UVCCM ni kuwadi wa ufisadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

UVCCM ni kuwadi wa ufisadi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Najijua, Apr 27, 2011.

 1. Najijua

  Najijua JF-Expert Member

  #1
  Apr 27, 2011
  Joined: Nov 5, 2010
  Messages: 1,029
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) uliundwa kwa lengo la kuwaunganisha na kuwaandaa vijana wa Tanzania ili kulinda na kutetea mapinduzi ya Afrika.
  UVCCM ilikuwa jumuiya miongoni mwa jumuiya za CCM iliyopewa jukumu la kuatamiza na kulea fikra za kimapinduzi na kurithisha uzalendo kwa kizazi cha vijana na chipukizi. Vijana wa CCM walikuwa mstari wa mbele katika kupinga dhuluma, rushwa, vitisho na aina zote za uonevu.
  UVCCM ilipoteza mwelekeo wa kuwa jumuiya ya kutayarisha vijana wenye maadili na kugeuka “chaka” la kuatamiza na kulea fikra za kifisadi. Sehemu kubwa ya vijana waliyopewa dhamana ya kuiongoza jumuiya hiyo wamefanywa na au wamejigeuzwa makuwadi wa kushabikia ufisadi ndani na au nje ya mfumo wa chama.
  UVCCM imeacha kuwa mkusanyiko wa fikra za kizalendo na kuwa ‘genge’ la vijana wenye hila, choyo, tamaa, na husuda kwa kutamani uwakala wa kifisadi.
  Wakati Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ya CCM ikinadi kujivua gamba la ufisadi, UVCCM imejivika ukuwadi wa ufisadi kwa jinsi ya kuifanya jumuiya hiyo ionekane tofauti na dhamira ya kuchukia na au kupambana na ufisadi wa aina zote uliyoifanya CCM ipoteze haiba ya kisiasa mbele ya wanachama na wananchi wa Tanzania.
  Kama jumuiya, na kwa jinsi ilivyosheheni viongozi waandamizi waliyowekwa kwa misingi ya kufanya kazi ya ukuwadi na baadhi ya mafisadi wenye majina ya kifisadi; UVCCM imepoteza mvuto kwa vijana wengi!
  Wakati wa enzi za chama kushika hatamu, UVCCM ilikuwa jumuiya muhimu sana katika kuhakikisha kwamba CCM inapata vijana makini wenye kutumia busara ya chama na hekima ya uongozi katika kujenga jamii ya vijana wenye ari na utashi wa kulitumikia taifa lao.
  Hata hivyo, baada ya CCM kugeuzwa kampuni ya mafisadi wenye hisa nyingi na kuharibika kwa mfumo wa ndani na mfumo wa nje – yaani, chama na serikali; vijana waliopewa nafasi ndani ya UVCCM wamekata tamaa mbele kwa maslahi ya mtandao wa kifisadi uliowekeza mtaji wa ufisadi ndani ya jumuiya hiyo.
  Japokuwa kwa sehemu fulani viongozi wa UVCCM wanaweza kuonekana kama si sehemu ya ufisadi wa kimfumo na wa ndani ya mfumo unaoonekana sasa kwa CCM; hata hivyo, ukweli unaofahamika ni kwamba viongozi hao hao ndio wale waliowekwa na mafisadi ambao CCM taifa wameapa kuwashughulikia!
  Ukiachilia mbali Mwenyekiti wa UVCCM taifa aliyelazimishwa na ‘mfumo wa kifisadi’ ndani ya jumuiya hiyo kujiuzulu kutokana na kuharibu ukweli juu ya umri wake; kuna mfumo tata ndani ya jumuiya hiyo unaosadifiana na ule uliyomo ndani ya CCM taifa.
  Jumuiya ya UVCCM, kwa zama hizi za ufisadi, imefanywa kama kitivo cha kufundisha na au kueneza itikadi ya ufisadi miongoni mwa vijana wanaodhamiria kubaki kwenye siasa za kifisadi kwa kutumiwa na au kuwatumia mafisadi waliyewekeza kwenye mfumo wa kifisadi ndani ya CCM.
  Hakika na ukweli unaopatikana kwenye mduara wa ndani wa vijana (viongozi waandamizi wa UVCCM) wana mafungamano ya kifisadi na mafisadi wa ndani ya CCM.
  Hata kama wengi wa vijana wanaoburuzwa na walio nje ya mduara wa uongozi wa UVCCM hawauoni mfumo wa ufisadi uliyoimeza jumuiya hiyo; bado kuna kila dalili za kuwepo kwa sintofahamu na au songombingo juu ya kuwepo kwa viongozi wa UVCCM wenye nafasi ndani ya jumuiya hiyo wanaotokana na mchakato uliyofummwa na au kutengenezwa na mafisadi na hatimaye kusimamiwa kifisadi hata kuifanya jumuiya hiyo kufanya kazi za kifisadi kwa maslahi ya mafisadi papa!
  Kwa jinsi hii, UVCCM imepasuka katika sehemu kuu tatu; kundi la viongozi mafisadi; kundi la viongozi wanaofanya ukuwadi wa kifisadi; na kundi la vijana wasiyokuwa na sauti ndani ya jumuiya. Kundi hili la mwisho, yaani kundi la vijana wasiokuwa na sauti ndani ya UVCCM ni kubwa na ndilo linaloonekana kutokujua nini kinafanyika kwenye mzingo wa ndani wa UVCCM.
  Vijana wengi wanaoburuzwa na mawazo ya watu wachache wenye fikra za kifisadi wamefanywa kama sehemu ya kuthibitisha utashi wa watu wachache wanaokula fadhila na au mapato ya ufisadi kwa tamaa na uchu wa kuongoza kifisadi!
  Na kwa jinsi mfumo wa ufisadi ulivyofumwa ndani ya jumuiya hiyo, kundi kubwa la vijana haliwezi kuona au kupata taarifa rasmi za utendaji wa ndani wa jumuiya hiyo.
  Hali hii inasababisha sehemu ndogo ya viongozi waandamizi wa UVCCM na wenye mafungamano na mahusiano na mafisadi papa wa CCM watawale maamuzi yote ya kijumuiya na kuathiri moja kwa moja utendaji wa jumuiya na CCM kwa jumla.
  Japokuwa neno lililotumika kubeba dhana ya makala haya, yaani ‘kuwadi’ si mujarabu sana kutumiwa kwa vijana wa CCM; imelazimu kulitumia kwa vile sifa na tabia za kuwadi ni kufanya ushawishi wa kufanyika kwa vitendo vya utalaleshi (ukuwadi). Na kwa kuwa viongozi wa UVCCM wamekuwa wakitumiwa na mafisadi katika kutimiza dhamira chafu juu ya kuharibu mfumo wa uendeshaji wa chama na serikali inayotokana na chama; kwahiyo, ukuwadi unaofanywa na viongozi wa UVCCM juu ya kuendesha siasa za kifisadi ni kinyume na maadili ya mwendo murua wa siasa kwa vijana.
  Kwa kuwa CCM imemezwa na ufisadi uliokomaa (wa kimfumo na wa ndani ya mfumo); na kwa kuwa mafisadi walioimeza CCM ndiyo waliowameza viongozi wa UVCCM; kwa hiyo basi, ni wakati muafaka kwa UVCCM (kama jumuiya) kujisanifu na kujisafisha kama inataka kubaki kwenye malengo ya kuundwa kwake.
  Na kwa jinsi hiyo, ndivyo inavyoweza kuwa kitivo cha kujenga fikra za kimapinduzi na kuatamiza uzalendo kwa vijana kutamani kufia nchi yao badala ya sasa vijana kufia ufisadi na au hata kujitoa muhanga kutetea na kusimamia miradi ya mafisadi!
  UVCCM imekuwa inasisitiza na kubariki misimamo ya kifisadi ndani ya mfumo tata wa ufisadi uliyojengwa na kusimamiwa na mafisadi wa ndani na nje ya mfumo wa jumuiya; na kwa jinsi ya kuifanya jumuiya ya vijana (UVCCM) kuwa kama wakala wa mafisadi katika kusimamia, kushabikia mambo yasiyofaa kama vile kupeana nafasi za chama na au serikali kwa misingi ya urafiki), udini, ukanda, uanafamilia, na vitisho vya kimamlaka; kuna kila sababu ya kudhani kwamba jumuiya hiyo ni tunda la ufisadi mpevu!
  Viongozi waandamizi wa UVCCM wamekuwa wakipatiwa usaidizi na baadhi ya wafanyabiashara wenye mafungano ya kifisadi katika kujenga msonge wa uongozi wa kifisadi ndani ya jumuiya na chama kadhalika.
  Hali hii imewafanya baadhi ya viongozi hao kujihusisha moja kwa moja na mitandao ya mafisadi iliyoundwa na mifumo ya kifisadi katika kutafuta kujijenga ndani ya CCM na nje yake ili kufanikisha malengo ya kuendeleza ufisadi ndani na nje ya mfumo wa uongozi wa chama na serikali kwa kipindi kirefu kinachokuja.
  UVCCM, hususani uongozi wa juu, umekuwa ukijijenga kwa misingi ile ile inayotumiwa na mafisadi waliyomo kwenye kamati kuu (CC) na halmashauri kuu (NEC) ya CCM kwa kutumia fedha chafu na au kujilimbikizia fedha kwa minajili ya matumizi kwenye chaguzi za ndani ya jumuiya na ndani ya chama kadhalika.
  Kwa kuwa sehemu ya viongozi wa juu wa UVCCM wana ushawishi ndani ya vikao vya maamuzi vya CCM,mafisadi wamepata mtaji wa kuwekeza ili kupata uungwaji mkono juu ya kupata manufaa ya kifisadi – malipo ya ukuwadi!
  Ni mara chache sana kuona viongozi wa ufisadi wakijitokeza hadharani kujibu tuhuma na au mapigo yanayotokana na mashambulizi juu ya ufisadi unaofanywa na watu hao wenye roho mbaya, uchu na tamaa ya kutumia fursa za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa manufaa binafsi.
  Kwa jinsi hiyo, mafisadi huwatumia viongozi wa UVCCM kujibu tuhuma na au mapigo kwa niaba ya mafisadi. Tulishuhudia viongozi waandamizi wa UVCCM walivyochukua dhima ya kuwajibia tuhuma za ufisadi mafisadi papa waliyoifanya CCM ijivue “gamba la ufisadi”.
  Katika hali isiyokuwa ya kawaida, viongozi waandamizi wa UVCCM walikwenda mbali hata kudiriki kuonyesha jinsi mafisadi walivyowalewesha na ulevi wa fedha chafu zinazotokana na ufisadi kwa kule kuonekana wazi kwamba na wao (viongozi wa UVCCM) wanatamani mapato ya ufisadi kwa vile wale wanaowasimamia wamewaahidi kula nao “sahani moja”.
  Kwa jinsi hiyo, wale wote waliokuwa wakiwashambulia mafisadi wanyamaze ili na wao (viongozi wa UVCCM na mafisadi wanaowasimamia) wale kama waliotangulia walivyokula!
  Hakika huu ni mtazamo mbaya wa kifisadi! Na kwa mwendo huu, jumuiya hii ya vijana wa CCM imekosa adabu na hadhi ya kuwa kitivo cha fikra za uzalendo! Ilidhaniwa kwamba kama jumuiya ya chama yenye dhima ya kuatamiza na kulea fikra za kimapinduzi na uzalendo kwa vijana wangechukuwa hatua za kuanzisha mapambano endelevu dhidi ya ufisadi; badala yake, UVCCM imechukua mwelekeo wa kuutetea ufisadi! Hii ni hatari kwa vijana!
  Kwa ujumla, viongozi waandamizi wa UVCCM wamemezwa na au kuwekwa kwenye mazingira ya kutumiwa na mafisadi kama vile walivyomezwa viongozi wa CCM taifa. UVCCM taifa wanatamani kuishi kifisadi kama wanavyoishi mafisadi papa wa ndani ya CCM taifa; na zaidi viongozi wa UVCCM wamefikia hatua ya kudhani kwamba jumuiya hiyo ni kampuni na au mali yao na wanafanya vile wanavyoona inafaa kwa utashi na au matakwa ya mafisadi wanaowatumikia na au kuwawakilisha na kuwakuwadia.
  Katika mazingira yenye kujenga chama chenye mwelekeo wenye aina zote za ufisadi, UVCCM imeamua kuanzisha mafungamano yenye taswira ya utetezi wa maovu na kuchukia ukosozi kama ilivyoanishwa kwenye kanuni na ilani ya kuanzishwa kwake.
  Vijana wamefanywa mtaji wa kuwatumikia mafisadi kwa jinsi ya malipo ya kifisadi kwa aidha kupewa posho au uongozi kwenye kada za chini ya msonge wa uongozi wa chama na au serikali. Vijana wamepoteza sura ya vijana wa enzi za akina Sethi Benjamin (aliyekufa akiunga mkono Azimio la Arusha).
  Siasa inayoendeshwa na UVCCM imekuwa ikitumiwa na baadhi ya mafisadi ndani ya CCM taifa katika kufanikisha mipango ya kimafia, kitapeli na kijambazi katika kuhujumu uendeshaji wa serikali.
  Vijana wamefanywa mtaji wa kufanikisha malengo ya kiuwendawazimu yanayoongozwa na watu wenye nia ya kuvuruga uendeshaji wa uhuru, haki na usawa wa uchumi, siasa na jamii!
  UVCCM wanashangilia mizania isiyo sawa baina ya walionacho na wasiyonacho kwa kuwa jumuiya hiyo imekuwa ikineemeka na mfumo wa kifisadi unaowapa fursa na nafasi mafisadi wenye uchu na uroho wa kutawala satwa ya maamuzi ndani ya chama na serikali.
  Ufisadi wa UVCCM na kushindwa kufanya kazi za kuihuisha jumuiya hiyo ili itoe mchango chanya kwa maendeleo ya vijana umeifanya kada ya vijana kumezwa na vijana (na hata watu wazima) wenye utashi wa kutumia jumuiya hiyo kama sehemu ya kufanikisha mipango ya kuingia kwenye mawanda ya uongozi kwa jinsi ambayo hakuna anayeweza kuona kwamba aliyepo anatokana na mtandao wa kifisadi.
  Na ndiyo maana, tunashuhudia minyukano na au vuta-n-kuvute zisizoisha ndani ya jumuiya hiyo na uingilaji kati wa mafisadi kwenye utendaji wake!
  Na kwa kuwa CCM taifa imedhamiria kujivua gamba la ufisadi; na kwa kuwa mafisadi waliyomo ndani ya CC na NEC ya CCM ndiyo waliyowekeza kwenye UVCCM; bado kuna kila sababu kwa UVCCM kuvunjwa na au kufumuliwa na kuundwa upya! Haya ni maoni yangu (mimi kama mwandishi).
  UVCCM imesheheni viongozi wanaofanya kazi ya ukuwadi wa kufanikisha ufisadi wa kimfumo na wa ndani ya mfumo; na kwa jinsi hiyo, kujivua gamba la ufisadi kulikofanywa na CCM ni budi kufanywe kwenye “chaka la ufisadi – UVCCM” ambako wamejificha wakuwadi wa mafisadi wanaotumika kuatamiza fikra za kifisadi kwa vijana na hatimaye kuifanya nchi ishindwe kupambana na adui huyu wa haki za wananchi – ufisadi!
  Vijana wa CCM, kama walivyo wengine Tanzania, wanahitaji uhuru wa fikra za kimapinduzi na uzalendo! Mapinduzi ya fikra yatakayowaondolea unyonge wa kutawaliwa na fikra za kifisadi.
  Vijana wa CCM wanahitaji mtazamo mpya wa kuchukia ufisadi, uonevu, vitisho na aina zote za dhuluma zinazofanywa na mafisadi wa ndani ya CCM waliochimbia ndani ya CC na NEC kwa kisingizio cha kufadhili chama na au kutoa usaidizi kwenye miradi ya kiuchumi ya chama au jumuiya huku wakizitumia fursa hizohizo kujijenga kifisadi.
  Vijana wa CCM wasitamani maisha ya kifisadi na kutumia fursa za ufisadi katika kujijenga katika uongozi wa chama na au kutafuta nafasi ndani ya serikali katika kuendeleza ufisadi wa kimfumo na wa ndani ya mfumo.
  Ni wakati wa kujenga fikra chanya juu ya kuwatumikia vijana wa Tanzania kwa uhuru, haki na usawa katika kuhakikisha kwamba aina zote za ufisadi zinatokomezwa ndani na nje ya UVCCM na CCM kadhalika. Hakuna manufaa ya kudumu kwenye ufisadi isipokuwa ni laana itakayokiangamiza chama na kukifuta kwenye ramani ya vyama vya wakulima na wafanyakazi.
  Mwisho wa makala hii natoa rai kwa vijana wa UVCCM na wengine; kuchukia aina zote za ufisadi wa kimfumo wa ndani ya mfumo.

  Kwa jinsi hiyo, vijana popote walipo wawachukulie hatua za makusudi mafisadi kwa kuwakataa na kuwaondoa kwenye nafasi zao ili kujenga mujtamaa murua kwa maisha yao na ya kizazi cha vijana wa Tanzania.

  Ni vyema vijana wakakumbuka vijana waliojitolea kulitumikia taifa hili kwa uhuru, haki na usawa na hata kukubali kufa katika kutetea maadili ya siasa ya kuwatumikia wananchi kwa haki, usawa na insafu.
  Tanzania bila ya ufisadi inawezekana; vijana watimize wajibu wao na wasimamie maadili ya taifa. Mungu ibariki Tanzania!
   
 2. K

  Kana Amuchi Member

  #2
  Apr 27, 2011
  Joined: Jul 21, 2009
  Messages: 70
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Never interrupt your enemy when he is making a mistake. As far as i am concerned, UVCCM can go hang.!
   
Loading...