Usaliti : Laana muhimu

654

Senior Member
Feb 1, 2012
172
40
NI shetani peke yake anaweza akamshangilia mtu anayefanya jambo baya la kuangamiza taifa pasipo kujali ilimradi apate faida ya kodi za wananchi.Ni mzazi wa mwanafunzi gani anataka mtoto wake akajifunze kwa kutumia vitabu na machapisho ya uongo halafu ahitimu darasa la saba pasipo kujua kusoma na kuandika?Kwa mara ya kwanza chini ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), taifa letu limeshuhudia idadi kubwa ya wanafunzi wakihitimu darasa la saba bila kujua kusoma wala kuandika, na kisha baadhi yao wanachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Tumeshuhudia serikali hii ya Rais Jakaya Kikwete, matokeo mabaya ya kidato cha nne kwa mwaka 2012 ambapo zaidi ya nusu ya wanafunzi waliofanya mitihani hiyo, walipata daraja sifuri.Haya yote yamefanyika wala hakuna anayeshtuka, kuanzia viongozi wakuu wa serikali na watendaji wa ngazi za chini wala hata CCM kama chama tawala, bado hawakuona haja ya kuibana serikali yao ichukue hatua kwa waliosababisha aibu hiyo.Kilichofanyika baada ya wapinzani kuchachamaa wakiwashinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na naibu wake, Philipo Mulugo wajiuzulu, serikali ilikimbilia kufuta matokeo hayo na kuyafanyia mabadiliko (Standardization), na kisha kuyatangaza upya, lakini yakiwa hayana mabadiliko zaidi.

Aibu hiyo ilikuja baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kuungwa mkono na wabunge wa CCM kuizima kibabe hoja binafsi ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) iliyohusu udhaifu katika sekta ya elimu.
Mungu hamfichi mnafiki, wiki hii wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Mbatia akaendeleza hoja yake ya kubainisha udhaifu kwenye elimu kwa kuonesha vitabu, mihutasari na mitaala kwa shule za msingi, vilivyoidhinishwa na serikali kupitia Kamati ya Kuidhinisha Machapisho ya Kielimu (EMAC) ili kutumia huku vikiwa na makosa lukuki.Mbatia alisema serikali imetumia fedha za chenji ya rada sh bilioni 55.2 kusaini mikataba na kampuni zaidi ya 10 kwa ajili ya kuchapisha vitabu na kuvisambaza kwenye shule za msingi.

Ukisoma vitabu hivyo, kwa raia mwema mwenye mapenzi mema na uzalendo kwa taifa lake, unaweza kutoa machozi na kushangaa viongozi wenye dhamana walikuwa wapi wakati vitabu hivyo vikiidhinishwa.
Mathalani, kitabu cha Jiografia cha darasa la sita kilichoidhinishwa na EMAC kwenye jalada lake kimeandikwa kimakosa ‘Jografia'.Vitabu vingine ni cha Hisabati cha darasa la nne, ambacho katika ukurasa wa 49, imeandikwa sifuri gawanya kwa sifuri jibu lake ni sifuri wakati jibu sahihi ni haiwezekani.Pia kitabu cha Hisabati kingine kinaonesha 2x7=15 na kitabu cha Uraia pia kinaeleza kuwa mtaa unaundwa na vitongoji mbalimbali na kuongozwa na wenyeviti wa vitongoji.

Mbatia akasema kuwa kampuni za Macmillan na Oxford zilizopewa jukumu la kuleta vitabu hivyo, zimeshafukuzwa nchini Kenya baada ya kugundulika kuwa vitabu vyao havina ubora wa kitaaluma.
Upo mtaala wa elimu ya msingi ambao unaeleza kwamba elimu hiyo ni kwa ajili ya kumwezesha mwanafunzi aweze kupata uelewa wa lugha ya Kifaransa itakayomwezesha kupata ajira.Halafu mtaala wa elimu ya awali unaeleza kuwa eti elimu hiyo ni kwa ajili ya kumwezesha mwanafunzi kukua kiuchumi, kisiasa na kijamii.Mbatia akasema kuwa vitabu vimetayarishwa bila ya kutumia mitaala, mihutasari ya mwaka 2005 iliyotumika katika utayarishaji kuwa mibovu, taratibu za kitaifa na kimataifa za utayarishaji kutofuatwa.

Pamoja na udhaifu wote huo, wabunge wa CCM hawakuwa na uzalendo wala utaifa ndani yake, badala yake waliweka ushabiki wa chama mbele kumlinda Waziri Kawambwa kibarua chake kisiote majani.
Huu ni usaliti kwa taifa, huu ni uuaji wa vipaji vya watoto wetu kwa kukubali kufunika kombe la udhaifu kwenye elimu na kulinda waziri dhaifu aliyeshindwa kutimiza wajibu wake.

Kwa usaliti huu, CCM inapaswa kulaaniwa na kila Mtanzania.

Walichokifanya wabunge wa CCM ni kupindisha hoja na kujiegemeza kwenye eneo dogo la mgawanyo wa orodha ya shule za sekondari 1,200 zitakazofanyiwa ukarabati wakidai ifumuliwe kwa vile Mkoa wa Kilimanjaro umependelewa zaidi ya mikoa mingine.
Wakaibua kisingizio kingine kuwa Kawambwa hasitahili kujiuzulu kwa vile wizara yake ina majukumu mengi yanayoingiliana na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Kama hiyo haitoshi, wabunge hao wakamtishwa mzigo wa matokeo mabaya Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk. Joyce Ndalichako pamoja na bodi ya baraza hilo kuwa walitumia mfumo mpya kusahihisha na kupanga madaraja bila kuwashirikisha wadau.
Wabunge hawa wasaliti wa elimu yetu wanasahau kuwa ndio waligatua madaraka ya Wizara ya Elimu na kuyapeleka Tamisemi, lakini siku hiyo wakajitia upofu ili kumlinda waziri wao potelea mbali wanafunzi wetu wakifundishwa uongo.

Wahenga wanasema ukweli unakuweka huru. Mbunge wa Mhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema kuwa hakuna tatizo lingine katika Wizara ya Elimu bali viongozi wake hawana uwezo wa kuongoza.Akasema tangu kuingia kwa Dk. Ndalichako na wasaidizi wake pale Necta, wameziba mianya yote ya wizi wa mitihani. Kwamba wanaompiga vita ni wale wenye shule binafsi waliokuwa wakisababisha wizi huo ili shule zao zionekane bora.Kwa hapa CCM ilipotufikisha katika kuzalisha taifa la watu mbumbumbu vichwani, wasioajirika, wasioweza kujitegemea, tuna sababu gani ya kuiruhusu iendelee kututawala? Tafakari!

Edson Kamukara writes for Tanzania Daima on Sunday
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom