Umenikimbia mpenzi

kwamtoro

JF-Expert Member
Nov 15, 2010
4,922
3,234
  1. Kipi kilokukimbiza?, natamani kukijua
    mahaba nimetimiza, kadiri nilivyojua
    mpenzi umeniponza, moyoni ninaugua
    kidonda nakiuguza, sijui lini tapoa.


  1. Nateseka na giza, mawazo yanisumbua
    maswali najiuliza, kipi nilokukosea?
    baadae najikaza, kuishukuru kadhia
    mola ataniliwaza, naye atanisaidia..



  1. Mapenzi yalinawiri, raha nikajiskia
    leo nini kimejiri?, mbona unanisusia
    tuliiweka dhamiri, tutahimili udhia
    leo bila tahayuri, mwenzio wanikimbia


  1. Vingi vimeniponyoka, wala mimi sikujali
    wengi wamenitoroka, ikawa kwangu sahali
    wewe nikikukumbuka, ninapata idhilali
    ahadi uliiweka , leo hii hunijali.?
Nakuombea salama, nikimbie utoweke!


  1. usije ukalalama, baadae ukumbuke
    nuru yangu umezima, niachie niteseke
    rabi tanipa salama, wala nisiadhirike


  1. Moyo wangu nilikupa, tena nikakuridhia
    leo hii wanilipa , unyonge bila hatia
    penzi umeshalitupa, kwengine waelekea
    mimi waniacha kapa, bila kunihurumia



  1. Ahsante nashukuru, nami nimeyakubali
    madhali sikukudhuru, nenda potelea mbali
    mola nitamdhukuru, anipe wangu asali
    yaILAHI YA KAHARU, nipe moyo nihimili.


  1. Nalia ninaumia, leo hii sina hali
    wajua nateketea, penzi letu kulijali
    mwenzangu wafurahia, umenitwisha jabali
    nami nimelipokea, nifanye mie jahili.



  1. Dunia yazunguka, waswahili wamesema
    wewe utanikumbuka, si hiyari ni lazima
    kwa wema nilikuweka, kwa maradhi na uzima
    leo hii watoweka , kwa mabaya wanisema


  1. Nenda "usotabirika", iko siku nitapona
    kweli nimefadhaika, kwani nilipenda sana
    leo umefarijika, mwenzio ninasonona
    kuna siku nitacheka, tena sio mbali sana.



  1. Mola wangu nisitiri, unipe subira njema
    unilinde YA QAHARI, unipe kilicho chema
    uniepushe athari, ya kupenda aso mwema
    uniongoze JALALI , uwe namimi daima.
 
Back
Top Bottom