USIMCHEZEE MTOTO WA WATU KWA KISINGIZIO CHA UCHUMBA, UTASHTAKIWA.......
Watu wengi na hasa vijana wanapokuwa wameingia kwenye mahusiano ya kimapenzi, maranyingi uhusiano wao wa mwanzo huwa unatawaliwa na uongo mwingi pamoja na ahadi lukuki, ambazo nyingi ni za uongouongo tu. Ahadi hizo huwa ni nyingi mno, na ahadi kubwa inayotamalaki mahusiano yao ni ile ahadi ya "bebi nakuahidi nitakuoa".
Hii inatokana na sababu nyingi, lakini kubwa ni watu kutokuwa wakweli tangu mwanzo wa uhusiano wao. Kwa hiyo, wengi wao huja kujitambua baadaye kwamba walikuwa wakidanganywa na wenza wao, na baya zaidi, ukweli huo wa kudanganyana unakuja kujulikana mwishoni kabisa wakati ambapo mtu huwa anakuwa ametumiwa vya kutosha!
Pamoja na udanganyifu huo ambao ni mbaya sana ukitokea, watendewa huwa wanakaa kimya huku wakijilaumu wenyewe na hivyo kutoa laana nyingi kwa watu waliowatendea, jambo ambalo kimsingi halisaidii lolote.
Hali hii ya kubaki na kidonda cha moyoni bila kujua wapi pa kwenda hutokea kwasababu watu (hasa vijana) wengi huingia kwenye uhusiano bila kujua haki za kisheria zinazotawala katika uhusiano wao huo wa kimapenzi. Wanadhani kwasababu mambo ya kimapenzi ni ya kibinafsi basi hakuna namna ya kulishughulikia kisheria. La hasha!!
Hivyo kwa andiko hili ninapenda kuwakumbusha vijana wa kike na wa kiume mnaovunjiwa uchumba kuwa Sheria inaruhusu kumshitaki aliyevunja ahadi ya uchumba. Kuvunja ahadi ya kuoa au kuolewa, kwa maana ya kuvunja uchumba ni kosa kisheria ambalo linaadhibiwa kwa fidia. Nenda kafungue kesi mahakamani ulipwe fidia ya muda uliopotezewa kwa kumsubiri mtu ambaye ni "laghai wa kimapenzi". Acha kulialia tu!!
Sheria haikukaa kimya na kuacha watu wachezewe halafu mambo yaishie hapo kama wafanyavyo vijana wengi. Ukisoma sehemu ya tano, kifungu cha 69(1) cha Sheria ya Ndoa, kinasema: “Shauri la fidia linaweza kufunguliwa kwa mtu yeyote aliyevunja au kukiuka ahadi ya ndoa na haijalishi ahadi hiyo ilifanyika Tanzania au pengine".
Jambo hili limewekwa katika sheria ili kulinda utu wa watu na kuthamini thamani ya mtu anayejitoa kumsubiri au kumngoja mwenzake kwa kutumaini kuwa siku moja atakuja kuolewa au kuowa mwenza huyo.
Sheria inatambua kwamba katika kipindi hiki cha uchumba, watu hupoteza muda, hali pamoja na mali vitu ambavyo haviwezi kuachwa hivi hivi bila kulipiwa baada ya ahadi kuvunjwa.
Swali:
Je zile zawadi walizokuwa wanapeana wapenzi wakati wa uchumba zinaweza kudaiwa mahakamani ili aliyekuwa amezitoa arudishiwe?? TUKUTANE SIKU NYINGINE............
Bujibuji