Utajiri wa nchi wazidi kuporwa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Utajiri wa nchi wazidi kuporwa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by EL+RA=UFISADI, Sep 18, 2010.

 1. E

  EL+RA=UFISADI Member

  #1
  Sep 18, 2010
  Joined: Jul 4, 2010
  Messages: 56
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Utajiri wa nchi wazidi kuporwa

  * Wizara ya Maliasili yaendelea kuwa pango la wizi
  * Ujangili, ukwepaji wa kodi za serikali washamiri

  MWANDISHI WETU
  Dar es Salaam

  LICHA ya serikali ya Tanzania kupoteza mapato makubwa kutokana na mikataba mibovu ya madini na ubadhirifu wa fedha za umma, uchunguzi mpya umebaini kuwa kiasi kikubwa cha utajiri wa nchi unaotokana na maliasili zake umekuwa ukiporwa na kutoroshewa ughaibuni na wajanja wachache, KuliKoni imebaini.

  Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Profesa Craig Packer wa Chuo Kikuu cha Minnesota nchini Marekani akishirikiana na wataalam wengine nchini Marekani, Uingereza na Tanzania, serikali inapoteza mapato makubwa katika sekta ya uwindaji wa kitalii.

  Ufisadi na usimamizi mbovu wa sekta hii umesababisha kuwepo kwa uwindaji holela wa wanyama pori unaofanywa na watalii kiasi cha sasa kutishia idadi ya simba na chui kwenye mbuga za wanyama za taifa.

  Utafiti huo umebaini kuwa uwindaji wa simba na chui nchini uko juu sana na unahatarisha maliasili hiyo ya nchi.

  “Idadi ya simba na chui Tanzania itaporomoka iwapo serikali haitahakikisha kuwa wanyama wachache zaidi wanauliwa na wawindaji,” imesema sehemu ya utafiti huo mpya wa profesa huyo wa Marekani.

  Inasemekana kuwa idadi kubwa ya wanyama pori hao wanawindwa Tanzania wakiwa kwenye umri ambao haukubaliki.

  “Tanzania hivi sasa ina idadi kubwa ya simba na chui kulinganisha na nchi nyingine za Afrika, lakini wanyama hawa wamekuwa wakiwindwa kwa idadi kubwa sana na wakiwa kwenye umri mdogo,” imesema sehemu ya utafiti huo.

  Serikali ya Tanzania sasa hivi inaruhusu simba 500 na chui 400 kuuliwa kila mwaka kwa kuwindwa na watalii kwenye mbuga za wanyama pori zenye eneo la kilomita za mraba 300,000.

  Hii ni sawa na wastani wa simba 1.67 kuuawa kwa kila kilomita 1,000 za mraba na chui 1.3 kwa kila kilomita 1,000 za mraba.

  Maeneo makubwa ya nchi yametengwa kama vitalu ambapo makampuni binafsi yamekuwa yakiendesha shuhuli za uwindaji wa kitalii.

  Serikali imeweka kikomo cha idadi ambayo wanyama pori wanaruhusiwa kuwindwa kila mwaka, lakini utafiti unaonesha kuwa kikomo hiki bado kiko juu na inabidi kishushwe zaidi.

  Pia kumekuwepo na madai kwamba wanyama wanawindwa kupita kikomo hiki kilichowekwa na serikali kutokana na usimamizi mbovu na baadhi ya maafisa wanyama pori kupokea rushwa kutoka kwenye makampuni ya uwindaji ili waruhusu simba na chui wengi zaidi kuuliwa na watalii kwa ajili ya ngozi zao.

  Utafiti huo uliochapishwa kwenye jarida la kimataifa la “Conservation Biology” umeonesha kuwa idadi ya simba kwenye vitalu vya uwindaji Tanzania imeshuka kwa asilimia 50 kati ya mwaka 1996 na 2008 kutokana na “uvunaji” usio endelevu wa maliasili za nchi.

  Ikilinganishwa na hifadhi za wanyamapori nchini Tanzania ambapo uwindaji wa simba hauruhusiwi, idadi ya wanyama pori hawa imebaki kuwa ya kuridhisha.

  Idadi ya chui imebaki kuwa ya kuridhisha kwenye maeneo mengi nchini, ingawa kumekuwa na upungufu wa wanyamapori hawa kwenye maeneo ya magharibi kaskazini na kuzunguka hifadhi ya Serengeti.

  Wataalamu wameonya kuwa huenda wawindaji wa kitalii sasa wanaanza kuwalenga chui zaidi baada ya idadi ya simba kuanza kupungua.

  Imeshauriwa kuwa serikali ya Tanzania ipunguze idadi ya wanyama pori wanaowindwa kila mwaka ili kulinda maliasili ya taifa isizidi kupotea.

  Watafiti wamesema serikali ipunguze kikomo cha uwindaji mpaka kufikia wastani wa simba 0.5 na chui 1.0 kwa kila kilomita 1,000 za mraba kwa mwaka, huku idadi kubwa kidogo ikiruhusiwa kwenye mbuga ya wanyama ya Selous.

  Serikali pia imeshauriwa kuhakikisha kuwa simba na chui wenye umri mkubwa tu ndiyo wanaruhusiwa kuwindwa.

  “Ingekuwa vyema kuhakikisha kuwa simba dume tu wenye umri wa zaidi ya miaka sita ndiyo waruhusiwe kuwindwa,” amesema Profesa Packer kwenye utafiti huo wa wanyamapori wa Tanzania.

  "Kwa miaka mingi, makampuni yamekuwa yakitimiza idadi ya wanyama wanaoruhusiwa kuwinda kwa kuuwa simba dume ambao bado hawajazeeka.”

  Watafiti wanasema utaratibu huu si endelevu kwani simba dume huwa wanauwa watoto waliozaliwa kutokana na simba dume wengine, hivyo kuwinda simba dume walio kwenye umri wa kuzalisha ni makosa.

  "Kama jambo hili likitokea mara kwa mara, idadi ya simba itaporomoka sana. Ni muhimu kuhakikisha kuwa simba dume wazee tu ndiyo wanawindwa,” amesema Profesa Packer.

  Wataalam wameshauri pia kuwa chui wenye umri wa miaka 7 na kuendelea tu ndiyo waruhusiwe kuwindwa.

  Kama serikali ya Tanzania itapuuza ushauri huu, uwindaji utaendelea kuwa holela na serikali itazidi kupoteza mapato yanayotokana na uwindaji wa kitalii, amesema Profesa Packer.

  Hata hivyo, ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kutoa takwimu kuhusu uwindaji wa wanyama pori wakati nchi nyingine za Afrika kama Zambia na Zimbabwe hufanya shughuli hizo kuwa ni siri.

  Hivi sasa kuna vitalu vya uwindaji vipatavyo 150, huku Selous ikiwa na vitalu 40 na ndiyo eneo muhimu zaidi la uwindaji hapa nchini.

  "Serikali ya Tanzania imekuwa ikipata mapato finyu kutoka kwenye makampuni ya uwindaji na hivyo kushindwa kulipa mishahara ya kutosha kwa maafisa wanyama pori,” amesema.

  Hivi karibuni, shehena kubwa ya meno ya tembo kutoka Tanzania ilikamatwa kwenye mji wa Hong Kong ikiwa ni uendeleaji wa kuporwa kwa maliasili ya taifa.

  Shehena hiyo ya tani 1.55 ya meno ya tembo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.4 (sawa na shilingi bilioni 2.1) ni mzigo mkubwa zaidi kukamatwa Hong Kong katika kipindi cha miaka kumi.

  Kukamatwa kwa shehena hii kumedhihirisha jinsi serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilivyoshindwa kabisa kuzuia ujangili wa wanyama pori na usafirishaji wa maliasili za nchi kwenda ng’ambo kwa njia za magendo.

  Kwa mujibu wa shirika moja la kimataifa lenye makao yake makuu jijini London nchini Uingereza linalojulikana kama “Environmental Investigation Agency,” karibu asilimia 50 ya biashara haramu ya dunia ya meno ya tembo inatokea Tanzania.

  Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, amewahi kusema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inanuka rushwa kutokana na kuwepo kwa ujangili wa kutisha na usafirishaji wa makontena ya meno ya tembo. Wizara hiyo pia imekuwa ikishutumiwa kwa usafirishaji haramu wa magogo kwa ajili ya mbao

  Mwaka 2007, shirika la TRAFFIC International lilitoa ripoti ya kutisha inayoonesha kuwa Tanzania inapoteza mamilioni ya dola za Marekani kila mwezi kutokana na biashara haramu ya magogo, mbao na mazao mengine ya misitu.

  Ripoti hiyo ilibaini kuwepo kwa ufisadi mkubwa, ukataji wa miti haramu na usafirishaji wa magogo kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria na pasipo kulipa kodi.

  Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utafiti uliofanywa kati ya mwaka 2004 na 2005 ulionesha kuwa Tanzania imekuwa ikipoteza mapato ya kodi ya dola za Marekani milioni 58 (sawa na shilingi bilioni 87) kila mwaka kutoka kwenye sekta ya misitu.

  Shirika hilo lilielezea hali hiyo kuwa kama “Janga la Taifa” na kusema kuwa zaidi ya nusu ya makampuni 28 yanayojihusisha na biashara ya magogo nchini yanamilikiwa na vigogo serikalini, wakiwemo maofisa waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

  (Source: KULIKONI)
   
 2. Baba_Enock

  Baba_Enock JF-Expert Member

  #2
  Sep 18, 2010
  Joined: Aug 21, 2008
  Messages: 6,798
  Likes Received: 157
  Trophy Points: 160
  Shame to Mzee Rukhsa!
   
 3. Njowepo

  Njowepo JF-Expert Member

  #3
  Sep 18, 2010
  Joined: Feb 26, 2008
  Messages: 9,297
  Likes Received: 381
  Trophy Points: 180
  Ivi ni lini tutaanza kuwa serious na resources zetu?
   
 4. Mundali

  Mundali JF-Expert Member

  #4
  Sep 18, 2010
  Joined: Sep 16, 2010
  Messages: 749
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 35
  Hao ni wanyama pori, magogo yanayovunwa na wachina je? Halafu wanatuaminisha kwamba serikali haina uwezo wa kuongeza mishahara. Viongozi goigoi noma!
  Vipi lile ombwe la uongozi limezibwa nini????? Maana magazeti uchwara yoooote ni JK kasema hivi kasema vile. Nia yao tukose kiongozi kwa miaka mingine mitano.
  SHAME CHAMA CHA MAPINDUZI.
   
Loading...