USHAURI: Mambo ya kuzingatia kabla ya kuacha ajira na kuingia kwenye ujasiriamali

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,407
Habari rafiki? Karibu tena kwenye kipengele chetu cha ushauri wa changamoto ambazo zinatuzuia kufikia malengo yetu na mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Hakuna kitu ambacho hakina changamoto kwenye maisha na hivyo kupeana mbinu mbadala ni kitu kizuri na inaweza kusaidia mtu kuchukua hatua na kuondoka kwenye changamoto.

Leo katika kipengele hiki cha ushauri wa changamoto, tutaangalia changamoto moja muhimu sana ambayo watu wanaipata kwenye ajira na hivyo kusukumwa kwenda kujiajiri au kuingia kwenye ujasiriamali.

Wote tunajua kwamba ajira mara nyingi zinabana, zinaweza kuwa zinabana muda, kipato au vyote kwa pamoja. Yaani pale ambapo unapata kipato kizuri, basi muda unakuwa umebanzwa sana. Na pale ambapo muda haujabanwa basi kipato kinakuwa kidogo.

Na kuna ajira ambazo unabanwa sana na bado kipato ni kidogo sana.Kabla hatujaangalia kwa undani ni mambo gani ya kuzingatia kabla ya kuacha kazi na kuingia kwenye ujasiriamali, tusome maoni ya msomaji mwenzetu;Mimi nimeajiriwa miaka sita imepita sijapiga hatua nataka kuacha kazi na kujiajili na sijui chochote kuhusu ujasiriamali naomba ushauri wako. M. L Hiyo ndiyo changamoto ambayo msomaji mwenzetu anaipitia.

Karibuni wote tuchambue kwa kina ili kuweza kumpa mwenzetu ushauri ambao utafanya mambo yake kuwa mazuri.Kwanza kabisa pole kwa changamoto hiyo unayopitia, kwa kuwa kwenye ajira miaka sita lakini hujaweza kupiga hatua yoyote.

Inawezekana ajira yako imekubana muda na hata kipato. Pia hongera kwa kufikiria kuingia kwenye ujasiriamali kwa sababu ni njia bora kwako kujitengenezea kipato kinachoendana na juhudi zako.

Kulingana na hali unayopitia, kuna mambo matatu muhimu nataka uyafikiri kwa kina kabla hujachukua maamuzi yoyote.
1. Kwanini mpaka sasa hujapiga hatua?
Usijibu kwa sababu mshahara ni mdogo, au kazi imebana, hapa nataka ujipe jibu halisi, kwa nini umeshindwa kupiga hatua? Kwa sababu nina imani kuna ambao wanafanya kazi kama yako, na wanalipwa kama unavyolipwa wewe ila wao inawezekana wamepiga hatua kuliko wewe. Hivyo hapa njoo na sababu za upande wako, achana kufikiria sababu za mwajiri wako kwa muda.
Inawezekana hujaweza kujitengenezea nidhamu ya fedha, kwamba ukipata mshahara unautumia wote mpaka unaisha halafu unaanza kukopa. Na hapa mara nyingi itakuwa imeanzia kwenye kushindwa kudhibiti matumizi yako na hatimaye yanakuwa yamezidi kipato.
Inawezekana pia una wategemezi wengi wa moja kwa moja na hivyo kipato chako kugawanywa mara nyingi na kukufanya ushindwe kupiga hatua.
Na pia inawezekana una matumizi mengi yasiyo ya msingi, labda umekuwa unanunua vitu kwa kusukumwa na hisia tu. Vitu kama nguo, au kutembelea maeneo ya starehe na kadhalika.Hapo nimetoa tu maeneo ambapo matatizo yako ya fedha yanaweza kuwa yanachochewa zaidi, ila wewe ndiye unayejua kwa upande wako ukweli uko wapi.
Kwa nini ni muhimu sana kujiuliza na kujijibu swali hilo?
Ni muhimu sana ujiulize na kujipa majibu ya swali hilo la kuhusu mchango wako wewe kwenye hali yako ya kipato kuwa ngumu. Hii ni kwa sababu hata kama utaacha kazi na kwenda kwenye ujasiriamali, sio kwamba tabia zako zitabadilika pale pale. Unaweza kwenda nazo kwenye ujasiriamali na mambo yako yakazidi kuwa magumu kuliko hata yalivyokuwa mwanzo.
Ni vyema ukajua ni wapi unapochangia ili uweze kujirekebisha kabla hujaingia kwenye ujasiriamali
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

2. Ukiacha ajira na kuingia kwenye ujasiriamali, mtaji unategemea kupata wapi?
Kabla ya kufanya maamuzi ya kuondoka kwenye ajira na kwenda kwenye ujasiriamali, ni vyema ukajua mtaji unaokwenda kuanza nao ujasiriamali unategemea kupata wapi. Kama kuna akiba zako ulizokuwa umeweka na kwa utafiti wako unaona kiasi ulichonacho kinakutosheleza kuanza biashara, basi hapo upo kwenye hatua nzuri.Ila kama unataka kuacha kazi na bado huna mtaji, na hujui utapata wapi, au unafikiria kukopa, unajiingiza kwenye matatizo zaidi. Kukopa ni njia nzuri ya kupata mtaji wa biashara, ila siyo nzuri kwa mtaji wa kwenda kuanza, hasa kwa mtu ambaye hana uzoefu kwenye ujasiriamali au biashara. Kama bado hujawa na chanzo cha uhakika cha mtaji, ambao sio mkopo, ni vyema ukafanyia hilo kazi kwanza.

SOMA; USHAURI; Tatizo La Kuanza Biashara Na Mtaji Wa Kukopa.

3. Huwezi kuanza kufanya kitu cha pembeni ukiwa kwenye ajira yako?
Swali la tatu muhimu kujiuliza na kutafakari ni je huwezi kuanza biashara hata ndogo ukiwa bado kwenye ajira yako? ni vyema kuliangalia hili kwa undani. Uzuri wa ajira ni kwamba hata kama kipato ni kidogo, bado utaendelea kukipata. Changamoto ya ujasiriamali ni kwamba huna uhakika wa kipato, unaweza kupata na unaweza kukosa. Na mwanzoni kwa mtu ambaye hana uzoefu, kuna kipindi kirefu cha kuendesha biashara bila ya kuwa na faida.
Angalia jinsi kazi yako ilivyo, angalia jinsi unavyoishi maisha yako, na ona kama kuna biashara unayoweza kuianzisha ukiwa bado kwenye ajira yako. kama utapata biashara hiyo ni muhimu kujua kwamba utahitajika kubadili sana mtindo wako wa maisha, ukianza na matumizi ya muda na matumizi ya fedha pia, ni lazima ujenge nidhamu kubwa kwenye maeneo hayo.
SOMA; Sababu Kumi(10) Kwa Nini Uendelee Kubaki Kwenye Ajira Kwa Muda Kabla Ya Kujitosa Moja Kwa Moja Kwenye Ujasiriamali.
Baada ya kujiuliza na kutafakari kwa kina kwenye maswali hayo matatu ni wakati wa kuchukua hatua sasa.
Je unakwenda kuacha kazi na kuingia kwenye ujasiriamali mara moja, au unakwenda kuanza kufanyia kazi tabia zako na kuanza biashara ukiwa bado kwenye ajira yako? hili ni swali ambalo unahitaji kujijibu wewe mwenyewe.Kama unakwenda kuacha kazi basi fanya hivyo na anza biashara mara moja, weka juhudi kubwa na jiandae kupambana na changamoto. Usikate tamaa.
Kama utakwenda kuanza biashara ukiwa bado kwenye ajira, basi jua ni biashara gani na anza mara moja.
Kwa kuwa huna uzoefu kwenye ujasiriamali na biashara, hapa nimekuwekea viungo (link) vya makala zitakazokupa mwanga kwenye hilo, bonyeza na usome.
Fanyia kazi haya uliyojifunza hapa na maisha yako hayatabaki kama yalivyo sasa.
USHAURI; Kuanza Biashara Kwa Mtaji Kidogo, Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuikuza.
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Biashara Kubwa Kwa Kuanzia Chini Kabisa, Hata Kama Huna Kitu.

TUPO PAMOJA
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
 
Back
Top Bottom