Ukitaka kugusa hisia za mwanamke, fanya yafuatayo..

Jielewe

Member
Jan 10, 2017
39
61
WANAUME wengi wanaamini wanawake, kwa kawaida, ‘wanapenda hela.’ Kwamba ukiweza kumhakikishia mwanamke 'uhakika wa kiuchumi' unakuwa umemaliza. Ingawa hatuwezi kupuuza ukweli kuwa uhakika wa 'kiuchumi' ni moja wapo ya mahitaji ya mwanamke, lakini si sahihi kuamini kuwa moyo wa mwanamke unaweza kuthamanishwa kwa fedha.

Fikra hizi walizonazo wanaume [kuwa anachokihitaji mwanamke ni fedha] zimeleta matatizo mengi katika mahusiano na ndoa. Kwa mfano, wapo wanaume ambao baada ya kuhakikisha wenzi wao wamepata mahitaji ya msingi, basi wanawatelekeza kihisia. Hali hii husababisha upweke mkubwa kwa wanawake hawa wanaojikuta hawana mtu wa karibu kuwasikiliza isipokuwa vitu.

mwanamke1.jpg


Upweke, kwa hakika, huzaa migogoro isiyokwisha inayowafanya wanaume [ambao kimsingi ndio wasababishi wa upweke huo] washindwe kuwaelewa wanawake. Kwa mtazamo wao, ni vigumu kumridhisha mwanamke. Wengine wanaenda mbali na kufikiri , 'mwanamke ni kiumbe mgumu kueleweka' kwa sababu, ‘hata ufanye nini...hata umpe nini hawezi kuridhika’.

Lakini wanachosahau wanaume wenye mawazo haya ni kuwa mwanamke kwa asili yake anayo mahitaji ya msingi ambayo yanapopuuzwa, chochote kinachofanyika kama mbadala wa mahitaji hayo hakiwezi kuwa na maana yoyote. Usipoweza kujua mahitaji yake halisi, unaweza kumpa chochote kile unachodhani anakihitaji na bado mambo yasiende kama unavyotamani iwe.

Kusema hivyo, haimaanishi sielewi kuwa wapo wanawake wengi wanaopenda kujipatia fedha kwa wanaume. Hawa ni wanawake wanaofanya biashara ya mahusiano. Kwao, hakuna sababu yoyote ya kuwa na uhusiano imara na wenzi wao isipokuwa mpangilio wa kujipatia vitu na fedha.

Hatuzungumzii uhusiano huo wa kibiashara kati ya mwanamume na mwanamke bali uhusiano wa dhati unaojengwa katika misingi ya upendo, uaminifu, kuelewana na ahadi ya kuwa pamoja katika dhiki na raha.

Hebu na tutazame mahitaji makubwa ya kihisia aliyonayo mwanamke mwenye upendo wa dhati kwa mwenzi wake.

Kupendwa kwa vitendo

Tulishaona kuwa hadhi ya mwanaume inategemea kwa kiasi kikubwa namna anavyoheshimiwa. Kwa mwanamke hali ni tofauti. Hadhi yake inategemea namna anavyopendwa na mwenzi wake.

Upendo kwa mwanamke unaeleweka anapoambiwa bila kuchoka na kuthibitishiwa kwa kutendewa vitendo kuwa anapendwa. Katika lugha ya kiingereza, hapa tungetumia neno affection, yaani matendo yanayoonesha mapenzi kwake.

Hata hivyo, lugha ya mapenzi hutegemea mambo mengi. Kuna athari za utamaduni, desturi na imani zilizopo katika jamii aliyokulia mwanamke. Hata hivyo, yapo matendo yaliyothibitika kuvuka mipaka ya kiutamaduni.
Mfano, kumwambia mwanamke unampenda mara nyingi iwezekanavyo, ni hitaji la msingi. Kwa mwanamume, kuambiwa anapendwa inaweza isiwe jambo la maana, lakini si kwa mwanamke. Mwanamke anatamani kusikia mara nyingi kadri inavyowezekana kuwa anapendwa.

Pia kuna vitu kama kupewa zawadi asizotarajia, kutumia muda wa mapumziko pamoja nae, kutoka naye kwenda mbali na nyumbani na mambo kama hayo yanayoonesha kuwa kweli unampenda.

Ndio kusema, ikiwa unataka kuugusa moyo wa mwanamke, akupe heshima unayoihitaji kama mwanaume, unawajibika kujua vitu gani mahususi ukimfanyia vinatuma ujumbe wa wazi kuwa unampenda. Usipoweza kumfanya mwanamke ajisikie kupendwa, anapoteza hamu ya uhusiano. Huchoka kihisia na anaweza kufanya mambo yasiyotarajiwa ili tu kuhujumu mahusiano.

Anataka kuwa kipaumbele chako


Mwanamke hapendi kujikuta katika mazingira ya kushindania nafasi ya kwanza na kitu kingine chochote iwe ni kazi, mtu au chochote kile unachokipenda wewe mwanamume.

Tulishaona kuwa kwa mwanaume, hadhi yake hutegemea zaidi namna uwezo wake unavyotambuliwa. Hali hiyo humfanya mwanamume atumie muda mwingi kufanya mambo yanaweza kumpa heshima katika jamii. Inaweza kuwa kazi, biashara, mamlaka na namna zozote zile zinazomwongezea uwezo.

Lakini wakati anapotumia muda mwingi katika mambo hayo, ni rahisi kuonekana ameyafanya mambo mengine kuwa ya muhimu kuliko uhusiano wake na mwenzi wake. Wanawake wengi hawapendi kujikuta katika hali hii. Hapa ndiko iliko tofauti.

Mwanamke hatamani kuwa kwenye nafasi ya ‘mengineyo’, ‘ziada’, ‘baadae’ ‘nikipata muda’. Unapomweka 'akiba' mwanamke hawezi kufurahia kwa sababu anatamani awe kipaumbele chako.

Mambo mengi huthibitisha kuwa umempa nafasi ya kwanza. Mfano kuwa na muda wa kuwa naye mara nyingi kadri inavyowezekana, kuahirisha mambo mengine ya muhimu kwa ajili yake, kuwahi miadi unapoahidi kukutana nae, kuwasiliana naye kwa karibu na mambo kama hayo. Unaposhindwa kufanya hivyo, mwanamke hupata ujumbe kuwa yeye ni mtu wa ziada baada ya mambo ya muhimu.

Kadhalika, ili kumwambia yeye ni kipaumbele, mwanamke anatamani kila unapoongea nae akili yako yote iko pamoja naye. Kuwa pamoja naye maana yake ni kuachana na vyote vinavyokuondolea uzingativu na kumsikiliza kwa makini.

Mwanamke anatamani unapozungumza naye ufuatilie anachokisema, umpe mrejesho kuwa unamwelewa na uonesha kuwa mwili, akili, hisia ziko pamoja naye kumsikiliza. Vinginevyo, mwanamke anakuoana kama hujaweza kumpa nafasi yake anayoistahili.

ndoa.jpg


Kueleweka kwa hisia zake

Tumekwisha kuona kuwa mwanaume, kwa kawaida, hutamani kupewa hadhi ya kuwa na sauti ya mwisho kwa kusikilizwa. Kwa mwanamke, hadhi yake hutegemea vile hisia zake zinavyoeleweka kwa mwenzi wake. Jambo hili ni gumu kidogo kueleweka kwa wanaume wengi kwa sababu nitakayoieleza.

Kwa kawaida, wanaume hutamani kutoa majibu kwa matatizo. Uwezo wa kuwa na majibu ni sehemu muhimu ya heshima ya mwanamume. Ndio maana mwanamke anapomfuata mume wake pengine ili kusikilizwa na kueleweka, mara moja akili ya mwanamume hufanya kazi ya kuchakata majibu haraka na kuyakabidhi kwa mwanamke. Uharaka wa majibu humjengea mwanaume hali ya kujiamini.

Hata hivyo, si wakati wote mwanamke anapokuwa na neno la kusema, basi hutamani kupata majibu kama ambavyo akili ya mwanaume inaweza kufikiri. Mara nyingi mwanamke anapolalamika, lengo lake kuwa ni kutafuta utulivu wa kihisia tu basi.
Mwanamke anatamani awepo mtu anayemwamini, anayeweza kusikiliza hisia zake kwa dhati bila kujaribu kuhukumu, kupuuza au kuelekeza vile anavyopaswa kujisikia. Anatamani liwepo sikio linaloaminika kwa mwenzi wake linaloweza kusikia na kuelewa kile hasa kinachomsibu nafsini mwake.

Mwanamke anapokutana na changamoto kazini, kwa mfano, anapoudhiwa na watu wengine, anapohitafiana na majirani, anatamani mwenzi wake awe mtu wa kwanza kusimama upande wake na kuonesha kumwelewa. Ukiweza kuwa msikivu wa hisia za mwanamke unamfanya akuamini kwa alama nyingi kwa sababu umemwongezea hali ya kujiamini kuwa anaye mtu wa karibu anayemwelewa.

Uwazi wa mambo na kuambiwa ukweli

Tofauti nyingine ya mwanamke na mwanamume ni namna wawili hawa wanavyouchukulia uwazi. Tulishaona kuwa mwanamume anapenda faragha na usiri. Mara nyingi usiri huwa ni njia ya kulinda hadhi yake. Kwamba kutokutabirika wala kujulikana anafanya nini hasa ni namna ya kujihakikishia mamlaka yasiyohojiwa na mwanamke.

Lakini katika macho ya mwanamke, usiri na faragha ni dalili ya kutokuwa mwaminifu. Sababu ni kuwa mwanamke anatamani zisiwepo siri zozote asizozijua katika kila kila kona ya maisha ya mume wake. Kujua mambo ya muhimu anayoyafanya mume wake kunamhakikisha kuwa ni kweli mume wake amempa nafasi ya kwanza.

Ikiwa unataka kuugusa moyo wa mke wako, jitahidi kuaminika kwa kufanya mambo yako kwa uwazi kadri unavyoweza. Mwambie unakokwenda, mwambie uliko, mshirikishe mipango yako, mshirikishe siri zako uzizoweza kumwambia mtu mwingine. Ukifanya hivyo, atakuamini na hatakuwa na sababu ya kukupeleleza.

Sambamba na uwazi, kuwa mkweli. Jenga mazoea ya kusema mambo vile yalivyo bila kulazimika kutumia uongo kuficha mambo usiyopenda yafahamike. Mwanamke anapogundua kuwa unayo tabia ya kusema uongo, ujumbe anaoupata ni kuwa wewe si mtu anayeaminika. Asipokuamini, mwanamke hawezi kukuheshimu kama unavyotamani.

Najua wanaume wengi hujitetea kuwa uwazi na ukweli kwa mwanamke ni jambo lisilowezekana. Sababu wanayoitoa ni kuwa wanawake wenyewe hawaaminiki. Ingawa upo ukweli kuwa wapo wanawake wanaoweka wenyewe mazingira ya kufichwa mambo ya muhimu na wenzi wao, hiyo haiondoi ukweli mwingine kuwa mahusiano ya karibu, kama ya ndoa, hayawezi kukamilika bila kuheshimiwa kwa misingi ya ukweli na uwazi.

Kusifiwa kwa ‘uanamke’ wake

Yapo masuala ambayo kwa mwanamke yanabeba wajihi (utambulisho) wake. Kwa wengi, ‘uanamke’ ni pamoja na vile anavyovutia kimwonekano na kimaumbile, namna anavyotekeleza majukumu ya ndani kama mwanamke na haiba yake kwa ujumla. Mwanaume anayetaka kugusa moyo wa mke wake ana wajibu wa kutambua na kuyasifia maeneo hayo.

Kwa mfano, mwanamke hutumia muda mwingi kujiweka katika mwonekano unaovutia. Anakwenda salon kwa masaa kadhaa tofauti na mwanaume. Mara nyingi anapojipamba lengo ni kumvutia mume wake. Msifie.

Jitahidi kugundua mabadiliko anayoyafanya katika mwonekano wake na msifie kwa dhati. Unapofanya hivyo, unaongeza hali ya kujiamini kwake na anapojiamini atakuwa na nguvu ya kukupa heshima unayoihitaji kutoka kwake.

Wakati mwingine, ni kweli umbile la wanawake hubadilika kwa sababu nyingi ikiwemo uzazi. Mwanaume asiyefikiri vizuri huweza kuonesha kutokuvutiwa na mwonekano wake. Hali hiyo inamwuumiza mwanamke hata asiposema. Sababu ni kwamba anatamani awe na mvuto kwa mumewe.

Hivyo, badala ya kukosoa vile anavyoonekana, mwanaume unayejitambua, utatafuta namna ya kujenga mwonekano uutakao kwa namna isiyojeruhi kujiamini kwa mwenzi wako.

Kwa mfano, kama kuna umbile la mwili unahitaji awe nalo, shirikiana naye kufanya mazoezi. Kama hupendi kitambi alichonacho, kwa nini usihakikishe umeondoa cha kwako ili uwe na haki ya kutokuridhishwa na cha kwake? Si sahihi kutamani wengine wawe vile tusivyo. Ndio kanuni ya maisha.

Kadhalika, sambamba na kumhakikishia kuwa mwenzi wako anavutia, fanya jitihada za kutambua vile anavyofanya majukumu yake kama mwanamke. Ikiwezekana msaidie kazi za ndani kuonesha kwa kiasi gani unatambua kazi kubwa anayofanya kama mwanamke hapo nyumbani.

Ni ukweli uliowazi kuwa wanawake wanafanya kazi nyingi za ndani kwa moyo. Kazi hizo zinawachosha mwili na nafsi wakati mwingine. Hawafanyi kazi hizo zote kwa lengo la kupata sifa za wenzi wao. Lakini wanapofahamu kuwa wajibu wao huo unatambuliwa inawapa nguvu ya kujituma zaidi.

Uhakika wa kiuchumi

Hili linaweza kuwa na sura ya kiutamaduni zaidi kuliko kimaumbile. Lakini katika mazingira yetu ya ki-Afrika, tafiti zinaonesha kuwa mwanamke [wa ki-Afrika] anatarajia kuwa majukumu mazito ya kifamilia hubebwa na mwanamume. Huo ndio ukweli. Mume wa ki-Afrika ndiye anayetarajiwa kujua wapi fedha zinakopatikana ili kukidhi mahitaji muhimu ya kifamilia.

Tambua kuwa ingawa ni kweli mwanamke anaweza kuwa na kipato chake kinachotokana na kazi halali, bado hapaswi ‘kulazimika’ kufanya kazi kuilisha familia. Mwanamke wa ki-Afrika amekuzwa kuamini kuwa kinachomhusu yeye moja kwa moja ni majukumu ya ndani ya familia na mume ndiye mwenye heshima (wajibu?) ya kushughulika kuhakikisha kuwa familia inapata mahitaji yake.

Heshima hii aliyopewa mwanamume wa ki-Afrika hufanya mwanamke [wa ki-Afrika] ahitaji kupata mume anayeweza kumpa uhakika wa kiuchumi. Mwanamume hohe hahe, mvivu na asiyeonekana kuwa na dalili za mikakati inayoweza kuleta uhakika wa maisha anapunguza uwezekano wa kuaminiwa na mwanamke.

Mwanamke anatamani kuwa na uhusiano na mwanaume anayejua kupambana kwa lengo la kuilisha familia. Mwanaume mwenye bidii ya kazi, mwenye ndoto na malengo makubwa, mwenye uwezekano wa mafanikio, kwa hakika, anaweza kugusa moyo wa mwanamke.

Tahadhari hata hivyo, ni kuwa, wakati mwingine bidii ya kazi kuenda sambamba na kusahau majukumu mengine kama tulivyoyajadili hapo juu. Mwanaume mwenye busara hujua namna ya kupangilia mambo yake vyema ili kimoja kisifanye kingine kisahaulike.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa uhakika wa kiuchumi hauwezi kukuhakikishia upendo wa bure mwanamke. Lakini, hata hivyo, upendo usioambatana na mipango na bidii ya kazi inayoweza kuleta uhakika wa kiuchumi, unaweza kukaribisha changamoto zisizo za lazima katika mahusiano.

Ndio kusema, ikiwa unataka kugusa moyo wa mwanamke, jambo la sita ni akili inayofikiri vizuri namna gani mwanamke unayempenda atapata uhakika wa mahitaji yake ya kila siku.

Chanzo: Jielewe
 
uzi wako wa usaili ulikua mzuri, mfupi unaeleweka, huu kwa mtu anayetumia simu atakuja kwenye kukoment moja kwa moja (hata mimi sijausoma). Ni mrefu sana.
 
Kinachowafanya wanaume wafikiri hivyo, ni ukweli kuwa hawana muda wa kuwapa wanawake kile wanachokihitaji. Wanatumia pesa kama shortcut. Hata umpe mwanamke fedha, kama hujawekeza kwenye hisia zake, bado hawezi kutulia na wewe.
una uwakika kuwa mwanamke wa sasa ukimpa hela hatulii.
embu jaribu umpe hivyo vingine vyote harafu eti pesa huna. utasimulia.
 
Usitafute hela, wewe jifunze jinsi ya kumfarahisha mtu ambaye hajui exactly anataka nini kwenye hii dunia.
Niwaze kutafuta hela na pia niwaze kumfarahisha mwanamke? Hiyo ni never na kama anahisi hapendwi asepe wanawake kibao wanatafuta hiyo nafasi yake wasiipate
 
Mods wa
uzi wako wa usaili ulikua mzuri, mfupi unaeleweka, huu kwa mtu anayetumia simu atakuja kwenye kukoment moja kwa moja (hata mimi sijausoma). Ni mrefu sana.
Mods wameunganisha. Nitazingatia maoni yako. Makala ndefu inachosha.
 
Back
Top Bottom