Viongozi wetu na sifa toka Ughaibuni! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Viongozi wetu na sifa toka Ughaibuni!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Jul 16, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Jul 16, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,412
  Likes Received: 81,450
  Trophy Points: 280
  Viongozi wetu na sifa toka Ughaibuni!

  Lula wa Ndali-Mwananzela Julai 15, 2009

  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  SAIKOLOJIA ya sifa inawafanya wanadamu kupeana sifa. Tunapongezana tunapopofanya vizuri au pale tunapoonyesha dalili za kufanya vizuri ili tujitahidi tufanye vizuri zaidi.

  Ni saikolojia hii inayowafanya watu wawashangilie wachezaji wao uwanjani, wa wazi kumshangilia mtoto anapojaribu kusimama kwa mara ya kwanza, na ni saikolojia hii inayotufanya tupeane zawadi katika kutambua juhudi au mchango wa mtu fulani. Kutokana na ukweli huo, mtu hapewi sifa kwa kuharibu au kuvurunda.

  Kwa mfano, mchezaji akigeuka na kufunga golini kwake washangiliaji wa timu yake wataonyesha wehu wakianza kushangilia japokuwa ni goli halali. Mtoto akiwa anafanya kitu kibaya humpi pongezi; bali unamfundisha nidhamu na wakati mwingine unamwadhibu ili asirudie kitu kile kile.

  Sasa inapotokea watu wanampa pongezi mtu anayeharibu au anayehujumu maslahi ya watu wake mwenyewe na mtu huyo akawa anashangilia, basi, kuna tatizo mahali fulani. Na mtu ambaye anafurahia sifa kwa mtu ambaye anaonyesha ushahidi wa kuvurunda, basi, tunaweza kusema kuwa anafurahia sifa za kijinga.

  Hali halisi ni kuwa makini hawezi kamwe kufurahia sifa asizostahili; hasa pale zinapotolewa kwa ajili ya kuzuga watu na kuwafanya watu wajisikie vizuri wakati wanajua kabisa mambo siyo mazuri. Ni sawa na wale ambao hushangilia baada ya mechi kuwa "magoli tumefungwa lakini chenga tumewala" . Kushangilia chenga wakati umefungwa ni kutafuta sifa za kijinga.

  Ukweli huu umeonekana siku chache zilizopita ambapo gazeti moja la serikali lilitangaza sifa ambazo viongozi wa Tanzania wamemwagiwa na Rais wa Marekani Bw. Barack Obama. Gazeti hilo lilianza taarifa yake kwa kutangaza kuwa "Rais wa Marekani, Barack Obama, ameisifu Tanzania kuwa ni mfano wa kuigwa katika bara la Afrika kwa kuwa na uongozi unaojali na kusaidia maendeleo ya watu wake. Obama amesema uongozi wa Tanzania umeonyesha mfano kwa nia ya dhati ya kuwasaidia wananchi kwa kuboresha huduma muhimu za kijamii."

  Gazeti hilo likaongeza kuwa Rais Obama aliahidi kuwa "kila atakakopita ataziambia nchi hizo za Afrika ziige mfano wa Tanzania" , na ya kuwa Obama aliiambia tovuti ya Allafrica.com iliyokuwa ikimhoji kuwa "Bila shaka mmeona kazi nzuri iliyofanywa na uongozi wa Tanzania ya kuelekeza nguvu zake katika kutoa huduma kwa wananchi wake, na popote marafiki wanapotaka kujikwamua wenyewe, tutakuwa nyuma yao kama washirika."

  Sasa kuna mahali hapa ambapo tunaweza kuona ukweli. Kwamba huduma mbalimbali za kijamii zimeongezwa. Shule zimeongezwa, mahospitali yameongezwa, kliniki n.k. Sasa kwa mtu yeyote ambaye ni mwepesi kuzugwa anaweza kuamini kabisa kuwa, basi, tunastahili sifa hizo.

  Kuna kuongeza huduma za kijamii mahali ambapo hauna njia nyingine isipokuwa kuongeza. Kwa mfano, kama mwaka huu kuna watoto 20 waliofaulu na shule moja yenye uwezo wa kuchukua watoto 20, ni wazi hakuna haja ya kuongeza shule nyingine. Lakini endapo inatokea kuwa, aidha kutokana na ongezeko la uzazi au uhamiaji, inatokea kuwa kuna watoto 50, basi, aidha watoto hao wote warundikane kwenye shule ya watoto 20 au madarasa yaongezwe au kujenga shule nyingine.

  Hali halisi ni kuwa kuongezeka kwa huduma nyingi za kijamii ni kuongezeka kutimiza mahitaji ya ongezeko la asili la watu. Tulipokuwa na watu milioni 25 tulikuwa na huduma za kijamii zinazoendana au kukabiliana na mahitaji hayo. Hata hivyo, tulipofanya sensa ya kwanza na kugundua kuwa tuna watu wengi zaidi na vile vile ongezeko la watu ni kubwa kuliko ilivyokadiriwa, tukajikuta tunalazimika kujipanga upya.

  Hata hivyo, ongezeko la watu na changamoto mpya za kijamii (kama ujio wa ugonjwa wa UKIMWI) vimetulazimu kuongeza mambo mengi kweli. Hivyo, kwamba tumeongeza huduma za kijamii ukweli ni kuwa hatukuwa na uchaguzi mwingine.

  Pamoja na jitihada hizo, bado hatujafika mahali pa kusema kuwa tumefanikiwa na kujiona mfano. Kweli tumepiga hatua, lakini ni hatua ambayo ilipasa tupige. Tutafanya kosa kubwa sana kuanza kulewa sifa kuwa tumefika! Tutaanza kubweteka tukiamini sifa za "wakubwa" kuwa tunafanya vizuri. Ushahidi uliopo hata hivyo unapiga kelele kinyume chake.

  Na zaidi ambacho kinanifanya nione sifa nyingine ni za kijinga ni pale viongozi wetu wanaponyanyuliwa juu kuwa ni "mfano wa kuigwa" ; kwamba wanatuongoza vizuri kweli kiasi kwamba Afrika nzima iwaige wao. Endapo viongozi wa Afrika watawaiga viongozi wetu, basi, bara la Afrika litaendelea kuwa kituko. Fikiria.

  Viongozi wetu katika uongozi wao mzuri na 'uliotukuka' walitutambia kuwa hata kama kula nyasi wananchi tule ilimradi tu Rais anunuliwe dege kubwa kwa gharama ya karibu Shilingi bilioni 50! Wanastahili pongezi!

  Viongozi wetu katika uongozi wao mzuri, na licha ya mapingamizi ya taasisi za kimataifa za fedha za IMF na WB wakaamua kununua rada ya kijeshi kwa gharama ya bilioni 50. Cha kuudhi ni kuwa bei halisi ya rada hiyo ni bilioni kama 30 hivi. Ikagundulika kuwa tumerushwa na dalali ambaye sasa hivi anatanua huko ng'ambo. Hakuna mtu yeyote aliyefikishwa mahakamani kwa uhalifu huo zaidi ya kuwepo dalili ya kushtakiwa kwa makosa ya kipuuzi! Wanastahili pongezi!

  Viongozi wetu katika uongozi wao mzuri na 'uliotukuka' hadi kupewa sifa na Rais wa Marekani wameinua majengo makubwa ya kisasa katikati ya Jiji la Dar es Salaam, majengo ambayo yanapendeza kwa vioo vyao na yenye gharama ya mabilioni kama yale ya Minara miwili ya Benki kuu ambayo thamani yake inazidi bilioni 300, na hilo jengo jipya la TAKUKURU lenye gharama ya karibu Sh. bilioni 4 (kwa ajili ya kuzuia rushwa ya kiasi gani!?) Wanastahili pongezi!

  Wanastahili pongezi kwa sababu wamefanikiwa kutandaza mabomba ya maji machafu katika kila nyumba katika jiji la Dar, wameweza kutengeneza mitaro ya maji machafu na maeneo mazuri ya watu wa "jamii" kuweza kupumzika na kufanya shughuli zao! – Wanastahili pongezi!

  Viongozi wetu hawa wanaopenda sifa nyepesi wanastahili pongezi kwa sababu wameweza hatimaye kutatua tatizo la maji katika nchi yetu! Kwa taifa lililozungukwa na maziwa makubwa Afrika na mito bwelele inashangaza wanataka sifa kwa kuzindua visima! Ati wameleta huduma za kijamii kwa kuwezesha bomba la kijiji kutoa maji. Wanastahili pongezi!

  Wanastahili pongezi kwa kuboresha huduma za kijamii kama shule za msingi. Chini ya uongozi wao shule zote za msingi zimefikia kiwango bora kwa kuwa na madarasa yanayokalika, madawati ya kutosha, vyoo vya kutosha na kila mwanafunzi anapata elimu katika mazingira bora. Wanastahili pongezi kwa sababu wameinua majengo ya shule hata kama hawakuinua elimu inayotolewa kwenye majengo hayo! Wanastahili pongezi!

  Viongozi wetu hawa, chini ya uongozi wao mzuri na wenye kumwagiwa "sifa na wakubwa" , wameweza kuondoa tatizo la umeme nchini kwa mikakati yao ya hali ya juu. Wanastahili sifa kwa sababu wameweza kutumia vyanzo vyetu vya maji, upepo, jua na makaa ya mawe kuondoa tatizo la upungufu wa umeme.

  Katika kuonyesha ubora wa uongozi wao, wameweza kuanza ujenzi wa bwawa kubwa la Stieglers ambalo likikamilika peke yake lina uwezo wa kutosheleza mahitaji yote ya umeme ya sasa! Wanastahili pongezi!


  Niseme nini tena? Sifa nyingine tunazozishangalia ni nyepesi mno.

  Kuweza kuelewa ni kwa nini sifa hizi ni za kutudhalilisha, fikiria maneno ya Rais Kikwete wakati akifungua jengo jipya la TAKUKURU pale alipodai kuwa asilimia 30 ya bajeti huishia mikononi mwa 'wajanja'. Kwa maneno mengine, kama bajeti yetu ingekuwa ni Shilingi trilioni 10, basi, Shilingi trilioni 3 zinaishia mikononi mwa 'wajanja'.

  [Maneno hayo ya Rais yanastahili kumfanya yeye na viongozi wenzake kuinamisha vichwa vyao kwa soni. Ati tunastahili sifa wakati kati yetu kuna watu ambao wanakula urithi wa watoto wetu kama mchwa, na bado tunataka kupewa sifa.

  Kisa kingine ni kuwa ati kuna mtumishi mmoja ambaye aliweza kula zaidi ya bilioni 30 za miradi ya Norway kwa muda wa zaidi ya miaka 10, na hadi sasa hakuna aliyefikishwa mahakamani. Ati tuigwe na nchi nyingine za Afrika!


  Ninaposikia sifa za namna hii huwa najiuliza malengo yake ni nini? Waswahili wana msemo unaoelezea kitu hicho. Wanasema ni "kuvishwa kilemba cha ukoka" na mwingine usemao "kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa" .

  Viongozi wetu wanajisikia kweli wanapopata barua za pongezi toka kwa wakubwa; wanaona raha mioyoni mwao balozi fulani akiwasifia.

  Ndio maana kuna mmoja alitamba ati Rais Mkapa anaheshimika sana huko nchi za nje. Mwingine akatuambia kuwa anatushangaa kwa nini tunawakosoa wakati wakubwa huko nje wanawasifia, akahoji "ni kitu gani ambacho wao (wakubwa) wanakiona ambacho" sisi hatukioni. Yaani, hawa viongozi wetu wanatuona sisi hamnazo. Kuwa tukipewa sifa na Wamarekani na wazungu, basi, tufanye sherehe.

  Hayo ni mawazo ya kitumwa. Subirini Watanzania wenyewe wawape sifa, subirini makundi ya wasomi wetu yawamwagie sifa. Siku mkiona maskini wa Tanzania wanawapa sifa, basi, mjue mmefanya kazi nzuri. Siku mkiona wanasheria na wanaharakati wanawapeni sifa, basi, mjue mko katika njia nzuri.

  Lakini haya ya kufanya mambo ili Wamarekani na ndugu zao wawape sifa yanaudhi. Vinginevyo kwa nini msiende kugombea kwenye hizo nchi zao na muwaongoze kwa namna mnavyotuongoza sisi tuone kama hata mtakaa mwezi mmoja ofisini!


  Kama mnataka kusifiwa, subirini msifiwe na Watanzania wenzenu; vinginevyo sifa hizi za viongozi wa ubepari duniani zitamibwetesha tu badala ya kumisaidia.

  Ushauri wangu ni kuwa, achaneni na sifa hizi nyepesi kutoka kwa vinara wa ubepari duniani. Subirini sifa za kweli za walengwa; yaani Watanzania. Nje ya hapo, nasi tutaanza kuwavisha vilemba vya ukoka! Si ndicho mnachotaka?
   
 2. Tatu

  Tatu JF-Expert Member

  #2
  Jul 16, 2009
  Joined: Oct 6, 2006
  Messages: 1,081
  Likes Received: 38
  Trophy Points: 145
  It's just too much "SUGAR-COATING" and POLITICALLY CORRECT nonsense when it come to LEADERS. They always do things which advances their self interest, nothing more, nothing less.
   
Loading...