Hawa 'mgambo' hawajatambua kwamba wao wanatumiwa kwa manufaa ya 'wakubwa', kuwakandamiza na 'kuwaweka sawa' wanyonge. Huu ni ule mfumo wa 'divide and rule', lakini ipo siku ambayo (Toba Yarabi!) wasio-nacho 'watachoka kabisa' na kuamua kushika sime, mapanga, mishale, upinde, mikuki, marungu na mashoka, na kuanza kuwavamia walio-nacho, wakianzia kwa vibaraka wao, ambao ni askari polisi, mgambo, na wengineo.
Kinachotokea Kenya ni vita kati ya wasio-nacho na walio-nacho. Mali nyingi za matajiri zimeteketezwa, maduka na majengo yamechomwa moto, watu wameporwa magari yao, wamevamiwa nyumbani mwao. Maeneo kama Westlands, Eastleigh, Lavington, Kyuna, na kwingineko, wenye-nacho ambao ni watu wanaomiliki magari ya kifahari wanaogopa kuyaendesha, kwa kuhofia kuvamiwa na wasio-nacho ambao wanaranda mitaani na silaha zao za kijadi, wakiwawinda walio-nacho.
Hawa mgambo wawe makini, kwani iko siku yatakuja kuwakuta. Wao pia ni wanyonge, lakini hawajapevuka kisiasa. Hawajui kwamba wanatumiwa tu... hako ka-mshahara kao kadogo ndiko kanakowafanya wawapore raia wengine ambao maisha yao ni ya duni, huku wenye-nacho wakichekelea na kuomba waendelee hivyo hivyo. Kama wangetaka waache, si wangewapa mishahara inayostahili?
Akina Kanali Massawe waache unafiki; kama ni suala la uhalifu, basi na hao askari mgambo walioiba mali halali za wamachinga wakamatwe, wachunguzwe na washtakiwe mahakamani.
Tuache unafiki!