Ukilaza wa wanafunzi vyuo vikuu, Rais Magufuli kasema kweli?

mwankuga

JF-Expert Member
Aug 30, 2010
334
120
Mwaka 2007,Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilitembelewa na watu muhimu sana japo kwa wakati tofauti.Watu hawa walikuwa Thabo Mbeki (aliyekuwa rais wa Afrika Kusini) na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Mseven.Ukiachana na Thabo Mbeki, Mseven ni uzao wa UDSM,hivyo alikuwa amerejea nyumbani.

Nilikuwa miongoni mwa watu waliokuwepo Nkrumah Hall kuwasikiliza watu hawa.Nilikuwa na hamu sana kumsikiliza Yoweri Gakuta Mseven kuliko Thabo Mbeki pengine kwa sababu nilikuwa simjui vizuri Thabo Mbeki.Lakini mwisho wa siku, Thabo Mbeki ndiye aliyenivutia sana.

Thabo Mbeki alikuwa ameongozana na Basil Mramba (wakati huo akiwa waziri).Basil Mramba alipata shida sana kuingia Nkrumah kwa sababu wanafunzi walikuwa wanamzomea,na wala hawakuogopa ugeni wa Thabo Mbeki.Walikuwa wanamzomea kwa sababu ya kauli zake, ikiwemo ya “hata kama wananchi watakula nyasi, ndege ya rais lazima inunuliwe”, na baadae ikagundulika ndege yenyewe ya rais ilikuwa “mtumba”.Hii ilikuwa kawaida kwa wanafunzi wa UDSM kutowapokea watu/viongozi ambao walikuwa na doa katika utumishi wao.

Ujumbe wa Thabo Mbeki na Yoweri Kaguta Mseven ulifanana, japo walikuja kwa wakati mmoja.Pamoja na mengine, wote waligusia namna viwango vya elimu vyuo vikuu vinavyoshuka, na namna wahitimu wa vyuo vikuu wanavyojihusisha katika kusaidia jamii zao.Thabo Mbeki alitoa mfano wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Tumbatu (Mali) kilivyovurugika, na kuwa na maktaba kama shule ya msingi.Thabo akawa anauliza kama tunashindwa kutilia mkazo kwenye elimu,Afrika haiwezi kwenda popote.

Mseven alianza hotuba yake kwa kusoma maneno kwenye Biblia (japo sikumbuki kitabu gani), lakini alimaanisha kwamba kama wasomi tumesahau wajibu wetu kwa jamii, na badala yake tumekuwa tukifanya mambo kinyume na yake tuliyotakiwa kuyafanya.Alizungumzia namna ambavyo tumekaa tu, huku nchi za Magharibi zikiendeleza ukoloni japo kwa njia zingine tofauti na zamani.

Lakini kabla ya hapo, nilihudhuria kongamano la Chadema pale DDC Mlimani.Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria makongano/mkutano wa chama cha siasa.Kongomano hilo lilihudhuriwaa na wanafunzi wengi kutoka UDSM na Ardhi University.Mtu pekee aliyenivutia sana katika uwasilishaji wa mada, alikuwa Tundu Lissu.Pamoja na mambo mengine, Tundu Lissu alizungumzia namna vyuo vikuu hasa UDSM vinavyopoteza mwelekeo, hivyo akawataka wanafunzi kupigania chuo kurudi kwenye mstari, ili wanafunzi waweze kujihusisha kwenye mijadala ya kulikomboa taifa.Ni wakati huo menejimenti ya UDSM ilikataza wanafunzi kujihusisha na siasa.

Miaka 10 baada ya ziara ya Thabo Mbeki na Yoweri Mseveni, John Pombe Magufuli anakuwa Rais wa Tanzania, naye akiwa ni uzao wa UDSM.Wakati anasoma Phd pale UDSM, Magufuli alikuwa waziri wa Ujenzi, lakini mtu wa kawaida sana,kwani hakuwa na makuu.Mara kadhaa alikuwa anapanga foleni kununua RB (Rice Beans) Cafeteria ya DARUSO.Hii ni nadra sana kutokea kwa mtu wenye cheo ngazi ya uwaziri.Hivyo Magufuli ni uzao halisi wa UDSM na anajua matatizo ya Chuo hicho kwa undani.

Wiki iliyopita alikuwa anazindua ujenzi wa Makataba mpya nay a kisasa pale UDSM, kitu ambacho kiliongelewa na Thabo Mbeki miaka 10 iliyopita.Pamoja na uzinduzi wa ujenzi wa maktaba hiyo, Rais Magufuli alizungumza mambo mazito sana yanayohusu elimu yetu.Moja ya vitu alivyozungumzia, na vyuo kuchukua wanafunzi wasio na sifa (yeye aliwaita vilaza) akirejea sakata la wanafunzi wa mpango maalum UDOM kurejeshwa nyumbani.

Lakini akasema kwa bahati nzuri katika uchunguzi wake, UDSM hakuna wanafunzi vilaza vinginevyo hata asingeenda kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba.Hapa ndipo najiuliza, ni kweli hakuna vilaza UDSM?

Siku chake kabla ya Rais kwenda UDSM, wanafunzi wa chuo hicho walikuwa na mgomo wakishinikiza Bodi ya Mikopo kuwapa fedha za kujikimu.Mgomo huo ulidumu kwa muda wa siku moja, siku ya pili Bodi ya Mikopo ikawapatia fedha zao.Huo ni mwendelezo wa wanafunzi wa vyuo vikuu kugoma, na sababu ikiwa moja tu, kuchelewa kupewa pesa za kujikimu.Kwa siku za karibuni, sijawahi kusikia wanafunzi wa chuo kikuu wakigoma kwa sababu zingine, mfano mauaji ya raia yanayofanywa na watu wasiojulikana, mfumuko wa bei, kupanda kwa bei ya sukari, sakata la escrow, bomoabomoa, uhaba wa hostel vyuoni,nk.

Je, huu sio ukilaza, kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu kushindwa kujihusisha na mambo ya Kitaifa na badala yake wawe wanagoma kwa sababu ya kutopewa pesa za kujikumu? Hata leo hii, ukisikia kuna Profesa Patrick Lumumba anatoa mhadhara Nkrumah Hall, na Ali Kiba yuko viwanja vya Chuo Kikuu, basi ujue kwa kiasi kikubwa mhadhara utapata msukosuko.Tuna aina ya wanafunzi wasiopenda kujisumbua.Leo hii nenda maktaba ya UDSM (ambayo inalalamikiwa ni ndogo), kama utakuta wanafunzi, labda kuwe na assignment.Ngoja nitoe mifano ya migomo ya UDSM ambayo ilikuwa na sura ya Kitaifa (Utaifa).

Mwaka 1966 unabaki kwenye kumbukumbu katika vitabu vyetu vya historia.Mapema mwaka 1966 wanafunzi wa UDSM walifanya mgomo mkubwa ambao ulitikisa Taifa.Mgomo huu unabaki kuwa wa pekee katika historia ya UDSM na Taifa kwa ujumla,kwa sababu kuu mbili.Madai ya mgomo wenyewe na matokeo yake.

Madai ya mgomo huo,pamoja na mambo mengine,ilikuwa ni pengo la walionacho na wasionacho kuongezeka,wanafunzi kujiunga na National Service wanapomaliza masomo na kulipwa asilimia 40 ya mshahara huku viongozi wengine wakiogelea kwenye utajili.
Inasemekana Mwalimu Nyerere alichukuzwa sana na mgomo huo,hasa baadhi ya mabango ,moja likiwa na ujumbe “BORA ENZI ZA UKOLONI”.Baadaye chuo kilifungwa karibia mwaka mmoja,na Mwalimu Nyerere alipunguza mshahara wake kwa asimilia 20.

Mwaka mmoja baadaye (1967) likazaliwa Azimio la Arusha likiwa na majibu ya baadhi ya hoja za wanafunzi.Kwa mantiki hiyo,mgomo wa UDSM ulipelekea kuzaliwa kwa Azimio la Arusha kwa kiasi fulani.
Mwaka 1978, wanafunzi wa UDSM wakawa mtaani tena.Dhima ya mgomo huo ilikuwa kupinga wabunge kujiongezea mishahara huku wananchi wakiishi maisha duni.Inasemekana mgomo huu uliungwa mkono sana na wananchi.Hiyo ni mifano tu ya mtiririko wa migomo katika chuo cha umma (UDSM).

Wakati migomo ya zamani ilikuwa kwa masilahi mapana ya Taifa,migomo ya sasa inatokana na wanafunzi kuwa wabinafsi kwa kujifikiria wenyewe.Migomo ya sasa ni kwa ajili ya boom,na si vinginevyo.Ndio maana nasema migomo ya sasa inatabirika.Kama wanafunzi hawajapata boom basi tegemea mgomo au wanapokaribia mitihani.

Haya yanasababishwa na aina ya wanafunzi tulionao kwa sasa.Enzi hiyo ukimsikia mwanafunzi wa Chuo Kikuu akiongea na jinsi anavyopangilia hoja, ilikuwa inakufanya uongeze juhudi ili nawe ujiunge na Chuo Kikuu/UDSM.Jinsi walivyokuwa wanatoa hoja kwa mpangilio na kuzitetea ungetamani tu.Mwanafuzi akiwa waziri katika serikali ya DARUSO,ungesema pengine anafaa kuwa waziri katika serikali siku zijazo.Lakini haya yote yamepotea.Viongozi wa vyama vya wanafunzi hautamani hata kuwasikiliza,kwa sababu wanaendeshwa na remote control na vyama vya siasa.

Wanafunzi wengi wamejikuta wakijihusisha zaidi kwenye siasa kuliko hata masomo.Hata maswala madogo ambayo yangeweza hata kumalizwa kwa mazungumzo yanashindikana na kupelekea migomo isiyokuwa na ulazima.Ukitazama kwa umakini, utaona kuna mahala vyuo vyetu vimejikwaa, hivyo kufanya kuwepo na wanafunzi vilaza.

Inawezekana kauli ya Magufuli, ya kuwepo na vilaza vyuo vikuu ikawa na ukweli kiasi fulani hata kama itakuwa tofauti na mtazamo wake.Kuna matatizo makubwa katika ufundishaji kutoka shule za msingi, sekondari hadi Chuo Kikuu.Kama wanafunzi wa shule ya msingi na Sekondari hawakuandaliwa vizuri, bila shaka vyuo vitakuwa na wanafunzi vilaza.Ni bahati nzuri sana, kwamba ukilaza umeonwa na Rais mwenyewe, hivyo ataweka mikakati ya kuweza kuepukana na ukilaza huo.
 
Andiko zuri, halijajikita kwenye malalamiko, limechambua uhalisia wa mambo. Ukilaza ni adui mkubwa sana wa maendeleo ya nchi, miaka hii ya karibuni imezuka tabia ya wale wanaochukua degree huku wakifanya kazi, wanacheza michezo ya kufanyiwa msaada wa mitihani, wananunua ubora wa elimu, madhara yake ni kuwa wasikilizaji wasioweza kuchangia chochote cha maana kwenye makongamano makubwa na kazini pia wanashindwa kuwa na tofauti ya utendaji yaani kabla na baada ya kujiunga masomoni UDSM.
 
Sasa wagome kisa escrow, Bei ya sukari inawahusu nini wao na kama hawapewi pesa za kujikimu unadhani wataishije na kama wakigoma leo kesho wanapewa unapata jibu gani hapo
 
Unaweza kusema mtoto ni kilaza kama mazingira ya kusomea ni sawa, walimu wenye Sifa wapo kila shule, uwiano sawa wa idadi ya walimu katika shule n.k. Siyo sasa ambapo mtoto wa shule ya kata anasoma mwenyewe au shule ina mwalimu mmoja ambaye ana fundisha masomo yote hata yale ambayo hakusoma chuoni na hivyo kutumia elimu yake akiwa shule kabla hajaenda chuo. Kwa upande mwingine kuna watoto wa wazazi wa tabaka la Juu na kati ambao husoma shule zenye kila kitu na baadaye kupewa mtihani sawa na wale wanaojisomea wenyewe bila walimu. Mtihani huo hauwezi kuwa kipimo cha kuamua kuwa nani ni kilaza kwani kama wote wangekuwa na mazingira sawa inawezekana walio feli mtihani nao wangefaulu.
 
Ndege ya Rais haikuwa mtumba. That's a cold fact. Labda ulie na bei. Naomba kunyoosha hapo tu.
 
Hayo yote uliyoyaandika je wewe wakati ukiwa unasoma Udsm hayakuwepo? Wewe uligoma au ni mgomo gani ambao wewe ulishiriki na ukaleta mabadiliko chanya kati ya hayo uliyozungumza ambapo yalikuwepo ukiwa udsm!! Migomo uliyoizungumzia hapa ni ya miaka ya 80 kurudi chini, enzi hizi ni tofauti na miaka hiyo, kwanza wasomi kipindi hicho walikuwa ni wachache na masuala ya siasa na elimu kwa wakati huo yalikuwa yametenganishwa sana! Mgomo ulikuwa ukiitishwa kulikuwa hakuna aliyesema kuwa nyuma ya mgomo kuna chama cha siasa kilichousimamia! Hivi sasa hakuna mgomo wowote utakaoweza kufanyika bila kusikia kuwa siasa zimehusika, kwamba chama flani ndicho kilichoratibu mgomo, na hapo lazima timua timua iwakumbe wanafunzi walioshiriki, siasa hivi sasa zinatawala vyuoni jambo ambalo endapo wanafunzi watagoma kwa kushurutisha serikali kushughulikia masuala ya kijamii kama uliyoanisha kitakachotokea ni wanafunzi kupigwa mabomu, kupelekwa mahabusu na mwisho hata kutimuliwa! Labda kwa boom, napo pia vitisho vipo!!
Kwa Tanzania hii hakuna mgomo au maandamano ya kuikosoa serikali yatakayozaa matunda 100%
 
Back
Top Bottom