Ukerewe: Mahakama(inayotembea) yawahukumu watu 7 kwenda jela miaka mitatu kwa kosa la kufanya uvuvi haramu

Chachu Ombara

JF-Expert Member
Dec 11, 2012
5,926
10,485
WATU saba wamehukumiwa kwenda jela miaka mitatu wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza na mahakama ya kutembea (mobile court) kwa kosa la kufanya uvuvi haramu, huku wengine 14 wakifikishwa katika mahakama hiyo kwa kosa hilo.

Watu hao wamefikishwa mahakama hiyo kufuatia opereshani maalumu iliyoanza Februari 18 hadi 28, mwaka huu, katika kisiwa cha Ukerewe.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa operesheni hiyo, Ofisa Mfawidhi wa Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi, Kanda ya Ziwa Didas Mtambalike, alisema wameamua kuboresha utendaji kazi dhidi ya kudhibiti uvuvi haramu kwa kutembea na mahakama ikiwa ni sehemu ya kurahisisha hukumu kwa wahalifu na kuondoa msongamano wa kesi mahakamani.

Aidha, Mtambalike alisema ndani ya siku 10 wamefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa 14 na kati yao saba wameshasomewa hukumu yao ya kufungwa miaka mitatu jela kila mmoja au kulipa faini ya shilingi milioni tatu na wote walishindwa kulipa fedha hiyo na kwenda kutumikia kifungo gerezani kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2009.

Aidha, alisema kikosi chake kimekamata makokoro ya sangara 60, vipande vya makila vilivyounganishwa 1,385, nyavu za dagaa 60, ndoano 4,700, pikipiki 35 na injini 17, huku kikosi cha halmashauri hiyo kikiwa kimekamata makokoro 48 ya sangara, 41 ya dagaa, nyavu za makila 870, ndoano 3,200, baiskeli 20 na pikipiki tano, jumla vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. milioni 500.

Mtambalike alisema operesheni hiyo imeanzia mkoani Mwanza kwenda Kagera, Geita, Simiyu na maeneo yote yanayojihusisha na shughuli hizo, huku akitoa wito kwa wavuvi kufuata sheria.

Ofisa Mfawidhi wa Rasilimali za Uvuvi Mkoa wa Kagera, West Allen, alisema kwa mujibu wa tathmini zilizofanyika zinaonyesha utumiaji wa nyavu za makila na zilizounganishwa umepungua, changamoto zimebaki kwa wale wenye makokoro na timba kutokana na mazingira ya ufanyaji kazi wao.

Aidha, Allen alisema kwa sasa nguvu kubwa itaelekezwa kwa matajiri wanaotengeneza na kuagiza nyavu hizo kutoka nje ya nchi na kuwa na mahakama kwenye operesheni inasaidia utunzaji wa vielelezo vya mshtakiwa.

Naye Ofisa Uvuvi Wilaya ya Ukerewe, Mussa Poland, alisema halmashauri iko tayari kuendelea kuunga juhudi za serikali kwa kuhakikisha wanaboresha vikosi vyao vya doria ili malengo yatimie katika kuelekea kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025 na kutimiza azima ya Tanzania ya viwanda.
 
Sheria imewekwa ili ivunjwe,na ukivunja sheria basi sheria hufuata mkondo wake.
 
Back
Top Bottom