambayo walikabidhiwa na hivyo ngazi za chini za matawi na kata kukosa usimamizi madhubuti.

Ni wajibu wetu sote kutafakari kwa kina juu ya mapungufu haya na ili tuweza kutafuta njia ya kuweza kuyasahihisha makosa ambayo yamejitokeza siku za nyuma , na ili tuweze kujipanga na kujiandaa na uchaguzi mkuu ambao uko mbele yetu hapo mwezi October mwaka huu .

Kwa mujibu wa katiba ya chama ibara ya 6.3.2 (a) inaeleza kuwa “kila uongozi uliochaguliwa au kuteuliwa wakati wa uchaguzi mkuu wa chama utashika wadhifa wake kwa kipindi cha miaka mitano.”swali la kujiuliza hapa je? Viongozi wetu wa Jimbo ,Kata na matawi wamekaa madarakani kwa muda gani? Je ? walichaguliwa kipindi gani? Je? Katiba inafuatwa kikamilifu? Maswali haya pamoja na mengine yanahitaji kupatiwa majibu na mkutano mkuu huu wa Jimbo.

Jambo la kutia moyo ni kuwa pamoja na mapungufu yetu kama chama bado wananchi wengi wanatuunga mkono kwa dhati na wameendelea kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Mpaka sasa wameshajitokeza wanachama kwenye kata 12 kati ya kata 15 za Jimbo la Vunjo ambao wameonyesha nia ya kugombea udiwani kwenye kata mbalimbali za Jimbo letu na hili ni jambo la kutia faraja sana kwa chama chetu. Tunapaswa kuhakikisha kuwa kila kata anapatikana mgombea Udiwani ili hatimaye tuweze kushinda Halimashauri na kuweza kusimamia rasilimali za Jimbo letu kikamilifu.

CHANGAMOTO ZINAZOLIKABILI JIMBO LA VUNJO.

1.ELIMU.

Waheshimiwa wajumbe ,

Jimbo letu lina changamoto kubwa sana katika suala la elimu kwani ukiangalia takwimu za wilaya na haswa kuhusiana na matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2009 zinaonyesha kuwa shule ya mwisho kiwilaya imetokea Jimbo la Vunjo nayo ni sekondari ya Ghona ambayo ipo kwenye kata ya Kahe Mashariki. Ila ukiangalia kwa undani tatizo kubwa lililoifikisha shule hiyo hapo ilipo ni kutokana na kukosekana kwa waalimu kwani shule hiyo haina mwalimu hata mmoja wa masomo ya sayansi .

Na hata ukiangalia matokeo ya mitihani ya kidato cha pili ya mwaka 2009 , shule ya mwisho kiwilaya inatoka Jimbo la Vunjo nayo ni Ghona shule ya Sekondari.

Matokeo ya mitihani ya darasa la saba kwa mwaka 2009 yanaonyesha kuwa shule ya mwisho kiwilaya inatoka Jimbo la Vunjo nayo ni shule ya Msingi Makaa ambayo ipo kata ya Kirua Vunjo Kusini, pia kwenye shule ambazo zilitoa wanafunzi ambao walipata 0 kwenye masomo yote kati ya shule hizo tatu mbili zinatoka Jimbo letu la Vunjo nazo ni Mbahe shule ya Msingi na Ruwa shule ya msingi.

Takwimu za Kiwilaya juu ya tathimini ya matokeo ya mtihani kwa shule kumi duni zinaonyesha kuwa kati ya hizo shule saba za Makami juu,Kiterini,Riata,Chekereni,Kochakindo,Nkosangana na Makaa zinatoka Jimbo la Vunjo. Hii na tofauti na hali ilivyokuwa mwaka 2008 kwani kati ya shule kumi duni ni shule moja tuu ya Jimbo la vunjo ilikuwepo nato ni Makami juu, nyingine 9 zilitoka jimbo la Moshi vijijini.

Hali hii haikubaliki kamwe kwenye jimbo ambalo lina Mbunge na Madiwani , na pia ni Jimbo lenye vyuo vya waalimu vya Mandaka, Marangu TTC na chuo Kikuu Tumaini , ni lazima suluhisho liweze kutafutwa mapema ili kuweza kuinusuru hali hii. Haiwezekani tukaruhusu hali kama hii na wakati huo huo hakuna wa kulisemea jambo hili.

Kuhusu ujenzi wa shule , maeneo mengi fedha za ujenzi wa shule zimeliwa na sehemu nyingine hakuna kamati za ujenzi za shule na hivyo kufanya zoezi zima la ujenzi wa madarasa, nyumba za waalimu kuwa na ufisadi mkubwa ndani yake. Kwa mfano katika shule ya msingi Shokony ambayo ipo kata ya Mwika kusini wazazi wametakiwa kuchanga shilingi 30,000 kwa kila mwanafunzi eti kwa ajili ya kujenga choo cha shule , na ikitokea mzazi anao wanafunzi wanne basi anatakiwa kuchanga shilingi 120,000 , hili jambo halikubaliki kamwe kwenye zama hizi .

Kwenye ujenzi wa shule za sekondari hali imekuwa mbaya zaidi kwani wananchi wamechangishwa ila hawajawahi kuelezwa juu ya taarifa za mapato na matumizi ile hali Halimashauri bado imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule hizo lakini fedha zimekuwa zikiliwa na nyingine kutumiwa kwa ajili ya shughuli nyingine ambazo zimeshapangiwa fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
Nitatoa mifano michache japo iko mingi sana , ujenzi wa madarasa mawili sekondari ya Mamba mwaka huu zilitolewa jumla ya shilingi 12,248,150 ila fedha hizo hazikujenga madarasa na badala yake fedha hizo wanasema kuwa zilienda kukamilisha kujenga viporo vya madarasa ya zamani , katika shule ya sekondari Kokirie zilitolewa jumla ya shilingi 10,143,800 kwa ajili ya kujenga madarasa mawili ila wanasema eti madarasa hayakujengwa kutokana na utendaji mmbovu wa kijiji na hivyo fedha hizo zimekaa Benki,

shule ya sekondari Himo zilitolewa 14,440,600 kwa ajili ya ujenzi wa maabara , ila taarifa ya Halimashauri inasema kuwa ujenzi huo haukufanyika na badala yake fedha hizo zilitumika kukamilisha viporo vya vyumba vya madarasa 8 na nyumba 2 za waalimu shule ya sekondari Mieresini , shule ya sekondari Iwa ilipewa shilingi 12,055,500 kwa ajili ya kujenga vyumba 2 vya madarasa , ila taarifa inaonyesha kuwa darasa moja limefikia hatua ya kupaka rangi na kuweka ceiling board na lingine limefikia hatua ya madirisha ila ujenzi huo umekuwa ukifanywa bila kuwepo na kamati ya ujenzi na pia wananchi wamekuwa hawashirikishwi hivyo matumizi ya pesa hayalingani na kiwango cha pesa kilichotumika.

Shule ya sekondari Kilimani ilipewa 8,994,700 kwa ajili ya kujenga Bwalo la chakula ila wanasema fedha hizo zilitumika kumalizia viporo vya madarasa manne , ila hapo hapo taarifa hiyo hiyo inaonyesha kuwa madarasa hayo yalikarabatiwa na fedha za TASAF kiasi cha shilingi milioni 32.

Mifano yote hii inadhihirisha kuwa zoezi la ujenzi wa shule za Sekondari limekubwa na ufisadi wa kutisha na hakuna hatua zinazochukuliwa kwa wahusika na hata fedha walizochanga wananchi hazijulikani zimefanya kazi gani ama zipo wapi kwani hizi ni zile zilizotolewa na Halimshauri na hata viporo vinavyodaiwa kumaliziwa havionekani na fedha zimekwisha.

2. MAJI.

Miradi ya maji nayo imekuwa ikitekelezwa imekuwa pia haiku wazi kwa wananchi kwani mradi mkubwa kama wa Kirua Kahe (KfW) fedha zilizotolewa ni 15,300,000,000. na ukiangalia taarifa ya Halimashauri inaonyesha kuwa kiasi cha shilingi 9,069,061,400 zimetumika kwa ajili ya kujenga vyazo 3 vya maji vya Monyo,Kinengena na Muwe, kujenga matanki 25 ya maji yenye ujazo wa 20-50 M3 kujenga PRT 148,Kuchimba visima 14 ukanda wa tambarare, kuchimba mtaro wenye 200km ,ulazaji wa mabomba 188 km na ufungaji wa matawi binafsi 2,107.

Jambo la kusikitisha ni kuwa baadhi ya maeneo matanki hayakuchimbwa na badala yake walipiga rangi matanki ya zamani yaliyokuwepo, wananchi walilazimishwa kuchimba mitaro hiyo, kubeba mabomba na hata katika kuunganisha matawi binafsi wananchi wanalazimishwa kununua mabomba yenye mita 70 hata kama anahitaji mita 10 za bomba na zile zinazobaki wanaondoka nazo mafundi bomba bila kuelezwa wanapeleka wapi.

Mradi huu pamoja na mingine mingi ya maji kama wa Himo ,Mabogini Kahe,mradi wa vijiji 12,kilema mandaka n.k inapaswa kufuatiliwa kwa ukaribu ili wananchi waweze kujua nini kinaendela kwani sisi kama viongozi ni wajibu wetu kufuatilia na kuweza kuwapa wananchi taarifa stahiki kuhusiana na miradi hii .

3. AFYA.
Kuna miradi mbalimbali kwa ajili ya Afya kwenye Jimbo letu nayo haiku salama sana kwani imekubwa na matumizi mabaya ya fedha zilizotolewa . Kwa mfano ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Himo , na maeneo mengine zimetengewa fedha nyingi hivyo ni wajibu wetu kufuatailia na kuweza kujua kama matumizi ya fedha hizo yako sahihi ama zinafujwa kama ilivyojidhihirisha kwenye miradi mingine.
Tunapaswa pia kujiuliza je? Ambulance zilizokuwa zimetolewa na wabunge wetu kama Jesse Makundi, na hata ya mbunge wa sasa Aloyce Kimaro ziliandaliwa kwa ajili yetu kama wananchi wa Vunjo ama zilikuwa ni miradi ya kibiashara? Kwani ya sasa ya mbunge Kimaro ambayo ipo hospitali ya kilema imekuwa ikigharimu shilingi 60,000 ili kuweza kumfikisha mgonjwa hospitali ya mkoa ama ile ta Rufaa KCMC sasa huu ni msaada ama ni biashara? Kwani bei ya soko ukikodisha gari kutoka Kilema mpaka Moshi ni kati ya shilingi 25,000-30,000.

4. KILIMO.

Jimbo letu ni miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wake wanaishi kwa kutegemea kilimo ,ila mpaka sasa hakuna msukumo wa kutosha na haswa kwenye suala zima la pembejeo za kilimo hazikutolewa za kutosha pamoja na ukweli kuwa wananchi walikuwa kwenye kipindi kigumu sana na walikuwa wanaishi kwa kutumia chakula cha msaada ila viongozi wetu pamoja na kuimba kilimo kwanza inashangaza kuwa maeneo ya uzalishaji hayatiliwi maanani.

Ni kwanini wakulima wa Vunjo wanazuiwa kuuza mahindi kwenye soko ambalo litaweza kuwapatia faida ? kilimo chetu kitaweza kukua na kuwa cha kibiashara kama hakuna soko la uhakikika?
Kahawa yetu watu wa Vunjo imekwenda wapi? Nani alihusika katika kufilisi KNCU na je amechukuliwa hatua gani? Haya ni maswali yanayohitaji majibu kama tunataka kweli kuboresha maisha ya wananchi wa vunjo kwani ni wakulima.

5. MAZINGIRA.

Jimbo letu linakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na ndio maana mpaka sasa maeneo mengi yanakabiliwa na tatizo la upungufu wa maji kutokana na vyanzo vya maji kukauka ,na ukame umekuwa ukiandama maeneo mengi ya Jimbo letu .Ni jukumu letu kama viongozi kuhakikisha kuwa tunalitia kipaumbele suala la uharibifu wa mazingira na ili Jimbo letu liweze kuondokana na tatizo sugu la kukumbwa na ukame kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia.

6. MIUNDOMBINU.

Sote tumeshuhudia hali halisi ya barabara zetu jinsi ambavyo zimekuwa hazipitiki na haswa katika kipindi hiki cha mvua za masika kutokana na kuharibiwa na mvua na nyingine ni kutokana na kutokufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara japo fedha zimekuwa zikitengwa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa kazi hizo zinafanyika. Hili ni suala kipaumbele kwani bila barabara hakuna uzalishaji ambao unaweza kufanyika na kuleta tija ya kutosha .

7. MASUALA MTAMBUKA.

Jimbo letu limebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya mapato kama vile KINAPA , uwepo wa mpaka kati ya Tanzania na Kenya na hivyo kufanya Jimbo letu kuwa ni eneo la Biashara ,tunapaswa kutumia kikamilifu fursa ya soko la pamoja kati yetu na nchi za Kenya , Uganda na Rwanda kwa ajili ya kukuza uchumu wetu. Wakinamama wanaofanya biashara za mpakani wanapaswa kujengewa mazingira yenye haki katika kufanya biashara na vyombo vya dola kama polisi na TRA wanapaswa kuwaelimisha umma nini maana ya soko la pamoja.

Mapato ya KINAPA yanapaswa kuwanufaisha wananchi wa Jimbo la Vunjo kwani ndio motisha kwao katika kuweza kuhifadhi mazingira ya Mlima Kilimanjaro na hivyo kuifanya theluji ya Mlima huu iweze kuwepo mpaka vizazi vijavyo.

Tuna changamoto ya gonjwa la Ukimwi , ambalo limesababisha kuwepo na idadi kuwa ya wajane na yatima kwenye Jimbo la Vunjo , ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya Ukimwi linakuwa ni zoezi la kudumu ili tuweze kupunguza adhari zinazotokana na ugojwa huo.

HITIMISHO.

Pamoja na changamoto nyingi amabzo zinalikabili Jimbo la Vunjo ni jukumu letu sote kujua kuwa tunapaswa kujipanga ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi kwa manufaa ya wananchi wetu na hivyo tuweze kurejesha heshima ya watu wa Jimbo la Vunjo na Kilimanjaro kwa ujumla wake .

Ninaamini kuwa kulijua tatizo ni mwanzo wa kuweza kupata ufumbuzi wa tatizo husika hivyo basi kila mmoja wetu anapaswa kujua kuwa ana wajibu katika kujenga chama ili hatimaye tuweze kushinda nafasi za udiwani , Ubunge na Urais na hivyo tuweze kukabiliana na changamoto hizi za Jimbo la Vunjo.

Tumeweza kuona majimbo yanayoongozwa na CHADEMA jinsi ambavyo wabunge wake na madiwani wameweza kukabiliana na changamoto hizo , hivyo njia pekee ya kuweza kutatua changamoto hizi za Jimbo la Vunjo ni kwa kuchagua Diwani, Mbunge na Rais wa CHADEMA

Baada ya kusema hayo naomba kutangaza rasmi kuwa nitachukua fomu ya kugombea Ubunge Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya CHADEMA kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2010, naomba mniunge mkono na tushirikiane kwa pamoja.

Kampeni zikianza nitaeleza kwa kina kwenye Ilani yangu ya Jimbo kuwa ninataka kufanya nini kwenye Jimbo la Vunjo na wananchi wa Vunjo kwa ujumla wake.

Nawashukuru sana kwa kunisikiliza, natangaza kuwa mkutano mkuu wa Jimbo la Vunjo nimeufungua rasmi.
John Mrema
Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halimashauri
 
chadema oyeee
Ili mojawapo ya majimbo yatakayokuwa tanuru wakati wa uchaguzi. Mpaka sasa hivi wapo Aloyce Kimaro,Augustine Lyatonga Mrema na John Mrema, atakayeshinda hapa atakuwa kama chuma cha pua...bungeni hakuna kulala.
 
Joto limepanda sana kwenye Jimbo la Vunjo na kwa muda wa wiki mbili JK anaenda vunjo mara mbili , kesho anaenda vunjo kwa ajili ya mkutano mwingine wa hadhara Himo baada ya ule wa awali uliofanyika wiki moja iliyopita ambao ulifanyika Marangu mtoni.

CCM wameendelea kuwatisha viongozi mbalimbali wa vijiji wa CHADEMA kuwa wasipokubali kurejea CCM watachukuliwa hatua , na hata kesho JK anaenda kumpokea kijana mmoja anaitwa Plasidius Solly ambaye aligombea uenyekiti wa kijiji Himo ila akawekewa pingamizi la uongo na mpaka sasa kuna kesi ipo mahakama ya wilaya ya Moshi , wameamua kumpa fedha ili afute kesi na ajiunge na CCM na kesho huenda akafanya hivyo.
 
Back
Top Bottom