Unataka kuunda BENDI? Sehemu ya Pili

John Kitime

Member
May 25, 2020
7
30
Katika makala ya wiki iliyopita niliandika mambo kadhaa ambayo ni muhimu kuyaweka mbele katika kusaidia kuunda bendi bora. Kimsingi ukiangalia mambo niliyoyataja utaona kuwa kuunda bendi kuna hitaji taaluma, na si kweli kuwa mtu yeyote anaweza kuunda bendi bora.

Kupenda muziki, kuhudhuria madansi mengi au kuwa na fedha za kununua vyombo au kufahamiana na wanamuziki maarufu sio kigezo cha utaalamu wa kuweza kuunda bendi bora. Unaweza kufananisha na yanayoendelea katika soka, watu wengi tunapenda soka na wengine tumecheza sana mchezo huo katika maisha yetu shuleni na mtaani, hakika huwa tunaweza kutoa maelezo ambayo kwa juu juu unaweza ukadhani yanafaa sana katika kutengeneza au kupanga timu, lakini hakika elimu hiyo pekee haitoshi kuwa taaluma ya uteuzi na upangaji wa timu.

Turudi kwenye muziki, baada ya kuwa sasa umeshajua aina na nia ya kuanzisha bendi, hakikisha umepata wataalamu waaminifu wa kukuchagulia vyombo bora ili usiishie kununua vyombo ambavyo wanamuziki huita ‘mafamba’, vyombo feki ambavyo utakuta baada ya muda mfupi vimeharibika au hata kushindwa kutoa sauti safi kuanzia upya wake. Hivi vyombo bahati mbaya vipo vingi kwenye baadhi ya maduka ya vyombo vya muziki nchini.

Nitoe msaada hapa wa kusaidia kujua kama unanunua ‘famba’ au chombo ‘original’

Ukiona chombo chenye jina kubwa, mfano Yamaha, Fender, Marshal, Korg, Soundcrafters, Seinheiser na kadhalika halafu kinauzwa kwa bei ndogo usifurahie ukadhani ni kwa nia njema, huo ni mtego hakiwezi chombo ambacho kinako tengenezwa kihalali kiuzwe kwa shilingi milioni moja, halafu kisafirishwe kutoka huko na kulipiwa kodi zote, kisha kikaja kuuzwa shilingi laki nne Tanzania. Chunga sana vyombo vya bei rahisi.

Jambo la pili ni kuangalia kama chombo kimeandikwa jina la nchi kilikotengenezwa, sheria za miliki bunifu zinalazimisha watengenezaji halali kutaja nchi kilipotengenezwa kitu mfano, utaona Made in China au Made in Korea, au Made in Japan au Made in USA na kadhalika, ukiona maandishi hayo yamekosekana, ujue hilo ni famba.

Watengenezaji halali huona fahari kutangaza mahala chombo kilipotengenezwa. Kuna ujanja mwingine hutumika wa kuweka maandishi kama USA Technology, au Japan Technology badala ya kuweka maandishi ya Made in…., huo ni utapeli tu wa kukudanganya udhanie kuwa mali hiyo inauhusiano na nchi iliyotajwa ni famba tu hilo.

Jambo jingine ni kuchunga sana usije ukasoma jina haraka haraka, utaweza kukuta majina kama Yamahe ukadhani Yamaha, Sonia ukafikiri Sony, Kogi ukadhani Korg, Sound Kraft ukadhani Sound Crafter huo ni uhuni tu wa kuweka majina yanayotaka kufanana na majina ya kampuni kubwa za kutengeneza vyombo bora vya muziki ili kudanganya wateja.

Na alama nyingine rahisi ya kugundua ‘mafamba’ ni aina ya boksi kilimofungiwa chombo unachotaka kununua. Kwa mfano unaambiwa mixer hii ni Yamaha na ukiiona ina jina la Yamaha, lakini kwenye kasha la kufungia mashine hiyo hakuna alama ya Yamaha hata moja ujue unanunua famba tu, ambalo limepitishwa mpaka kufika dukani kwa kificho ili wenye kampuni ya Yamaha wasije wakashtukia nembo yao kutumika vibaya. Nadhani hako kaelimu ka haraka haraka kanaweza kusaidia kupunguza kutumia fedha nyingi kununua mali feki.

Baada ya haya yote hakikisha nyaya na soketi unazonunua nazo ni zenye ubora. Kununua nyaya za umeme za bei rahisi au vifaa vingine vya umeme vya bei rahisi ni njia moja wapo ya kuharibu hata vyombo vizuri vya gharama kwa muda mfupi.

Asilimia kubwa ya bendi nilizowahi kutembelea hazijali kununua vitu vya kawaida kama top plug au soketi, hivyo huunganisha nyaya kienyeji, mahala zinapoungana waya huwa hakuna gundi maalumu ( insulating tape) na nyaya huwa wazi jambo hatari kwa mtu yoyote ambaye atagusa nyaya hizo. Baada ya kuwa na vyombo vizuri ni muhimu kuwa na fundi mitambo anaejua kazi yake.

Ni jambo la ajabu sana, bendi nyingi humpandisha cheo mbeba vyombo kuwa fundi mitambo na kumkabidhi vyombo vya mamilioni mtu ambaye hana elimu yoyote ya ufundi wa vyombo na sauti. Tajiri mwenye gari la shilingi milioni 5, hatakubali kumkabidhi gari msukuma mkokoteni asie na leseni, lakini tajiri huyo huyo atamkabidhi vyombo vya milioni 30 mtu asiye na cheti chochote cha fani ya umeme wala ufundi mitambo!!

Kinachofuata ni ukusanyaji wa wanamuziki

Niliandika katika makala iliyopita kuwa si busara mtu anaetaka kuanzisha bendi kukusanya wanamuziki kutokana na mtizamo wake au rafiki zake, pia usifanye kosa ya kukusanya wanamuziki kwa kutokana na umaarufu wao, katika zama hizi mtu anaweza akatumia njia nyingi na kuwa maarufu sana lakini si mwanamuziki mzuri sana.

Katika tasnia ya burudani kujitafutia umaarufu huku kumepachikwa jina la ‘branding’, chunga sana kuna watu wamejitengenezea ‘brand’ nzuri lakini ni ‘famba’. Sasa kwa kuwa unajua nia ya kuanzisha bendi, tafuta mwanamuziki mzuri unaeona anauwezo wa kuongoza wenzie, na ambae atakuelewa nia yako ya kutengeneza bendi, mpe kazi ya kukusanya wanamuziki wenzie uwezekano wa kupata bendi nzuri ni mkubwa zaidi kwa njia hii.

20190726_175406.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom