Viongozi wa Dini wakati wenu ndio huu

Viongozi wa Dini wakati wenu ndio huu

Mapambano Yetu

JF-Expert Member
Joined
Aug 14, 2012
Posts
1,133
Reaction score
2,128
Tanzania imeendelea kuwa ya matukio. Leo viongozi wa dini wako kimya juu ya Yale yanayoendelea Dodoma. Wanasubili hatua za mwisho, utasikia Mchakato haukuwa wa haki, serikali ilipuuza maoni ya wananchi, ingejadiliwa rasimu ya Warioba, serikali haina dini na kauli nyingine nyingi. Hivi hawa nao si watu wa matukio kweli? Wonders

Update tarehe 29/08/2014


JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA

TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA

Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es salaam , tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo: Tunaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya Maoni ya WANANCHI kuhusu mabadiliko hayo na kutuletea Rasimu yenye maoni mengi ya Watanzania bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsi na kabila. Pia tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama Randama, Nyaraka zenye maoni ya wananchi, picha, tafiti mbalimbali na hata orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni katika Tume. Tume pia iliweza kuandaa Tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za Tume na Maoni yote yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume iliandaa Rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya WANANCHI. Tume imedhihirisha kuwa, ilitenda KIZALENDO na, kwa mantiki hiyo, wajumbe wote bila kujali vyama vyao, dini zao na upande wa Muungano walikotoka, waliweza kujadili kwa uwazi na kweli na mwisho wakaridhiana katika kila Ibara iliyopendekezwa. Hili linatufundisha kuwa Katiba ni MARIDHIANO na si jambo la maslahi ya kisiasa, bali ni suala la maslahi ya WANANCHI. Tunaamini kuwa kila Mjumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya WANANCHI aliheshimu kiapo chake na hivyo kufanya kazi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hili.

Baada ya Tume kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao kweli kwa uovu” (Warumi 1:18). Katika mijadala ya Bunge Maalum la Katiba (BMK) yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya maslahi kwa WANANCHI, na ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa yanadhihirisha hili: Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa bila sababu za msingi kutolewa wakati mchakato unaendelea. Hali hii imefanya zile nyaraka na kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa. Kwa sababu hiyo, tumeona Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha takwimu na taarifa mbalimbali ambazo WANANCHI hawawezi kuzipata kwa ajili ya kuoanisha baina ya kinachojadiliwa Bungeni na kilichomo katika Rasimu na viambatanisho vyake vyote. Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na kwa maslahiya nani? Bunge la Katiba limeshindwa kusimamia Kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na kuridhiwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Kushindwa huku kusimamia kanuni kumesababisha vurugu ndani ya Bunge Maalumu na kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata Katiba bora ya nchi yetu. Matumizi ya ubabe na wingi wa Wabunge wa Chama Tawala (CCM), badala ya Kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na Chama Tawala dhidi ya maslahiya WANANCHI. Mijadala katika Bunge Maalumu la Katiba imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume. Hali hii imelifanya Bunge Maalumu la Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza heshima na hadhi yake. Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa KATIBA NI MATOKEO YA TENDO LA MARIDHIANO NA SI SUALA LA MASLAHI YA KIKUNDI CHA WATU WACHACHE. Hatua iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa BMK unaoendelea umeondoa kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge, ukomo wa ubunge, n.k., na kuwezesha maoni na maslahi ya Chama Tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia ya kulinda maslahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora. Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo; 1. Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya Katiba kwa uwazi. 2. Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa na Chama Tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na sio kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977. 3. Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano muafaka, uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977 yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda Rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba. 4. Kwamba baada ya Bunge Maalum la Katiba kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi katika Bunge la Katiba. 5. Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko katika Rasimu ya piliya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni. 6. Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba Mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi. Jukwaa la Wakristo Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba AMANI ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya. Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya mshikamano, umoja na amani ya Taifa letu. Ifahamike kuwa WANANCHI wa Tanzania wako juu ya Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe WANANCHI wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa tu Chama hicho kimeyapuuza na kimekataa Maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi. “Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutabakari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenyekuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”. (Rejea Warumi 1: 28-32)

IKUMBUKWE KUWA RASIMU YA PILI YA KATIBA NI WARAKA HALALI NA RASMI NA NDIYO MAWAZO YA WATANZANIA NA TUNAHIMIZA KUWA KATIBA NI YA WANANCHI NA INAHITAJI MARIDHIANO NA SIO UBABE. Imetolewa leo Agosti 28, 2014 Na MKUTANO WA JUKWAA LA WAKRISTO Tanzania Episcopal Conference (TEC) The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT) Christian Council of Tanzania (CCT) The Seventh Day Adventists (SDA)


Updates tarehe 3/September/2014


Leo saa Sita Mchana hapa Dodoma, wajumbe wa Bunge la Katiba Kundi la 201 ambao wametoka katika makundi ya Kidini wamekutana na kutoa tamko lifuatal;o kuhusu mwenendo wa Bunge la Katiba....

TAARIFA YA WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA TOKA WAJUMBE 201 KUHUSU MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA

Sisi Wawakilishi wa Jumuiya na Taasisi za Dini, tuliopendekezwa na Taasisi zetu na baadaye kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, na kula kiapo cha utekelezaji wa jukumu hili kubwa. Tukiamini kuandaa Katiba Mpya kwa maridhiano ya Kitaifa kwa wananchi wote, tulipokea jukumu hili kama wajibu wetu Kitaifa. Aidha tunaamini kwamba katika kupata maridhiano ya Kitaifa ni muhimu kuheshimu kila wazo na fikra inayotolewa na kuunganisha fikra hizo kwa usahihi, kwa njia ya kidemokrasia kwa kupiga kura na kukubaliana na matokeo ya wengi.

Kama ilivyoelezwa hapo awali, kabla ya kuanza shughuli za Bunge Maalum, kila mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu na mtiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo wake na ufahamu wake, kufanya kazi zinazomhusu, bila upendeleo na kumuomba Mwenyezi Mungu amsaidie.

Tumeshangazwa na kusikitishwa sana kuona kwamba mchakato wa kutayarisha Katiba itakayopendekezwa na Bunge hili kwa wananchi, unachafuliwa taswira yake. Bunge Maalum la Katiba linachafuliwa na, shughuli zake kuingiliwa na kupotoshwa na wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge, Makundi, Taasisi na Vyombo mbali mbali vya habari, uhalali na ukweli wa shughuli za BungeMaalum la Katiba unapotoshwa. Wananchi wanaaminishwa yasiyo na ukweli.

Upotoshwaji huu umezua mijadala mbali mbali katika jamii ya Watanzania na bado linaendelezwa kama ifuatavyo:

1. Kwamba Bunge Maalum la Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe wenzetu walioondoka wameliondolea uhalali wake kwa vile hwapo, wakiwepo Bungeni basi uhalalai wake utakuwepo -utapatikana; 2. Inadaiwa kwamba Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zinavunjwa ovyo ovyo; 3. Inadaiwa pia, kwamba kinachojadiliwa sasa katika Bunge hili ni Waraka mwingine na si Rasimu iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyowasilishwa rasmi Bungeni na kuanza kujadiliwa na wajumbe; 4. Inadaiwa na watu na Taasisi mbali mbali, kwamba viongozi wa dini, wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, na wajumbe wa Kundi la 201, wanapewa rushwa. Isitoshe Vyombo vya habari vimeandika tuhuma kama hizi. 5. Inadaiwa pia kwamba wajumbe waliomo katika Bunge hili ni wachache, ukilinganisha na hao walioko nje ya Bunge hilo; 6. Bunge hili, kwa tuhuma hizo, lazima lisitishwe au livunjwe na Mhe. Rais.

Kabla ya kuanza kuusahihisha upotoshwaji huo, sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini mbali mbali na Wajumbe wa Kundi la 201 katika Bunge Maalum la Katiba, tunapenda kufahamisha umma wa Tanzania mchakato wa kutayarisha Katiba Mpya ulivyo kisheria.

Tunapenda kuwafahamisha Watanzania wenzetu kwamba mchakato huu una hatua tatu kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mpaka hivi sasa ni hatua moja imekamilika. Hatua ya pili ndiyo inayoendelea, na hatua ya tatu bado haijaanza.

Hatua ya kwanza ni ile ya uandaaji wa Rasimu. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 iliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya kifungu cha tano cha sheria hiyo. Tume hii ilipewa jukumu la kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba, kuanisha na kuchambua maoni ya wananchi na kisha kuandaa rasimu ya Katiba. Kazi hiyo ilifanyika kwa kipindi cha takriban miaka miwili na hatimaye Rasimu ya Katiba ilikamilika.

Hatua ya pili ilikuwa ni kuipeleka Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba, ambalo liliundwa kwa shughuli maalum ya kuandika Katiba inayopendekezwa, ili ifikishwe kwa wananchi ambao wataamua waikubali au waikatae kwa kuwa wao ndio wenye maamuzi ya mwisho. Hawa ni Watanzania wote wenye uwezo wa kupiga kura kwa kutoa maoni yao. Hoja ya Mamlaka ya Bunge hili hatujazungumzia kwa vile imefikishwa Mahakama Kuu ya Tanzania ili kupata tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hili. Tunachoweza kusema ni kwamba jukumu kuu la Bunge hili ni kutengeneza Katiba inayopendekezwa na Bunge ili ifikishwe kwa wananchi waipigie kura ya maoni. Hatua hii ya pili bado inaendelea.

Hatua ya tatu ni pale Bunge Maalum la Katiba tutamkabidhi Mhe. Rais Katiba inayopendekezwa ambayo itafikishwa kwa wananchi ili waikubali kama wataridhika nayo au kuikataa kama haikidhi matarajio yao.

Hatua hii ni ya mwisho wananchi wakiikubali tunapata Katiba Mpya wakiikataa, tunaendelea na Katiba tuliyonayo.

Kilichotokea ni kwamba, wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge hili wameamua kuukiuka utaratibu uliowekwa kisheria. Badala yake wamepeleka Rasimu ya Katiba kwa wananchi wakati mchakato wa kutayarisha Katiba inayopendekezwa bado haujakamilika.

Sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini, ambao kuuhubiri, kuutangaza na kuusimamia ukweli ni moja ya majukumu yetu katika jamii, tumesikitishwa sana na taarifa potofu zinazosambazwa kwa makusudi na makundi, taasisi na vyombo vya habari mbali mbali na tukiwa wajumbe wa Bunge hili ambao tunafahamu kwa kina na tunaridhika na kila hatua ya mchakato huu. Tuna wajibu wa kusahihisha upotofu huu, unaoendeshwa kwa makusudi na hivi kuwaeleza Watanzania ukweli na hali halisi inayojiri hapa Bungeni. Watanzania msifadhaishwe na wala msibabaishwe. Hali ni shwari. Mchakato unaendelea kwa amani na utulivu.

Katika kusahihisha upotofu unaozungumzwa kupitia mijadala na midahalo mbali mbali katika jamii, tunaomba kufafanua hali ilivyo kama ifuatavyo:-

TUHUMA KWAMBA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUKOSA UHALALI Jambo hili si kweli hata kidogo kwani kuna wajumbe wa aina tatu Bungeni ambao wamewekwa na kutambuliwa kisheria. Hawa ni kama wafuatao: 1. Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 2. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. 3. Wajumbe 201 walioteuliwa na Mhe. Rais, baada ya kupendekezwa na Taasisi, Mashirika na makundi mbali mbali nchini, Uhalali wa Bunge unakuwapo wakati wajumbe kutoka makundi hayo matatu wapo Bungeni, na si Vyama vya Siasa pekee. Iwapo kwa mfano wajumbe wa 201 wakiamua kutoshiriki katika shughuli za Bunge, basi sehemu moja muhimu ya Bunge haitakuwapo na uhalali wa Bunge hautakuwepo. Hata hivyo, Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zimeweka idadi ya akidi ambayo ni nusu ya wajumbe wote wa Bunge Maalum. Akidi hii ikifikiwa Bunge huendelea na shughuli zake. Akidi hii hufikiwa kila wakati BungeMaalum linapokutana. Hii inamaanisha kwamba Bunge Maalum la Katiba linaendesha shughuli zake kwa misingi ya sheria na taratibu zilizojiwekea. Bunge lina uhalali wa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.

TUHUMA KWAMBA KANUNI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA ZINAVUNJWA Suala hilo halijawahi kutokea. Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zilipitishwa na wajumbe wote kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sheria Namba 83. Vile vile uendeshaji wote wa shughuli za Bunge zinafanywa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Maalum. Kanuni hizo zinatoa fursa ya Bunge Maalum kuzirekebisha pindi inapobainika ipo haja ya kufanya hivyo kwa mujibu wa kanuni Namba 87.

WARAKA MWINGINE UNAJADILIWA NA SI RASIMU YA TUME Hili nalo si kweli. Tunawahakikishia Watanzania wote kwamba sisi kama Wawakilishi wa Taasisi za Dini miongoni mwa wajumbe wa Kundi la 201, kwa ujumla tunasema hii si kweli. Ni upotoshaji wa makusudi. Tunaijadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ibara kwa ibara. Ibara nyingi zimeachwa kama zilivyo. Kuna ibara ambazo zimeboreshwa au kurekebishwa, kuna ambazo zimeondolewa na kuna nyingine mpya ambazo zimewekwa ili kuweka mambo ya msingi ambayo Rasimu haikuyazingatia au haikuyaona.

WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI, WAJUMBE WA KUNDI LA 201 WA BUNGE LA KATIBA KUPEWA AU KUPOKEA RUSHWA Sisi Wawakilishi wa Taasisi za Dini na Wajumbe wa Kundi la 201 wa Bunge hili tumesikitishwa sana na taarifa hii iliyosambazwa na baadhi ya watu, na kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari aidha kupitia kwenye mijadala, midahalo na makongamano mbali mbali. Baadhi yetu sisi Viongozi wa Kiroho tumeapishwa viapo vya uadilifu katika uongozi wetu wa kiroho na tuko mstari wa mbele kuongoza waumini wetu kuepuka dhambi ya tamaa ya fedha, na kusema uongo. Taarifa kama hizo hazionyeshi heshima kwa dini au nafasi zetu za kipekee katika uongozi wa kiroho. Taarifa hizi zinatangazwa kwa makusudi na watu mbali mbali kupita vyombo vya habari kwa malengo ya kisiasa na kutudhalilisha sisi Viongozi wa kiroho mbele ya umma. Tunaomba tabia hii ikomeshwe.

TUHUMA KWAMBA BUNGE KUWA NA WAJUMBE WACHACHE Hili nalo si kweli. Wajumbe wanaohudhuria Bunge wanakidhi akidi inayohitajika kwa mujibu wa kanuni.

HOJA YA KUSITISHWA AU KUVUNJWA KWA BUNGE MAALUM Hii ni hoja inayozungumzwa katika mijadala mbali mbali katika jamii. Msingi wa hoja hiyo ni kutokuueleza umma ukweli ulioko Bungeni kwa kupeleka taarifa potofu kwa wananchi kwamba Bunge Maalum limekosa mwelekeo. Hatuoni sababu za hoja hii kutiliwa maanani kwa kuwa hakuna sababu za msingi na za kisheria za kufanya hivyo.

HITIMISHO Kumekuwa na taarifa mbali mbali zenye malengo ya ama kuingilia shughuli za Bunge hili au kutudhalilisha sisi wajumbe ambao si Wabunge au Wawakilishi. Wajumbe 201, ambao mchango wao katika mijadala ya Kamati mbali mbali umekuwa na uzito wa pekee, hautambuliki katika taarifa hizo ambazo zimejaa malengo ya kisiasa zaidi kuliko ukamilishaji wa shughuli za Bunge Maalum. Kuna taarifa nyingine zimesambazwa zikiwa na upotoshaji mkubwa, licha ya kwamba Taasisi zinazosambaza taarifa hizo zina wajumbe wake katika Bunge Maalum. Wajumbe hao wangeweza kuzielimisha Taasisi zao ukweli ulipo hapa Bungeni, na hivyo kuwafikishia wasomaji wao taarifa zilizo za kweli na ili kulijengea Bunge hili heshima machoni pa umma wa Tanzania na Kimataifa. Udhalilishaji kama huu unatuumiza hata sisi wajumbe ambao kwa hiari yetu tuliamua kubaki Bungeni na kuyatimiza hayo ambayo tulitumwa tuje tuyakamilishe. Kama tulivyosema hapo awali ni wajibu wetu kama Viongozi wa Dini na Wajumbe wa Bunge hili kuutaarifu umma hali halisi katika shughuli za Bunge Maalum na kuwasihi wapotoshaji kwamba wauheshimu ukweli na wawaheshimu watanzania kwa kuwaeleza ukweli. Ahsanteni sana. ……………………. ………………………… SHEIKH HAMID MASOUD JONGO ASKOFU AMOS JOSEPH MUHAGACHI BAKWATA KIKRISTO TAREHE 3 SEPTEMBA, 2014
 
Tanzania imeendelea kuwa ya matukio. Leo viongozi wa dini wako kimya juu ya Yale yanayoendelea Dodoma. Wanasubili hatua za mwisho, utasikia Mchakato haukuwa wa haki, serikali ilipuuza maoni ya wananchi, ingejadiliwa rasimu ya Warioba, serikali haina dini na kauli nyingine nyingi. Hivi hawa nao si watu wa matukio kweli? Wonders

Subiri kuna jiwe limetupwa la udini gizani .likifika likiwapata utawasikia .let's wait and see
 
Amekeni maaskofu amkeni mashekhe, huu ndio muda wa kusimamma imara bila hofu. CCM wameshaanza kunajisi maoni ya wananchi. Na mmekuwa mkisisitiza maoni ay wananchi yaheshimiwe. msisubiri mpaka mambo yaharibike! TEC< CCT>SHURA YA MAIMAMU>BAKWATA<PCT MPO AU mpo usingizi wa pono? IT is time to act now. SI mnaona wanachokifanya CCM?
 
Katika watu ninaowashangaa na kuwadharau ni viongozi wa dini wa nchi hii. Utawaona wakiwa kimya kabisa wakati wanapoona chama tawala kinavunja sheria za nchi na kukiuka utawala bora. Sasa ngoja wapinzani walianzishe hapo utawaona wote wakijifanya ni bonge la washauri huku wakiwahi kupiga picha na viongozi wa serekali na chama tawala wakiwa mbele ya Tv wanatoa matamko na kujifanya kuiombea nchi yetu amani. Nadhani mnakumbuka yule shehe aliyelia kinafiki pale bungeni kwamba baba wa taifa katukanwa na Tindu Lissu. Leo yuko wapi wakati hata akidi haitimii hapo bungeni!? Viongozi wa dini acheni kujidhalilisha kwa kusubiri kuandaliwa matamko na viongozi walioko madarakani wakati wanachezea utawala bora.
Watu wengine japo sio sehemu ya mada hii ni wanasheria, utawaona ndani ya ofisi zao na magari mazuri wakiwa na masuti mazitomazito, huku kusibiri kesi za viwanja lakini hili la katiba huwezi kuwatofautisha na watu wa vijijini wenye uelewa finyu wa sheria.
 
Amekeni maaskofu amkeni mashekhe, huu ndio muda wa kusimamma imara bila hofu. CCM wameshaanza kunajisi maoni ya wananchi. Na mmekuwa mkisisitiza maoni ay wananchi yaheshimiwe. msisubiri mpaka mambo yaharibike! TEC< CCT>SHURA YA MAIMAMU>BAKWATA<PCT MPO AU mpo usingizi wa pono? IT is time to act now. SI mnaona wanachokifanya CCM?
Hawa mara nyingi ndio vichochezi wa vurugu. Leo wako kimya, mchakato ukimalizika utasikia wanaubuka na matamko hafifu. Kinga ni bora kuliko tiba.
 
Tanzania imeendelea kuwa ya matukio. Leo viongozi wa dini wako kimya juu ya Yale yanayoendelea Dodoma. Wanasubili hatua za mwisho, utasikia Mchakato haukuwa wa haki, serikali ilipuuza maoni ya wananchi, ingejadiliwa rasimu ya Warioba, serikali haina dini na kauli nyingine nyingi. Hivi hawa nao si watu wa matukio kweli? Wonders

Viongozi wa dini walishauri UKAWA warudi bungeni wakagoma laana ya viongozi wa dini UKAWA mliowadharau itawala huko mliko nje ya bunge.Ndio maana wameamua kunyamaza na kujilalia kimya.
 
Viongozi wa dini walishauri UKAWA warudi bungeni wakagoma laana ya viongozi wa dini UKAWA mliowadharau itawala huko mliko nje ya bunge.Ndio maana wameamua kunyamaza na kujilalia kimya.
Walikaa na UKAWA kuzungumza kwa mapana na marefu juu ya sababu zilizowatoa bungeni? Mbona wenyewe walikuwa mstari wa mbele kutuaminisha juu ya Yale waliyohitaji? Kutokana na uchakachuaji unaoendelea bungeni, huoni dalili za viongozi wa dini kujiingiza hatua za mwisho kupinga Yale yatakayo kuwa yamepitishwa?
 
Back
Top Bottom