Pistol
Senior Member
- Oct 13, 2015
- 194
- 86
Rais Magufuli akimjulia hali mgonjwa alipofanya ziara kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Waziri mkuu Majaliwa akiwa kwenye ziara
Rais wa China Xi Jinping akifanya ziara mkoani Jiangxi kujua hali ya maisha yua wanakijiji.
“Utumishi wa umma” ni maneno ambayo kwa sasa ni kama yamepoteza maana. Kama hayajapoteza maana, basi maana yake halisi imepindishwa. Zamani neno “utumishi” lilikuwa na maana kuwa mtu anayechaguliwa au kuteuliwa kuwa kiongozi, maana yake ni kuwa amepewa dhamana ya uongozi ambayo anatakiwa kuitumia kufanya kazi kwa niaba ya anaowaongoza. Lakini kwa muda sasa kumekuwa na kawaida ya kusikia kuwa mtu anapochaguliwa au kuteuliwa kwenye nafasi fulani ya utumishi wa umma, neno tunalotumia zaidi ni “ameula”. Kibaya zaidi ni kuwa, baadhi ya wale wanaokuwa kwenye nafasi za utumishi wa umma, badala ya kutumikia umma na huufanya umma kuwatumikia wao.
Kuna wakati lilikuwa jambo la kawaida kusikia kuwa baada ya mgombea ubunge kukutembelea kuomba kura, ukimpigia kura basi usubiri kukutana naye karibu na uchaguzi unaofuata. Ingawa hali hii imeanza kubadilika, bado haijafikia kiwango ambacho watu wa majimboni tungekipenda.
Tangu serikali ya mheshimiwa Magufuli iingie madarakani, kumekuwa na dalili zinazoonesha kuyavika maana halisi maneno “utumishi wa umma”, tofauti na hali iliyoanza kuzoeleka ya “umma kuwatumikia viongozi”. Ziara zilizofanywa na mhe Rais na Waziri mkuu kwenye maeneo yenye matatizo kama vile Muhimbili na Bandari, na hatua walizochukua baada ya ziara hizo vimefanya imani kwa viongozi tunapowachagua ianze kurudi. Kauli mbiu ya serikali ya sasa “hapa kazi tu”, ina maana kubwa.
Inapotajwa kazi tu, kwanza ina maana ujue ugumu wa kazi yenyewe na hata ujue namna ya kufanya yenyewe. Kama utakaa ofisi tu na kusoma ripoti zilizoandaliwa bila kujua hali halisi ya maisha ya watu unaowafanyia kazi, basi kazi yako itakuwa na mashaka.
Nimekuwa nikiangalia dhana ya utumishi wa umma kwa viongozi wa China, inatekelezwa kwa vitendo toka ngazi ya juu. Nimekuwa nikijaribu kuangalia jinsi viongozi wa hapa China wanavyotumia muda wa siku za mapumziko kufanya kazi.
Pamoja na kuwa tunasikia Rais wa China au waziri mkuu wa China ameenda mji fulani kwa mapumziko ya sikukuu, ukweli ni kuwa wanakwenda kufanya kazi ya kujionea wenyewe hali za maisha ya watu wanaowatumikia. Wenzetu wa China ingawa hawana kauli mbiu ya “hapa kazi tu”, lakini kivitendo kwao kila siku ni kazi tu. Rais Xi Jinping wa China alifikia hata hatua ya kukumbusha kuwa Chama cha kikomunisti kinatakiwa kukumbuka jukumu lake la kutumikia umma.
Walichotuonesha Mh Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa kimetufurahisha wananchi, na kinatupa moyo wa kuwaunga mkono. Kama kikiendelea kwa msukumo walioanza nao, bila shaka mengi yatabadilika na utumishi wao kwa umma wa watanzania utakuwa na maana halisi.