Vijana nguvu kazi inayotumiwa vibaya kwa hasara ya Taifa

Phillipo Bukililo

JF-Expert Member
Dec 29, 2015
18,487
13,612
Jana mchana nikiwa nakatiza katika maeneo karibu na Posta ya zamani nikielekea maeneo ya pale kanisa la Saint Joseph pembeni kidogo ya Shule ya forodhani, jamaa fulani walipita na gari kwa kasi, bahati kwao wakaangusha mfuko uliokuwa na fedha, kwa haraka zilikuwa kama shilingi milioni tatu au nne. Kitendo cha fuko lililokuwa na fedha kuanguka katikati ya barabara, kilitosha kuwafanya vijana wengi waibuke kutoka posta ya zamani, wengine waibuke kwa haraka kutoka katika vile vibanda vya wakatishaji tiketi za boti ziendazo Zanzibar. Yaani watu hawakujali magari mengi ya saa saba mchana, wote walikimbilia barabarani wakaanza kupigania fedha zilizoangushwa na gari iliyopita kwa kasi. Kilichonifanya niwe makini zaidi ni ukweli kuwa vijana karibu wote waliogombe fuko la fedha wana umri kati ya miaka 18-35, umri wa kuzalisha lakini wapo vijiweni.

Likanijia wazo kwamba serikali ina kazi ngumu sana katika kutatua tatizo zito sana la ajira. Ipo haja kwa serikali kuimarisha kwa nguvu zote elimu ya ufundi (VETA), ili wahitimu wengi zaidi ya masuala ya ufundi waweze kuingia moja kwa moja katika ajira za viwanda ambavyo vilitumika kama agenda ya CCM wakati wa uchaguzi. Tanzania ya viwanda haiwezi kuwepo ikiwa tuna uhaba wa mafundi na vijana wengi wenye elimu ya ufundi, upo uhusiano kati ya viwanda na ufundi wa aina mbalimbali. Bajeti ya wizara ya elimu iboreshwe kwa lengo la kuipatia nguvu sekta ya ufundi.

Kingine muhimu ni serikali kuyatumbua majipu katika sekta nzima ya michezo. BMT na TOC ni majipu yanayohitaji kutumbuliwa tena mapema sana. Haingii akilini kamati ya olimpiki kimataifa inaipatia TOC fedha nyingi kila mwakani lakini kwenye olimpiki tunapeleka watalii badala ya kupeleka washiriki. Uongozi wa TOC ni wa miaka mingi sana,hauna kabisa ubunifu unaotakiwa katika karne ya sasa. Hiyo BMT haina ubunifu wowote ule, viongozi wake wanachokijua ni kusoma risala wakati wa kukabidhi bendera ya Taifa wakati washiriki wanajiandaa kwenda kuwakilisha taifa. Serikali izifumue upya kabisa hizi taasisi mbili yaani BMT na TOC ili ziweze kuendana na mahitaji ya ushindani katika sekta zote za michezo.

Tanzania ina nguvu kazi kubwa sana, lakini inapotea mitaani, huku wakati mwingine ikisubiri watu kwa bahati mbaya waangushe mifuko ya fedha ili waweze angalau kupata milo ya siku mbili au tatu. VETA itazamwe upya, ili vijana wengi waweze kupata elimu ya ufundi wa aina mbalimbali. BMT na TOC na zenyewe ni majipu yenye kuchangia kuwafanya vijana wengi washindwe kuitumia michezo katika kujipatia ajira.

Hizi ajira za kuendesha boda boda na bajaji zipo mijini na zinategemea zaidi maendeleo ya sekta nyingine, sio za kutegemewa kama ndio kila kitu kwa maisha ya vijana. Ufundi na michezo ni vitu vinavyopaswa kutazamwa kwa umakini sana ili jeshi kubwa la wasio na kazi haswa vijana liweze kusaidiwa. Haya ni maoni yangu tu, wadau karibuni kwa mijadala.
 
Back
Top Bottom