radika
JF-Expert Member
- Jul 15, 2014
- 20,450
- 32,292

Maria Sarungi Tsehai
[HASHTAG]#ChangeTanzania[/HASHTAG], Kwanza TV, Compass Communications, all in [HASHTAG]#Tanzania[/HASHTAG]
Kuwa kama maji!
Mabadiliko siku zote hutujaza na hofu hata kama hatutaitambua au kukiri na hii ni kwa sababu hulka yetu kama binadamu tunapenda kila kitu kibaki kama kilivyo. Sehemu kubwa ya maisha yetu tunaitumia kulilia “enzi zile” tukiamini kwamba ndiyo ilikuwa bora zaidi. Na tunatikisa vichwa na kusema “Natamani tungekuwa kama enzi hizo”.
Lakini kiukweli maisha ni mabadiliko, tena mabadiliko kila wakati yasiyo na ukomo. Hata Maria wa sasa si Maria huyohuyo wa jana — kuna mambo nimejifunza, vitu nimeviona, matendo nimeyatenda yanayobadili nilivyo, hapo bado sijagusia mabadiliko ya kimaumbile — sote tunakua na kuzeeka na hatimaye kufariki.
Sasa nimeanza na haya ili tuje kwenye mada yetu ya Mabadiliko. Katika uongozi hususan katika siasa, neno Mabadiliko hupendwa sana na kikundi ambacho kinapambana kushinda na kushika hatamu ambao kwetu tunapenda kuwaita Upinzani. Na Mabadiliko ni neno la kutia hofu kubwa mioyoni mwa wale ambao kwa wakati huo wameshika hatamu za uongozi. Na kadri wanavyoendelea kuwepo madarakani ndivyo wanafikiri mambo yanatakiwa yaendelee kuwa hivyohivyo na neno Mabadiliko huzidi kuwatisha. Alafu wapo wale ambao wanaingia kushika hatamu wakiwa na lengo kuu la kuleta mabadiliko lakini wakishaonja asali ya uongozi wanagundua kile walichokuwa wanapinga kumbe ni kitamu! Basi wanarudi kwenye hali iliyopo (status quo) na kuanza kwa hofu kubwa kupinga mabadiliko yaleyale waliyokuwa wanayahubiri. Tena hawa ndiyo wanakuwa na hofu kubwa na hutumia nguvu nyingi zaidi kwa msukumo wa hofu hii kupinga mabadiliko
Haya ulizeni: haya yote yanahusiana vipi na maji? Ni hivi — wenzetu wanaofuata falsafa ya Tao huko bara la Asia wana msemo au ushauri unaosema “Kuwa kama maji”.
Dunia imefunikwa kwa 71% na maji. Miili yetu 60% ni maji. Ubongo na moyo wetu ni 73% maji na mapafu yetu ni 83% maji. Maisha yetu ni sehemu kubwa maji.
Mvua juu ya mto inaonyesha wazi jinsi maji yanavyobadilika
Maji ina nguvu kuliko kitu chochote lakini ni laini, haibebeki na mkono, haina harufu wala haina umbo.
Maji hubadilika na hali ilivyo kama kuna baridi inageuka kuwa barafu au theluji, kama kuna joto kali sana inageuka mvuke, lakini hali ikiwa ya kawaida inageuka kuwa maji — kitu kilekile kinahimili hali zote bila kuathiri mazingira — yaani inakubali kubadilika bila kupoteza kiini kinachokifanya iwe maji yaani hydrogen na oxygen. Tupo hapo?
Basi kuwa kama maji!
Kiongozi anayetaka kuhimili mabadiliko ajifunze — kuwa kama maji! Asiwe kama jiwe. Jiwe ni imara lakini lazima hatimaye utapata njia ya kuibomoa au kuilipua na itavunjika vipande vipande na kusambaratishwa.
Kuwa kama maji!
Kiongozi anapokumbana na changamoto kubwa iliyosimama njiani asitumie misuli kutaka kupambana na kuitoa changamoto, bali aizingire aielewe alafu ailainishe mpk changamoto inabomoka kama mwamba unavyobomolewa na bahari na kuanguka na kuyeyuka katika maji na kuwa sehemu ya bahari.
Kiongozi, kuwa kama maji!
Maji kwa karibu
Mabadiliko hayazuiliki, tofauti pekee ni jinsi mhusika anavyoyapokea na kuyahimili mabadiliko. Je atakuwa kama jiwe na hatimaye kusambaratishwa au atakuwa kama maji na kubadilika kuweza kuhimili hali iliyopo?
[HASHTAG]#ChangeTanzania[/HASHTAG]
Fuatilia hashtag [HASHTAG]#ChangeTanzania[/HASHTAG] na @ChangeTanzania kusoma mawazo ya watu mbalimbali kuhusu mabadiliko wanayotaka kuona Tanzania.