Utamu wa biriani

Ado Shaibu

Member
Joined
Jul 3, 2010
Posts
99
Reaction score
111

UTAMU WA BIRIANI
Utamu wa biriani
Si harufuye puani
Au rangiye machoni
Haitoshi asilani

Uzuri wa biriani
Tonge liende kinywani
Ladha nono ulimini
Rahaye paka moyoni

Mithili ya biriani
Mke hapimwi machoni
Uzuri wa maungoni
Hautoshi niamini

Uzuri wa mke jamani
Awe mjuvi jikoni
Tabia njema moyoni
Na ufundi ubaoni

Kisha ‘achaji’ kichwani
Akushauri mwandani
Mume ukiwa gizani
Akurudishe mwangani

Biriani ya thamani,
Hailiwi majiani
Watu huketi mbachani
Wamejisitiri ndani

kama kwako wa thamani
Mithili ya biriani
Chukua umweke ndani
Siwe kama wa mwituni

Sasa uwanja ni wenu
Wanawake zamu yenu
Mume afaaye kwenu
Sifaze tupe fununu

©Ado Shaibu ( Komredi wa Malenga )
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…