Vita vya washairi

Idd Ninga

JF-Expert Member
Nov 18, 2012
5,136
4,297


1)Washairi kulumbana,ni nani alianzisha ?

Washairi kugombana,lini tutatamatisha

washairi kuchukyana,jambo hili linatisha

Vya maneno vinachosha,vi vita vya washairi.



2)Washairi kupambana,jambo lisifurahisha

Washairi kuungana,itaja tufunganisha

Washairi kushikana,yaweza tuunganisha

Vya maneno vinachosha,vi vita vya washairi.



3)Washairi ndugu moja,mungu katukutanisha

Tushaikaneni pamoja,manenoya twangusha

Na subiri tukingoja,kabla kujitamkisha

Vya maneno vinachosha,vi vita vya washairi.



4)Washairi kupendana,babu alitufundisha

Washairi kuzozana,kuna mengi litafisha

Upendo na kupendana,nuru kutaiwakisha

Vya maneno vianachosha,vi vita vya washairi.


5)Kujiona ni mabingwa,ndiyo sumu twajilisha

Baraka zote zafungwa,kitungo nawajulisha

Kama balaa lajengwa,na miba tunajivisha

Vya maneno vinachosha,vi vita vya washairi.



6)Tushikaneni mikono,bila kujitenganisha

Tuviache vimaneno,vya weza tuchonganisha

Na kuleta malumbano,kisha kutupiganisha

Vya maneno vinachosha,vi vita vya washairi


7)Hovyo hovyo semeana,jambo hili lakondesha

Ni ya nini kupondana,ni maovu twaendesha

Tupendaneni kwa sana,sanaa kunenepesha


Vya maneno vinachosha.vi vita vya washairi




8)Kushaanza kulogana,tuhuma twazifurusha

Haya tena twatajana,zetu jina twaangusha

Hivi twavyofurushana,sifa zetu twachachusha

Vya maneno vinachosha,vi vita vya washairi


SHAIRI -VITA VYA WASHAIRI

MTUNZI-Idd Ninga wa Tengeru Arusha

iddyallyninga@gmail.com

+255624010160
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom