Hivi karibuni baada ya Agizo la Rais kutokuruhusu mabinti wa shule waliopata mimba (wamekuwa tayari wazazi) kuendelea na shule, kumekuwa na malumbano katika kila kona ya nchi na majadiliano makali kwenye mitandao ya kijamii, kuhusu uhalali wa Agizo hilo. Lakini swali ni "Tatizo la mimba za utotoni likabiliwe vipi?'. Sio nia ya bandiko langu hili kutoa jawabu ila kuibua mjadala katika maono mapana ya mahusiano kati ya mwanamke na mwanaume, Tanzania.
SEHEMU YA KWANZA
Kuna hoja kwamba harakati za wanawake kujikomboa kutokana na unyanyasaji wa kijinsia, kujiletea maendeleo na kuwa jamii inayotambulika kama binadamu sawa, hazifanikiwi na wala hakuna matumaini ya kutosha ya kufanikiwa. Kwamba kuwepo kwa sheria kali, zenye mlengo mmoja wa kuzuia vitendo vya aina yoyote ya ubaguzi wa kijinsia na unyanyasaji wa wanawake, hakuzuii wala kuondosha unyanyasaji huo. Ukweli wa hoja hizi ni upi? Kama kuna ukweli ni kitu gani kifanyike ili kuondoa dosari hizi katika jamii? Je, Mkutano wa Beijing 1995 umekwishaleta mabadiliko gani katika mtizamo wa kijinsia kijamii, kisiasa na kiuchumi? Sheria mpya ya kujamiana, je, ni jawabu la kuondosha vitendo viovu dhidi ya wanawake, binadamu wanyonge na dhaifu?
Hayo ni baadhi ya maswali mengi tu ambayo yamo ndani ya vichwa vya watu wanaopenda na kupigania haki na usawa kwa wote. Kwa jinsi ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini ulivyokuwa unapingwa na Jumuiya yote duniani na ndivyo unyanyasaji kijinsia unavyopingwa na jumuiya yote duniani. Lakini, pengine ambalo halieleweki bayana ni jinsi gani unyanyasaji huu unaweza kuondolewa kwa kasi zaidi kuliko ilivyo. Kwamba ni budi kutunga sheria kali kali au kurejea utamaduni, mila na desturi za jamii ambazo inaaminika zimechangia kuleta tofauti hizi.
Hoja hii inatokana na hisia walizokuwa nazo wanaume kwa wanawake wa Tanzania kufuatia kupitishwa kwa sheria mbalimbali zinahusu mahusiano katika jamii kati ya wanaume na wanawake. Sheria hizi ni kama vile Sheria ya Ardhi ya Vijiji (1999), Sura ya 113 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002; Sheria ya Ndoa (1971); Sheria ya Mirathi (1989); na Sheria ya Makosa ya Kujamiana (1998) na agizo la Rais kutokuruhusiwa mabinti waliopata mimba shuleni kuendelea na shule.
Wako ambao wanaamini kwamba sheria hizi na magizo ya Rais, yatadhibiti na kuondosha vitendo viovu dhidi ya wanawake. Msingi wa kutungwa sheria hizo, na agizo la Rais, ndio yanayowapa hawa matumaini ya aina hii. Lakini kwa upande mwingine, wako wa kundi lingine ambalo linaamini kwamba wanawake wengine wanaitumia sheria hizo, na/au agizo la Rais kulipiza kisasi au kukomoana kwa nia ya kujitajirisha au kukidhi matakwa yao binafsi. Hakuna la ajabu kwa wenye fikra za aina hiyo kwani hata nchi zilizoendelea, zenye sheria ya aina hiyo, wako wanaoitumia vibaya. Pengine liletalo utata ni pale sheria zinapoonekana kwa wengi, ama kwa kutokuzielewa au kutokuwa wazi kuhusu uhusiano wa kawaida kati ya mwanamke na mwanaume kwamba hata kukonyeza ni kosa sheria. Kwa hofu hiyo hawa wanajiuliza ni kwa jinsi gani watu wawili wataanzisha mapenzi pasipo kuonekana kwamba mmoja anamnyanyasa mwenzake kijinsia.
ITAENDELEA